Wednesday, 19 March 2008

Chiligati alivyovuruga kijiwe chetu

JUZI katibu wa umbea wa Chama cha Chui Chatu na Mafisi (CCM - si Chama cha Mapinduzi), Yohana Chilingamiti, alichokoza kijiwe chetu.

Alisema eti kijiwe chetu kinamshambulia bosi wa chama chake. Tamko lake lilikuja sanjari na lile la Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, John Chiligati, akidai wapinzani wanatumia kashfa ya EPA kumchafua Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete! Kwa hiyo wanaodaiwa kushambuliwa ni Mpayukaji Msemahovyo na Jakaya Kikwete. Kwa vile chama cha Chui Chatu na Mafisi si maarufu kama nambari wani, basi tutazama kwenye hili la pili.

Leo baada ya kumlaani katibu wa umbea wa CCM, mpinzani wa Kijiwe, tutajadili tamko la Chiligati wa CCM ya Tanzania. Pia Kijiwe kimepata mwanachama mpya aitwaye Tumbwelizeni. Sisi tunapenda kumuita Tumbomlizeni au Mchumia Tumbo. Huyu ni mpenzi, mwanachama na shabiki wa CCM. Inasemekana zamani alikuwa Kanjanja na alikunywa na kuchanjia maji ya bendera. Hivyo ni kichaa wa chama chake.

Mgosi Machungi analianzisha. “Wgoshi imesikia matusi ya John Chiigati eti wapinzani wananchafua Jakaya? Kweli amejua kutitukana waahi. Hivi nani anaweza kukojoa bahaini akasema ameongeza maji?”

Mchumia Tumbo hangoji. Anaamua kuhami chama lake. “Mgosi tutakosana. Huna hata heshima. Kwanza Chilgati si mtu mdogo kama wewe. Hivi mnataka mfanyiwe nini ndiyo mridhike?”

Mgosi sasa kaguswa pabaya. “Jamani timuhuumie ndugu yetu mgonjwa ah soe, Mchumia Tumbo. Hivi huoni wapi Chiigati ametukana!” Anakwanyua kombe lake la kahawa na kupiga tama mbili, tatu na kuendelea.

“Anasema wapinzani wanataka kumchafua rais! Hivi nani anaweza kuchafua kitu kilichochafuka miaka mia iiyopita? Kwa vie yeye anaipwa na kuteuliwa na rais, basi wote anaona tina makengeza kama yake. Timwambie pasonae:rais anajichafua mwenyewe na wapambe na marafiki zake.”

Mchumia hangoji Mgosi amalize. Anaivaa mic. “Kwanza ni Chiligati siyo Chiigati. Pia yuko right. Nani haoni maenedeleo tuliyofikia kama taifa? Tunaongoza kwa uwekezaji barani. Nchi ina amani. Tumesuluhisha hata ugomvi wa majirani zetu.”

Kabla ya kumalizia, Mzee Maneno anadandia mic. “Kijana mgeni wetu umesema vyema. Kwanza sijui umetokea mkoa gani?”

Mbwa mwitu anaongezea. “Nchi yetu inapaa kama dege la Lowasha. Tunaongoza kwa kuwa na serikali tajiri yenye mashangingi mengi na Wahindi wengi mamilionea.”

Mchumia anajiwahi kujibu swali la mzee Maneno akipuuza kijembe cha Mbwa mwitu. “Suala hapa si mtu anakotoka wala katoka lini bali hoja yenye mashiko mzee wangu.”

Mzee Maneno anasema: “Umenena vyema. Kweli CCM yako imeleta maendeleo. Ni kweli nchi yetu imefufua uchumi kiasi cha kuweza kuzalisha mamilionea kama kina Jeetu Patel, Balaliii, Magerezi, Kagoda na wengine. Kweli tunaona makampuni ya kitapeli yanavyozalisha pesa bila kufanya lolote."

Kabla ya kuendelea Mchunguliaji anadandia mic. “Mzee wangu umesahau. CCM kweli imeleta amani. Huoni wamachinga wa kibongo wanavyofukuzwa ili wamachinga wa Kichina na Kihindi wapate amani? Huoni pale EPA, Richmond, Dowans, IPTL na watukufu wengine wanavyotengeneza pesa kwa amani?”

“Mchunguliaji umesahau. Ndiyo maana Chiligati ameamua kuwakumbusha wapingaji kuacha mchezo mchafu wa kumchafua rais msafi na kipenzi cha watu. Na walaaniwe.” Anachomekea Mkurupukaji.

Kijiwe hakina mbavu jinsi Mshamba anavyoingizwa mjini. Naye anaanza kushtuka kuona anasifiwa ujinga.

Mzee Ndomo anatia guu akiwa anakenua meno yake yaliyoharibiwa na pombe za kienyeji. “Kijana tukusaidie. Huyo mtukufu wako unayeona kachafuliwa ana usafi gani wa halisi zaidi ya sifa za wapuuzi wachache? Kwa maneno jamaa ni msafi. Lakini kivitendo nnnh…huko usiende. Ila watakucheka kijana angalia.”

Msomi leo hangojei. “Mie huyo jamaa namfahamu sana. Tulikuwa wote JKT. Kwa vile kilikuwa hakikupanda aliamua kuzamia huko huko. Si mnajua wakati ule? Hata ukiangalia yanayosemwa yanaonyesha ukihiyo wa mhusika, kwani siri?"

Anakamua kombe lake na kuendelea. “Kama ni ugomvi wa mgeni ndugu yetu Mchumia Tumbo sina ugomvi nchi imepiga hatua. Nadhani ni nchi pekee duniani unapoweza kutumia ofisi ya umma unavyotaka na usipate taabu wala adhabu. Ni nchi ambako kuwajibika ni upuuzi na upumbavu wa hali ya juu!

“Nani anataka mambo ya Kizungu wakati sisi ni Waafrika? Nani anataka viongozi wanaofuatwa fuatwa na wanuka jasho wakati ni viongozi wao? Sisi kweli tumepiga hatua kweli kweli. Tunawapenda watu kuliko watu wowote. Hamkuona juzi rais wetu kipenzi cha watu alivyowapatanisha Wakenya ingawa pale Unguja kidogo atamaliza.”

Mchumia kapata upenyo. Anadandia. “We kweli msomi! Wapo wanaodhani ameshindwa Pemba ilhali anataka kushughulikia kwa makini ili kusiwe na ubishi na hatari kama Kenya.”

“Hiloo! Umesifiwa kunya unaanza kuharisha! Hivi unaelewa anachosema msomi au ndiyo huko kupayuka?” Anapayuka Mchumia tumbo.

Msomi anaamua kumuokoa Mchumia tumbo. “Huyu msimuonee. Kama viongozi wake ni hivyo yeye mnategemea nini? Hujui jogoo aliwafundisha vifaranga kunanihii ndani!”

Anajikakamua na kubwia kahawa kidogo na kuendelea. “Mchumia nakusifu sana kwa welewa wako mkubwa wa mambo. Inaonekana una welewa mkubwa kama viongozi wako hata chama chako. Hakuna kitu kinafanya niwapende CCM kama kutoficha ukweli wao. Nimesikia Mgosi akisema eti rais si msafi. Mzee wangu.”

Anamgeukia Machungi na kuendelea. “Tukubaliane. Rais karithi usafi wa Bwana Msafi, Clean Benjamin Mkapa. Huoni wanavyofanana na kuheshimiana. Hata pale wapuuzi walipomsingizia Mkapa na mkewe kuwa aliiba, rais hakuwaamini.

Na kwa kuwakomesha aliwaambia Mkapa, mkewe, rafiki wala mwanawe hawaguswi na yeyote. Wana kinga hawa. Kwanza hawawezi kuiba. Wana shida gani? Hawa si wavivu wa kufikiri kama wapingaji wanaotapatapa. Upo hapo Mchumia.” Anamgeukia Mchumia anayeonekana kutabasamu lakini kwa mashaka na mshangao asijue kinachomaanishwa.

“Kitu kingine ambapo Chiligati kapatia kiasi cha kumpongeza ni kusema wanataka kumkatisha tamaa rais na kujipatia mitaji ya kisiasa."

Anaendelea Msomi. “Inaonekana wapingaji hawajui dhana nzima ya maendeleo. Hawajui rais ameleta maendeleo sana? Sisi ni nchi pekee yenye kuweza kumgharimia gavana wake wa zamani wa Benki Kuu kuishi kwenye mahoteli makubwa huko Marekani. Hii si sifa kidogo. Sisi ni nchi pekee duniani inayoweza kugawana madini yake na wageni vizuri ili kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.”

Wakati Msomi akiendelea kumchamba Mchumia, Mzee Kidevu anaonekana kukerwa kiasi cha kumnong’oneza Kapende sikioni. “Mbona Msomi simuelewi! Au kaishahongwa pesa ya EPA?”

Kapende. “Siyo hivyo mzee wangu. Inaonekana leo kaamua kutumia vijembe akiwaambia walioko chini ili wa juu waelewe. Anafunga nyama.”

Msomi anaendelea: “Hawa hawaoni rais wetu alivyoteuliwa na waziri mkuu wa Finland kuwa mkurugenzi kwenye ulaji fulani huko?”

Kabla ya kumaliza, Mkurupukaji ambaye ndiyo anaingia anakurupukia mic. “Msomi leo umechemsha. Yaani unafurahia rais wako kudhalilishwa kwa kuteuliwa na waziri mkuu kama wake hata kama ni Mzungu!

Huu ni ukoloni na kufilisika jamani. Hii njaa itatumaliza.”

Akiwa anajiandaa kumjibu, askari wa city walituvamia tukatimka!

Source: Tanzania Daima Machi 19, 2008

No comments: