Thursday, 13 March 2008

Taifa linakwenda wapi?

KAMA kuna sifa Tanzania imebaki nayo si nyingine bali kuparaganyikiwa na kutekwa na mafisi watu na mafisadi karibu katika kila nyanja, kuanzia nyumbani hadi Ikulu.

Nitatoa mifano. Leo tunaletewa habari kuwa mafisadi wanarejesha pesa waliyokuwa wameiba. Ajabu na serikali inapokea bila hata kuchelea kuvunja sheria ilizochaguliwa kuzihami. Je, kwa kufanya hivi serikali inajitofautishaje na mafisadi? Kwanini isiwakamate na kuwapeleka kunakowafaa? Kuonyesha nchi imeharibika kiasi gani, serikali inapokea pesa kwa mlango wa nyuma na kuficha majina ya wezi hawa!

Leo tuna wabunge wanaojulikana kughushi vyeti. Raia wema wamekwenda hadi mahakamani kutaka wahalifu hawa waadhibiwe bila mafanikio. Kisa? Serikali na chama tawala wameamua kupindisha sheria ili kuwanusuru wahalifu hawa. Je, serikali na chama si magenge ya kihalifu yaliyojificha nyuma ya madaraka?

Tuna wabunge wanaojulikana kukamatwa wakitoa rushwa. Ajabu bado wako bungeni wakiitwa waheshimiwa wakati ni wala na watoa rushwa. Je, serikali inayoweza kuwavumilia wabunge watoa rushwa na kuendelea kuwalipa pesa ya wananchi si serikali inayokula rushwa kwa njia ya kusaidia kutendeka kwa jinai hii? Je, chama chenye wabunge watoa rushwa kinanusurika na kuwa mshirika wa jinai hii?

Leo tuna utitiri wa wachungaji matapeli hadi bungeni. Mbona tuliambiwa siasa na dini havichanganyikani? Je, wabunge wachungaji si makada wa chama wanaotumia ushawishi wao kuwaumiza waumini wao kwa kuwalisha siasa chafu? Je, chama chenye uchafu na hila kama hizi si cha kidini ingawa kila uchao kinasema wananchi wasichanganye dini na siasa? Je, huu si usanii na utapeli wa kichama na kitaasisi?

Leo tuna waganga wa kienyeji wanaotumia vyeo vya uprofesa na udaktari ilhali ni mbumbumbu wasio na elimu hata ya kidato cha sita!

Leo tuna matapeli waliovamia majoho na kujiita wachungaji wakitumia luninga na redio kutangaza uongo kwa kumsingizia hata Mungu! Ajabu nasi kama hadhira, tunameza uchafu wao kwa vile tuna shida. Au ni kwa vile tu wajinga?

Ajabu ya maajabu, hata serikali inayopaswa iwe mkombozi wa wananchi, inatoa baraka kwa utapeli na jinai hii kwa kutoa leseni kwa matapeli hawa. Niulize haya unayapata wapi? Nitakujibu. Wapo wengi ninawajua nawe unawajua nao wanajijua. Mtu anakurupuka na kuanza kutangaza anafanya miujiza ya kuponya. Matapeli wenzake wanajitokeza kwenye luninga na kutoa ushuhuda wameponywa! Ebo! Kama unaponya kwanini usiende Muhimbili ukawaponya wagonjwa waliojazana Moi?

Mojawapo ya jukumu la serikali ni kuhakikisha wananchi wanalishwa huduma safi na stahiki. Je, serikali inayovumilia jinai hii si mshirika wa jinai yenyewe? Je, kwa serikali ya namna hii hata viwango vya huduma tunazopata kuanzia vyakula, madawa, elimu hata huduma za kiroho vilivyo chini ya kiwango si kosa lake? Je, serikali kama hii si ya kitapeli na kisanii?

Wapo wanaowaita watu wawape utajiri ilhali wanakwenda kuibiwa. Kama unatoa utajiri kwanini usiipe serikali yetu inayokesha na kushinda ikiombaomba na kukopakopa? Kwanini usiwasaidie watoto wetu wanaopigwa kalenda kila uchao wa elimu ya juu kuhusu mikopo?

Leo watu wanasema pesa iliyotembezwa wakati wa uchaguzi iliibwa serikalini na ndiyo hizi kashfa tunazoshuhudia kila uchao. Si chama wala serikali waliojitokeza kutoa maelezo! Je, hapa hatujawa na serikali na chama tawala vya kihalifu?

Anayebishia hili ajiulize ni kwanini kumekuwa na kelele za ufisadi, lakini hakamatwi wala kutangazwa mtu? Je, hapa tunamuuliza mwizi amtaje mwizi? Nani atamkamata nani iwapo lao ni moja? Nani atamtangaza nani iwapo wote ni wahalifu?

Kuna malalamiko kuwa mkurugenzi mmoja Ikulu ni fisadi kutokana na jinsi alivyotumiwa kwenye mchakato wa kuelekea uchaguzi. Huyu anajulikana alivyotumia kalamu yake vibaya kuudanganya umma. Ajabu ya maajabu anaendeleza ufisadi wake huu na kulipwa pesa ya kodi ya wale aliowadanganya. Je, nchi haijawa ya hovyo?

Mwaka juzi tuliambiwa kuwa serikali ilikuwa na mpango wa kupunguza mashangingi baada ya vyombo vya habari kufichua uwepo wa magari mengi ya bei mbaya yasiyoendana na uwezo na uchumi wetu. Iulize serikali. Imefikia wapi kwenye mkakati huu? Sana sana utakuta imeongeza magari haya. Je, kwa kuwa na serikali inayosema hili na kesho ikajipinga, hatujawa nchi ya wasanii na matapeli?

Gazeti hili limeishaandika tahariri zaidi ya kumi likikumbushia ahadi ya rais kurejesha nyumba zetu zilizoporwa na serikali iliyotangulia. Sasa ni mwaka wa tatu tangu ahadi hii itolewe na hakuna kilichofanyika. Je, kwa kuwa na serikali na viongozi wasiofuatilia wanayosema nchi haijawa ya wasanii na matapeli na waganga njaa?

Leo tuna mgogoro wa kulanguliwa huduma ya umeme ambapo imegundulika kuwa pesa tunayolanguliwa inaishia kuwalipa kina Richmond na IPTL. Ajabu wananchi tunaumizwa tumeshindwa kuchukua hatua. Je, sisi si jamii ya matapeli na wasanii?

Kinacholea upuuzi huu ni ile hali ya kuwa na jamii ya watu vidokozi. Anaibiwa huku naye anakwenda kudokoa kule ilimradi liende. Niliwahi kuonya kuhusu jamii ya ‘pesa ya kula’. Tumekuwa wa hovyo kiasi cha hata salamu zetu kuwa za hovyo. Utamsikia mtu anasema naenda kubangaiza, akimaanisha anakwenda kazini. Anasema bila aibu anatafuta pesa ya kula. Je, ya kuolea, kustarehe, kusomea na kutibiwa ataitafuta lini?

Hapa ndipo hatari ya kuwa na jamii na taifa lenye malengo mafupi inapojitokeza. Huwezi ukaishi kutafuta pesa ya kula tu. Mbona kunguru wasio na akili wanaishi bila wasiwasi ilihali wewe mwanadamu unajigeuza hayawani wa kutumikia tumbo kiasi cha baadhi yetu kuanza kutumia utumbo kufikiri badala ya ubongo.

Ukiangalia malipo waliyopewa mafisadi kuanzia wa EPA hadi Richmond na mambo waliyofanya utaona ukweli wa ninalosema. Ni wa hovyo hawa. Wamepewa pesa ya hovyo wakafanya vitu vya hovyo na kuipeleka nchi kwa hovyo.

Hupenda kuwaita vyangudoa hawa. Hawana tofauti na vyangudoa ambao hujivua nguo na kuuweka peupe utupu wao ili wapate pesa ambayo hatima yake itaishia kuliwa.

Hata ukiangalia kashfa kama ANBEN, Fosnik, Tanpower ukalinganisha na uzito na thamani ya dhima waliyokuwa wamepewa wahusika, utagundua upogo huu. Nyerere anaheshimika na kuogopeka dunia nzima kiasi cha kuwaangusha walio hai akiwa marehemu kutokana na kutokuwa na malengo ya hovyo na mafupi kama ya sasa.

Hakuna kitu chenye thamani kama sifa njema ambayo ni bora kuliko hata uturi. Leo wavitaka vyote uchafu na uturi utaweza? Mfano, rais alitahadharishwa kuhusu mkewe kuwa na NGO kama za wake wa marais waliopita. Nani anajua wafadhili wake na kiasi cha fedha inazopokea na kutumia bila kukaguliwa kimahesabu. Rais amekuwa haoni jinsi EOTFL ilivyomchafua Mkapa? Hakika tumekuwa taifa la hovyo.Source: Tanzania Daima Machi 13, 2008.

No comments: