Wednesday, 17 June 2009

Bajeti ya Mheshimiwa Mpayukaji Waziri Wa Pesa


HUWEZI kuamini. Jana niliota nikiwa Waziri wa Pesa, Mstaafu Mkulu! Baada ya kula magimbi na mbwanda, kama mlalahoi, nilijibwaga kitandani jirani na Bi Mkubwa.

Tulidurusu tuliyodurusu na kila mmoja akageukia upande wake na kuuchapa usingizi. Mara naanza kuota nikitoka ofisini kwangu Magogoni naelekea Uwanja wa Ndege wa Mwalimu kupanda pipa kuelekea Idodomya kuwadodomya na kuwabamiza mkenge walevi.

Nimekula suti ya bei mbaya niliyoinunua Paris na tai ya udhulungi. Nimeulamba kweli kweli kiasi cha kumuacha Bi. Mkubwa akiugulia, huenda huko nitapata dogodogo wa kuniliwaza baada ya kukausha koo nikiwaweka sawa walevi.

Kufika airport natoa maelezo kwa dereva na wasaidizi wangu na kujitoma VIP lounge tayari kupaa. Haichukui muda wanakuja wasaidizi wangu kuniashiria niingie kwenye lango la kuelekea kwenye pipa.

Ndani ya pipa nawakuta wasichana wenye kutabasamu kila saa. Wananikaribisha na pipa linaanza kutimua kuelekea Kipawa tayari kuelekea Dom. Baada ya kutoka uwanjani naelekea kwenye hoteli ya bei mbaya na kubadili suti tayari kuingia bungeni.

Naingia bungeni nikiwa na mkoba wangu wa maangamizi ya pesa ya umma (MPU). Wapiga picha wa vyombo mbali mbali vya habari wananipiga picha kama hawana akili nzuri.

Kwa mikogo na bashasha, natokomea ukumbini na kwenda moja moja kuanza kusoma bajeti ya serikali yangu ombaomba.

Naanza. Mwishiwa Spika, waishiwa wabunge, mawaziri na wananchi kwa ujumla. Watukutu, ifuatayo ni bajeti ya mwaka wa fedha 2009/10.

Utangulizi

Kwanza niseme wazi, hii ni bajeti ya ukombozi wa mlevi na uchaguzi ambayo haijawahi kutungwa katika historia ya taifa hili.

Mwishiwa Spika

Bajeti ya mwaka huu imeongezwa kwa asilimia 365 kutoka bilioni nonihino hadi zilioni moja na ukwaju. Nakohoa na kuendelea. Shughuli za utawala zitakula asilimia 88 na za maendeleo tisa, huku mengineyo yakitumia idadi iliyobaki.

Nchi yetu imeendelea sana hivyo tumepunguza shughuli za maendeleo na kuongeza utawala ili kuwa na utawala bora.

Pia, tumelenga kumkomboa mlevi hasa katika kipindi hiki cha kuvurugika kwa uchumi wa dunia. Ingawa awali nilichemsha nikasema mtikisiko hautalikumba taifa la walevi, niligundua: wataalamu wangu walitafsiri vibaya Kiingereza.

Nilichomaanisha, taifa lingetikisika sana. Hii ndiyo sababu ya kila tatizo mnaloona nchini. Wanaosingizia ufisadi msiwasikilize. Hawajui mambo ya uchumi na kuchuma.

Mwishiwa Spika

Kama nilivyosema hapo awali, bajeti hii ni ya ukombozi wa walevi. Katika kuiandaa tumeangalia mambo mbalimbali na kuyapa vipaumbele.

Mwishiwa Spika

Mwakani tuna uchaguzi. Tumejitahidi kulegeza masharti kwa wananchi ili waweze kutupa kura za kuula. Kufanya hivyo, tumeondoa kodi ya vitambi na vitimbi.

Pia tumepandisha bei za vileo ili kuwaepushia walevi kulewa na kupiga wake zao ukiachia mbali kusahau kupiga kura.

Mwishiwa Spika

Wananchi wa jimbo langu, la mkuu, waziri wa pesa wa zamani na mengine ya marafiki zangu yatanufaika sana na bajeti hii. Tutatengeneza barabara ziendazo na zitokazo huko kuepusha mashangingi yetu kuharibika.

Pia, tutazijenga na kuwa na njia tano kuepusha usumbufu na upotevu wa muda wa waheshimiwa wanapokwenda huko kwa ajili ya ama sherehe za ndoa, ubarikio ama graduation. Pia itaepusha kuvunjika migongo wanaposafiri kuelekea huko.

Pia, tutaagiza mashangingi mengi hata kwa ajili ya nyumba ndogo zetu hata kama wenzetu Kenya kwa uzembe wao wameyapiga marufuku. Hatuna haja ya kuogopa kutumia mashangingi. Tunatumia pesa ya umma haiumi.

Mwishiwa Spika

Kwa majimbo ambayo barabara zake hazitaonekana kwenye bajeti wavumilie hadi watakapotoa mawaziri wa pesa na wakuu. Pia, wajue hii si adhabu. Tumeacha kuzitengea pesa kwa sababu ya kuepuka kuongezeka kwa machinga jijini.

Barabara zikiwa nzuri, watu watakimbia vijijini kiasi cha kuathiri sekta ya kilimo ambayo ni tako la taifa. Hivyo bila tako taifa litashindwa kukaa hata wakubwa hawataweza kukaa na kufaidi viyoyozi. Tutapanua kilimo vipi? Usitake kujua.

Mwishiwa Spika

Pia, tumepungaza bajeti ya elimu hasa ya juu. Hii ni kutokana na ukweli kuwa walevi wamesoma sana kiasi cha kuwa na wabunge wenye PhD hata kama ni za kuchongwa.

Hivyo hatuhitaji wasomi tena. Hivyo pesa ambayo ingepotea bure huko itaenda kwenye kununua mashangingi mapya na kukarabati ikulu na ofisi za mawaziri.

Mwishiwa Spika

Walevi watafaidika na bajeti hii. Japo wengi walinilaumu kwa kufungua tawi la DESI jimboni mwangu, nilitaka kupata uzoefu jinsi ya kueneza utajiri wa wote ili kutimiza ile ahadi ya maisha bora kwa wote aliyotoa mkuu.

Mwishiwa Spika

Kutokana na sababu za kiusalama, sitataja kiwango cha pesa zilizotengwa kwa baadhi ya taasisi nyeti kama ikulu, ulinzi, huduma za bunge, viwanda na uwekezaji na nyingine zinazoangukia kwenye category hii.

In fwact, I mean. Calculations za bajeti hii zime-base kwenye projection na trajectory ya uchumi wa kisasa wa karne ya sayansi na tekelinalokuijia.

Mwishiwa Spika

Kwa mfano ukitaja bajeti ya viwanda na uwekezaji utawafukuza wawekezaji. Hivyo mwishiwa spika, nisisitize; bajeti hii itamkomboa mlevi kutokana na kupanda kwa asilimia 365.

Mwishiwa Spika

Nitaje vyanzo vya mapato ya serikali.

Kwanza ni kodi. Hii italiingizia taifa pesa sawa na asilimia sitini. Hivyo asilimia arobaini iliyobaki tutakopa na kuomba wakoloni, sorry, wafadhili. Na hapa nisisitize. Walevi wakiona tunakwenda sana ng’ambo waelewe tunakwenda kutafuta pesa ya kujazia kwenye bajeti.

Mitumba itatozwa kodi kubwa isipokuwa ya magari ya kifahari. Hatuwezi kuendekeza mitumba hata kwenye miili hata kama vichwani tu mitumba.

Mwaka huu safari za mawaziri mikoani kuelimisha umma juu ya bajeti hazitakuwapo. Badala yake tutakwenda kuanza kampeni kabla ya tume kutangaza. Pia tutakwenda majuu kuvutia wawekezaji kama waziri wa zamani Niziro Kadamage.

Mwishiwa Spika

Bajeti ya mwaka huu ni ya uwajibikaji na kupambana na ufisadi na wizi wa kura na fadhila. Mwaka unaokwisha wa pesa tulivunja rekodi ya kusamehe kodi. Mwaka huu nitakufa na mtu.

Hapatakuwa na cha EPA, Tax exemption and tax profligacy hata kama inahitajika pesa ya takrima kwenye uchaguzi ujao. Kila mtu ajijue.

Nimetenga asilimia 13 ya bajeti kwa ajili ya kuhakikisha pesa ya bajeti haiibiwi kama ilivyokuwa huko nyuma. Kabla ya kuendelea nasikia miguno na mpuuzi mmoja anasema. “Mbona wizi ndani ya wizi!”

Nikiwa nimefura, nilipayuka kwa hasira nasema. “Mtake msitake mwaka huu mtafunga mikanda ili kunogesha mambo.” Nikiwa naendelea kujiotea si Bi Mkubwa aliniamsha kwa kipepsi akidai nawaota hawara zangu tena kitandani kwake!

Alisema: “Mume wangu, yaani umefikia mahali kuwaambia hawara zako wafungue mikanda ili mambo yanoge mbele yangu!” Najibu. “Mbona nilikuwa naota nikiwa waziri wa pesa nikisoma bajeti bungeni mke wangu.”

Hakieleweki kitu. Mara tunaanza kupigana tukigombea bajeti ya ndoto na maangamizi ya pesa ya umma. Tulirejea kwenye mazonge sawa na mlalahoi yoyote ambaye kwake bajeti ni kilio ili wakubwa watanue.

Na hii ndiyo tuliyomaanisha tuliposema maisha bora kwa wote. Wote sisi, si wote wote. Mwenye akili na aelewe na mwenye masikio na asikie, ili tusianze kulaumiana kuwa hatukutekeleza ahadi zetu.
Chanzo: Tanzania Daima Juni 17, 2009.

No comments: