Wednesday, 17 June 2009

Kikwete, Musa hadi Farao na Yusufu!

MCHUNGAJI Lawi Mwankuge wa kanisa la Moravian Ruaha Kidatu, Morogoro alikaririwa na TBC1 hivi karibuni akihoji; “yuko wapi Yusufu wetu wa kuwasaidia viongozi wetu”;

Hii ni baada ya kutangazwa bajeti iliyoua misamaha ya kodi kwa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO).

Kwa wanaokumbuka kauli mbinu ya rais Jakaya Kikwete (wakati ule Musa) ya kuwatoa watu Misri (kwa Benjamin Mkapa) kwenda Kanani ( ambako sasa kumegeuka kubaya zaidi ya alipowakuta), watakubaliana nami: kwa sasa, Kikwete hana sifa tena ya kuitwa Musa kama alivyoingia. Mchungaji ametusaidia. Amemlinganisha na Farao.

Kwanza hajatekeleza ahadi hata moja ukiachia mbali kuzidi kuvuruga. Kwa mfano, Kikwete aliahidi kupambana na ufisadi kama njia moja wapo ya kuokoa pesa ambayo ingetumika kuwaletea watu maisha bora chini ya kauli yake mbinu nyingine ya maisha bora kwa wote. Bahati mbaya sana , maisha bora kwa wote yamegeuka kuwa maisha bora kwa wote waliomzunguka Kikwete na si watanzania kama walivyohadaiwa. Mafisadi wanatetewa hata na mawaziri wake bila ya kuogopa wala bosi wao kuwakemea!

Pili, Kikwete aliahidi kuwa na nidhamu ya matumizi ya pesa ya serikali. Kwa taarifa ya ripoti ya mdhibiti mkuu wa fedha za serikali (CAG), tangu aingie madarakani, karibu kila mwaka, serikali yake inapata alama chafu katika suala hili. Amekuwa akitumia pesa nyingi kusafiri nje ukiachia mbali kuwaachia watuhumiwa wa wizi wa mabilioni yanayosemekana kutumika kumuingiza madarakani.

Tatu ameunda serikali kubwa sana kuliko ya mtangulizi wake ukiachia mbali kuwavumilia na kuwateua watu wanaotia shaka. Mfano wa karibuni ni kumteua Peter Mayunga Noni kuwa mkuu wa Benki ya raslimali (TIB) huku Noni akiwa ametajwa wazi wazi kwenye wizi wa pesa toka benki kuu kwenye mfuko wa madeni ya nje (EPA). Rejea kutajwa na mwanasheria Bhyidinka Michael Sanze aliyesema alishuhudia majadiliano ya wizi huu. Bahati mbaya si Noni, wala Mkapa au watajwa wengine wamekanusha madai ya mwanasheria huyu.

Rejea kuendelea kuwanyamazia na kuwabakiza kazini mwanasheria mkuu wa serikali na mkurugenzi wa Takukuru walioguswa moja kwa moja kwenye kashfa ya Richmond .

Ziko wapi nyumba za umma zilizotwaliwa na Mkapa na mawaziri wake na Kikwete akiwamo? Iko wapi vita ya kupambana na wauza mihadarati na majambazi? Ajabu, Kikwete alijitutumua kuwakamata majambazi wakubwa. Lakini baada ya kukuta kuwa kumbe wengi ni wafadhili wa CCM zoezi hili lilikufa kifo cha mende huku Kikwete akiendelea kuuaminisha umma kuwa ataukomboa. Kwa mdomo ameukomboa sana . Kwa matendo ameupeleka hata zaidi ya Misri. Kama tutaangalia rekodi ya Kikwete, bila shaka, tutagundua kuwa umma ulioahidiwa kwenda Kanani umeishakatiza Misri. Karibuni utaingia Sudan !

Ajabu ya maajabu, Kikwete aliwahi kukiri kuwa anayo orodha ya majambazi na wauza mihadarati! Kama kweli anayo kwanini asiwashughulikie? Ana maslahi gani na biashara hii?

Ukimlinganisha na Mkapa aliyemlinganisha na Farao hadi akatunga kauli mbiu ya kuwapeleka watu Kanani, Kikwete ni sawa na kichuguu mbele yam lima .

Tutatoa sababu. Katika muhula wake wa kwanza, Mkapa alijitahidi kubana matumizi ya pesa ya serikali huku akiubana mfumko wa bei. Pia aliziba mianya ya ukwepaji kodi kiasi cha kutunisha mapato ya taifa yatokanayo na kodi. Kwa ufupi alionyesha dira ya taifa ingawa baada ya kulewa madaraka huku akivutiwa na ushawishi wa mkewe mjasirimali, katika muhula wa pili, Mkapa alibomoa kila jema alilokuwa amelijenga. Na laiti asingefanya hivi, angeweza kuvaa hata viatu vya mtu aliyemtengeneza, Mwalimu Julius Nyerere.

Kwani Mkapa alijiingiza kwenye unyakuzi machimbo ya makaa ya mawe ya Kiwira yakiwa ni kongwa atakayokwenda nayo kaburini ukiachia mbali shutuma lukuki kumuelekea mkewe aliyeanza biashara kwa kuanzisha NGO ya Fursa sawa kwa wote ingawa wote walikuwa wote anaowajua yeye na mumewe. Hapa hujaongelea uwekezaji wa kijambazi ulioongozwa na cha juu.

Mkapa atakumbukwa japo kwa ubaya kwa kuigawa benki yetu ya Biashara (NBC) kuihujumu Tanesco kwa kuruhusu shemeji zake waiingize kampuni ya kikaburu ya Net Group Solution ambayo kimsingi iliiua na kuthibitisha ilivyokuwa Net Problems.

Pigo la mwisho la Mkapa ilikuwa ni kulewa madaraka na kuwa na kiburi. Alianza kuwashambulia waliomkosoa (akina Yusufu). Alifikia hatua hata ya kuwafutia wengine uraia na kuwazodoa hadharani kuwa nao walikuwa wachafu kama yeye. Kikwete anatumia mbinu ya kujifanya hasikii. Yote hii ni kibri na ukosefu wa utawala bora.

Ya Mkapa sasa ni historia. Anaishi kwa kulindwa na rais Kikwete. Kitendo hiki kimewashangaza na kuwachukiza wengi. Wazungu husema: show me your friends I will tell you who you are. Nionyeshe marafiki zako nitakwambia wewe ni nani.

Hapa ndipo, kwa mara nyingine u-Musa wa Kikwete unayeyuka kiasi cha mchungaji Mwankuge kumlinganisha na Farao.

Farao aliwatesa waisraeli sawa na Kikwete anavyofanya. Kwani aliwatwisha mzigo wa kunyonywa na kudhalilishwa. Wizi wa EPA, Richmond , Dowan, IPTL, TICT, CIS, NSSF, ANBEN, Tanpower, Fosnik na mwingine mwingi hauna tofauti na matendo ya Faroa.

Kwanini tuendako maneno ya Mwankuge yanaweza kubeba ukweli usiopingika? Kikwete haonyeshi kujifunza wala kurekebika hata abebwe namna gani. Jiulize. Sasa ni mwaka wa tano tangu aingie madarakani. Ameishatimiza ahadi gani? Hata aliposhauriwa kuachana na uwaziri wa mambo ya nchi za nje yaani kupoteza muda mwingi na pesa ughaibuni, hakuacha. Hivi karibuni jarida la kimataifa linaloheshimika la The Economist lilimtolea uvivu na kusema: ziara zake zinalihujumu taifa. Kama kawaida yake, hakujibu wala kujali.

Ameendelea kumvumilia malkia wake kuendesha biashara ya NGO sawa na ya mke wa mtangulizi wake. Ingawa Mkapa anachukiwa kwa aibu na uroho alioonyesha kwa kukwapua mali ya umma, ukiwaweka kwenye mizani na Kikwete, Mkapa anaweza kuwa bora. Maana kwenye muhula wa kwanza angalau alionyesha nini maana ya utawala.

Wachambuzi wengi wa mambo wanakubaliana kuwa kama Kikwete atachaguliwa kwa muhula wa pili na akaendelea kama alivyo sasa, ataiacha nchi pabaya kiasi cha kuweza kuzusha hata vurugu na amani tunayojivunia ikatoweka. Hapawezi kuwa na amani ya kweli bila haki.

Akina Yusufu tumesema hadi makoo yamekauka. Mwenzetu ana kinywa kipana lakini hana masikio kabisa. Anajua kusema si kutenda. Yeye ni mtu wa kucheza na hadhira jukwaani lakini mwoga wa kuingia kwenye medani. Huu ndiyo watani wake huuita usanii. Tatizo si kuwepo Yusufu bali Yusufu wapi awasikilize.

Kama tutamtendea haki Kikwete, si vibaya kumlinganisha na Farao. Hata wakati Farao anaweza kuwa na nafuu. Kwa sababu hakuwaahidi waisraeli ukombozi wowote.
Chanzo : Tanzania Daima Juni 17, 2009.

No comments: