The Chant of Savant

Wednesday 3 March 2010

Kitabu cha “Saa Ya Ukombozi"


Kwa muda mrefu, wasomaji wangu -niliowataarifu kuwa nimetunga kitabu cha “Saa Ya Ukombozi-”, wamekuwa wakiulizia, kwa shauku, lini kingetoka.

Kwanza, niwaombe msamaha kwa kuchelewa kutoka. Pia niwashukuru kwa subira yenu. Yote ni kutokana na sababu ambazo ziko juu ya uwezo wangu.

Nikiri kabisa. Nilitoa taarifa ya ujio wa kitabu hiki nilipopata mchapishaji wa kwanza aliyeishia kuwa tapeli aliyekuwa akitaka dola zaidi ya kuchapisha kitabu bila kufanya hivyo. Nadhani roho itamsuta.

Kwa vile kitabu ki’shatoka, haya ya kusahau. Tuenga na kusonga mbele.

Nichukue fursa hii, rasmi, kuwataarifu watu waliokuwa tayari kunisaidia kukisoma na kukipitia kitabu pindipo kikitoka. Hawa ni Profesa Issa Shivji, Jenerali Ulimwengu na padre Privatus Karugendo aliyenitambulisha kwa mchapishaji. Maskini hatujawahi hata kuonana!

Je “Saa Ya Ukombozi” kinahusu nini, kimechapishwa na nani na wapi? Kimechapishwa na Tanzania Education Publisher Limited (TEPU) ya Bukoba Kagera na kupewa namba ya ithibati ISBN 978 9987 07 039 8.

Hapa lazima niseme wazi. Bila msaada wa mzee Pius. B. Ngeze, mkurugenzi mtendaji wa TEPU, kazi hii ingechukua muda mrefu. Nimefaidika na kuchota toka kwenye uzoefu wake kama mtunzi. Namshukuru mzee huyu kwa namna ya pekee. Aliweza kupata cheti cha ithibati ya lugha toka Baraza la Kiswahili, jambo ambalo nisingeweza.

Kitabu hiki, kama lilivyo jina lake, ni riwaya inayoelezea maisha ya wananchi wa nchi ya Mizengwe; nchi iliyozungukwa na kutekwa na mizengwe karibu katika Nyanja zote za maisha.

Nchi ya Mizengwe ni ya kubuni japo inashabihiana sana na nchi nyingi barani Afrika kwa mengi. Hata sera zake za ubinafsishaji uliozaa ufisi, ufisadi na ubinafsi zinafanana. Hata watu wake wanalandana sana japo ni wa kufikirika.

Kutokana na nchi ya Mizengwe kutawaliwa kwa mizengwe, wananchi wa kawaida walijikuta kwenye utumwa uliozaliwa na kile walichopigania wakidhani ni uhuru kumbe Udhuru! Wanakijiji wa Githakwa hawakuona mantiki ya kuwa mashahidi wa maangamizi yao tena ukitumika ‘uhuru’ uliogeuka udhuru walioumwagia damu kwa miaka mingi.

Wanakijiji cha Githakwa, kijiji kilichogundulika kuwa na vito vya thamani visivyopatikana kokote isipokuwa Githakwa wanajikuta wakiuzwa bila wao hata serikali kuu kujua! Mbunge wao, Harry mtoto wa mpishi wa zamani wa wakoloni na msaliti Livingstone Kupata, anawauza kwa mwekezaji wa kizungu Glutton Sucker mwenye kampuni la Get Rich in Goon’s World Co (GRGW) kwa kushirikiana na mkuu wa mkuu wa wilaya Mrongo Kumbakumba, mkuu wa mkoa, Gibbons Dikupatile na waziri wa fedha ambaye ni shemeji yake Harry baada ya kupewa chao -ten percent- ambayo imegeuka muuaji mkuu wa chumi za nchi nyingi na watu wake.

Wakati yote haya yakijiri, si rais wala wananchi wengine wana taarifa ya hujuma hii iliyofichwa kwenye uwekezaji wa kifisadi, ubinafsishaji vinavyogeuka kuwa ufisi na ubinafsi. Kila mwenye madaraka ana-Chukua Chake Mapema hata kwa kuwauza watu wake na mali zao. Kila chura analia kivyake na kila mbuzi anakula zaidi ya urefu wa kamba yake!

Katika kisa hiki, mzee mmoja maarufu Njema anawaongoza wanakijiji kupambana na jinai hii. Kwa msaada wa vyombo vya habari na mashirika ya kupigania haki za binadamu, wanakijiji wanafanikiwa kuwashinda wezi hawa wa mchana tena wa kuzaa wenyewe.

Vyombo vya habari vinalipua ‘bomu’ kiasi cha rais aliyekuwapo ziarani ughaibuni akitumbua kustuka na kujaribu kuchukua hatua asiweze. Kwani ushindi wa wanakijiji unageuka chachu ya kuanguka kwa utawala mbovu wa Mizengwe. Kwa mara ya kwanza, mapinduzi ya kulikomboa taifa yanaanzia kijijini na kusambaa nchi nzima na hatimaye kuangusha serikali chafu na chovu kwa amani kupitia sanduku la kura.

Kwa ufupi, riwaya hii inaudurusu na kuzulu uhuru na dhima nzima ya kuwa huru. Inaona shaka na uhuru wa baadhi ya nchi barani Afrika unaowanufaisha watawala waliojigeuza miungu pamwe na walamba viatu wao. Watu wa kawaida hawaruhusiwi kutia mkono kwenye deste nao wale halua!

Riwaya inahimiza umma kushika hatamu. Inashadidisha umma uutathimini na kuuhoji upya uhuru wanaoambiwa ni wao wakati si wao. Katika kufanikisha hili, tofauti na mapambano ya mtutu wa bunduki, mauaji na ghasia, riwaya hii inawahimiza waathirika waishio kwa matumaini kuupigania na kuupata uhuru wa kweli kupitia kwenye sanduku la kura.

Riwaya inahimiza watawaliwa kuhakikisha wanawawajibisha watawala kama sehemu ya uwajibikaji wao. Kila mmoja awajibike kwa mwenzake. Inawataka watawala wawatumikie watawaliwa badala ya kuwatumia kama punda wa kuwabeba wao na mizigo yao.

Riwaya inapinga ufisi, ukuku, umbwa, ukondoo, usindano, ukijiko na tabia nyingine kama hizo; inashajihisha usimba, umizani na utambuzi, utendaji na ulinzi wa haki.

Hapo ndipo utamwona mhusika mkuu, Mzee Njema, akipambana na uongozi mbovu kuanzia kijijini mwake hadi wilaya na,hatimaye, taifa. Cheche ya shujaa inawasha moto unaouamsha na kuukengeua umma kiasi cha kuangusha serikali dhalimu ya Mizengwe kupitia sanduku la kura.

Riwaya hii ni onyo na karipio kwa tawala zote zandiki na fisidi kubadilika na kuacha kufanya mambo kwa mazoea. Business as usual kwenye kulea na kufuga ufisadi na unyonyaji wa wananchi wa kawaida inapaswa kumalizwa na wananchi wenye bila kutegemea mjomba au nani.

Ukiachia dhana nzima ya ukombozi kisiasa, kuna changamoto ya kujikomboa kijamii hasa kimila. Hii nayo imechukua sura maalum kwenye kitabu ambapo watoto wawili wa mzee Kupata, mmoja ameoa mzungu na mwingine kuolewa na mzungu. Wazungu hawa wameleta kizunguzungu kutokana na matendo yao huku na wanakijiji wakiwaacha wazungu hoi kutokana na maisha yao ambapo wazungu wanawashangaa kulala na mbuzi nyumba moja wakati wao wanalala na kula na mbwa!

Somo kuu la riwaya hii ni kufanya maasi na mapambano matakatifu kwa njia ya amani. Ni fundisho kuwa, kama kura ikitumika vilivyo, inaweza kumkomboa mpiga kura. Hivyo basi, kama mzee Njema na wanakijiji, inatubidi kusimama kidete kulinda uhuru, haki, raslimali na taifa letu kwa ujumla badala ya kulia lia na kulalamika.

Hakuna njia muafaka na mujarabu kama kutumia vizuri kura yako wewe mpiga kura. Hakuna ukombozi kamili kama kushiriki mchakato mzima wa kuendesha na kufaidi nchi yako wewe mwananchi. Hii yote inawezekana pasipo woga wala kukubali kuhongwa, kuburuzwa na kugeuzwa mnyonge wa kunyongwa.

Kama wanakijiji wameweza kwanini taifa lisiweze? SAA YA UKOMBOZI NI SASA NA MKOMBOZI NI WEWE UNAYENYONYWA.

Dokezo, baada ya “Saa Ya Ukombozi”, jiandae kupata “Nyuma Ya Pazia” ambapo nchi ya Mafuriko iliyofurika neema imegeuka kuwa mafuriko ya nakama na zahama huku ikiraruriwa nyuma ya pazia na watawala mafisi itadurusiwa vilivyo na kiini cha ufisadi kufichuliwa baada ya kutimliwa waziri mkubwa Edmond Mpendamali Mwaluwasha. Pia kuna vingine vya ‘Kwetu ni wapi?”, “Niogopeni Ukimwi”, “Hekima”, “Aya Za Ukombozi”, “Lulu Yangu Tanzania” na “Vimbwanga Vya Mpayukaji.”

Kila la heri na kitabu chenu ni hicho someni na mchambueni bila kusahau kukitumia katika kutatua matatizo na mazonge yenu.
Piga simu namba 0784 780079 upate nakala yako.
Chanzo: Nkwazi Mhango

5 comments:

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Inaonekana ni riwaya dhati pevu inayopaswa kusomwa na kila mpenda maendeleo. Kwa sisi tulioko nje tutakipataje?

Ninaomba ufanye utafiti wa vyuo vinavyofundisha lugha za Kiafrika hapa Marekani kisha uwaandikie watu wa maktaba hizo wakiagize. Wataka kula dola ati!

Ninaweza kukusaidia kufanya hivyo kwa maktaba ya hapa Chuo Kikuu cha Florida.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Ndugu yangu Matondo,
Shukrani kwa mwanga na msaada wako. Kusema ukweli nami niko mbali na nyumbani. Ila kama utaniunganisha na vyuo hivyo nitakushukuru bila ukomo. Sina neno. Unaweza kuanza mchakato hata leo bila kikwazo chochote.
Kila la heri,
mail yangu ni nkwazigatsha@yahoo.com

Sirili Akko said...

Nashukuru kwa habari hiyo njema,maana nilirudi sana bookshop kukiulizia ikaonekana kama nataka kumchumbia mfanyakazi wa hiyo bookshop.

Akko.

Nkwazi Mhango said...

Pole sana ndugu na rafiki yangu Akko. Hata hivyo kama huyo mdada unaona anakufaa na huna jikio ruksa.
Kama umepata nakala yako nimefarijika sana.
Pia nitumie fursa hii kumkumbusha ndugu yangu Matondo kuwa bado nangoja kusikia kutoka kwake ili tuone tutakavyopeleka Saa Ya Ukombozi kwa nchi ya Obama. Tutakuwa lau tumetoa changamoto kuwa nasi kama Wabongo bado tuna bongo ingawa wengi husoma vitabu toka kwingine. Tumekuwa tukipeperusha jina la Shaaban Robert bila kumsaidia. Ni wakati muafaka kumsaidia. Maana waandishi wetu kama Prof. Kezilahabi sasa wamezeeka. Lazima vijana tuwapokee kijiti ili tuendelee kupeperusha bendera yetu kitaaluma ingawa kisiasa hatuna bao. Kwani vyangudoa na manyang'au wa kisiasa wamelinajisi na kulibaka jina zuri Tanzania. Tunapaswa kuwaonyesha kuwa hawajatumaliza. Saa ya ukombozi ni sasa.

Simon Kitururu said...

Asante kwa taarifa Mkuu mie ntakisaka!