How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do
Monday, 29 March 2010
Nilitabiri mkanipuuza
NILIPOTABIRI ambayo yangeikumba nchi ya Tanzia, wengi waliniona chizi anayejifurahisha. Nilitabiri: Kahaba wa makahaba aitwaye mzuri kwa jina la HAKIJA, aliye machukizo ya machukizo aliyeinyakua na kuitawala nchi hii ya uzuri wa ajabu, atawaalika wenzake wainajisi ardhi kiasi cha kuwageuza watumwa Watanzia.
Ni kahaba huyu aliyekataliwa na nabii Musa akionya: “Watakuja wengi kwa jina langu wakiwaaminisha watawapeleka Kanani. Lakini watawapeleka machinjioni baada ya kuwaibia na kuwanajisi nyinyi na ardhi yenu. Wataacha maafa kwa vijukuu zenu baada ya kuwatesani.” Hamkumbuki? Nabii Musa alimkataa kiumbe huyu wazi wazi ili anusurike. Hakubabaishwa na urembo na tenzi zake.
Hamkumbuki! Mlionywa. Uzuri, mnaodhani HAKIJA anao, umeficha ukatili na uoza visivyo kifani! Ni mchafu kuliko hata uvungu wa ndoo. Hafai hata kuaminiwa kiporo, achia mbali mali za thamani na uhai wenu.
Muone mara ngapi ndipo muamini unabii? Mlifanya kosa kupuuzia unabii huu. Sasa mmeishajionea gharama yake. Je, mtaendelea na wehu na ujuha kumwacha kahaba azidi kuinajisi ardhi? Au mnataka mpigwe na kwa mapigo ya vyura na nge ndipo mgutuke maskini majuha nyie.
Pia nilionya: mtakamatwa na kufungwa kongwa na kuelekezwa majili kama kondoo kwa malipo ya vitu uchwara na kujilisha pepo.
Japo niliongea kwa lugha rahisi, watanzia hawakunielewa! Kama wapo walionielewa, walinipuuzia wakiendelea kufanya ufuska wao chini ya utawala wa kahaba mkuu.
Leo natoa tahadhali nyingine kwa watu wa Tanzia. Ni juzi tu nilisikia kuwa sarafu yenu ya Kwenje inaghushiwa na wakubwa zenu ili kupata mitaji ya kuwanunulia upuuzi nanyi muwape kura ya kula. Haya yamesemwa mchana juu ya uchafu huu.
Kwanza, nalaani japo sihusiki. Kama jina lenu, sasa mmefikia kwenye kitanzi na mwisho tutatangaza tanzia. Yaani mnachezea pesa yenu wenyewe tena kwa kutumia mamlaka zenu wenyewe kisa eti kuwawezesha makahaba wachache kuendelea kuwatawaleni! Ni hatari na aibu sina mfano.
Maadui hawa wa kweli wamewahadaa na kuwatengenezea maadui bandia. Nanyi mmekubali! Kimsingi, maadui ni wao si hao wa kutengenezwa. Mnadanganywa kuwa ni bora na salama wakati hamna lolote.
Mgekuwa wa maana na bora msingefanyiwa mnayofanyiwa-ujambazi na unajisi wa mchana. Ni nani akuheshimuye kwa kukugeuza changudoa kimaisha? Hakuna heshima katika kulambana vichongo na kushindiliana visu tena kama jamii.
Walianza na kuhomola wakapigiwa kelele na kuumbuka ingawa hawakushughulikiwa. Wako wapi akina HEPA zaidi ya kugeuka mahepe? Nambie. Wako wapi akina Kagodoka bint Ikuru, Richmonduli na wengine? Sasa wameanza kuchonga sarafu na kuighushi!
Uchumi wenu sahauni ndugu zangu watanzia mliovamiwa na makahaba na majambazi kutoka kila kona ya dunia. Kila siku wanaingia kwa ndege, treni, mitumbwi, meli hata mabasi nanyi mnaangalia tu! Mmekwisha amkeni.
Kama hamjui jueni. Hii ndiyo siri ya uchumi wenu kuendelea kuwa nusu kaputi wakati wa viinchi vidogo tu uking’ara. Mnatawaliwa na wezi na majambazi wajivikao utukufu. Msipofutu hili jueni mmekwisha tena vibaya.
Sasa natabiri jingine kubwa lao. Baada ya kughushi sarafu kesho wataghushi shahada za uchaguzi. Hapa ndipo fumbo la ushindi na vishindo ulipo siku zote ingawa hamjawahi kung’amua.
Nilionya kuwa maadui zenu ni watu wenu wale wale wajivishao utukufu na utoaji wa haki wakati wao ndiyo kikwazo cha haki na maendeleo yenu.
Pia niliwaonyeni kuacha umbwa na ufisi ambapo mnalishwa nyama za wenzenu kwa kuungwa na kukaanga. Narudia tena kwa lugha rahisi. Msipoacha tamaa na ujuha wa kupenda kuhongwa upuuzi mmekwisha na msinililie siku mtakapojikuta majilini.
Ingawa ni ujuha na utoto kuchezea sarafu yenu, tatizo kubwa ni nyinyi wavivu wa kufikiri na kufanya maamuzi magumu. Hawa wanaofanya hivi nao ni majuha kama nyinyi ingawa wanajiona wajanja. Kwani wanaishi katika leo na kuipuuzia kesho, wasijue kesho ni bora kuliko leo!
Wao watafanya ukahaba wao na kutoweka. Tanzia ilikuwapo na itakuwapo milele. Je, ni nani mpumbavu aachaye miiba kwenye shamba ili imchome mwanae kesho? Wambieni waelewe ingawa hawana masikio. Kwa vile hawana masikio, tumieni lugha ya nyuki ambao bila moto huwa hawaondoki mzingani.
Niliwaonya mbabane na kujua kila kipato cha mtu awe mkubwa au mdogo mkaniona wa jana. Mlitanguliza ujuha wa ujanja kupata au kuwahi.
Yako wapi sasa? Haya mmeambiwa kila kitu kuwa sarafu yenu si salama wala nyinyi na nchi yenu si salama. Mtakuwaje salama wakati mwaelekea majilini? Nchi inachezewa kama mnavyochezewa. Sarafu inahujumiwa kama inavyohujumiwa ukiacha mbali nyinyi na vizazi vyenu.
Tanzia imnekabidhiwa mikononi mwa wageni wenye uchu kama fisi wakijiibia watakavyo na kuhamisha utajiri wenu wakati nyinyi mnanyongwa na ulofa. Tieni akilini sasa. Chukueni hatua sasa.
Wanakuja kwa gea mbali mbali, uwekezaji ambao kimsingi ni uchukuaji. Utalii na akila aina ya mbinu wakisaidiwa na vyangudoa wao waliozaliwa Tanzia. Hakuna kuishiwa kama mtu kujiibia mwenyewe hasa anapokuwa amekabidhiwa dhamana hii na umma.
Juzi mliibiwa TiRaeLo na hao hao kwa kisingizio kuwa wenzao wameshindwa. Kwani hawakuambiwa kuwa hawa jamaa ni watupu? Lakini nani angesikia wakati alikuwa akisikia na kuona kwa ten percent? Halafu mbweha hawa hawa eti wanawaaminisha wanaweza kuwavusha nanyi kwa ujuha na utaahira wenu mnawaamini!
Kama nyinyi si wanafiki basi ni vichaa wa aina yake chini ya jua. Mshikwe wapi mshtuke? Mliwe vipi hadi mchukie? Muibiwe vipi ndipo muone hasara? Mdhalilishwe kiasi gani ndipo muudhike? Ashakum si matusi huenda mliumbika bahati mbaya. Ni ajali ya kimaumbile huenda.
Nimalizie kwa kuwaasa kuwa adui wenu mkubwa ni nyinyi mnaotoa mwanya kuwaalika makahaba kuinajisi ardhi yenu takatifu. Chukueni hatua sasa na wakati ni huu. Acheni uroho na ujuha woga na kuishi kwa matumaini. Habari ndiyo hiyo.
Hivi kuku wako akianza kula mayai huwa unamfanyia nini? Je, wale uliowaamini kulinda sarafu yako wanapoanza kuighushi utawafanya nini kwenye kipute cha Oktoba? Kazi kwako. Lo! Kumbe nilikuwa naota!
Chanzo: Tanzania Daima Machi 24, 2010.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment