Thursday, 11 March 2010

Uchaguzi Oktoba: Chukua tahadhari

OKTOBA mwaka huu utafanyika uchaguzi mkuu. Huu ni msimu wa wanasiasa kuwa karibu na wananchi, hasa wapiga kura.

Ni wakati wa usawa kuonekana miongoni mwa makundi mawili yaliyokuwa yakiishi kama mbingu na ardhi kwa miaka mitano.

Hakika, huu ni wakati wa ahadi nono na nyingi ambazo mwisho wake ni kilio kwa walioahidiwa na kicheko kwa walioahidi.

Katika msimu huu, kila mtu hujiona mjanja ingawa sivyo. Mpiga kura hujiona kama amepanda chati kiasi cha kupendwa na kuwa sawa na waheshimiwa.

Na waheshimiwa waliokuwa wakiishi mwezini hujishusha na kujumuika na wapiga kura ili wawalize na kutoweka.

Ukiachia mbali wapiga kura, lipo kundi la waandishi wa habari wanaotumikia matumbo yao. Hawa maadili yao yamo tumboni mwao. Akili zao pia zimo zaidi tumboni kuliko kichwani.

Kwao huu ni wakati mzuri wa kuwinda na kuvuna. Hujipeleka kwa wanasiasa hasa mafisadi wakiwa tayari kupata mradi wa kuzoa uchafu wao na kuwapamba kwa kila namna.

Hawa ni hatari kuliko hata wapigakura hasa wa mashambani ambao huangamizwa kwa ujinga wao.

Hapa ndipo waandishi wanakuwa hatari kwa maana ya kutumia taaluma ya ukombozi kufanya maangamizi.

Kwani nani amewasahau waandishi “wadandizi;” wale wanaoitwa waandamizi, walioajiriwa kuisafisha Richmond ukiachilia mbali kutumiwa na mgombea fulani mwenye kutia kila aina ya shaka kuukwaa ulaji?

Hyo ilikuwa mwaka 2005, na baada ya hapo baadhi yao wamezawadiwa vyeo uchwara kama shukrani kwa kuuza utu na taaluma yao.

Kuna kundi jingine la wanasiasa nyemelezi wanaosifika kwa kuhamahama vyama. Hawa wana njaa kuliko hata moto uunguzao kila kijacho mbele yake.

Wako tayari kulamba matapishi yao hata kwa kuahidiwa peremende; yaani vyeo vidogo kama “kufinyangiwa” ofisi kwenye chama tawala.

Kitengo kilichogeuka dampo la wahamaji hawa ni ofisi za propaganda ukiachilia mbali uenezi wilayani.

Wapo wengi waliokuwa na sifa ya kuwa “samba” kwenye upinzani. Waliondoka upinzani kwa mbwembwe na kuishia kuwa “tairi za spea” za chama tawala.

Katika hali hii, mhusika hujikuta hawezi kwenda mbele wala nyuma, bali kujigeuza mtumwa wa tumbo lake lisilo na shukrani.

Hali huzidi kuwa mbaya hasa pale vyama vinapokuwa na “wenyewe” kama wasemavyo katika baadhi ya vyama. Katika hali hii, nyemelezi hujikuta kama mtalaka atafutaye chuo kingine asijue kila aendapo hutiliwa shaka.

Swali kubwa linalokabili wahamaji ni kwanini waliachika kwenye ndoa zao za kwanza.

Kwa vile wahusika hawana manufaa kwa kambi wajiungazo nazo, isipokuwa kutaka kuzitumia kwa maslahi yao binafsi, huwa tayari kubeba kila aina ya unguliko na sononeko; wakijitahidi kuwaridhisha mabwana zao wapya bila mafanikio.

Huishia kuwa vihongwe wawezao kubebeshwa kila upuuzi alimradi mkono uende kinywani.

Kuna wafanyabiashara wenye pesa chafu na utajiri utokanao na jinai. Hawa huwadhamini wagombea fisadi ili kuwatumia kufanikisha tenda nono na mikataba ya aibu.

Kupitia urafiki huu wa mashaka, nchi huuzwa na watu wake. Madini na raslimali nyingine hushindwa kuukwamua umma kutoka kwenye bahari ya umaskini wa kunuka.

Maskini hawa huingia ndoa ya mauti kwa taifa; nao kama makundi tajwa hapo juu, hutumia tumbo kufikiri badala ya ubongo.

Wafanyabishara wachafu siyo kwamba wanawadhamini wanasiasa wachafu tu, bali pia nao siku hizi wanaingia kugombea uongozi ili waweze kuutumia kujitajirisha na kuwakamua wafanyabiashara wenzao kwa kufanikisha mipango yao.

Hawa ni hatari kuliko hata wale wa mwanzo ambao huhitaji mtu wa kuwafanyia mipango na shughuli zao serikalini.

Tumekuwa tukiwalaumu sana wanasiasa, lakini kuna ukweli ambao lazima tuukubali. Jamii mbovu huchagua viongozi wabovu kama kielelezo cha ubovu na uoza wake.

Huwezi kudai na kupewa takrima ukala halafu akupaye ukampa kura yako ukategemea akuletee maendeleo.

Kwa mafisadi hawa, majimbo yao si wapiga kura, bali matumbo yao. Hata taifa lao si wananchi, bali matumbo yao. Na hii ndiyo siri ya nchi kuzidi kutopea kwenye ufisadi huku umma ukigeuka watazamaji japo, kimsingi ndio unaoathirika kuliko watawala.

Je, umma unakaa kimya kutokana na kujua udhaifu wake wa kuendekeza takrima badala ya maslahi au kwa vile haujui la kufanya?

Je, umma uambiwe mara ngapi ili ujifunze? Kwa vile msimu wa kuongopewa na kuahidiwa kila aina ya vinono na pepo umetimia, kama jamii, hatuna budi kuzidi kutahadhalishana ili hapo baadaye tusiendelee kutumiwa na kudhulumiwa.

Tutakuwa jamii kipofu wa ajabu kuendelea kurudia makosa kila msimu wa uchaguzi.

Leo tuna watu wanaojulikana, wameghushi vyeti vyao vya taaluma na hawataki kuachia ofisi kwa vile mamlaka zilizowateua zimeamua kukaa kimya.

Kama wapiga kura tuna kila sababu na uwezo wa kutowapa kura wagombea wa aina hiyo, kwani tumejua hawafai.

Kuna ndoa fifi kati ya wanasiasa na baadhi ya waandishi wa habari. Waandishi watovu wa maadili hujikuta wakiwinda na kuwindwa na wanasiasa wachovu na wachafu ambao wanatafuta watu wa kuwapamba na kusafisha uchafu wao ili umma uwakubali ilhali hawafai kabisa.

Vyombo vya habari vya msimu huzuka na kufa baada ya uchaguzi. Vingi hujikuta vikigeuzwa nyumba ndogo za wanasiasa mafisadi kwa kuvinunua na kuvimiliki bila vyenyewe kujua.

Uongo na lugha chafu husikika na kusomwa kila uchao kwenye vyombo vya habari. Mtasikia na kushuhudia mengi. Muhimu ni kwa wapiga kura na wananchi kwa ujumla kutokubali kuburuzwa kwenye mtego huu hatari.

Maana kufanya hivyo ni furaha ya msimu ambayo mwisho wake ni kilio cha milele. Kipindi hiki ni hatari kwa jamii na taifa kwani huja na lugha tamu na ahadi lukuki ambazo hawawezi kutekeleza hata moja.

Wengi wanajiuliza: Hivi inakuwaje mtu mzima hukosa kumbukumbu kiasi cha kubariki na kupogolea mauti yake na jamii yake?

Kitu kimoja ni dhahiri; kwa kutoangalia nyuma na kutia kumbukumbu, tunaweka rehani vizazi vijavyo. Kwa kuendeleza upuuzi huu, kuna siku wajukuu zetu watayachapa bakora makaburi yetu na kuyafukua kuchunguza uwezo wetu kifikra.

Haya shime wananchi tahadharini wanasiasa uchwara na nyemelezi wanaodandia vyama kama nyani kwenye matawi ya miti.

Tahadharini. Wakati wa kudanganywa na kuibiwa unakaribia na kila kitu kiko wazi. Nyasi zimetandazwa ugani. Farasi atashindwaje kufungiana nyama na nyangwa?
Chanzo: MwanaHALISI Machi, 2010.

No comments: