Friday, 19 March 2010

Msimchezee God kwa njaa zenu

Hivi karibuni kwenye mgogoro wa kupitisha nishati maeneo ya Nonihino nilijikuta hoi bin taaban baada ya tapeli mmoja aitwaye Ka-Tortoise kusema: ataamuru umeme usiwake! Nani ametumerogwa hadi kuvumilia wezi na wachumia tumbo hawa? Baya zaidi, tumeamini na kusajili utapeli huu!

Mpiga debe mpya wa nambari wani Gus Lyatongolwa anajua ninachomaanisha. Alitapeliwa na tapeli huyu na kuaminishwa: angeukwaa ukuu asijue atausikia bombani.

Kama sikosei, hawa ndiyo wanaowahadaa wapumbavu na majuha wetu kuwa viungo vya mazeruzure ni dili la ukwasi wakati ukwasi unategemea juhudi au ufisadi wako kutegemea wewe ni nani na uko wapi.

Kama wewe ni mwandishi wa habari kanjanja na changu, huna haja ya kutapeliwa. Watapeli wanasiasa wachafu wakutumie kufanya kazi zao chafu mwisho wa yote mtumiane na kuiangamiza jamii kwa uroho na ujuha wenu. Huwaoni waliohongwa vyeo tena kwenye jumba jeupe baada ya kufua nepi za jamaa yangu?

Nilitabiri: Lyatongolwa angejirejesha nonihino baada ya kubanwa mbavu nikaonekana mchochezi! Muulize sasa. Yuko wapi? Kama anatoka Moshie kwenda Bongo (Sisiemu), basi ameshafika Ubungo Kimara akamalizwe kabisa.

Pia nilitabiri: Silva Rweyependekeza angegeuka zigo kwa Chekacheka. Mlidhani wivu wa kike. Yuko wapi zaidi ya kugeuka nakama na kupayuka hovyo hovyo kama chizi?

Nilitabiri kuwa ujambazi wa Richmonduli utabarikiwa na wale ambao huwezi kuwadhani na ule wa HEPA utaepwa na mambo yawe shwari huku wakuu wa kaya wakiiba sana kiasi cha kutumia kuliko kipato, nilionekana chizi na mvuta bangi. Naaambieeee yako wapi? Wezi, mafisadi na manyang’au wamesafishana ingawa hawatatakata milele huku walevi wakibakia kutoa mimacho kama bundi! Shauri yenu mtaendelewa kuliwa hadi mkome. Mie mwenzenu simo nitapambana nao kieleweke.

Nilitabiri kuwa kile mlichoaminishwa kuwa lilikuwa chaguo la God kingegeuka kuwa chaguo la mafisadi huku likiwageuza walevi shamba la bibi wasijue la kufanya. Nilitabiri mambo mengi sana tu.

Katika utabiri wote nilivumilia sikupayuka tena. Hili la kumchokoza bwana God wangu kuwa atatumika kishirikina kuzuia umeme usiwake sinalo subira wala kutaka radhi. Nalaani utovu huu wa nidhamu kwa aliyenifinyanga na kunijalia kupayuka nikaeleweka na kuogopewa. Kwanini wale jamaa zangu wasimkalie itikafu akaipata au nao ni yale yale danganya toto?

Bwana mkubwa Imma wa Maria na Yosefu aliwahi kusema: Watakuja wengi kwa jina langu na watapotosha wengi. Kwani si wote wasemao Bwana Bwana watauona ufalme wa mbinguni. Tahadhalini wengi ni mbweha na mbwa mwitu watawararua mkome kama mnavyoraruriwa na njaa kaya.

Je tukiangalia wasanii kibao waliojitosa kwenye majoho sawa na wanasiasa tunajifunza nini? Je si kuishiwa kwa namna yake hadi kufikia kuahidi miujiza isiyowezekana? Mungu hawezi kuzuia umeme kuwaka. Maana yeye ni wa mwanga wala si wa giza kama hawa watu wa giza wanavyotaka tuamini na kuelewa kuwa wanaweza kufanya miujiza wakati miujiza yao ni usanii na ujambazi mbuzi tu.

Jamani, k ama mna nguvu kiasi hiki kwanini mnaishi kwa kuwaibia walevi kwa kuwatoza mshiko wa jina la God kila uchao? Kwanini hamzitumii hizo nguvu kuondoa umaskini, magonjwa na ujinga mnaoutumia kuwaibia?

Juzi Ngelanija alipotangaza kuwa mradi wa kutupatia umeme sisi walevi wa maeneo ya Mwenge na vitongoji wake utaendelea nilifarijika na kufurahi. Maana nilishamlima barua yeye na bosi wake waache kuendekeza upuuzi mdogo mdogo kwenye masuala ya umma. Kwa jinsi barua ilivyokuwa noma hawakujibu. Sasa nawapongeza kwa kutekeleza maagizo yangu kuwa katika shughuli za umma tuepuke wafanya biashara tena wachuuzi wa roho za makapuku kama Ka- Tortoise, Rwakata.. malizia mwenyewe, Gaman... malizia pia na wengine wengi waliovamia jiwe kama magabacholi na mafisadi wengine.

Hakuna kitu kinauma kama tapeli wa kawaida kujivisha usemaji wa Bwana God wakati ni mchumia tumbo na mwizi wa mishiko ya matoleo tu. Hili sukusi limenikumbusha, audhubillahi mina shaitwan rajiim, shehena mmoja aitwaye Yaya bingwa wa kuwatabilia mauti wenzake wakati naye ni mfu mtarajiwa kutokana na afya yake kuwa migogoro hadi kufadhiliwa kwenda Uhindini kujiganga.

Mie napenda matapeli wanaosema wazi wazi kuwa ni matapeli na siyo watu wa majoho na wanapolitiki uchwara waliotamalaki kaya hii. Hamumuoni mzee Lyatongolwa anavyohanikiza kutangaza mapenzi yake mapya kwa Njaa Kaya? Jamaa hafichi uchovu wake ingawa amesema yeye ni mkwasi kuliko jamaa yangu wa Kupinda pinda kwenye Mizengwe.

Kwanini Ka-Tortoise asifanye kama Lyantogolwa ambaye ukapa umemfanya arambe matapishi yake mchana kweupe kwa kutangaza wazi wazi kuwa ataipigia kampeni nambari nonihino? Kumbe waliosema kuwa jamaa ni pandikizi na hakurejesha kadi ya kigwena cha Idodomya hawakukosea! Kuna haja ya kujiuliza. Tunawauza ndugu zetu kwa vipande thelathini vya fedha kwa faida ya nani?

Hakuna kilichonishangaza kama Lyatongolwa kumvaa Sammy Sixx akisema kuwa ni mchochezi wakati naye ni nyemelezi. Hapa kuna haja ya kutia akilini. Hawa wote wawili ni wasanii na wanajuana kama wacheza karata tatu. Ukiwafuata umeliwa unajiona ingawa huko nyuma walikuaminisha kuwa wanaweza kukuokoa wakati ni mbwa mwitu wa kawaida na simba marara.

Hakuna kitu kinasikitisha kama baba zima kujigeuza changu kwa sababu ya kujaza tumbo lisiloshiba wala kushukuru. Hamkumsikia mheshimika mmoja akimwaga shikamoo kwa sana kwa watoto wa shule? Hivi huyu hawezi kutongoza vitoto vyetu? Maana hajui tofauti ya mkubwa wala mdogo. Acheni kutuzengua na upuuzi wenu. Sasa tazama tumepoteza muda tukilumbana na wachovu kiasi cha kutucheleweshea nishati kwa walalakizani wetu.

Yote haya ni kutokana na kuwa na lisirikali lisilo na maana wala udhu linaloogopa kila fisadi na tapeli kutokana na uchafu wake. Kimsingi, hapakuwa na sababu ya kukaa meza moja na Ka-Tortoise kumpa nafasi ya kutafuta umaarufu uchwara.

Hata hivyo tushishangae hili. Hamuoni lisirikali linavyoendelea kuwaendekeza akina Ewassa na Roast Tamu kwa kuendekeza suluhu uchwara wakati kinachopaswa kufanyika ni kuwapeleka majambawazi hawa lupango mara moja?

Jamaa aliniacha hoi aliposema eti kaya itawaka moto ambao hakuna atakayeuzima kabla ya kunywea na kuja na ngonjera za miujiza. Unataka uwake moto gani zaidi ya huu unaotuunguza kiasi cha kuwa kaya ya wanuka njaa? Au ni kwa vile unashiba hizo sadaka za majuha uliowatwisha mkenge kuwa ungetatua matatizo yao wakati tatizo lau kubwa ni wewe na wengine kama wewe kwenye majoho na politiki?

Kabla sijasahau, mmesikia mpya ya jamaa zenu wa Richmonduli kutaka kutubamiza mkenge mwingine kwa kutuuzia nyenzo zao feki kwa kutumia jina jipya la Dowani? Hivi kaya hii imerogwa na nani mwe!

Tumalizie na ndoa iliyoshika kasi kati ya Karumekenge na bi mkubwa wa Madevu. Nimeamini Karumekenge na Madevu ni kiboko. Una habari Calf ndiyo imedidishwa huko nyika? Tuliwahabarisha kuwa kimsingi genge hili liliundwa kwa maslahi ya upwa hamkutuamini wala kuelewa somo. Kamuulize Profesa Haruna pale kunani zaidi ya kutoa macho.

Baada ya kufunga ndoa yao mpya ya mkeka kwa kulazimishwa na EU jamaa wameuchuna utadhani mambo ndiyo yamekwisha. Walevi wetu wa huko nao kwa ulimbuikeni wameuingia mkenge kichwa kichwa na kudhani matatizo yao ndiyo yamekwisha! Jamani mwaliwa ati.

Tumalizie na Ka-Tortoise. Umeme usipowaka nitakupa bi mkubwa wangu bure. Usipowaka jua wewe ni tapeli tu.

Ngoja niwahi zangu msurur u wa dala dala.
Chanzo: Tanzania Daima Machi 17, 2010.

No comments: