Thursday, 11 March 2010

Bangi nibangue nipambane na Njaa Kaya

BAADA ya kuja na waraka wa uchafuzi wa uchaguzi nimegundua kuwa bila kufanya utafiti siwezi kushinda kuondoa Njaa Kaya, hivyo nimeunda Taasisi ya Mpayukaji Syndicate Bureau of Research and Propaganda (MSBRP).

Kama kawaida, makao makuu ya asasi hii ni Kwa Mfuga Mbwa Bongo. Kazi adhimu na muhimu ya taasisi hii ni kuhakikisha nayafanyia utafiti mateso ya wanakaya na walevi wote ili niwaeleze wanayopaswa kufanya kujikomboa kutokana na Njaa Kaya.

Katika kufanikisha adhima hii ya ukombozi, nimegundua nyenzo mbili za kiakili, yaani ulabu na bangi. Maana bila kuutwika na kuvuta ndumu, kaya hii huishi na ukiishi ni kwa muda kabla ya BP hata Shell havijakudedisha kutokana na matatizo na kuchanganyikiwa ukiachia mbali njaa iliyoivamia kaya ambayo kwenye utafiti wangu nitaiita Njaa Kaya.

Kwanza nitoe tahadhari. Wale jamaa zangu wanaohongwa na wanaoniuzia mibangi yangu wasipoteze muda kuniwinda. Sina pesa ya kuwahonga ukiachia mbali mie kutaka nipelekwe lupango huenda nikala bure kuliko kuuawa na Njaa Kaya uraiani.

Isitoshe kazi hii ya ukombozi inalenga kuwakomboa hata wao waachane na maisha ya kutegemea rushwa na jinai nyingine zinazowadhalilisha ukiachia mbali kuhatarisha ajira na sifa zao.

Utafiti wangu umegundua kuwa takribani nusu ya wanakaya wamegeuka komba, yaani wanakula mlo mmoja kwa siku. Hii ni idadi kubwa kuliko hata ya wapiga kura za kula. Baya zaidi, wakati wanakaya wakiishi kama komba kwa mlo mmoja, kuna watu miongoni mwetu wanashiba, kusaza na kutapanya si pesa wala chakula! Ni ufisi na ufisadi kiasi gani?

Nimegundua kuwa bei ya kashata inapanda kutokana na kugeuzwa kitafunio huku kahawa na tangawizi vikigeuzwa chai kutokana na njaa mifukoni. Anayebishia hili aje kijiweni aone watu wanavyofungua kinywa kwa kahawa, tena ya kubomu.

Habari ndiyo hiyo. Ila kuna watu wetu, tena wakubwa wanaojiita wenzetu, wala hawashindii kahawa wala kashata bali mikuku, mirosti na makoro koro mengine ya bei mbaya na kutamanisha. Hawa wanaitwa watu wala au wala watu kwa lugha ya kijiweni kwetu.

Watu wala hawa hutumia pesa itokanayo na mapato ya kaya na kijiwe hata kwenda kutanua nje ya kaya, huku sisi tukiangamia kwa njaa kaya. Hakika hawana roho zaidi ya uroho miilini mwao.

Hata hivyo nao wana njaa ya mawazo. Vichwa vyao vimekonda kwa njaa ya maarifa na kujitambua bila kusahau kutambua hatari inayowakabili huko tuendako. Wangekuwa na tone hata la akili wangewezaje kuponda mabilioni ilhali wamezungukwa na bahari ya wanuka njaa?

Kutokana na uroho na upogo wa wenzetu hawa wasio wenzetu kitu, wamesababisha idadi ya walevi na wavuta ganja kuongezeka. Hamkusikia waliovuta sana bangi hadi wakatwambia kuwa tule majani ili wao watanue na ulevi wao madaraka na bangi za kujilisha upepo wasijue baadaye tutawatoa mapepo ya ushufaa kwa kuwafikisha kwa pilato?

Muulize rafiki yangu Pesa Tatu mwana wa Basie mtoto wa Meku na bosi wake Tunituni wa Makapu anayeishi kama bundi.

Kitu kimoja hakujua. Watu wakila majani kama mimi wanafyatuka akili kiasi cha kuweza hata kuwabonda watalii mawe wanapokwenda sehemu kufanya utalii na usanii! Mwanafyale upo mwana wakwa?

Bangi si mchezo ndugu zangu. Unawakumbuka jamaa zetu walioivuta wakajiona wao ni wanajeshi kiasi cha kujiita makamanda wakati ukweli ni makavimada wa nambari nonihino na mafisadi? Wameishia wapi zaidi ya kuula wa chuya na kuanza kuzomewa kama vyangu? Ndugu yangu Six wa Kiwembe upo?

Huwezi kupambana na Njaa Kaya kama una njaa kichwani. Heri yangu mwenye njaa tumboni kuliko kichwani. Ukiwa na njaa kichwani utawachuuza wenzio usijue nawe utachuuzwa.

Katika utafiti wangu nimeandika kitabu cha taarifa kiitwacho SAA YA UKOMBOZI ambapo swali kuu ni ukombozi unaowalenga wenye njaa matumboni na wenye njaa vichwani. Wenye njaa ya tumbo wamekondeana, lakini vichwa vyao vina afya. Kwani hawaachi kuuliza kulikoni.

Wenye njaa vichwani wao ni kama mafisi. Wanadhani mambo hayatabadilika. Wanajidanganya kwa kusuluhishana kinafiki wasijue dhuluma haina suluhu zaidi ya kumnyonga mwenye kudhulumu.

Katika kuvuta bangi na kuandika kitabu cha ukombozi, nimegundua kuwa kuna haja ya watu kuvuta sana bangi ili iwabangue wapambane na watesi wao bila msamaha wala huruma.

Njaa Kaya ni hatari. Maana wakati wenye njaa vichwani wakijiridhisha, wenye njaa tumboni wanazidi kuteswa na kudhalilishwa. Juzi juzi nusu bi mkubwa wangu aingie kishawishi pale mwenye duka alipomhusudu na kutaka kumhonga kibaba cha unga. Bahati mbaya alikataa.

Je, ni wangapi wanaanguka kwenye mtego huu wa Njaa Kaya? Kimsingi Njaa Kaya imetengenezwa na waroho wachache ili kuwaibia wapiga kura ya kula ambao huipiga ili wengine wale nao wakijiaminisha watakula wakati wataliwa na Njaa Kaya.

Wanaliwa kwa upuuzi kama kanga, gongo, vibandiko, muziki na hata ahadi hewa. Kwani mwenye njaa hana mwiko mara nyingi. Hana tofauti na kutu ambayo hula kila kitu ikipatacho. Njaa Kaya imetambaa kila mahali.

Si juu, si chini, si kwa wadogo wala wakubwa, si kwa viongozi wa dini wala nani. Njaa Kaya ni hatari usiambiwe. Heri hata ya miwaya maana kuna dawa za kuzuia magonjwa nyemelezi.

Ingawa wengi hawataki kukiri, kaya imejaa wavuta bangi, tena watu na heshima zao. Bila kuvuta bangi na kulewa unawezaje kula wewe, nyumba yako, marafiki zako, walamba viatu wako na hata nyumba ndogo huku wanakaya wakiteketea kwa njaa usihofu wala kumuogopa Mungu?

Bila kulewa unawezaje kukubali kugeuzwa kijiko ambacho huchota chakula kisile sawa na kupiga kula ya kura. Hebu kwa mfano jiulizeni. Ni kwanini walaji wa kaya wanatumia doshi nyingi kuliko kipato chake kama siyo uvutaji bangi na ulevi tena wenye madaraka miongoni mwa walevi?

Nimeamua kuongeza kuvuta bangi na kutangaza hadharani ili nikamatwe na kupelekwa lupango maana naambiwa wafungwa wanakula mara tatu kiasi cha wengine kuweza kusoma na kuondoka na madigrii. Ila mtakaotaka kuniigiza ‘think twice’. Maana ukiswekwa lupango shosto wako kama hana roho ngumu ndiyo usahau. Atahongwa ili kukimbia Njaa Kaya na mwisho wa yote muishie kuikwaa miwaya. Pia Lupango kuna kale ka mchezo ka kugeuzana. Kama wewe si kidume kama mimi ujue hilo.

Pia bangi zangu zinanituma kusema kuwa Njaa Kaya inasaidiwa na uroho, woga na upofu. Hebu vuta kidogo halafu ikubangue uone utakavyowachenjia wanaokula. Ukivuta huwezi kufungwa kamba za kupelekwa peponi wakati ni wa motoni.

Lazima uwe na mapepo kuahidi na kuahidiwa pepo wakati mwisho wa yote unakumbana na Njaa Kaya. Bahati mbaya hata wa kuyapunga hayo mapepo hayupo kutokana na shetani kuvamia nyumba za Godi. Tuliowategemea wamegeuzwa mbwa na walamba viatu kutokana na Njaa Kaya.

Jiulize. Wale waliolipiwa matibabu ughaibuni wameishi wapi zaidi ya kuliwa na Njaa Kaya?

Pia katika utafiti wangu wa kibangi bangi nimegundua kuwa ujambazi uwe wa bunduki au peni utaongezeka kipindi hiki. Utashindwaje kuongezeka iwapo kila mtu ni jambazi kwa nafasi na namna yake?

Msijesema nawatukana wateule kusema kila mtu ni jambazi. Ujambazi ni ile hali ya kuiba au kupora haki au mali ya mwingine finishi. Je, hili halifanyiki hadharani, tena likiungwa mkono na kupendwa? Nani anaongelea ujambazi wa HEPA au Kagodoka ukiachia mbali ule wa Richimondu uliohalalishwa hivi karibuni?

Kilichonichekesha ni kumsikia Six akitapatapa kuwa ataendelea kupambana na ujambazi wakati yuko kitanda kimoja na majambawazi! Ni jibwa gani kibogoyo linaweza kumng’ata mtu? Kweli Njaa Kaya hatari!

Katika utafiti wangu nimeibuka na mikakati madhubuti ya kukomesha Njaa Kaya. Nimegundua kuwa nikifanya yafuatayo nitashinda na kuwakomboa walevi:

Mosi, nitavuta bangi na kunywa sana ili nipate ithibati ya kuandika na kuyatangaza haya ninayoandika.

Pili, nitapayuka kama sina akili nzuri hadi kieleweke. Sitakuwa kama akina Six. Nina ithibati na mapenzi ya kweli kwa kaya yangu.

Tatu, nitaanza kuwawinda wanaoshiba matumboni na kufa kwa njaa ya ubongo ili ama ziwe zangu ama zao. Hapa ndipo kitabu cha SAA YA UKOMBOZI kilipojichimbia.

Nne, kuwahamasisha walevi kutowaamini walioshiba. Maana mwenye njaa amjua mwenye shibe ingawa mwenye shibe hamjui mwenye njaa. Kwa vile wote wana njaa japo hawajui, nitaendelea kuwajulisha bila kuchoka.

Tano, nitawaumbua warongo na waimbaji wa ngojera na sanaa nyingine.

Sita, kuwasaka na kuwazomea wenye vitambi na tabasamu wakisikia urongo na kejeli za ukombozi wakati wao ndio kikwazo kikuu. Lazima waeleze siri ya mafanikio yao ambayo ni maangamizi yetu tunaoteswa na Njaa Kaya.

Naona ndata wanakuja. Acha nikitoe kabla hawajanitia mikononi. Saa ya ukombozi ni sasa. Bangi nibangue nipambane na Njaa Kaya.
Chanzo:Tanzania Daima Machi,10,2010.

No comments: