How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do
Wednesday, 21 July 2010
CHADEMA kuweni makini na akina Sabodo
Wagiriki husema: "Timeo dona ferentis" au “Timeo Danaos et dona ferentes. “waogope wale (wagiriki) hata waje na zawadi.” Kitendo kilichotangazwa na vyombo vya habari, kwa sana, hivi karibuni baada ya mwana CCM Jaffar Sabodo kuipa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) msaada wa shilingi 100,000,000 huku akiwa ni mfadhili na mkereketwa wa CCM, kilinikumbusha wosia huu wa kigiriki.
Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman alikaririwa akimshukuru mfadhili huyu mpya. Kusaidia au kusaidiwa si jambo baya kama anayefanya hivyo ana udhu na anafanya hivyo kwa nia nzuri. Alisema: “Kwa kweli tunashukuru sana hii ni historia mpya katika siasa za vyama vingi nchini, ni wajibu wa wafanyabiashara wakubwa kuona umuhimu wa kusaidia vyama vyote makini nchini bila ubaguzi wala woga, mzee umeonyesha njia naamini itakuwa ni mfano kwa wengine wenye uwezo.”
Ndege kaunasa mtego hapa. Huwezi ukawatumikia mabwana wawili. Wazungu husema either you be grass eater or meat eater in this game.
Kilichonisukuma kujenga shaka juu ya msaada huu ni ukweli kuwa sikusikia sehemu yoyote CHADEMA wakiulizia usafi wa mtoaji ukiachia mbali historia yake kujulikana vilivyo hasa alipowashambuliwa wazee maarufu wa CCM baada ya kumkosoa rais Jakaya Kikwete kuwa hachukui maamuzi magumu. Hii ni baada ya kumuona yuko kitanda kimoja na mafisadi.
Hivyo basi, kwa moyo huu wa mwenyekiti kushukuru na kupokea bila kuuliza, sitashangaa kusikia akina Kagoda nao wakichangia kiasi cha upinzani wa Tanzania kugeuka kama ule wa Kenya kutokana na tamaa ya kuchuma.
Kuepuka kujidhalilisha na kudhalilishwa kwa viongozi na vyama vyao, kuna haja ya serikali kugharimia uendeshaji wa vyama husika. Mbona tuna pesa ya kusamehe kodi ukiachia mbali kuwaacha mafisadi na matapeli waliojificha nyuma ya wakubwa kutoweka na pesa yetu? Mbona tuna pesa ya kuchezea kwenye ziara nje tena zisizo na ulazimu wala tija?
Kwanini watu binafsi, tena wanaobebwa na serikali kupata hizo pesa zao chafu, waweze kuvisaidia vyama na serikali isiviendeshe kifedha kwa mujibu wa sheria?
Tuwakumbushe CHADEMA. Sabodo huyu aliacha kizaazaa alipoishutumu taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF) kuwa ilifanyia ubadhilifu pesa aliyoipa kama msaada. Baadaye ilikuja kugundulika vinginevyo na mhusika wala hakukanusha zaidi ya kuficha uso wake na kutokea CHADEMA sasa. Je CHADEMA wamejihakikishia vipi kuwa hatawafanyia mchezo huu kutokana na kuwa karibu sana na uongozi wa sasa ambao CHADEMA pekee kwenye upinzani imeujeruhi sana kwa kufichua uchafu wake mwingi kuanzia EPA, Richmond, Deep Green Finance na mwingine mwingi?
Is CHADEMA going to hell in a handbasket? Smahani kuchanganya kiingereza na kiswahili. Najaribu kufikisha ujumbe na onyo langu.
Kwa wanaojua wafanyabiashara wengi walivyo tegemezi na wafadhili kwa CCM, atashangaa hii jeuri ya Sabodo inatoka wapi bila baraka za chama chake!
Maana si siri. Kama alivyowahi kupayuka (kutokana na kujisahau) waziri mkuu wa zamani Fredrick Sumaye kuwa bila kujiunga na CCM, hakuna mfanyabiashara au mtu yeyote angeweza kufanya mambo yake yanyoke. Tumeona wengi waliokuwa wamekaribia kufa kiuchumi kama Thomas Ngawaiya, Augustine Mrema, Masumbuko Lamwai, Warid Kaboro, Tambwe Hiza wakijirejesha huko ili wanusurike ukapa.
Swali analopaswa kujiuliza kila mwenye nazo na mapenzi na CHADEMA, ni kwanini CCM inaweza kumuacha Sabodo awaunge wapinzani wake mkono wakati wao wakiwapatiliza kama hakuna namna?
Kwa faida zaidi, wanaodhani huu ni wasi wasi tu wajiulize ni kwanini mfanyabiashara tena mwenye udhu Bakhresa alipokisaidia chama cha wananachi (CUF), CCM na serikali yake walianza kumhujumu kiasi cha kutaka kuangusha biashara zake? Kama hakuna namna Sabado ni nini ukilinganisha na Said Bakhresa?
Kwa anayejua jinsi mtandao wa wafanyabiashara hasa wale wafananao na Sabodo walivyo watatanishi, atahoji na kutia shaka kama mimi.
Kama Sabodo aliweza kuwageuka watu makini na jasiri kama MNF ikiongozwa na majabali kama Joseph Bukuku na watu safi kama Salim Ahmed Salim ukiachia mbali kuwaingiza kwenye utata lulu kama Joseph Warioba, CHADEMA ni nini? Kuweni makini na ikiwezekana pesa zake arudishiwe.
Kimsingi mtu kama Sabodo si saizi ya CHADEMA bali waganga njaa kama wale mnaowaona wakijigonga na kujigeuza nyumba ndogo ya Kikwete na CCM yake kama mlivyoshuhudia huko Dodoma hivi karibuni ambapo mmoja alijivua nguo si kawaida.
Kuona hatari inayoweza kuikabili CHADEMA, hata ukiangalia staili iliyotumika kukabidhiwa hivyo vipande thelathini vya fedha ni ya kudhalilisha ukiachia mbali kuashiria mengi kwa wenye akili. Kwanini Sabodo awaite nyumbani kwake viongozi wa chama kana kwamba anawapa zawadi binafsi badala ya kukutana nao ofisini kwao hata hotelini?
Hakuna ubishi. CHADEMA si mwiba tu bali mkuki hata mshale kwa CCM. Hivyo lazima ishughulikiwe na wa kufanya hivvyo si wengine bali makada wake kama Sabodo. Kweli penye udhia penyeza rupia. Walisema wahenga.
Hata ukiangalia maneno ya kumshukuru ya kinara wa mapambano dhidi ya ufisadi toka upinzani,Dk Willbroad Slaa unagundua anavyoanza kulainishwa. Alikaririwa akisema : “Natoa mwito kwa vyombo vya dola, kuacha kuwatisha Watanzania wenye mapenzi mema wanaochangia vyama mbadala kama CHADEMA kwani kufanya hivyo ni kuhujumu taifa na kukwamisha maendeleo ya nchi.”
Angekuwa hajawa-cornered even induced, Slaa bila shaka angechomeka neno walio na fedha safi siyo itokanayo na ufisadi au wenye kutia shaka.
Je alisahau au naye ameanza kuishiwa kama tuliowaona Dododma?
Kwa leo sisemi mengi. CHADEMA imefungua ukurasa mpya wa ushirikiano ambao bila shaka kwangu ni ule wa dubu na kudu.
Nimalize na maneno ya Shakespear. “Alas, poor Yorick! I knew him, Horatio.”
Chanzo: Gazeti la Dira la 18 Julai 2010.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment