Wednesday, 7 July 2010

Safari hii sitaki mavuvuzela kijiweni


KWANZA niseme wazi tena mapema na kwa msisitizo. Mwaka huu umekuwa mbaya sana kwangu.

Walatini huita Annus Horribilis. Licha ya mama watoto kunusurika kwenye ajali kule kwa kina ‘Mura’ mie mwenyewe nimenusurika mara nyingi tu.

Pia sikutimiza ahadi hata moja nilizowapa walevi waliponichagua kitsunami zama zile ili kuongoza kijiwe chao ambacho kimegeuka mali yangu binafsi. Mwenzenu naona aibu ingawa najikaza kisabuni.

Kinachosaidia ni kwamba kwenye mchezo wa sanaa msanii hapaswi kuona aibu vinginevyo ningeishaumbuka zamani gani!

Mambo yangu ni tofauti na mkuu wa kaya ya Tanzia kule karibu na Danganyika ambaye alivurunda lakini bado akajisifu kuwa hakuvurunda ndiyo maana genge lake la ulaji la kiama limempa nafasi nyingine ya ulaji wa bure.


Nilikuwapo pale mitaa ya Dom wakati akijigamba alipokuwa akitangaza azma ya kuula tena ingawa picha halisi ni sawa na yangu. Nilimuona akiitangaza familia yake.

Hatua hii ilitusaidia wengine kujua wanafamilia wake ambao walikuwa hawajulikani kutokana na kutoka kwenye nyumba ndogo zake. Nina mpango wa kumshitaki kwa kuiba sera yangu ya ufamilisho, ujikoisho na udugusisho.

Ukitaka kujua nimaanishacho angalia kazi wanayofanya kwa sasa akina Rizi na Mira ambaye wengi hammjui kutokana na utata wa familia yenyewe na nyumba ntobhu.

Hakuna kilichofanya mwaka huu niuone nuksi kama tishio la baadhi ya wazee wa kijiwe kunitaka nisigombee tena ulaji kwenye kijiwe kutokana na kuvurunda na kuonyesha uchanga badala ya ukomavu, ukiachia mbali kuzungukwa na kashfa kibao za kupunyua njuluku za kijiwe.

Nani kasahau nasaha uchwara za kina mzee Kidevu almaaruf Warihaba, Mchunguliaji almaaruf Kareshi Mati na wengine wengi? Si walisema sifai hata kuwa mjumbe wa nyumba kumi achia mbali rais wa kijiwe!

Najua njaa ndiyo ilisababisha mashambulizi yote haya. Maana tangu nikitaifishe kijiwe mimi familia yangu na marafiki zangu, walevi wamekuwa maskini kiasi cha kushindikia kahawa na kashata.

Na hii imesababisha bei ya kashata na kahawa kupanda kiasi cha watu kutamani wazikwe hai. Wengi wananionea wivu ninavyotanua huku wao wakitanuliwa na njaa na ukapa. Mie nshawambia mara nyingi: raha jipeni wenyewe mie siwapi.

Hapa sijaongelea jamaa zangu wa majoho walioanza kuniita mnafiki kwa vile sikutimiza ahadi yangu ya kuwapa uwanja wa kufanya mihadhara kwenye kijiwe.

Nakumbuka nilipowafunga kamba kuwa utawala wangu utawakomboa waende nchi ya maziwa na asali hawakujua nitawanyonya hadi wakonde na kukoma!

Walevi ni watu wa ajabu. Wanauziwa mbuzi kwenye gunia halafu kwa ujinga wao wanalalamika. Nilidhani kipindi hiki wangestuka waninyime kula ya kura. Ila kwa walivyo wepesi wa kusahau na wapenzi wa kuishi kwa matumaini, hata ngwe hii ya lala salama nitapeta.

Hakuna cha maziwa wala asali kuchanganywa kwenye kahawa wala mikate zaidi ya kashata kavu na lugha laini na wakati mwingine mipasho wanaponiudhi kuchokonoa ulaji wangu.

Baada ya kukaa na kutafakari, nimegundua mbinu mpya ya kuendelea na ulaji-nayo ni kuwakwepa wana mitandao yangu ya ulaji na kutumia wana familia yangu ingawa wapo washenzi wanaosema: mtandao ni mtandao hata uwe wa mke na watoto wako.

Hawajui nawapigia debe watoto na wake zangu hata nyumba ndogo ili hapo baadaye nao wagombee nafasi nyeti kijiweni. Hii ndiyo siri ya kumpa mwanangu mikoba kwenda vijiwe vyote kusaka wadhamini wangu mwaka huu. Mwaka huu situmii vuvuzela hata kidogo.

Kwanza walevi wameishawashtukia licha ya kuchoka na longo longo zao. Nikiangalia kiongozi wao mgosi Machungi Makambale alivyochafuliwa na kashfa ya mwanae na wizi wa kashata, sina hamu na vuvuzela hata kidogo.

Si unajua tena. Hawa jamaa zangu wa mitandao wananitumia wakidhani mie bwege. Ingawa wengi wanadhani tunatumiana, kimsingi wananitumia. Kwani kwa kutumia kisingizio cha kuiba pesa ya kijiwe kuwahonga walevi, nao huchota nyingi kuliko hata zile wanazohonga kiasi cha kuniachia mizigo ya kashfa.

Nani mara hii kasahau ile kashfa niliyoita EPA ya HEPA?

Bado kuna ile ya iliyomeremeta wakati mimi nikimetuka. Hapa sijataja kashfa kama MAWAWA ya Bi. Nkubwa ukiachia mbali ile ya kutumia mipesa kibao kutanua na kupaka nkorogo ikuu yangu ambayo wabaya wangu wanaiita pachafu pa pachafu palipokuwa patakatifu pa patakatifu enzi za mtume yule.

Hapa hujagusa matumizi mabaya ya watu wangu hasa wauzaji na wasimamizi wa kahawa. Bado hujagusa matumizi mengine mabovu ya nyumba zangu ndogo na washikaji wangu wengine ambao sitaki wajulikane.

Sitamtangaza mtu hata walamba viatu wangu. Nawatangaza mwanangu na mke wangu ambao nikishindwa ndio watakuwa waathirika wa kwanza na isitoshe baadaye watagombea ulaji.

Maana ujiko na ulaji wa dezo vitakuwa vimeyeyuka. Nimegundua hata hii pesa ya wizi tunayoiba na kina Roasttamu haiwezi kufua dafu bila kubadili mbinu.

Hapa hapendwi mtu bali njuluku. Kadhalika hafagiliwi mtu bali ndugu.

Ulaji hasa ukuu wa kijiwe si mchezo! Unaweza kuamini kuwa kila mwezi wazee wa ukoo wangu wanapokea wanafamilia wapya? Ulaji umeiunganisha familia yangu iliyokuwa haina mpangilio ingawa wengi wanasema kinachofuatwa hapa ni ulaji potelea mbali! wale vyangu niliopasua nao amri ya sita miaka ya sabini wananiletea wanaharamu kila uchao.

Hivyo usishangae kuona sura ngeni kila uchao kwenye safu ya wanafamilia wangu. Naomba Subhana: wale vyangudoa wa kizungu niliojivinjari nao nilipokuwa nje wasije nao wakaleta wanaharamu wa kichotara. Hata hivyo nani atauliza iwapo kila mtu ananizimia na kuniabudia ili nimmegee mabaki? Hayo tuyaache maana nyumba hutunza makubwa.

Pia nina wasi wasi na washikaji wangu kama Mzee Maneno almaaruf kama Sam Sixx ukiachia mbali Msomimkata tamaa almaaruf Mariko Mwanadosha.

Hata huyu Mpemba almaaruf Wakushaini nimeamua akitoe ili akagombee huko ili asinivurugie madili wala kuwa tishio hapa hasa mrithi wa ufalme huu wa kijiweni.

Dunia hii waja tuna dhambi we acha! Msiyeni Mulungu akale Mulungu walijisemea wanyasa.

Naona Riziki na kundi lake wanakuja kusaka wafadhili. Acha nikitoe nisije nikamnasa mtu makofi ndata wakanizoa bure.
Chanzo: Tanzania Daima Julai 7, 2010.

No comments: