How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Monday, 26 July 2010

Lowassa anataka kumdanganya nani?


Hivi karibuni watanzania walishuhudia mbinu mfu za kutaka kumrejesha aliyekuwa waziri mkuu aliyefurushwa na kashfa ya Richmond, Edward Lowassa zikianza kufanya kazi.

Tenda hii chafu ilikabidhiwa kwa Shirika la Habari Tanzania (TBC) chini ya mkuu wake Tido Mhando ambaye alimuandalia kipindi cha kujisifia na kujisafisha asifue dafu .

Pamoja na lengo zima kuwa kumjengea mazingira ya kumrejesha Lowassa kwenye hadhira kiasi cha baadaye kuzoeleka na kushiriki kwenye siasa za kitaifa, walioandaa mkakati huu na Lowassa mwenyewe walikurupuka.

Hata ukiangalia maneno ya Lowassa hayamjengi zaidi ya kumbomoa. Na kazi hiyo akiifanya mwenyewe kwa mbinu na kinywa chake.

Hebu tutoe nukuu hii halafu tuifanyie uchambuzi. “Mimi si mtu wa kukaa ofisini na kungoja nifungue mafaili. Linapokuja suala la kulishughulikia sihofii kufanya makosa ninapoamua ku-push (kulisukuma) jambo.”

Sasa kama Lowassa yuko tayari kufanya makosa ili kusukuma jambo ana jipya gani la kutufanyia zaidi ya kufanya makosa?

Maneno haya ni ushahidi tosha kuwa alipokuwa akisukuma watendaji watekeleze maslahi yake binafsi kwenye kashfa ya Richmond hakuogopa matokeo. Ndiyo maana ilikuwa rahisi kwake kubwaga manyanga baada ya shinikizo la kutaka aachie ngazi kutolewa.

Na kwa maneno haya Lowassa hana haja ya kuilaumu kamati teule ya Bunge iliyompata na hatia eti kwa kumnyima fursa ya kujitetea wakati walitoa taarifa kuwa kila mtuhumiwa anaweza kufika mbele ya kamati wakati wowote na Lowassa hakufanya hivyo kutokana na sababu alizojua mwenyewe. Ajilaumu mwenyewe na ku-push bila kuogopa consequences.

Kitu kingine hasa kilichonisukuma kuandika makala hii ni ile hali ya Lowassa kujigamba kuwa ana rekodi nzuri kikazi mahali pote alipofanya kazi jambo ambalo si kweli. Kama Lowassa angekuwa ni mkweli na ana rekodi nzuri mwaka 1995 baba wa taifa marehemu Mwl. Julius Nyerere asingemzuia kugombea urais.

Tumkumbushe chanzo cha ugomvi wake na mwalimu. Ugomvi wa wawili hawa ulianza pale Lowassa alipokodisha ndege kwenda kuchukua fomu za kugombea urais Dodoma akampa lifti mgombea mwingine wakati ule, Jakaya Kikwete kitendo ambacho kwa mwalimu kilikuwa na tafsiri mbili.

Mosi, kuthibitisha uvumi kuwa Lowassa amejilimbikizia mali nyingi ambayo haina, hajawahi na hayuko tayari kuitolea maelezo. Huu ni ushahidi fika wa ufisadi na kutokuwa muaminifu kama ilivyokuja kuthibitishwa na kashfa ya Richmond anayojitahidi kuikwepa na kuirahisisha.

Pili, jambo hili pia lilitafsiriwa na mwalimu kama utoto kwa Kikwete kujihusisha na mtu wa aina ya Lowassa. Ndiyo maana alisema kuwa Kikwete hakuwa amekomaa kuwa rais kama alivyokuja kuthibitisha hata baada ya kupita miaka kumi. Hapa ndipo urafiki wa Kikwete na Lowassa ulipochimbuka hasa kujulikana kwa umma. Ni urafiki huu huu wa mashaka kama mwalimu alivyoutilia shaka. Na bila kujibu tuhuma hizi Lowassa atamaliza waganga na dawa wala nafuu hatapata. Maana laana ya marehemu huwa si rahisi kuikwepa wala kuifutu hata ajidanganye na urafiki wake na Kikwete ambao umegeuka mzigo kwake, Kikwete na taifa.

Ni vizuri Lowassa akakubaliana na ukweli na hali halisi hata kama ni kidonge kichungu kuwa wakati huu ambapo ufisadi umegeuka sera kiasi cha kuzidi kuwaumiza na kuwachukiza watanzania walio wengi, maneno ya mwalimu yanazidi kupata ithibati kuliko hata wakati ule alipoyatamka akiwa hai.

Na isitoshe kwa kujiuzulu kwa hiari yake ni kukiri kuwa shutuma zilizokuwa zikimkabili zina ukweli. Ingekuwa mahakamani asingeruhusiwa kukata rufaa kama anavyofanya sasa.

Hata kuwa wa kwanza. Akitaka kujua ninachomaanisha, aangalie watu kama John Malecela aliowagomea kuwania urais walivyojaribu na kushindwa hata baada ya mwalimu kutoweka. Na Lowassa ataishia kama Malecela atake asitake. Na dawa ya hili ni kukubaliana na ukweli badala ya kujidanganya na kuudanganya umma.

Watanzania bado wanakumbuka athari za ufisadi wa Richmond ambapo waliwekwa kizani kwa mwaka mzima ili kushinikiza mitambo yake inunuliwe. Wanakumbuka bado jinsi umeme unavyozidi kuwa aghali kutokana na kulanguliwa ili kufidia hasara zitokanazo na uchafu kama Richmond.

Pia madai kuwa chochoko choko zote za kuifukua Richmond yalilenga kumpokonya uwaziri mkuu Lowassa ni uongo. Ingekuwa hivyo basi mawaziri wengine waliojiuzulu na wengine kupanguliwa wasingefanya hivyo maana aliyekuwa akitafutwa ni yeye. Hebu soma maneno yake:“Bado naamini tatizo lilikuwa ni uwaziri mkuu. Waziri Mkuu si mtu wa kusaini mkataba, ni mtu wa kusukuma...ile kamati (teule) ilikuwa na fedha nyingi, sijui ilitumia kiasi gani, kwani walisafiri hadi Marekani kuwahoji watu halafu hawakuja kabisa kunihoji...bado naamini kamati teule ilifanya makosa.”

Lowassa kimsingi anatapatapa. Kama anaamini na aliamini kuwa kamati ile ilifanya makosa basi asingeachia ngazi. Angeionyesha makosa na kutumia ukweli huo kuendelea kuwa madarakani. Anachofanya Lowassa licha ya kutokuwa saizi yake ni kulidhalilisha bunge, kamati yake na kulitukana taifa akitetea maslahi yake binafsi. Aambiwe ukweli kuwa muda wa kujadili kurejea kwake kwa mara ya pili ulikwishapita na hatafanikiwa hata afanyeje.

Na kuonyesha ukweli huu unaweza kurejea maneno ya Lowassa mwenyewe kuonyesha anavyojidanganya na kuwadanganya wengine. Alipoulizwa atafanya nini, alijibu “Nafsini mwangu I’m clean (sina kinyongo) mimi naiacha historia iwahukumu kwa haki.”

Lakini ukirejea maneno ya kuwa hakutendewa haki na tume ilikosea, Lowassa hana kinyongo tu bali hata ngoa na unywanywa. Na kwa kuzingatia haya ndiyo unaona jinsi Lowassa anavyotapatapa na kulipiza visasi. Hasemi yu safi kuhusiana na kashfa bali moyoni. Je uchafu wake wa Richmond mbona hakutaka kuuongelea?

Japo amejitahidi kuwashutumu waandishi wa habari na kuwaonyesha kama watu ambao hawana elimu ya kutosha, bado Lowassa huyu huyu anawatumia waandishi tena makanjanja kuwachafua wenzake hasa wale waliokuwa kwenye tume ya Mwakyembe au waliounga mkono hoja ya kuwajibishwa. Kuna magazeti yanajulikana na waandishi wake tena wasio na hata hicho cheti cha uandishi wa habari kama wale wa Tazama.

Dokezo la mwisho ni kwamba ukiondoa mwl. Nyerere, hakuna waziri mkuu aliyewahi kuwa rais. Hii ni kutokana na kupewa madaraka haya makubwa na kuonyesha utendaji wao kiasi cha kuwaachia wengine nao waongoze. Rejea harakati za kina Joseph Warioba, Cleopa Msuya, Salim Ahmed Salim, John Malecela na Fredrick Sumaye. Lowassa ni nani na ana nini ukiachia mbali kufanya nini zaidi ya kuliingiza taifa kwenye kiza na hasara? Anadhani tumesahau? Thubutu!

Pamoja na wanasiasa wetu kutuchukulia kama watoto hata mataahira, kuna mambo mengine hayawezekani. Haiwezekani kufufua maiti katika karne hii hata kama aliyekufa alikuwa rafiki wa Kaisari. Ni vigumu kwa Lowassa kurejea kwenye uongozi wa juu. Kama inawezekana basi na Liyumba anaweza kuteuliwa kuwa gavana wa benki kuu aliyoihujumu na kuiibia. Je inawezekana? Heri kuota usiku kuliko mchana. Tusipoteze muda kujadili jinsi ya kufufua maiti.
Chanzo: Dira ya Tanzania Julai 26, 2010

2 comments:

Anonymous said...

Mzee umenikuna. Huyu fisadi wa mafisadi anapaswa kuandamwa hadi akome na kukomaa. Harudi mtu hapa aambiwe huyu mmeru anayejiita mmasai. Wamasai hawawi hivi. Lowassa ni fisadi wa hatari ulimwenguni si Tanzania tu.
Big up kaka.

o'Wambura Ng'wanambiti! said...

Katika Tz kila kitu chawezekana!!!!

Hata vile ambavyo kwa akili ya kawaida unaona si sawa kwa Tz ni sawa tu :-(