Wednesday, 21 July 2010

Karibu soko la pamoja tuchanganyikiwe


RAFIKI zangu kule Karatu walikuwa wanauliza eti soko la pamoja la Afrika Mashariki limejengwa wapi?

Wambie ni kwenye vichwa vyao. Wakisema mbona hawalihisi, wambie watalihisi tu ni suala na muda tu. Wambie wasiwe na haraka neema zake wataziona ambapo watakuwa na watumishi karibu kila aina kutoka Kenya na Rwanda.

Usishangae na genocide na genocide philosophy vikawamo kwenye soko bila kusahau wembule toka kwa M7 ambaye atauza demokrasia ya mwituni na jinsi ya kutawala kifamilia akisaidia kuongeza soko hii ya Njaa kaya.

Poleni sana kwa kuchanganyikana na nyang'au na wanyonya damu. Mtanyolewa bila maji na mjute. Mie simo. Kwani si juha mie ati!

Bila shaka kwenye soko hili lazima bidhaa ya Philip Onyancha yule mnyonya damu maarufu wa dhehebu la waabudu shetani (Devil worshipper's cult) itakuwapo.

Akina dada poa au changu wa Bongo nao wajiandae kwa ushindani. Kutojua Kiingereza kutawatupa nje ya soko la pamoja. Mambo ya look my milk is standing hayana nafasi hapa tena.

Hapa sijagusia washitakiwa kuwa wabongo ikizingatiwa kuwa hivi karibuni walihusishwa kwenye jaribio la kumuua mkuu wa zamani wa majeshi ya Rwanda, Luteni Jenerali Nyamwasa Kayumba kule sauzi.

Hapa bado hujagusia mibomu, bunduki na mashine za kutungulia madege toka Somalia, bila kusahau wawekezaji toka huko ambao wengi watakuwa maharamia bila shaka.

Pale Rwanda wamejiandaa kutuletea ile bidhaa maarufu ya kufungia wanywanywa ukiachia mbali kuwafuata waliokimbilia nje na kuwamiminia risasi kabla ya Burundi kuja mgombea mmoja kwenye uchaguzi.

Tusishangae siku moja kuona ndege ya bwana mkubwa ikitupiwa mawe kama si makombora kutoka Somalia. Hamkuona AL-Shabaab walivyoingiza bidhaa zao Kampala kwenye kilele cha Kombe la Dunia?

Wale wezi wa benki sasa wanaweza kufanya biashara watakavyo, kwani bidhaa yao inahitajika kwenye soko jipya. Walimu feki na wengine hao ndiyo sisemi.

Academia na Internationals zetu zitajaa hadi zifurike huku ujinga ukizidi kufirika vichwani baada ya mifuko kupakuliwa na kubakia mitupu kwa kulipia upuuzi huu.

Kwa wale wabongo ambao biashara yao ya ngozi na mifupa ya zeruzeru ilikuwa imedoda jiandae kusafirisha nje hasa kwa wale wanyonya damu pale Nairoberry.

Unyakuzi wa ardhi nao ndiyo usiseme. Hamkuwaona akina Londi walivyohomola pale? Huu ni mwanzo tu. Ni biashara itakayolipa sana kiasi cha kufanya watu mabilionea ingawa watakuwa si wabongo.

Hapa hujagusia ile sumu hatari iitwayo njonjoison ambayo ilidodesha soko la kwanza lililokufa mwaka 1977.

Wabongo mmeambiwa na wakubwa wenu msikonde. Hili soko ni mali kwenu. Ni kweli. Msishangae kesho mkakalibisha katiba mpya ili kuchukua nafasi ya hii viraka mliyo nayo ukiachia mbali kuwa na serikali ya umoja wa kitaifa kama Kenya.

Najua mna ardhi mnayokalia bila kutumia. Japo wakubwa zenu wamewatahadharisha kutouza ardhi kwa wageni, mnaweza mkauza tu. Kwani kilichobaki nini iwapo nanyi mmeuzwa kwenye soko la pamoja?

Kwanza, mna bahati. Hamna ongezeko kubwa la watu wala watu wasio na ardhi kama jamaa zangu pale Murang’a na Kibuye bila kusahau kule Ngozi na Bugenyuzi.

Kinachokera ni ukweli kuwa wakati jamaa hawa wasio na ardhi wakimwagwa kwenu, ardhi yao imekaliwa na watu wala wachache na wageni!

Ndugu zangu kina Aterere, Omera na Mulembe pale Kenya mtegemee kununua bidhaa iitwayo EPA, Richmonduli hata Kagoda.

Bahati mbaya sana kwenu ni kwamba wenye jeuri ya kununua bidhaa hizi ni wala watu wenu muwaitao watawala!

Bila shaka hapa mtabadilishana na ile bidhaa maarufu iitwayo Kibaki Toka, yaani kujiapisha usiku baada ya kuiba sorry kuchukua kura za Jaduong Maduong Odinga mwana wa Amoro. Hamjasikia fununu kuwa Zenj imeishaanza maandalizi ya kutumia bidhaa hii kwa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa ulioanzishwa kwa shinikizo la The Hague kwa kina Ocampo? Maendeleo hayo na mema ya soko holela la pamoja.

Japo wabongo wamelazimishwa kuingia kwenye soko hili na kuachwa kwenye mataa, hawana haja ya kuchukia. Watafurahi tu watakaposhuhudia utitiri wa wasasi wa dili baada ya kuchoshwa na wale wa kihindi. Hapa mitandao ya dili itapanuka.

Msishangae kuwaona jamaa zangu wenye mamlaka wakiagiza Goldenberg toka Kenya huku waganda wakituuzia imla wao atawale soko hili.

Bongo mama mkarimu ana mengi ya kutoa. Jamaa zangu kule Kaspul Kabondo, Nyakach, Emuhaya, Ithekahuno, Wajir, Mutito, Matuu hadi Wote bila kusahau Cyangungu, Ruhengeri, Murindi, Rwimpasha hata Bugarama msikonde. Kuna bidhaa iitwayo mauaji ya vikongwe kwa imani za uchawi.

Hata wale jamaa zangu wa Bubanza, Bururi, Bwiza, Ngozi hata Apuk apar, Bunyaruguru, Soroti, Tororo, Lira na Mbale hamtaachwa nyuma.

Hapa bado hatujaongelea madini bwerere ya Bongo kama vile gold, tanzanite, almasi hata uranium kwa kina Kony kuwalipua wabaya wao, ukiachia mbali kutangazwa yanapatikana toka kwenye jamaa zangu wa unyakuzi wa kila kitu yaani man eat man and everything. Hapa bila shaka watapata ushindani mkali toka kwa jamaa zangu wa fisadi eat everything.

Dzipapa! Dzipapa! Lamkani kudzecha. Yaani papa papa amkeni kumekucha! Ndugu zangu wa kule Shika Adabu, udigoni na udurumani kwa ujumla tunaelewana nadhani.

Hakuna cha soko holela wala huria wala la hela kwenye kijiwe cha mzee Mpayukaji chaguo la Mungu na kipenzi cha walevi. Aaamin.

Mpayukaji (El Commandante)
Chanzo: Tanzania Daima Julai 21, 2010.

No comments: