How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Thursday, 29 July 2010

Ridhiwan Kikwete usikonde tuko nyuma yako




Bwana mdogo,
Naamini u mzima baada ya kuhangaika na kusaka wadhamini wa mzee nchi nzima.Haikuwa kazi nyepesi. Ni heshima na jukumu la pekee kwako na vijana wote wa taifa hili. Wote tuko nyuma yako na mzee.

Kudos kwa kufanya vitu vyako Yanga ambapo wabaya wetu wanasema umevurunda kwa kuweka mtu wako. Wanakuita kiji-rais kidogo simply because mzee ni rais. Wapuuzi hawa. Hawakujui siyo! Wamuulize Yusuf Masauni uliyemshuguhulikia baada ya kutishia ulaji wa mshikaji wetu Benno . Pia wanaweza kumuuliza Kifukwe uliyemnyima ulaji Yanga akaamua kususa na kundi lake ; kama urais wako ni wa kurahsisha hivyo.

Niliwahi kuwasiliana na mama yako wa kufikia kuhusiana na jinsi watu wanavyotusakama kwa kuwafagilieni. Leo nimeona ni bora kuwasiliana nawe wakati nikijiandaa kuwasiliana na mzee hapo baadaye.

Nimetumia njia hii tokana na kujua wazi kuwa ulipokuja kwetu Mbamba Bay kusaka wadhamini wa mzee sikupata nafasi ya kukuamkua na kukupa salama zangu za upendo wa dhati.

Niseme wazi. Mimi ni shabiki wako damu damu kiasi cha kuwa tayari kumwaga damu yangu kupambana na wale wanaokuonea wivu kwa ulaji unaoupata kutokana na kuzaliwa na kijiko cha dhahabu kwenye nasaba ya kifalme na mzee kukupigia vuvuzela ili hapo baadaye uule.

Kuna watu hawajipendi wala kulipenda taifa hili-wanaokusakama. Hawa ni maadui wa mshikamano na amani ambavyo mzee amevidumisha. Wanasema eti wewe na rafiki yako Januari Makamba ambaye pia ni msaidizi wa mzee mnabebwa. Hivi hawa watu wana akili kweli? Kuna ubaya gani wa mwana kubebwa na baba au mwana kumpigia ndogo ndogo mzee hata kuanza kujaribu kuvaa viatu vyake akiwa hai kama mnavyofanya?

Maadui hawa wa taifa wanakwenda mbali wanadai kuwa mama yako naye anatumia mgongo wa mzee kujineemesha! Hivi hawajui kutesa ni kwa zamu na, isitoshe, hakuna biashara inayoweza kufana bila kuwashirikisha wana familia? Wamesahau ahadi ya mzee ya maisha bora kwa wote yaani baba mama wana na maswahiba!

Eti kwa vile wewe ni mwanasheria, wangetaka uende kutoana jasho na mahakimu ukiwatetea wahalifu ilhali kuna ulaji wa dezo kwenye chama cha mzee! Hawa ni wapuuzi. Mwanangu usiwasikilize. Wakiendelea kukuzonga uwatolee uvivu na kuwapa: wawambie wazee wao wagombee urais waone utamu wake.

Mie sioni makosa yako wala ya mzee. Kwanini asifanye kama watangulizi wengine kama vile mzee Abeid Karume, Hassan Mwinyi, John Malecela, John Nchimbi, Yusuf Makamba na wengine ambao wamevitengenezea vitegemezi vyao ulaji wsa chee katika ngazi za juu?

Kwanini hawataki nawe uwe kama Daktari Hussein ambaye anatesa kutokana na mzee kumpa ulaji? Hawajui siku moja akiukwaa ukuu anaweza kukulipa fadhila kama ambavyo mzee alimlipa fadhila baba yake kwa kumtengeneza? Mzee kaona mbali.

Wasioona mbali wanataka awe kama wao. Mzee anajua: huko tuendako ulaji hautategemea uwezo wa mtu bali nasaba yake kama inavyoanza kujengeka. Huu ni mfumo mzuri tuliokopa toka kwa wahindi ambao wametutawala kiuchumi nchini. Bila hiyo wale watoto wa wakubwa waliotuhumiwa hata kughushi na kuanza kampeni mapema wangekuwa wameishachukuliwa hatua. Lakini ni nyani gani anaweza kumsulubu ngedere wakati wote wala mahindi?

Mfano, kuna kosa gani kwako kupewa kiwanja kwenye maeneo tulivu ya bahari kule Masaki au Mikocheni kama wengine? Kuna kosa gani, kwa mfano, kuwapa tafu washikaji zako kwa kumshauri mzee awape ulaji kama wanavyompakazia yule rafiki yako Lau wa Masha... wee koma, wa kampuni la IMMA.

Kabla sijasahau, naomba umpe salamu zangu Bro Miraji ambaye nilimuona juzi akiwa ametinga T-shirt yenye picha ya mzee iliyoandikwa 2010 ikimaanisha mwaka wa utukufu wa mzee, familia na maswahiba zake. Inapendeza sina mfano.

Kuna wajinga wanadhani kuwa wewe kupewa mikoba na mzee ni kutokana na kutoamini wana mitandao yake. Hawa wamenoa kweli kweli. Hawajui kuwa hata familia yaweza kuwa mtandao ukiachia mbali kupeana ujiko wa hapo baadaye! Wajinga kweli kweli.

Hawa hakika ni vipofu. Kwanini msomi aliyekubuhu kama wewe ujivunge ilhali huku mama ambaye elimu yake tuiache anatanua kwa kubuni mradi wa MAWAWA (Maulaji ya Wake za Wakubwa? Hawajui kuwa nawe una majukumu kwa ndugu na wazazi wako hasa bi mkubwa asiyeishi na dingi? Huu ndiyo wakati adhimu wa kuhomola na kutanua. Ukitaka kuona uzuri wa ushauri wangu, waulize watoto wa Che Nkapa hata bi mkubwa wake. Baada ya mzee kuachia ngazi hawasikiki wala kutanua kama walivyokuwa wakitanua wakati mzee akiwa high.

Japo watu wasiojua chess nzima wanamlaumu mzee kwa nepotism. Kwanza, hawajui kiingereza vizuri. Hawajui kuwa nepotism ni mfumo uliokubalika katika taifa letu kiasi cha kulikomboa kwa kuzalisha mashujaa wengi watokanao na damu takatifu. Bila nepotism Yesu kweli angekuja? Alikuja kwa sababu ya nepotism ya binadamu dhidi ya viumbe wengine. Hii tuiache ni falsafa kubwa iitwayo metaphilosophy.

Hata ule mradi wa mama yao wa Fursa kwa First Family and Friends (FFFF) hauna wachangiaji. Nani achangie watu wasio na mamlaka; ili apate nini? Wasio na busara wanaona kama ni upuuzi kwa mzee kuanza kukupa mikoba. Wanasahau kuwa kadri mambo yalivyo hasa kushukiana ufisadi atakapokuwa ameachia ngazi lazima awe na mtu wake jikoni kama alivyofanya mzee Ruxa.
Bila hiyo mizimu kama Loliondo hata IPTL yangemuandama hadi siku ya kufa. Huoni anavyoenziwa na kutanua kwa amani kana kwamba huko nyuma hakuacha waa?

Turejee kwa Mzee. Lazima adhaminiwe kuonyesha alivyo chaguo la Mungu na kipenzi cha watu. Anayebishia hili aangalia mabilioni aliyochangiwa hata na akina Matonya kutokana na kumzimia. Watakataa kumdhamini iwapo amekuza uchumi kiasi cha serikali kuwa tajiri kiasi cha kusamehe mabilioni ya EPA? Anayebishia hili aangalie misamaha ya kodi na pesa inayopotea kwenye ufisadi na serikali isishughulike nayo.

Nchi yetu sasa ni tajiri kiasi cha kushinda nchi zote za kiafrika kwa kununua na kugawa mashangingi. Rejea tukio la hivi karibuni huko Kilimanjaro ambapo afisa tawala wa mkoa huo Hilda Gondwe alijiuzia shangingi lenye thamani ya shilingi 155,000,000 kwa shilingi milioni sita tu. Kama si ishara ya utajiri wa serikali ni nini? Angalia serikali ilivyowagawia nyumba wakuu wake huku ikitenga mabilioni kujenga nyingine. Mifano ni mingi. Hebu jikumbushe jinsi urais wa Bongo ulivyo aghari. Unadhani urais wa 50,000,000,000 ni mchezo? Kama mtu mmoja anatumia kiasi hiki bila kugusia cha wabunge, huo umma una mafweza kiasi gani?

Angalia Dar Es Salaam ilivyopendeza kutokana na ile minara shufaa ya Balali na EPA na msongamano wa migari anayojisifia mzee hata kama inanyonga watu wetu hovyo. Uliza akina Kagoda wameishia wapi zaidi ya kuendelea kutesa na kupewa maulaji mengine.

Bwana mdogo, naona nisikuchoshe. Kaa ukiamini sisi vijana tunakuunga mkono na kukubali kuwa mrithi wa mzee hapo baadaye. Udumu mshikamano wa baba na mwana. Zidumu fikra za mzee kumtawaza mwana mapema. Walatini husema Noli prohicere maccaritas ad porcos yaani usitupe vito kwa nguruwe. Kadhalika nami naamini nimefanya kinyume.

Nifikishie salamu kwa mzee na hata bi mkubwa na swahiba yako Januari. Wambie tunaviona na kuvikubali vitu vyao hasa mafanikio ya MAWAWA na mradi wako wa wadhamini.

Salamu maalum kwa Januari. Mwambie kitabu chake juu ya ushambaa kimetushinda kutokana na kutumia lugha ngumu. Hivyo wapiga kura tuna shaka kama atatuelewa. Maana yeye ni wa wasomi na ikulu kusema ule ukweli.
Wako Kijana mwenzio akuungaye mikono na miguu,

Nkwazi Mhango pacha wa Mpayukaji Msemambovu , aka El Commandate
Mtandasi,
Mbamba Bay.
Chanzo: Tanzania Daima Julai 28, 2010.

1 comment:

Anonymous said...

Mpayukaji una akili kweli? Maana ulivyomuwashia moto huyu dogo kama anasoma hataacha kukuwaza kila aendapo. Big up kichaa wangu.