How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do
Wednesday, 25 August 2010
Uraia wetu unauzwa kama njugu
INGAWA mchakato wa kupata vitambulisho vya utaifa bado unaendelea, huku kukiwa na mawazo tofauti kwamba ni mradi mkubwa kwa wakubwa wachache waroho kujipatia mabilioni ya fedha, visipopatikana nchi itatawaliwa na wageni hata magaidi.
Hii ikichangiwa na uhamiaji kugeuka kuwa duka la kulangulia pasi za kusafiria na nyaraka nyingine muhimu, Huko tuendako hali itakuwa mbaya zaidi.
Nani hajui kuwa kuna 'Watanzania' wengi wa kughushi na kununua? Nenda ofisi ya vizazi na vifo uone watu wanavyonunua 'Utanzania' kama njugu. Kwani hili halijulikani? Jiulize. Wale wakimbizi wa kiuchumi wanaoingizwa kwa maelfu kutoka Asia huishia wapi zaidi ya kununua Utanzania na kuwa Watanzania safi? Nani anajali?
Katika eneo zima la Afrika Mashariki, ni uraia wa Tanzania unaoweza kununuliwa na si kununuliwa tu bali kwa bei ya kutupa. Ukimwambia Mkenya, hata awe mroho kiasi gani wa pesa kuwa unaweza kununua pasi ya Kenya, cheti cha kuzaliwa au uraia atakushangaa na kudhani unapaswa kupimwa akili.
Lakini ukija Tanzania, kuuza uraia sawa na haki nyingine ni kitu cha kawaida. Nimekuwa nikionya tabia ya umbwa na upanya unaoendeshwa na ufisi ufanywao na mafisadi wachache ama wenye madaraka au wasio na madaraka lakini makuwadi wa wenye madaraka. Sasa tazama. Tunaipeleka nchi kuzimu.
Matukio ya hivi karibuni yaliyowahusisha waliokuwa wakiwania kuteuliwa kugombea ubunge kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) huko Nzega hivi karibuni, yamefichua udhaifu wa mifumo na nchi yetu. Wagombea wawili wa ubunge Hussein Bashe na Hamis Andrea Kigwangala yanapaswa kutufungua macho.
Hebu fikiria. Mtu ambaye anasemekana si raia anapewa madaraka makubwa nchini bila mamlaka kujua. Tunaambiwa Bashe ni Msomali ingawa anakanusha. Anajaribu kujitetea. Analeta hati za uthibitisho wa uraia wake kwa nyaraka za mwaka jana! Kwa nini uraia wake uthibitishwe mwaka jana na si kabla ya kupewa nyadhifa kubwa sawa na zile alizovuliwa kwenye umoja wa vijana?
Tunaambiwa amefanyiwa fitna na mahasimu wake yaani Benno Malisa makamu mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM- UVCCM, na swahiba wake mkuu Ridhiwan Kikwete mtoto wa mwenyekiti wa CCM na rais wa jamhuri.
Je, kwa nini mahasimu wake watumie kigezo cha uraia kama hakuna ukweli? Je walijua kuwa si raia na kwa vile alikuwa anaweza kulinda maslahi yao, hili halikuwahangaisha hadi alipotishia maslahi yao?
Je, tunao wakubwa wangapi kwenye CCM wenye udhaifu huu unaotumiwa na wenzao kuwatumia? Je, ni kwa nini mtu anapokosana na vigogo wa CCM au watoto wao ndipo anakuwa si raia? Je, wanawapa ulaji watu wasio raia wakijua udhaifu wao ili wawatumie vizuri kwenye kuhujumu nchi? Hili linawezekana.
Rejea kashfa zenye kuhusisha mabilioni ya shilingi kutendwa na wakubwa zetu kwa kushirikiana na mawakala wao wa kigeni hasa wahindi. Tuna mifano mingi mkubwa ukiwa ule wa VG Chavda ya wizi wa mabilioni na ununuzi wa mashamba ya mkonge.
Je, alipogundulika wakubwa zetu waliomtumia walifanyaje ili kuficha nyuso zao? Walimtimua nchini badala ya kumfikisha mahakamani kwa kuhofia angemwaga mtama kwa kuku.
Kinachoshangaza sana ni kile kilichoripotiwa na vyombo vya habari kuwa kuna uwezekano Bashe alijitetea kwa kutumia nyaraka zinazosemekana ni za kughushi. Je amechukuliwa hatua gani? Nani atamshitaki iwapo wengi wanaopaswa kushinikiza nao wamegushi vyeti vya taaluma na hakuna anayewagusa?
Hata ukichunguza kashfa ya Richmond iliyomfurusha waziri mkuu wa zamani na swahiba wa Rais Kikwete, Edward Lowassa, kashfa ya ununuzi wa rada na ndege ya rais. Nyuma ya kashfa hizi kuna wakubwa fulani na kundi la wageni nyemelezi wanaosemekana kumilki uchumi wetu kwa asilimia 99. Je hapa tunaweza kujidai tuko huru? Je hapa watawala wetu si mawakala wa kawaida tu wa mitandao ya kijambazi ya kimataifa?
Kashfa ya Bashe ni ushahidi kuwa tusipoua mitandao ya kibiashara na kisiasa tutakuja kustukia nchi yetu imeuzwa kwa wageni ambao kwa sasa wameelekeza nguvu zao kwenye ubunge ili watunge sheria za kuwalinda na maslahi yao ambavyo ni hatari kwa mstakabali wa taifa.
Chanzo cha hii yote ni kumomonyoka kwa maadili ambako kumechukuliwa na madili ambapo mtu hulala maskini na kuamka bilionea na hakuna mamlaka inayombana aeleze alivyoupata utajiri wa ghafla hivi.
Uhamiaji wanauza pasi za kusafiria. Kigezo cha kufanya hivi ni pesa badala ya sheria. Kuna 'Watanzania' wa kuchongwa wanaopata pasi za kusafiria hata vyeti vya kuzaliwa bila hata kuweka mguu uhamiaji. Watakwendaje iwapo kuna mawakala wa kufanya kazi hii chafu?
Hali ni mbaya sana. Baadhi ya watendaji wa uhamiaji wana watu wao nje ya ofisi zao wanaowakuwadia watu wanaotaka pasi 'chap chap' kwa mshiko wa hali ya juu.
Kimsingi tusipokengeuka na kupambana na ufisadi na utawala wa kifisi na binafsi wa kubabaisha, tutazua vurugu huko tuendako. Hebu fikiria. Mtu anatoka India jana. Kesho anakuwa raia hata bila kujua lugha ya taifa.
Leo nitatoa mfano wa hapa Kanada. Mtu yeyote haruhusiwi kuwa raia wa Kanada hadi aijue historia ya nchi na moja kati ya lugha mbili za taifa yaani Kiingereza na kifaransa. Na muombaji hutahiniwa kuthibitisha hili.
Pia kupata uraia wa Kanada humchukua muombaji miaka mitatu ambayo anapaswa kuishi nchini humu bila kutoka hata siku moja mbali na zaidi ya mwaka wa kungojea matokeo. Maombi ya uraia huchukua muda mrefu. Hii ni kuzipa mamlaka muda wa kutosha kufanya uchunguzi juu ya muombaji ili zisitoe uraia kwa mtu asiyefaa.
Muombaji lazima awe na rekodi safi. Asiwe na kesi ya jinai au kuwahi kuhukumiwa kwa kesi ya jinai. Je, hali nchini mwetu ikoje? Mfuko wako.
Na wanaofanya uchafu huu washukuru ujinga wa raia wa kawaida wa kutojua madhara ya kuchezea uraia wao. Lakini kutokana na kupanuka kwa mawasiliano na matatizo yasababishwayo na wageni, kuna siku watu wetu watajua haki zao na kuzidai saa nyingine kwa njia yenye kuvuruga taifa.
Hivyo wahusika badala ya kutumia vigezo vya nani si raia na nani ni raia kisiasa, wanapaswa kufanya hivyo kisheria tena kwa maslahi ya vizazi vijavyo. Nchi ya Ivory Coast imegawanyika na kufikia karibu na kusambaratika kutokana na kuachia wageni wanaosemekana toka Burkinabe wajiishie na kufanya wasio paswa kufanya hadi wakajiona wana haki kuliko wananchi na kuiingiza nchi kwenye machafuko yanayoendelea kuigharimu chi hii iliyosifika kwa ustawi na utulivu wake.
Leo wananchi wa Darfur nchini Sudan wa makabila ya Fur, Masariti na Zagawa wanauawa na wageni waliowakaribisha yaani makabila ya Bargwu, Dajo Tama na mengine walipokimbia njaa nchini mwao Chad miaka ya 80.
Serikali haramu ya Khartoum inawatumia wageni hawa kuwaua wenyeji wao wakisaidiana na Janjaweed.
Tufupishe mada. Tanzania na watanzania tusipoacha kuangalia vijisenti kidogo vya kukidhi mahitaji binafsi ya kilafi, tutauza nchi yetu kwa wageni ambao hapo baadaye hawatakuwa na huruma nasi.
Kuna haja ya uhamiaji na serikali kwa ujumla kuachana na umachinga wa kitu muhimu kama uraia. Na Watanzania tuachane na tabia ya kuwa watazamaji hasa pale haki zetu zinapoporwa na wezi wachache wenye nafasi.
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 25, 2010.
Masha na Makamba wanamdanganya nani?
Hakuna kitu kilichonistua kama majibu ya ajabu ya waziri wa mambo ya ndani Lawrence Masha pale alipotakiwa na waandishi wa habari kuelezea msimamo wake kuhusiana na sakata la mgombea ubunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Nzega aliyeenguliwa kwa sababu ya kutokuwa raia, Hussein Bashe.
Alipoulizwa nini msimamo wake alijibu kuwa suala la uraia wa Bashe halina utata!
Alikaririwa akisema: “Hakuna utata kwenye uraia wa Bashe. Naweza kusema hivyo.” Jibu hili la ajabu liliwachanganya waandishi wa habari hadi kuzidi kumchimba na kutaka kujua kama Bashe ni raia au si raia alizidi kujichanganya na kuwachanganya wananchi. Alisema : “ Nasema hakuna utata kwenye uraia wa Bashe na siwezi kuzungumzia suala hilo zaidi. Sikilizeni, hili suala halina umuhimu kama mnavyolizungumzia.”
Hayo ndiyo majibu ya mtu anayeitwa waziri tena wa wizara ya mambo ya ndani. Hebu msomaji tufikiri pamoja. Je kwa majibu haya waziri umeelewa nini? Je kwa majibu yalivyo, ulitegemea yatolewe na mtu mwenye dhamana ya waziri? Je kwa majibu hayo, unaelewa nini kama Bashe ni raia au si raia?
Hebu tuendelee kudodosa udhaifu wa waziri tena mwanasheria. Alipoulizwa kuhusu uraia wa aliyechukua nafasi ya Bashe ambaye naye anadaiwa si raia wa Tanzania bali Burundi waziri alikaririwa akisema : “Nimeagiza watu wangu walifuatilie ili waweze kunipa taarifa.”
Wakati waziri akisema suala la uraia wa mgombea wa CCM aliyechukua nafasi ya Bashe unafuatiliwa, Katibu mkuu wa CCM, Yusuf Makamba anasema hivi: “"Tunachojua mgombea wetu ni raia." Je hapa nani anasema ukweli na nani anasema uongo? Tumwamini nani kati ya waziri mwenye dhamana na katibu mkuu wa chama chake? Je Makamba anapata jeuri wapi kutolea maelezo jambo ambalo hana mamlaka nalo kisheria? Je haya ndiyo matokeo ya chama kushika hatamu au kuwa juu ya serikali? Tusaidiane. Nchini mwetu kati ya chama na serikali nani mwenye kuwa juu ya mwingine? Haya maswali yanaweza kuonekana ya kichokozi. Lakini tunapaswa kujua nchi yetu na mifumo inayotutawala ili tuweze kuwa tayari kupambana na wale wanaovunja sheria kwa kuingilia mamlaka ya wenzao kiasi cha kuuibia na kuupotosha umma.
Kinachotia shaka na kuvunja moyo ni ile hali kuwa utawala mvurugano wenye kuingiliana umeanza kukubalika kiasi cha wahusika kuwa mamlaka ndani ya mamlaka na kuweza kuamua lolote bila kuchelea lolote. Hebu angalia majibu ya Makamba aliyotoa alipoulizwa kama chama chake hakitaathirika kama mgombea wake atabainika si raia. Alijibu: "Tatizo la nini wakati nimesema yeye ni raia?" Kumbe Makamba akishasema fulani ni raia hata kama si raia anakuwa raia! Je namna hii tutafika? Je bado tunahitaji watendaji kama hawa wasiojua wanachosema na madhara yake ukiachia mbali kutosoma alama za nyakati?
Laiti wangejua kuwa hata kupayuka kuna wenyewe na si wote wanaweza kupayuka wakawa salama!
Makamba amefanya utafiti upi na lini kujua kuwa mgombea wao ni raia iwapo malalamiko yalitolewa baada ya kamati kuu kumaliza kikao chake?
Je huu si ushahidi kuwa serikali yetu inajiendea tu kiasi cha watendaji wake kutojua hata mipaka ya mamlaka yao kiasi cha kuruhusu wakuu wa chama kutolea majibu masuala ya serikali ambayo hawahusiki nayo kama kwenye sakata hili? Je namna hii tutaujua ukweli na kutendewa haki? Je watendaji kama hawa wasiojua hata majukumu yao ukiachia mbali kujisemea wanapaswa kuendelea kuwa kwenye ofisi za umma?
Kama waziri wa mambo ya ndani mwenye kila wapelelezi na taarifa chini yake hajui nini hali ya uraia wa Bashe kweli atajua maadui wa taifa hasa wakati huu wa kukua kwa sayansi na teknolojia?
Sijui kama waziri anajua hata idadi ya watu walioomba uraia wa Tanzania ukiachia mbali idadi ya wahamiaji haramu waliomo nchini?
Je imekuwaje rais akateua mtu anayeonekana kupwaya wazi kwenye nafasi hii nyeti kwa usalama wa taifa hili? Je wako wangapi kama yeye ambao kimsingi wanatuangusha kama taifa? Nadhani hapa ndipo ilipo siri ya uwekezaji wa kijambazi usio na tija kwa taifa. Kadhalika hapa ndipo unaweza kuona madhara ya kujuana, kulindana. Rejea kutoshughulikiwa kwa wale waliotuhumiwa kughushi vyeti vya taaluma wanaoendelea kufaidi matunda ya nafasi ambazo hawana ujuzi nazo. Je tunafanya hivi kumkomoa nani zaidi ya vizazi vijavyo ambavyo tusipoangalia vitakuja kufukua makaburi yetu na kukojolea mabaki yetu kama ishara ya kulipiza kisasi kwa upuuzi unaofanyika sasa hivi.
Leo nimetumia suala la Bashe ambalo, kwa wasfu wa mhusika ni dogo tu, kuonyesha tulivyo kwenye hatari ya kuangamiza taifa letu kutokana na ombwe la uongozi. Bila kubadilika na kuteua watu makini kwenye nafasi nyeti kama wizara ya mambo ya ndani, kuna siku tutajikuta pabaya na tusijue la kufanya.
Kwa yanayoendelea, kama rais Jakaya Kikwete asingekuwa mbali na umma, alipaswa kuchukua hatua na kutatua matatizo sugu kama vile kughushi, ufisadi, uzembe na kadhia nyingine. Lakini hata hivyo tusimuonee. Kama hakuthubutu kushughulika, achia mbali, kutatua matatizo haya kipindi kilichopita, ni miujiza gani itafanyika kipindi anachosaka afanye hivyo wakati ni lala salama? Tuwakumbushe wapiga kura na wananchi. Kipindi cha kwanza cha urais wa rais mstaafu Benjamin Mkapa kilishuhudia mafanikio ya kupigiwa mfano aliyokuja kuyafuja kwenye kipindi cha lala salama.
Hivyo ni kazi kwao kujua nani anapaswa kuaminiwa nchi yao msimu huu kutokana historia kuwa mwalimu na shahidi mzuri. Wakati pekee wa kurekebisha hili ni kwenye uchaguzi angalau kama siyo kubwaga wote kuwapunguza.
Nisiwachoshe kwa hoja. Nimalize kwa kuuliza swali ambalo mnapaswa kujiuliza na kuwauliza wahusika hata wasipojibu ili mjue la kufanya hapo Oktoba. Je Makamba na Masha nani mkweli na wanamdanganya nani na kwa nini?
Chanzo: Dira ya Mtanzania Agosti 21, 2010.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
3 comments:
Najua wahusika wanasoma, na najua wanastahili kuelewa japo wanaweza kutojielewesha.
Lakini siku yaja
KAZI NJEMA SAANA KAKA
Mbona mada hii haifahamiki au ni chuki huyo juu picha ya kwanza ni mtanzania yeyote anayezaliwa TZ ni mtanzania usitazame rangi, watanzania si weusi tu ungefikiria kabla ya kuandika mada hii.
Nkwazi hajakosea. Wahindi karibu wote wana uraia wa nchi zaidi ya moja ingawa wazawa hawaruhusiwi. Tulifunguliwa macho juu ya hili na Amir Jamal waziri wa fedha wa serikali ya awamu ya kwanza. Alipokufa alizikwa kwao Kanada!
Hata hao akina Dewji, Rostam na wengine wana uraia wa nchi mbili na hata ukichunguza uraia wao ni matatizo matupu.
Kuna wabunge wangapi waafrika nchini India, Pakistan, Bangladesh na Iran?
Tuache kujikomba kwa magabacholi. Ni minyoo inayoua uchumi wetu.
Post a Comment