The Chant of Savant

Tuesday 19 July 2011

Kikwete vunja baraza la mawaziri


Ingawa rais Jakaya Kikwete ni mugumu kujifunza na kubadilika, kashfa ya hivi karibuni ya wizara ya madini na nishati kutoa rushwa ya shilingi 6,000,000,000 ili kupitisha bajeti yake itamvua nguo kama si kupima usafi wake na serikali yake.

Tangu aingie madarakani miaka sita iliyopita, Kikwete amekuwa na kawaida ya kuwakingia kifua mawaziri wake wenye utendaji usioridhisha.

Si uzushi. Katika baraza la mawaziri la Kikwete kuna vimeo vingi kuanzia Dk Hussein Mwinyi anayewajibika kwa mauaji ya Mbagala na Gongo la Mboto, William Lukuvi, Mary Nagu, Makongoro Mahanga na Emanuel Nchimbi wanaotuhumiwa kughushi shahada.
Pia wamo mawaziri wanaolegalega kama vile Dk Shukuru Kawambwa, Profesa Jumanne Maghembe na Sofia Simba, Hawa Ghasia, Vuai Shamsi Nahodha na William Ngeleja .

Simba anasifika kwa kuwakingia kifua mafisadi wazi wazi huku Ngeleja akijulikana alivyoliingiza taifa kizani huku kila siku akitoa visingizio na uongo kuwa mgao wa umeme utatafutiwa dawa na isipatikane zaidi ya kuongezeka.
Wengi wanashangaa walichomfanyia Kikwete hadi akalitoa taifa kafara ili kuokoa wateule wake.

Sasa wamenogewa kiasi cha kuzidi kumvua nguo. Hivi ni kashfa kiasi gani kwa wizara kutoa rushwa ili kupitisha bajeti yake? Je hapa Ngeleja na Adam Malima na katibu mkuu wa wizara David Jairo wanapaswa kweli kuendelea kulipwa pesa ya umma kwa kutumia vibaya pesa na ofisi za umma? Je nchi na pesa hii ni vya Kikwete kiasi cha watanzania kujiona kama hawahusiki wakati wanahusika? Wao ndiyo waathirika wa mchezo huu mchafu ambao ni mauti kwao na taifa lao. Hizi bilioni sita zimetoka wapi zaidi ya kodi za wananchi? Je bajeti inayotolewa rushwa ili ipite haina mshikeli?
Je wabunge watakubali kuendelea kudhalilishwa na kuonekana kama wapenda rushwa?

Ingawa Ngeleja ameonekana kuwa mmoja wa wateule wasioweza kuguswa na yeyote, kwa hili, kama Kikwete kweli ana busara ya kawaida, hatamvumilia zaidi ya kumtimua mara moja. Je kwanini Kikwete anasitasita kuwawajibisha mawaziri wa hovyo? Je ni ile hali ya kuogopa naye wasiseme yake ya nyuma ya pazia?

Wakati umefika kwa wananchi kumlazimisha Kikwete kuvunja mtandao wake wa walaji wanaochafua ofisi za umma na kutumia vibaya pesa ya umma. Hawa si mawaziri kitu bali mafisadi wa kawaida waliojificha nyuma ya madaraka. Haiingii akilini dhambi kama hizo hapo juu zipite bila kuadhibiwa na wananchi waridhike na utawala wa serikali inayovumilia madudu haya. Je tatizo ni nini? Ni ile wananchi wetu kujifanya watazamaji wakati ndiyo wachezaji?

waziri mkuu Mizengo Pinda ameishafungua mashitaka rasmi kwa rais na wananchi. Tungoje tuone wahusika watachukua hatua zipi. Pinda alikaririwa akisema,"Kwa jinsi jambo hili lilivyokaa, hakuna jinsi mtu unavyoweza kulitetea hata kidogo, nilitamani sana kwamba nije hapa niseme kwamba uamuzi wangu mimi ni huu, lakini haikuwezekana," alisema Pinda na kuongeza: "Kwa dhati kabisa naomba wabunge tuwe na subira, mara tu mheshimiwa Rais atakapotua South Africa (Afrika Kusini) jioni ya leo (jana), nitamuarifu na ninaamini tutaelewana kuhusu hatua za kuchukua."
Je Pinda atalifanyia kazi hili vilivyo au ni sanaa kama kawa? Yetu macho. Tutafakari.

5 comments:

malkiory matiya said...

Rais mtalii kazi yake ni kula raha, kufanya maharusi ya ndugu zake badala kutatua matatizo yanayokabili taifa kama hili la kiza! Tumeliwa, kwa kweli, hapa nitamkubuka Nyerere kwa kwa kauli yake kuwa ikulu ni pahala patakatifu!

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Bwana Markiory, Habari za siku nyingi kwanza? Kwa taarifa yako ikulu iliacha kuwa mahali patakatifu baada ya mwalimu kuondoka. Kwa sasa ikulu ni mahali pa takata na patakatakatifu au tuseme patakachafu kwa sana. Tulie na kuomboleza kwani mama yetu Tanzania anaendelea kuuawa na mbwa mwitu na mbweha wenye madaraka.

malkiory matiya said...

Mhango mimi ni mzima kabisa. Nakubaliana na wewe kuwa ikulu ni pahala pa takachafu! nasubiri kiongozi mfano wa Jerry Rawlings, atakaye kuwa radhi kuwapiga risasi mafisadi wote kwa nia ya kulijenga taifa mpya ambayo haijaambukizwa na ufisadi.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Bwana Malkiory, katika kizazi hiki cha laana usitegeme kutokea mtu kama Rawlings. Akitokea mtu wa maana atatokea sana sana mwizi kama Mwinyi au Mkapa ambao ndiyo waliomuumba mwizi wa sasa.
Hebu angalia wanajeshi wetu walivyo kama vyangudoa kwa wanasiasa. Mara hii umemsahau kauli ya yule mpuuzi anayeitwa Abdulrahaman Shimbo wakati wa sakata la ufisadi wa Kikwete na wenzake? Hawa si wanajeshi bali viwavi jeshi waitwao wanajeshi. Tanzania ilikufa siku alipong'atuka Mwalimu Nyerere. Tanzania kwa sasa ni Tanzia au Bongolalaland kama nipendavyo kuiita kwenye kijiwe changu.

malkiory matiya said...

We ache tu waendelee kuchuma rasilimali za nchi yetu bila aibu. Lakini ipo siku kama siyo wao basi watoto wao, wajukuu zao au hata vitukuu zao watahukumiwa na watanzania wazalendo watakaojitokeza. Tuendelee tu kupambana hadi siku ya mwisho!