Monday, 16 January 2012

Kuna harufu ya kujuana kwenye balozi zetu


Mindi Kasiga aliteuliwa hivi karibuni kwenda kwenye ubalozi wetu Washington. Huyu anasadikiwa kuwa na uhusiana na Rahma Kharoos Kasiga anayedaiwa kuwa nyumba ndogo ya bwana mkubwa na mkurugenzi wa kampuni ya mafuta iliyoibuka baada ya bwana mkubwa kuwa madarakani. Wengine wanasema ni mtoto wa dada yake Anna Mkapa. Mindi anaonekana akiwa na wadau wake mmojawapo akiwa Adam Gile. Hatujui kama huyu Gile ana uhusiano na Gile wa Richmond.
Kwa sasa tatizo la ajira nchini ni kubwa kuliko wakati wowote katika historia ya nchi yetu. Sambamba na hili ni kutamalaki kwa vitendo vya rushwa, kughushi, kujuana na kubebana katika ajira hasa zile nono. Kuna maeneo yanayopigiwa kelele na wananchi wa kawaida kwa sababu wao hawahusishwi katika ajira nono kwenye maeneo haya. Miaka mitatu iliyopita kuliibuliwa uoza wa kutishwa kwenye ajira za Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Kuligundulika majina mengi ya watoto au jamaa wa karibu au watoto wa marafiki wa vigogo kwenye ajira ya BoT kiasic ha kuliamsha taifa kuanza kujiuliza wahusika waliajiriwaje kule kwa wingi vile. Katika majina ya vigogo ambao watoto wao wameajiriwa BoT yalikuwamo majina kama Mwinyi, Lowassa, Mungai na mengine mengi tu. Hata hivyo, sijui ni kutokana na uzito wa majina na nafasi za wazazi wa waajiriwa kwenye jamii, suala hili liliachwa lijifie huku wahusika wakiendelea kuhomola. Hata ukienda kwenye taasisi nyingine zinazolipa vizuri au kuwa na nafasi nzuri ya rushwa kama vile Mamlaka ya Mapato, Uhamiaji, Utalii na madini, mbuga za wanyama, na kwingineko, utakuta mchezo ni ule ule. Watu wachache wenye majina wamepandikiza watoto wao kwenye maeneo haya huku watoto wa maskini wakiendelea kuteseka bila ajira.

Eneo jingine ambalo halikuwa likijulikana kuwa kichaka cha ajira za watoto wa wakubwa ni kwenye balozi zetu nje ya nchi. Ajira za nje zimekuwa siri kubwa ambayo si rahisi kwa mwananchi wa kawaida kujua au hata kufikiria. Hapa hatujaongelea nafasi mbali mbali yaani scholarship zinazotolewa na nchi marafiki ambapo wanufaika wengi ni wale wale-watoto wa vigogo, watoto wa marafiki wa vigogo na hata vigogo wenyewe.

Katika pita pita yangu kwenye vyombo vya habari mbali mbali nilikuta na kitu kilichonistua kidogo kiasi cha kusumbua akili yangu na kujenga dhana hata shaka na ajira za watanzania walioko kwenye balozi zetu nchi mbali mbali. Katika matukio mawili matatu kwenye habari, nilikutana na majina makubwa matatu haraka haraka. Hii ilinifanya nijiulize: je wapo watoto wa ngapi wa vigogo au hata vigogo wenyewe kwenye balozi zetu nje ambapo bila shaka wanalipwa vizuri? Je wameteuliwa au kuajiriwa kwa sifa za kitaaluma au kujuana au vyote? Je watanzania wamejulishwa na kuridhika na hili lililonistua au nao watastuka kama mimi?

Majina makubwa matatu niliyopambana nayo ni kwenye balozi mbili, yaani ule wa Umoja wa Mataifa na ubalozi wa Tanzania nchini Kanada. Majina haya ni ya Rose Mkapa afisa utawala wa ubalozi New York. Mkapa jina la familia ya rais mstaafu Benjamin Mkapa.

Kwenye ubalozi wa Ottawa Canada, nilikutana na majina kama Richard Tibandebage ambaye ni afisa ubalozi. Kwa wenye kumbukumbuku, marehemu Andrew KajunguTibandebage alikuwa Balozi wa zamani wa Tanzania nje kwa muda mrefu chini ya awamu ya kwanza.

Joseph Sokoine, ni naibu balozi wa Tanzania nchini Kanada. Je huyu ni mtoto wa aliyekuwa waziri mkuu katika awamu ya kwanza, Edward Sokoine?

Yupo mwingine mwenye jina kubwa; naye ni Salome Sijaona balozi wa Tanzania nchini Japan. Je huyu ana uhusiano na Lawi Nangwanda Sijaona alikuwa mmojawapo wa mawaziri wa mwanzo?
Majina mengine ya vigogo ni ya Jaka Mwambi balozi Urusi ambaye alikuwa mkuu wa mikoa mbali mbali na naibu katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) bara na Adadi Rajab ni balozi Zimbabwe kamishina wa makosa ya jinai wa zamani.

Jina jingine kubwa ni la Maura W. Mwingira ni afisa ubalozi New York. Je huyu Mwingira ana uhusiano na kigogo mwingine, Augustine Mwingira mmojawapo wa mawaziri kwenye serikali ya awamu ya kwanza na mkuu wa mkoa kwenye serikali ya awamu ya pili.

Pia yupo Mindi Kasiga afisa habari wizara ya mambo ya nchi za nje. Kasiga ni jina linalohusiana na Rahma Kharoos Kasiga ambaye wengi wamemjua alipoibuka baada ya rais Jakaya Kikwete kuingia madarakani.

Orodha haikamiliki bila jina Msekwa. Jacob Msekwa ni naibu balozi wa Tanzania nchini Sweden. Je huyu ana uhusiano na Pius Msekwa ni makamu mwenyekiti wa CCM. Jacob hayuko peke yake. Wapo Msekwa wengine ambao ni Erick Msekwa na marehemu Julius Msekwa. Msekwa wawili walio hai bado wanaishi ulaya.

Kigogo mwingine ni Ali Karume balozi wa Tanzania nchini Italia. Huyu anajulikana kuwa mtoto wa rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume Pia Ali ni mdogo wa rais mwingine wa zamani wa Zanzibar Amani Abeid Karume.

Radhia Msuya balozi Afrika Kusini analo jina kubwa la Msuya. Hata hivyo, hatuna uhakika kama Msuya huyu na Cleopa David Msuya waziri mkuu wa zamani wana uhusiano. Uchunguzi mwingine unaonyesha kuwa Radhia Msuya ni mdogo wake Asha Rose Migiro ambaye kabla hajawa balozi kamili alikuwa London kwenye ubalozi wetu akiwa afisa ubalozi msaidizi. Inasemekana Radhia Msuya ana ndugu yake mwingine Fatma Mtengeti ambaye anafanya kazi kwenye ubalozi wetu huko Uingereza.

Mwingine ni Joyce Kafanabo ubalozi wa Tanzania Marekani. Kwa kumbukumbu ni kwamba Peter Kafanabo alikuwa kigogo wa CCM aliyewahi kuwa mkuu wa mikoa mbali mbali nchini. Pia yupo mama Mnanka kwenye ubalozi wa Tanzania nchini Marekani. Je huyu ana uhusiano na Bhoke Mnanka ambaye alikuwa mmoja wa mwaziri wa kwanza wa Tanzania huru.

Kwa ufupi, maswali ni mengi kuliko majibu. Hivyo tungeshauri wahusika lau wajibu huku wananchi wa kawaida hasa waathirika wenye habari kuhusiana na mchezo huu wazianike angalau umma ujue kinachoendelea. Kinachopaswa kupigwa vita ni kuhakikisha huu mchezo wa kujihudumia na kurithishana madaraka unakufa. Leo tumeongelea walioko nje ubalozini. Bado wale waliomo kwenye ngazi za uwaziri kama vile Hussein Mwinyi na Adam Malima.

Chanzo: Dira Januari 2012

3 comments:

Anonymous said...

Naomba niseme machache kuhusu swala hili hata tukilia na machozi ya damu TZ yetu imeharibika sana ukienda ofisi zote serikalini majina ni yale yale hayabadiliki kama si mtoto ni mjomba au shangazi au nyumba ndogo maskini tusiokuwa na majina katika uongozi tutaoza hapo hapo mimi nakuunga mkono hakuna hata vijana katika bunge letu ni wakuhesabu hawataki hata kustaafu kuwachia na vijana wafaidike haiwezekani

Anonymous said...

Hakuna uhusiano wowote kati ya Salome Sijaona na Lawi Sijaona. Ni majina tu.

Nikkiiobp said...

Hakuna uhusiano wowote kati ya Salome Sijaona na Lawi Sijaona. Ni majina tu.