Salaam aleikum waarahmatullahi wabarakatuhu. Alhamdulilah Wasalatu Wasalaam Ala Rasulullah Wa-ala-alihi Wa-as-habihi Ajmain.
Wapendwa wasomaji walevi na wanywa kahawa wote duniani na hasa nchini Daganyika bin Bongolalaland, mnajimu wenu mkuu Shehe Mpayukaji Msemavyo Mpakazaji wa Waambie anawaletea utabiri wa mwaka 2012 kama unavyoonyeshwa na nyota.
Kwanza, niweke wazi; sitabirii njaa wala umaarufu uchwara. Nimesomea haya madudu kuanzia Clairvoyance, poltegeistry, vampireology, psychometry, thouthtography, astronomy, astrology, cosmology, astrophysics, stigmata, dogmata, doppelganger, bilocation na madude mengine mengi ya kutisha ambayo nikiyaorodhesha yanatosha kuwa makala.
Kinyota, mwaka mpya unaonekana utakuwa mwaka wa ongezeko la matatizo.
Hii ni kutokana na nyota kuonyesha kuwa matatizo yatazidi ilhali wanaopaswa kuyatatua wakigeuka kuwa tatizo kubwa.
Nyota iliyotawala mwaka huu ni nge ikiuma kila kitu kuanzia maisha ya mtu binafsi hadi jamii kwa ujumla.
Kama nge, wenye mamlaka watawala wasio na mamlaka kiasi cha waliwa kuanza kujitambua na kujaribu kupinga uliwaji huu unaofanywa na hawa majahir murakhab.
Kadhalika, nyota zinaonyesha kutakuwa na ongezeko la vimbunga na mafuriko mbali mbali kuanzia maofisini hadi baharini.
Vimbunga hivi vitawakumba baadhi ya waliomo maofisini kiasi cha kujikuta kwenye hali ambazo hawakutegemea.
Kadhalika, ufisadi utaongezeka kutokana na ile hali ya kila mtu kujifanyia atakavyo na muda mwingi kupotezwa kwenye kusaka ngawira badala ya kuhudumia wahudumiwa. Mahospitalini, mahakamani, vituo vya polisi hata kwenye ofisi za ajira kutaongezeka rushwa kiasi cha kutisha.
Itafikia mahali, mwaka huu, haki kuuzwa kama njugu kutokana na mkanganyiko na mvurugano huu wa kinyota.
Kuongezeka kwa ufisadi kutasababisha ughali wa maisha na umaskini vitu ambavyo, kama vitatumika vizuri, kinyota, vinaweza kuleta ukombozi wa walio wengi.
Hii itategemea na wahusika watakavyojitambua na kutambua matatizo yao ya kweli ambayo ni watu na mfumo wanaousimamia kujitajirisha kwenye migongo ya maskini walio wengi.
Kuongeza chumvi kwenye kidonda, mwaka huu utashuhudia makapi mengi kuzidi kurudufiwa (recycling) ambapo wanasiasa waliokataliwa na wapiga kura majimboni mwao, watapewa ulaji kiasi cha kuwaacha waliowakataa vinywa wazi kwa hasira na mshangao na mfadhaiko.
Nyota pia zinaonyesha kuwa kukuwapo na ongezeko la vita ya mitandao ya ulaji na kumalizana katika kuusaka ukuu ambao siku hizi umegeuka dili hasa kutokana na kuwa nyenzo ya wanaoukwaa kula wao ndugu zao, familia zao hata wapambe zao hata bila kunawa.
Siku hizi ukuu si utumishi bali utumikishaji ambapo mwenye kuwa nao ni muungu mtu hapa duniani kutegemea na watakaomrithi.
Kama akiwa na bahati mbaya akarithiwa na watu wenye usongo na kaya yao basi humsweka lupango hata kumnyotoa roho kutokana na madhambi yake ya ukuuni.
Kama akipata vibaraka au marafiki zake basi hutanua maisha yeye na ukoo wake. Hamjaona wakuu wa zama zile ambao watoto wao nao wanatesa kiasi cha kuota hata kuwarithi wakuu wengine? Leo siwataji kwa majina ingawa hata kuku anawajua.
Sambamba na kuongezeka kwa mitandao, usanii pia utaongezeka kiasi cha kuongezeka kwa viongozi wa kiuroho wenye uroho wakisingizia Mungu wakifanya miujiza hata kufikia kukufuru kuiombea kaya badala ya kuiambia ukweli.
Hamkuwasikia wale nilio waonya kwao kuwa ni mbwa kwenye ngozi ya kondoo? Narudia, shauri yenu mtaliwa mwajiona.
Natabiri kuwa ataibuka mzee mwingine sawa na yule wa Loliyondo awalize wengi wenye kutaka mafanikio bila kutoa jasho ua kuficha magonjwa wanayougua kwa kuogopa kuambiwa ukweli kuwa wengine wameikwaa miwaya.
Atatokea mkoa gani? Atatokea katika mkoa mmoja kati ya pande za mashariki, magharibi, Kaskazini, Kusini na Kati. Atatokea muda gani toka sasa? Atatokea wakati ujao.
Pia natabiri kuwa vigogo watano watakufa mwaka huu. Kwa vile sitaki kuwatisha, sitataja majina yao wala vyeo vyao leo.
Ila watarudisha namba kati ya mwezi wa tatu hadi wa 11. Pia, wengine wataaanguka anguka hovyo mara kwa mara. Ingawa mvua zimenyesha na kusababisha mafuriko, mgao wa umeme utaongezeka sambamba na bei za umeme na nauli.
Pia natabiri kuwa ndoa ya chama cha Convention of Unreasonable Fellas (CUF siyo Chama cha Wananachi) na Convention of Conmen and Mafioso (CCM-siyo Chama cha Mapinduzi) itakuwa hatarini kiasi cha kugeukana kwa kushuku kutuhumiana kufikia malengo fichi.
Wawili hawa watashikana uchawi na kushutumiana kutapeliana.
Pia nyota zinaonyesha kuwa kutakuwa na poromoka zaidi la uchumi na thamani ya madafu.
Hii itatokana na kuongezeka kwa wezi wa madafu karibu kila mahali.
Nyota zinaonyesha kuwa pamoja na pigo hili kiuchumi, wakuu wataendelea kujisifia kuleta maendeleo huku wakiongezeana ulaji kuanzia kupandisha mishahara yao na kuongeza walaji hasa makapi, wana familia marafiki na waramba viatu.
Kutakuwa na ongezeko la wanachama wenye kidomo wanaopinga ulaji wa wakuu wa Vyama vya unoko na ulaji na hawa watatimuliwa.
Misiba midogo itaongezeka kiasi cha mkuu kupata fursa nyingi za kwenda matangani kuliko hata safari za kwenda ughaibuni ambazo nazo zitaongezeka chini ya visingizio mbali mbali.
Kadhalika ajali za barabarani zitaongezeka kutokana na kuongezeka kwa haraka za kutafuta njuluku kufidia kulanguliwa mafuta.
Mwisho kabisa kuna marais wanne wa muda mrefu wataangushwa kwa aibu kwa sababu nyota zao wote ni mizani.
Mizani itaanza kuelekea upande wa umma huku ikiwaacha wakiporomoka kama masuke.
Watawala hawa watakaoanguka nchi zao ziko upande wa kaskazini mwa nchi yetu.
Kwa upande wa kusini, rais mmoja bishololo mpenda mabibi ataumbuka na kuwa kwenye mgogoro mzito na waliomweka madarakani hasa vijana.
Pia katika nchi jirani na rais huyu bishololo mfalme mpenda kuoaoa ataingia kwenye matatizo ya kiuchumi kutokana na kuzidisha mabibi na matumizi huku wananchi wake wakiendelea kuwa maskini.
Kwa ufupi huo ndiyo utabiri wa mwaka mpya 2012. Kuhusu utabiri wa kijiwe, hii ni chiri yangu.
Chanzo: Tanzania Daima Januari 11, 2012.
No comments:
Post a Comment