Wednesday, 18 January 2012

Kumbe na vyama vya upingaji vinatuogopa!

SISI pamoja na kujadili mada zetu chini ya uhuru wa kaya wa kila mwanakaya kuwa na haki ya kusema atakalo ilimradi asivunje sheria, hatukujua kuwa kumbe mada zetu zinavilaza baadhi ya vyama vya upingaji bila usingizi.

Nasikia hata lisirikali huwa halipati usingizi hasa likisoma haya ninayoandika toka kijiweni kutokana na kuwa ukweli mtupu. Naona yule anaguna. Kamuulize Njaa Kaya kama hanijui wala kunijadili kwenye vikao vyao.

Siku moja alitaka tukutane anilipe fadhila nikamtolea nje. Mie sibabaishwi na pesa ya wizi wala madaraka yatokanayo na uchakachuaji na kuchafuana. Anyway, hapa leo si pake.

Ngoja nijongee kwenye mada ya rero. Leo sitaki kuzungusha kwa vile na wao hawakuzungusha. Nani alijua kuwa kumbe vijiwe vyetu vya kahawa vinakisumbua chama cha calf au ndama ambacho wengi hupenda kukiita CCM namba mbili yaani Chama Cha Magamba B? ukweli sasa umefichuliwa na vyombo vya habari kuwa kumbe kijiwe chetu siyo moto kwa Njaa Kaya peke.

Ni umeme kwa vyama vya upingaji hasa calf ambayo imeamua kuwafungulia baadhi ya vigogo wake mashitaka ya kuongelea mambo ya chama kwenye vijiwe vya kahawa.

Maskini ng’ombe hawa hawakujua kuwa nasi ni chama tosha hata kama hatuna usajili. Tofauti yetu na Kaf ni kwamba mimi mzee Dk, Profesa, Al Haj Mchungaji Mtume Mpayukaji Msemahovyo wa Mpakazaji siyo changu kama made… wao.

Sitishwi na vi-ofa uchwara iwe vya urahisi au hata umakamo. Mie siyo ngangala wala ngungule bali msomi wa Harvard University. Mie ni kijigoo na si changu kama mtu wao hata kama ana kichaka cha made...

Sina haja ya kumuandama changu huyu aliyewekwa kinyumba na Chata la Mafisadi wa magamba. Nimuandame wa nini wakati mwisho wake umeishakaribia hasa baada ya mjumbe machachari toka Ginigi na Wawe ameishafanya kazi hiyo? Nimuandame wanini wakati aibu aliyojiingiza inamtosha? Nyie ngojeni muone maajabu ya Mwajabu kukosa adabu bila sababu hasa pale made… atakapofuliwa kama Kafulia ingawa alitaka kuwambatia wenzake.

Tatizo la siasa za matumbo ni kila mmoja kutaka kumnyotoa mwenzie roho ili ale yeye. Mtakapoendelea na upuuzi huu hawa walevi wetu watatetewa na nani? Ajabu na walevi walivyo wa hovyo wezi wakitimuana wanakwenda kwao na kuwaongopea nao wanaiingia mkenge kuwatetea kama ilivyotokea kwa Dave Kafulia.

Hamkusikia walevi wa kule mwisho wa reli wakisema eti watahama naye wasijue jamaa hawawakilishi wao bali tumbo lake? Ya Kafulia kufulia tuyaache maana alishaonyesha asivyo na maana pale alipolialia na kumshika miguu Ku-Mbatia akimwaga michozi hadharani kama kichanga.

Ingawa calf wamechemsha na kujivua nguo, tunakubaliana nao kuwa vijiwe vya kahawa vinatisha. Badala ya wao kuangalia wapi wamejikwaa wanakazania kushutumu waliokoangukia!

Nani alijua kuwa ni vijiwe vya kahawa vilivyofichua nyumba ndogo za watawala hata akiwamo mkuu? Nani anabisha kuwa vijiwe vya kahawa ndiyo vimevichua yaliyokuwako nyuma ya pazia kuhusiana na jamaa wa mabondeni ambao hawataki kuhama kwa sababu ya kulinda biashara yao haramu ya gongo na unga?

Hata Richmonduli, kwa taarifa yenu, ilifichuliwa toka kwenye vijiwe vya kahawa amini usiamini.

Hawa jamaa badala ya kushughulikia matatizo yao wanabaki kuviandama vijiwe. Hivi kweli, kwa mfano, kuna mantiki na haja ya kuvilaumu vijiwe kwa uroho na upuuzi unaofanywa na vyama kama calf?

Watu wanaiba mali za chama halafu wakisemwa kijiweni wanaanza kugeuza hili kuwa kosa la jinai kuliko wizi wanaofanya! Watu wanaanzisha vyama bila sera halafu wakinangwa wanaanza kunung’unika! Kuna kipindi nashindwa kutofautisha vyama vya upingaji na chama twawala. Maana wanapingana huku wakiwala wanachama.

Juzi mwanakijiwe wetu tuliyekuwa tumempandikiza kwenye chama cha Calf, Amri Kirungu alituletea taarifa kuwa ameshitakiwa mbele ya kamati ya nidhamu feki iliyoundwa kumdhibiti Hamada wasijue itawakotea puani kuwa anazungumza mambo ya chama kwenye vijiwe vya kahawa! Ebo! Walitaka aongelee mambo ya calf kitandani au chooni? Stupid all of those who accuse other for what they actually do more than those they accuse.

Samahani. Nimepandisha Mwenembago hadi kuongea kisodoma! Ingawa wametutupia lawama kwa kufichua mambo yao ya aibu, wangoje sasa wakione cha moto kwa kuchezea hata mahakama baada ya kuwapiga stopu wao wakaendelea na ujinga ujinga wasijue zao zinahesabika.

Kumbatia alimfulila Kafulia sorry, Mariam Sefu Sahaulifu anataka kumnyotoa roho jamaa wa Ginigi na Wawe eti kwa vile alikuwa akija kijiweni kwetu na kumwaga siri za ulaji wake na wezi wengine waliotamalaki kwenye vyama vya ulaji viitwavyo vya upingaji.

Hata Rushid Amadi akitimuliwa na ile nyumba ndogo ya chama cha mafisadi na siri za kufanywa nyumba ndogo kwa chama cha Calf zimeishamwagwa tena kwenye vijiwe vyetu vya kahawa na sasa tunamwaga kwenye vijiwe vyetu vya magazeti.

Wao wamewafukuza nasi tumewapokea kijweni kwetu. Kwa sasa Hamada na Kafulia ni wanakijiwe wetu wapya wanaotupa hata siri za mjengoni na jinsi yule mama wa kucheza makidamakida anavyowaburuza na kuwatisha kiasi cha mjengo kugeuka genge la kutetea ujambazi na ufisadi.

Mimi kama rais na mwenyekiti wa vijiwe vya kahawa, natoa mwaliko kwa wanasiasa wote watakaofukuzwa waje vijiweni wamwage stori ili tuzisambaze kwa walevi na wanywa kahawa tuone hawa wanaojiandaa kugombea ukuu kama watapata kura.

Hata hawa jamaa wanaolangua umeme na wese tumeishapata taarifa zao na tunapanga kuwatokea siku moja na kuwagadafi kama siyo kuwamubaraka siku moja. Tuna mpango kamambe wa kuhakikisha tunawaleta walevi toka vijiwe vya jirani hasa kule kwa wakora Nairobbery waje waeleze ni kwanini kwao bei ya umeme na wese viko chini wakati sisi viko juu kama hakuna mkono wa watu wanaoleta wachukuaji wao kama yule Richmond na Downs wanaolipana nyuma ya pazia kwa kuwaibia walevi maskini. Shame on them! Hii kaya imeharibika kiasi cha kustahili kukameroniwa.

Chanzo: Tanzania Daima Januari 18, 2012

No comments: