Wednesday, 25 January 2012

Mpayukaji kuhamia Kenya

ZAMANI ungeniambia kuhamia nchi kama Kenya ningekufikisha mahakamani kama si kukunyotoa roho. Hata hivyo, nikiri. Imani na mawazo uchawara ya namna hiyo sina tena. Wazungu husema to make a U-turn. Nami nimefanya hivyo. Nimejipiga mtama kweli kweli baada ya kuchoshwa na ujambazi na upuuzi ninaoshuhudia kila siku na kila mahali kwenye kaya.

Ingawa zamani tuliwaita ndugu zetu wa Kenya wakora, nyang’au na majina mengine mengi tusijue sisi ndiyo manyang’au, kwa sasa wana nafuu kimaisha kuliko sisi. Mzee Mchonga mwana Musa alizoea kuwaita man eats man bila kujua atarithiwa na man eats everybody and everything.

Hakujua kuwa kutazaliwa Kiwila thieves na EPA thugs! Uliza: sasa tuko wapi zaidi ya kuwa na manyang'au squred? Wakati sisi tukipiga mbio kwenda nyuma wao wanapaa kwenda mbele. Wana uwezo wa ku-export hata wafanyakazi uchwara kuja kwetu kufanya kazi nzuri na kuondoka na mshiko wa haja wakati sisi tukiangalia.

Wajua siri yao nini? Kujituma, ubunifu na Kiingereza chao cha I dhink mbus has many more passangers than its capacity. Hamkumsikia jamaa kutoka huko ambaye alinyakwa Manyara akifanya kazi ya kupaka rangi milango na madirisha ilhali aliingia nchini kama TX? Mpo hapo waliwa? Hayo tuyaache.

Mwenzenu nimeamua kuhamia Kenya kutokana na sababu za maana sana hasa kushindwa kuishi kwa kubangaiza au kudokoa toka kwa umma. Siko tayari kuishi maisha ya shilingi milioni moja wakati mshahara wangu ni laki mbili. Siko tayari kuishi kwa kutegemea jinai au kubomu kama lisirikali lenu.

Nahama kwa sababu Kenya: Umeme ni bei nafuu si kama hapa ambapo kundi la majambazi limeamua kwenda nje na kuleta wachukuaji na kuwaita wawekezaji halafu linawatumia kutuibia pesa yetu na kutupandishia umeme kila siku.

Mie siyo taahira kuendelea kununua hata kiza tena kwa bei ya kulanguliwa. Inatisha sana kuona nchi yenye vyanzo vingi vya maji kulangua umeme wakati Kenya ambayo inanunua umeme kutoka Uganda inauza umeme huo huo wa kununua kwa bei nafuu kuliko wetu wa kuzalisha wenyewe.

Sababu nyingine inayonihamishia Kenya ni kuepuka kulanguliwa mafuta wakati Kenya ni bei nafuu. Huwa nashangaa. Je, Kenya wananunua mafuta wapi ambapo sisi hatujui kiasi cha kuendelea kuchezeana namna hii? Sina uhakika hata gesi itakuwa bei mbaya ingawa tunaichimbua wenyewe huko Songosongombingo.

Je, ni wangapi wanajiuliza swali kama hili? Kenya hawana WEKULA kama shirika la kudhibiti bei ambalo hapa kwetu kazi yake si kudhibiti bei bali kuzipandisha hovyo hovyo. Sababu nyingine inayonipeleka Kenya ni ile hali ya uchumi wao kukua huku wetu hapa tunaukalia tu.

Kivutio kingine ni kwamba Kenya wana katiba mpya inayohimiza haki na usawa. Wakati wao wakivuna na kufaidi kuwa na katiba mpya sisi tunaendelea kuzungushana na usanii wa kipumbavu kutetea masilahi uchwara na ya kipuuzi ya kikundi cha wezi wachache wasiosoma alama za nyakati.

Kutokana na katiba ya Kenya kuweka usawa, nahamasika kuhamia huko. Naamini nitatendewa haki kiasi cha kuwa na uhakika wa maisha. Hivyo nikiugua sitaambiwa kwenda kwenye mahospitali yasiyo na dawa wakati wao wakihudumiwa kifalme huko Apollo India. Isitoshe hospitali yao ya rufaa ya Kinyatamanyata iko fiti kichizi.

Kivutio kingine kinachonikimbizia Kenya ni ile hali ya rais kutokuwa juu ya katiba. Nakumbuka. Hata baba Dave hawaruhusu kina Dave na wenzake kuibia Kenya kwa kisingizio kuwa dingi wao ni mdosi na mkubwa wa goverinoma. Noma kuibia Wakenya. Hawana mchezo, hata uwe mkubwa kama tembo watakugadafi hata kabla hujatanua pesa yao. Hamuoni pesa yao inavyopaa wakati madafu yakizama utadhani yamefungiwa nanga?

Kutokana na Rahisi kutokuwa juu ya katiba, hata haja ya kuwa na FFU hakuna. Hivyo hakuna wanyanyasaji na wauaji watumiao virungu wanapoamrishwa na wauaji wenzao kuua wale wanaowaonyesha kweli ili iwaweke huru. Kwa nilivyo na kidomodomo, nimeona nijihamie mapema kabla ya wanoko hawa kunishukia kama walivyowashukia Chakudema kule AR mwaka juu na kunyonga watu kama hawana akili nzuri.

Pia nahamia Kenya ambapo majaji wanaheshimiwa na kutenda haki. Ni juzi tu rafiki yangu Jaji mkuu msaidizi Nansi Barasa alijikuta kitanzini baada ya kukataa kupigwa sachi na mlinzi kiasi cha kuudhika na kumvuta pua ambayo sasa imesababishwa naye avutwe ukuu!

Pia napenda sana majaji wa Kenya ambao huchaguliwa na si kuteuliwa na mtu mmoja tena asiyejua sheria ambaye mara nyingi anaweza kuathirika na ushawishi kiasi cha kuendekeza udini, ukabilia na ushoga.

Pia nahamia Kenya ili siku moja niteuliwe kuwa balozi ughaibuni nami nijisikie kinoma. Maana mabalozi wa Kenya umangani si kama wa Danganyika ambao wengi ni re-cycled ukiachia mbali balozi zetu kujaa watoto wa vigogo na magogo.

Anayebishia tuhuma hizi aiulize serikali orodha ya wafanyakazi wa balozi zenu muone kama hamtapasuka kwa presha. Mie hainihusu! Kazi yangu ni kuronga na kuwafumbua macho. Sasa kama mtaridhia kuendelea kuliwa hiyo ni shauri yenu. Narudia, tumieni akili badala ya masaburi.

Kitu kingine kilichonivutia kuhamia kwenye nchi ya nyayo, ni ile hali ya uchumi, sarafu na mambo kufanyika kitaalamu kuliko hapa ambao mambo si mambo bali mambo hovyo hovyo. Cha mno nakwenda kuwekeza Kenya kwenye Kayanite na kuutangaza Mlima Kimaranjaro maana vyote viko huko.

Hivyo, msijedhani nimeishiwa na uzalendo. Hasha! Kenya ni wazalendo kuliko nyinyi kwa sababu wameweza kuimarisha hata mabenki yao kiasi cha kuweza kuja kuwekeza humu wakati yenu mmeyachinjilia mbali na EPA zenu.

Hivyo nikiwekeza Kenya nitakuwa na uhakika wa biashara yangu. Hii ikichangiwa na gharama nafuu za umeme na bei ya kuingia kichwani ya wese, ndiyo usiseme. Huenda one day nitakuja kuwekeza huku baada ya kaya kukombolewa.

Nimalizie kwa kuwapa nyuzi. You know what? Kumbe ule mradi wa Kiwila umeishauzwa tena kwa Tunituni na rafiki yake Dani son of Jonah wake zao na watoto zao bila kusahau hata wakwe wa kike, kiume na jinsia zote.

Ama kweli wabongo ndiyo waliwao! Habari nilizo nazo toka FBI ni kwamba dili hili likikamilika wezi hawa wakubwa wataiibia kaya zaidi ya madafu 1, 0000, 0000, 0000 na ushei.

Acha niwahi kwenye mazishi ya kaya.
Chanzo: Tanzania Daima Januari 25, 2012.

No comments: