Wednesday, 4 January 2012

Tumemaliza mwaka kwa kumalizwa

INGAWA kila mmoja, kwa wale waliobahatika kuumaliza mwaka 2011, ana furaha kuumaliza, ukweli ni kwamba: tumeumaliza kwa kumalizwa hasa kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Dk. Al Haj, Profesa and what not true and false, Mpayukaji nilikuwa na mpango wa kwenda kijijini kuhiji. Lakini nilishindwa kutokana na ughali wa maisha hasa kupanda kwa wese kiasi cha kuwapa kisingizio fisi watu wetu kupandisha nauli kiasi cha kutisha. Kilichonishangaza ni ile hali ya wenye madaraka kuwa bize na ulaji wao badala ya kushughulikia jinai hii ambapo wauza wese waliunda serikali ya kijambazi ndani ya kaya.

Ukiachia mbali ughali na ulanguzi wa wese uliotusababishia mateso makubwa akina yakhe kwa kuishi kwenye nchi yetu kama wapangaji na wakimbizi, kulikuwa na tatizo jingine kubwa tu.

Badala ya kutatua matatizo ya walevi, wahusika walipoteza pesa nyingi kujinoma na sherehe za miaka 500 ya udhuru walioupachika jina la uhuru. Mabilioni ya madafu yaliliwa kwa kisingizio cha adhimisho hili la aibu. Unawezaje kuadhimisha aibu ukajisifu kuwa nawe si mtoto riziki?

Kitu kingine kilichoupamba mwaka uliokwisha ni mafuriko ya kujitakia kutokana na uvunjaji wa sheria na miundo mbinu mbovu na kichwa ngumu nayo yaliongeza pigo kwa walevi. Wengi walisombwa na kuuawa na maji huku wengine wengi akiwamo mgosi Machungi kuishia kwenye makambi ya wakimbizi wa mafuriko wakipokea misaada utadhani waliistahiki.

Ajabu eti wajanja hawa wameisharejea mabaondeni tena wakidai kuwa hawako tayari kuhama! Yaani wao wanataka kila mwaka tupoteze pesa na muda kushughulikia matatizo ya kujitakia siyo? Iko wapi nguvu ya serikali hapa? Nenda kule kamata weka ndani na ikiwezekana tupa rupango wale wote watakaojifanya hawataki kuhama ili kulinda biashara zao za gongo na bwimbwi. Nini hasira nao hawa jamaa. Na bahati yao mie serikali yangu ni ya kijiweni tu.

Kwa vile nafasi haitoshi, sitachonga sana. Mwaka 2011 ulishuhudia vituko vya wakubwa hasa pale marafiki wa damu walipogeuziana kibao na kuvalishana magamba baada ya kuvuana nguo mchana kweupe. Jikumbushe kipute baina ya Ewassa na Njaa Kaya kule kwenye kamati ya NECK au shingo la chama kilichogeuka kiama.

Mwaka 2011 pia kujuana kulizidi kiasi cha makapi yaliyosusiwa na wapiga kula ya kura kudufiwa na kupewa ulaji kwenye vijiwe vya nje. Nani mara hii kawasahau akina Bat (Popo)ilda Kwaherini, Phil Mammal, Dolorous Kamaliza, Mwanatunu Mainzi, Stela Ma-tomatoes na makapi mengine mengi? Kuna watu wamekosa aibu. Yaani unawapelekea watu makapi halafu unajisifu!

Katika mwaka 2011 wakuu walizurura sana duniani kiasi cha kuitwa Vasco da Gama wa kizazi hiki. Wakati wenzenu wakizurura tena kwa kutumia njuluku zenu, mwenzenu nilisafiri kikazi kwenda Tunisia, Masri, Libya, Cote de Voire, Syria na Yemen kushuhudia maimla walivyokuwa wakifurushwa na kuadhibiwa kama vibaka kama ilivyotokea kwa Kashafi baada ya kumshauri akaniona hamnazo kama hawa ninao washauri kila siku wao wakaishia kunichukia na kutaka hata kunibambikizia kesi za uchochezi na uhaini. Mie sitaacha kusema.

Ufisiahadi ndiyo usiseme. Mwaka 2011, kama kawa, njuluku ziliendelea kuibiwa huku wahusika wakijifanya hamnazo wala hayawahusu. Nani mara hii kasahau ujambazi wa UDAR ambapo wahusika wanajulikana na bado wako kwenye ofisi za kijiwe wakitanua wakati walipaswa kwenda rupango?

Kama siyo kufikiri kwa masaburi wahusika wangeishafikishwa kwa pilato na kukatiwa mvua zao mchana kweupe. Lakini nani amfikishe nani kwa pilato wakati wote ni akina Yuda Iskarioti? Hivi kweli ni halali nyani kumuadhibu ngedere wakati wote mchezo wao ni uleule? Je, hawa wajinga wanaowafuga nyani nao kweli si nyani maradufu?

Mwaka 2011 haukuishiwa vituko. Huko mjengoni nako kulikera baada ya wezi waitwao wadharauliwa kujiongezea madafu ya makalio ilhali wakiwaacha walalanjaa wakihaha kufukuzia njuluku ili wasukume muda. Nani anawajali wananchi iwapo wananchi wanaowakilishwa na ngulu mbili hawa ni matumbo yao na nyumba zao ndogo? Nani awajali wafu wasiojijali? Je, hapa mwenye kosa ni nyani au hata wale wamleao kwa kumuengaenga wakati walipaswa kumfanyia kweli bila kumuangalia usoni kama walivyofanya walibya kwa Kashafi?

Tukija kijiweni, uchumi wa kijiwe ulizidi kuporomoka kutokana na kutokuwa na uongozi makini na wenye akili zaidi ya uroho na roho mbaya. Ila good news kwa waroho wenye uongo ngozi ni kwamba kipato chao kiliongezeka kutokana na kuwageuza walevi shamba la bibi nao wasifurukute.

Kwa taarifa za kijasusi nilizopata ni kwamba kaya ilizidisha umatonya kiasi cha kutaka kugeuzwa shoga na hao wanaotupa sarafu kwenye bakuli. Nasikia baada ya kwa Mulla Omar na Iraki, tunafuatia sisi kwa kumwagiwa njuluku ingawa hakuna la maana tunalofanyia hiyo pesa zaidi ya kurejeshwa ughaibuni kwa mlango wa nyuma kutokana na ujuha wetu.

Pia mwaka 2011 ulishuhudia watasha wakitaka kutu-cameron. Ingawa tulifaragua kukataa ushoga, je, sisi si mashoga kiuchumi? Maana, hiyo misaada tunayopewa inatokana na kodi za hao hao mashoga. Unakula pesa ya kiti moto halafu unasema huli kiti moto siyo? Ni utoto na ujuha kiasi gani? Mie nshasema. Mtu hata awe mtasha au nani akinijia na hoja zake za ushoga nachomoa panga langu na kumkatilia mbali kwa kumtenganisha kichwa na kiwiliwili. Hata hivyo tujisute. Inakuwaje kaya yenye kila rasilimali kuwa kapuku kiasi cha mkuu wake kujisifia ujuha na uhodari wa kutembeza bakuli? Acha jamaa watudhalilishe. Maana tunajidhalilisha wenyewe.

Kuna kipindi najikuta ni kicheka kwa huzuni kutokana na kushuhudia ushoga wa kisiasa tunaofanya. Nani mara hii kasahau kwa mfano Madevu kuwekwa kule Zaainzibaa baada ya kumwaga damu za wafuasi wengi waliodhani anawapigania kumbe wasijue alikuwa anawatumia kufukuzia ulaji? Je, hawa nao si mashoga wa kisiasa kama yeye?

Lo! Kumbe ni mwaka mpya! Herini ya mwaka mpya wa bundi. Sii yuu.

Chanzo: Tanzania Daima Januari 4, 2012.

No comments: