The Chant of Savant

Saturday 24 October 2015

Ushauri kwa wapiga kura


  • ... , Dr John Magufuli for CCM and Mr Edward Lowassa for Chadema
            Leo ni moja ya siku inayowasumbua wengi. Kwani ni siku ambayo kura za watanzania zitaamua nani awe rais wao kwa miaka mitano ijayo. Hata hivyo, ukipita mitaani unaweza kutabiri kirahisi nani ataibuka mshindi. Katika siku hii ambayo ni muhimu sana –si kwa wapiga kura tu –bali watanzania wote, nitoe ushauri wa mwisho. Katika kipindi chote cha kampeni –katika makala zangu –nimejitahidi kumfagilia yeyote kati ya wagombea.
Naweza kusema kuwa rais mtarajiwa anajulikana kutokana na maongezi vijiweni, maofisini, kwenye vyombo vya usafiri hata majumbani. Pamoja na rais kujulikana, ngoja nami niongeze sauti yangu leo kupitia nafasi hii. Yafuatayo ni mambo ya kuzingatia katika kupiga kura.
Mosi, mpiga kura lazima aangalie mgombea anayekidhi matarajio yake na si kwa maneno bali hata matendo yake binafsi. Hapa lazima kuangalia historia ya mgombea. Nasema hili kutokana na psychology iliyojitokeza ambapo watu wanasema wako tayari hata kuchagua shetani hata jiwe ilmradi wakiondoe chama tawala. Sidhani kama mawazo ya namna hii ni sahihi na yanajenga.
Pili , wapiga kura watafakari kwa makini kauli mbinu iliyotawala yaani, mabadiliko. Wajue kuwa mabadiliko yanaweza kuwa hasi hata chanya na bado yakaitwa mabadiliko. Hivyo, tunapoongelea mabadiliko tujikite kwenye mabadiliko chanya na si mabadiliko hatari ya kubadili vya na kuweka watu wasiofaa. Mfano, wapo wanaoona kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hakifai kwa vile ndicho kimesimamia uoza uliopo. Ni kweli, je mgombea binafsi ameshirikje? Hili ni swali muhimu kutokana na ukweli kuwa wagombea wanaoonekana kuwa tishio ambao mmojawao atakuwa rais yaani Dk John Pombe Magufuli na Edward Lowassa, wamezaliwa, kulelewa na kukulia CCM hata kama mmojawapo ameijiunga na upinzani kwenye dakika za mwisho tokana na kuamini kuwa hakutendewa haki. Hivyo, Magufuli na Lowassa hawawezi kukwepa lawama au pongezi tokana na matendo na rekodi za CCM kiutendaji.
Tatu, wapo wanaojinasibisha na marehemu baba wa taifa , Mwl Julius Nyerere aliyewahi kusema kuwa watanzania wanataka mabadiliko. Na wakiyakosa ndani ya chama watayatafuta nje yake. Hata hivyo, wanashindwa au wanakwepa kuendelea na wosia huu adhimu wa mwalimu. Kwani katika wosia huu alimalizia kwa kusema kuwa bado CCM ndicho chama ambacho kilikuwa kinafaa. Nadhani, alichosema mwalimu ni kwamba watanzania wanachukia na wamechoshwa na ufisadi. Hivyo, tunapotaka kutumia wosia wa mwalimu, tuwapime wagombea kwa kuangalia wanauchukia au kuushiriki vipi  ufisadi. Sidhani kama kuna mtu mwenye akili timamu anaweza kubisha kuwa wawili wanaoongoza katika kinyang’anyiro hiki ni watu wawili tofauti japo wote wanaungana kwenye historia zao na CCM. Sidhani kama watanzania watatumia mihemko na kukata tama wakachagua mtu wanayejua fika hana mpango na maslahi yao zaidi ya maslahi yake binafsi.
Nne, wapiga kura wanapaswa kutafakari na kudurusu mambo kama vile afya za wagombea, ahadi zao, historia zao  na  hata sera zao. Waepuke kufanya jambo la maana kama kumpata kiongozi kwa miaka mitano kuwa suala sawa na kwenda kununua nyanya. Kura zao zitaamua mustakabali wao na wa taifa kwa ujumla. Mfano, vyombo vya habari vyenye uthubutu vimelalamikia afya za baadhi ya wagombea. Nao kwa –ma kuogopa kumwaga mtama kwenye kuku wengi au kutokuwa na majibu –wameshindwa  kutoa utetezi. Hii maana yake ni kwamba lisemwalo lipo na kama halipo basi laja.
Tano, kwa vile mabadiliko yanayotakiwa ni yale yatakayowahakikishia watanzania kuwa kuna mwenye nia na uwezo wa kupambana na ufisadi, basi warejee kutafakari kauli za wagombea  hawa wawili juu ya kupambana na ufisadi. Watafakari usayansi na uwezekano wa ahadi za wahusika. Mfano, Dk Magufuli alisema ataunda tume au tuseme mahakama maalumu ya kushughulikia watuhumiwa wa ufisadi ambao rais anayeondoka aliwagwaya au kujifanya hasikii kutokana na sababu ajuazo. Lowassa amejitahidi kutogusia suala la ufisadi kabisa. Wapo wanaoona kuwa ameepuka kuingia malumbano juu ya tuhuma za uongo na za kweli vinavyomkabili. Pia, wapo wanaomkosoa kama mtu ambaye hawezi kupambana na ufisadi. Kimsingi,ni kwamba watanzania watakuwa wamepoteza fursa adimu –kama watazugwa na wakakubali ima kutokana na hongo au lugha tamu –wakamchagua mtu fisadi au hata mgonjwa.
Sita, wapiga kura waepuke ushabiki wa vyama. Kwani rais atakayechaguliwa atakuwa rais wa watanzania wote wakiwamo vya vyama pinzani na wale ambao walimnyima kura au kutopiga kura kabisa. Hivyo, tunapaswa kuweka utaifa wetu mbele kuliko vyama vyetu au mapenzi a kibubusa. Kinachopaswa kuzingatiwa ni ukweli kuwa rais akishachaguliwa,  hakuna mechanisms za kumuondoa hata aboronge namna gani hadi amalize miaka mitano. Hivyo, kuchagua rais si jambo la kubabaisha wala la kufanya maamuzi mepesi zaidi ya kujikita kwenye mambo ya msingi kama baadhi yalivyoainishwa hapo juu.
Tumalizie kwa kuwataka watanzania wawe makini wasije wakachagua mtu atakayewaingiza kwenye matatizo zaidi ya haya wanayotaka kuondoa. Tusisitize kuwa wasichague mtu wanayeshuku afya yake ina ugogoro au ambaye hata ithibati na ujasiri wa kuongelea, kukemea hata kupambana na ufisadi.
Wekeni kwenye makini .Tukutane wiki ijayo. Nawatakia uchaguzi wenye busara na wa amani. Amina.
Chanzo: Tanzania Daima Okt., 25, 2015.

No comments: