Saturday, 31 October 2015

Wadanganyika wote tumeshinda na tusherehekee basi

  • ... to be a close race between John Magufuli (left) and Edward Lowassa
Baada ya wadanganyika wote kushinda kwenye uchakachuaji uliopita –kama ilivyokuwa wakati wa kampeni –ni wakati wa kushangilia kwa pamoja. Naona yule anatikisa kichwa akidhani naongea kwa nguvu ya mupipi na bangi na si bongo. Ngoja basi niprove pwenti kwanini nayasema haya nisemayo.
            Nina sababu ya kushangilia sawa na wewe. Ngoja basi. Mbona hivyo lakini? Si ungoje nikukufikishe badili ya kuhemkwa hata kabla sijafanya vitu vyangu?
            Basi okey. Poa, ngoja ngoja huumiza matumbo. Ngoja nikupe dozi ya kwanini unapaswa kuja kushangilia nami.
            Mosi, kwanini tushisherehekee kwa kuonyesha ulimwengu mzima tulivyo kaya ya amani hata kama tunaumia? Nani alitegemea Chama Cha Mafwisadi kama watani wao wanavyokiita kupeta? Ngoja niulize kidogo. Je hapa mnailauma CCM au wapingaji wenye pupa mliofanya kosa kuamini longo longo zao wakati nao walikuwa wakitafuta ulaji? Ngoja nifafanue. Hivi mlitegemea kada wa CCM aishinde CCM akiwa kwenye upinzani? Nani aliwaroga nyie ambao hamkujua kuwa jamaa hakuondoka kule kwa hasira bali kuwakomesha viherehere waliokuwa wakimpakazia kaya nzima kuwa yeye ni fisadi? Wako wapi sasa baada ya kupwakia matapishi yao na kuweka heshima, imani na vyama vyao rehani wakichezea kwenye nyavu za jamaa na chata lake? Ngoja niulize kilevi. Kwanini wadanganyika ni wagumu wa kuisoma na kuilewa historia? Yaani mara hii mmesahau jinsi Lyatongolwa alivyoizamisha Eni Si Si ara Mageuko? Ajabu ya maajabu sijui kwa sababu ya umaimuna au uroho na upogo mmeruhusu Eddie Luwasha azamishe vyama vinne kwa mpigo! What a titanic blow dudes! Hayo ya wachovu na waroho wa maulaji tuwaachie wenyewe.
            Pwenti ya pili, kwanini tusisherehekee iwapo tumerejesha ngoma ile ile ili itufanyie mambo yale yale nasi tusifanye lolote kama ambavyo tumefanya kwa miaka zaidi ya thelathini? Juzi juzi walikuwa wakiuza wanyama hai, sasa ngoja muuzwe nyinyi wadanganyika kwa ujuha wenu wa kutegemea wasanii wa kisiasa wawakomboe. Mie simo. Hauzwi mlevi hapa.
            Pwenti ya tatu kwanini wote mnapaswa kusherehekea ni kwamba kuisha kwa kampeni na uchakachuaji ni jambo la kufurahia. Angalau sasa walevi wanaweza kwenda kupiga kazi kama zamani badala ya kutegemea kula dezo na kujazwa ahadi za akina Abunwas na makando kando yake. Nenda mkachape kazi wenzenu waanze kula. Kama mlishindwa kuuliza ni kwanini deni la kaya limeumka kwa haraka unadhani hawa mliowapa watashindwa kuhomola kwenye shamba hili la bibi?
            Pwenti ya nne ni kwamba japo wote tumeshinda, washinda wa zaidi ni wawili yaani Dokta Kanywaji Makufuli anayekwenda kuenjoy pale Magogoni na Eddie ambaye ushindi wake ni kwenye maeneo mawili yaani kushinda hata kabla ya kuingia kwenye debe kwa kuwachanganya UKAUA hadi wakaingia kwenye anga zake akawaua tena kwa mpigo. Kama nilivyoeleza ushindi wa pili ni kuwalazimisha mahasidi wake waliomvurugia ulaji hapo mwaka 2008 kwa kufichua ulaji wake na kuleta mswaada uliomfanya ateme uwaziri mnene. Ni ajabu kuwa wanasiasa wetu huwa hawana kumbukumbu. Kwanini hawakujiuliza swali lipi la:Jamaa atupende kwa lipi wakati sisi ndiyo tuliasisi maanguko yake?  Pamoja na mibangi na ulevi wangu, kama ningekuwa UKAUA jamaa wala asingenipata wala nisingejiingiza kichwa kichwa kudhani nimepata wakati nimepatikana. Ushindi wa jamaa huyu hauna kifani. Kwani jamaa walidhani watamtumia akaisha kuwatumia na kuwazika huku akiondoka akichekelea. Nashauri CCM wampe nishani ya mikakati. If anything, the dude is a guru in strategies so to speak. Sitatafsiri kwa leo kwa wale wasioumanya ung’eng’e tusameheane. Ningekuwa nimeishauweka ningeweza kutafsiri. We aliyekuwa ukizungusha kichwa sasa umeona mantiki ya kusema wote tumeshinda? Tuonane wiki ijayo.
Chanzo: Nipashe Okt., 31, 2015.

No comments: