Tuesday, 6 October 2015

Kijiwe chatuma wajumbe Bondeni kupinga ufisadi
            Baada ya wachovu wa Bondeni kwa mzee Madiba kulianzisha, Kijiwe kimeamua kuwaunga mkono kwa kuwateua Msomi Mkatatamaa, Mgosi Machungi na Mijjinga kwenda kuwapa tafu.
Kabla ya kufikia uamuzi huu, Mgosi ndiye aliyelianzisha, “Wagosi mnaonaje tikatuma wajumbe Bondeni kushiiki kwenye maandamano ya kupinga ufisi na ufisadi kwenye kaya ie?”
            Mijjinga anakamua mic, “Naunga mkono wazo hili la kimapinduzi mia kwa mia. Kwa vile wenzetu wanaishi kwa kutapeliwa kama sisi, lazima tuonyesha mshikamano hata kama jamaa wakati mwingine huwa hawana maana kwa kufanya mauaji ya kibaguzi.”
            Kapende anakwanyua mic, “Mie naona kama wasauzi hawastahili kuungwa mkono. Utawasaidia watashukuru lakini wakishapata wanakutolea mapanga na kudai  urejee kwenu kama walivyowafanyia ndugu zetu hivi karibuni jambo ambalo nitalilaani maisha yangu yote.”
            Msomi anaamua kutia guu, “Nakubaliana nawe kwa namna moja na kupingana nawe kwa namna nyingine. Kimsingi, kwenda kule siyo kwa ajili ya wasauzi tu bali kuwaonyesha wezi na mafisadi wetu kuwa tunaweza kufanya kweli kama walivyofanya wasauzi. Pia tunakwenda kule kujifunza jinsi walivyoorganize move nzima au vipi?”
            “Hapo nimekupata msomi wetu. Kama ni hivyo, hata mimi naweza kutia guu kule na kuonyesha makeke ili nitie tizi tayari kuwakabili mafisadi na majambazi wetu ambao kwa sasa wamehanikiza kutuahidi vinono tusijue wakishapata ulaji watatugeuza sisi vinono,” anajibu Kapende huku akibusu kombe lake la kahawa.
            Sofia Lion aka Kanungaembe anaamua kutia guu kwa chati, “Naona mnapoteza muda, fedha na mawazo. Yenu yamewashinda mnashobokea ya wenzenu. Nani si fisadi hapa au hajawahi kula fedha ya ufisadi?”
            “Da Sofi hebu tuombe radhi. Wewe ni wa kutuita watu wazima na wasafi mafisadi? Hebu thibitisha kama ambavyo huwa unawataka wengine wafanye,” anajibu mheshimiwa Bwege akionyesha wazi kukereka.
“Unataka ushahidi upi wakati ufisadi umekuwapo na hakuna tulichofanya kupambana nao. Hii maana yake ni kwamba tunaridhika na kufaidika nao vinginevyo tusingengoja kwenda kujifunza toka Bondeni. Unaweza binafsi ukawa hujawahi kula fedha ya kifisadi. Ila kimfumo umeishafanya hivyo hasa ikizingatiwa kuwa kwa sasa hakuna anayeuliza fedha inayomwagwa kwenye kampeni inatoka wapi na imepatikana vipi. Nadhani kaka yangu tumeelewana.” Sofi anajitetea kiasi cha kuonyesha kumshawishi kidogo mheshimiwa Bwege ambaye anakatua kashata yake na kukuna kichwa.
Alhaji Mpemba anaamua kutia guu baada ya kurejea kutoka Makka baada ya kunusurika kukanyagwa na kunyotelewa roho, “Yakhe ulivosema waweza kuwa na ukweli japo si kwa yote ulosema. Mie wallahi sioni ubaya kujifunza na kufanya kweeli kama wenzetu wa Bondeni. Nadhani walofanya wenzetu ni kutukumbusha kuwa tukishikamana twaweza. Hivo tusikatishane tamaa wala kuogopa kwenda kule kujifunza ati.”
Kanji anakula mic, “Mimi penda sana dugu yangu ya Sauzi. Veve kama najua ile Juma naibia vao, taunga kono yeye. Juma nachukua juluku najenge jumbani yake. Hii baya sana dugu yangu.”
“Kanji ni Zhuma siyo Juma. Unashindwa hata kutofautisha jina jepesi kama hili! Ukisikia majina kama Sibusiso Sibulele si utatukana bure?”    anachomekea Mbwamwitu.
“Hiyo Silele Sisiso gumu sana dugu yangu,” anajitetea Kanji na kuacha kijiwe kikiangua kicheko kwa ubukanyaji wake.
Mipawa anakula mic, “Ni kweli usemayo Kanji.  Heri ya Zuma anajenga kwao kuliko wetu wanaotoroshea nje na kutuacha maskini huku njuluku yetu ikifaidiwa na waswizi na wakameruni na wengineo kule majuu. Natamani tuwachome moto badala ya kupoteza muda kuandamana wakatuma ndata uchwara watunyotoe roho wakati nao wanaibiwa. Sijui ndata wetu wameingiliwa na kitu gani maana huko nyuma hawakuwa hivyo?”
Mzee Maneno naye anaamua kula mic baada ya kumeza kashata yake, “Heri kufa umesimama kuliko kufa umepiga magoti. Kwanini kuogopa kujaribu mbinu hizi na zile wakati mafisadi wanafanya hivyo kama vile kuhama magenge yao na kujiunga na mengine na kutaka wapewe ulaji watugugune zaidi kama inavyoendelea? Acha twendeni Bondeni hata lau tutanue kama Njaa Kaya ambaye miaka yote kwenye ulaji amefanya kazi kubwa mbili yaani kutanua ughaibuni na kuchomoa njukulu zetu na wezi wenzake.”
“Hiyo isikukondeshe. Kwani punde atajiunga na Ben Tunituni Makapi aliyependa sana kuzurura. Kimsingi, kosa wanalofanya ni kusahau kuwa cheo ni dhamana. Tambo zote zitaisha mwishoni mwa mwezi huu,” Msomi anaronga huku akibofya kisimu chake.
Mzee Maneno anachomekea, “Wana shida gani wakati wameishahomola?”
“Unadhani haya Makufuli hayatawafuna hawa jamaa kwa kufanya kosa kumuamini kuwa atawahifadhi kama walivyohifadhiana? Wangejua wakamuunga mkono Eddie huenda angewaonea huruma. Yangu macho mtanikumbuka watakapogeukana kwenye ndoa hii ya mashaka,” anachonga Kapende.
Mijjinga anampinga Kapende, “Sitegemei nyani kumfunga ngedere. Inaonekana unalewesha na hizi ahadi za kisanii anazotoa jamaa ukidhani ni mwenzako. Huyu ni mwenzao na si mwenzako ohooo! Ngoja aingie au apigwe chini utaniambia. Huyu kumbuka ni mwanasiasa. Sina imani na wanasiasa mwenzenu kusema ule ukweli. Ingekuwa amri yangu ningewataka wachovu wawabidilishe kama nepi kama wanavyobadili vyama.”

Kijiwe kikiwa kinanoga si akapita fisadi Jimmy Rugemalayer! Acha tumfukuze ili kumfanyia kitu mbaya.
Chanzo: Tanzania Daima Oktoba 7, 2015.

No comments: