Sunday, 18 October 2015

Wasanii ni wakereketwa au njaa na upogo?

Kampeni za uchaguzi mkuu zinazoendelea zimefichua uoza mkubwa sana hasa kuhusiana na tasnia ya sanaa hasa za maigizo. Japo ni haki ya wanasanaa kuchagua ni wapi pa kuuza huduma yao, kufanya hivyo lazima kuenende na maslahi ya taifa. Maana bila taifa hakuna wasanii wala wanasiasa au aina yoyote ya tasnia na nyanja. Katika kampeni zinazoelekea ukingoni, kumejitokeza “mapenzi” ya ajabu kwa chama tawala yaani Chama Cha Mapinduzi (CCM). Kwanini tunasema hivi? Msanii akikodiwa sawa na mwenye bodaboda au taxi kazi yake ni kumfikisha abiria wake aendako. Hiyo ndiyo kazi halali inayofanya apewe ujira.  Zaidi ya hapo ni kukiuka miiko na maadili ya kazi husika. Hetu tutoe mfano zaidi. Si kazi ya dereva wad ala dala au taxi au bodaboda kujenga uhusiano wa ndani na wateja wao zaidi ya ule wa kikazi. Hili ni takwa la aina yoyote ya kazi iwe ndogo au kubwa. Inashangaza kuona wasanii waliokodiwa kutumbuiza wakaishia kuhutubia mikutano ya siasa wakionyesha wazi kushambulia upande fulani huku wakiuhami upande mwingine. Hii si kufanya sanaa bali siasa kwa mgongo wa sanaa. Wasanii wa namna hii wanapaswa kuonywa na ikiwezekana kuchuliwa hatua. Kwanini iwe haramu, kwa mfano, viongozi wa kidini kuonyesha ushabiki wa siasa lakini iwe halali kwa wanasinii?
Juzi juzi tumewasikia baadhi ya wasanii wakilaani upinzani kana kwamba ni wapinzani wao. Hii siyo sawa. Msanii kama dereva wa daladala, bodaboda na taxi hapaswi kubagua wateja wake. Msanii ni sawa na barabara. Hapaswi kubagua magari. Hata rubani wa ndege –pamoja na hadhi ya nafasi yake –hawezi kuwabagua abiria wake. Je wasanii wanatenda jinai hii kwa jamii kutokana na uhaba wa elimu au makusudi mazima ili kujiweka karibu na chama chenye ulaji ili wapate ulaji? Tumewaona wengine wakigombea ubungu wa dezo na kubwagwa chini wakiishia kutoa nadhiri kuwa wao ni wanachama wa CCM hadi kufa.  Nadhani tatizo jingine hapa ni ile hali ya siasa kuwa biashara inayoingiza utajiri wa haraka bila kutoa jasho. Ndiyo maana wasanii, wanataaluma, wafanyabiashara hata wahalifu wanawania nafasi za kisiasa.  Kwa vile wanasanii sawa na wanajamii wowote wana haki ya kushiriki siasa, basi wavae kofia moja ya usanii au ya siasa lakini siyo kuchanganya. Kufanya hivyo si kutenda haki hata kidogo. 
Kinachogomba ni ile hali ya wasanii kufunga ndoa na chama tawala kwa sasa wakati ni chama kile kile kilichotelekeza maslahi yao hadi watu binafsi kama Msama Promotion walipoingilia kuwaokoa na wizi mkubwa wanaoendelea kufanyiwa na wafanyabiashara wa kihindi. Kwani hii ni siri? Ni ajabu kuwa wasanii hawa hawa wanaotumiwa nao wakajiachia kutumiwa kesho utawasikia wakilia serikali hawajali wakati wao hao hao ndiyo wametumiwa kuiingiza madarakani. Wapo wanaodhani kuwa kinachowasumbua baadhi ya wasanii ni njaa na uwezo mdogo wa kupembua mambo.  Msanii anapaswa kuwa kioo cha jamii. Anapogeuka kuwa dodoki la jamii kidogo inatia shaka na –kama sikosei –mhusika anaanza kuuzika usanii wake. Maana unapokubali kutumiwa kama msanii, basi ujue unaondoka kwenye mstari na kufanya vitu ambavyo vitawapendelea watu fulani na kuwaumiza wengine. Sambamba na wasanii wanaojirahisi na kujiruhusu kutumiwa ni waandishi wa habari nyemelezi almaaruf kanjanja. Nadhani kadhia ya waandishi wa habari sawa na wasanii kutumiwa kufanya kazi chafu za wanasiasa na vyama vya siasa zilianza hapo 2005 ambapo waandishi waliokuwa wakionekana nguli walitiwa mifukoni mwa wanasiasa fisadi waliokuwa wakiwania madaraka. Wapo waliofanikisha kazi hii chafu na hovyo na kulipwa fadhili. Kadhalika wapo wengi walioshia kutumiwa kama vyangudoa wasiambulie ujira wowote. Baada ya kumaliza kuwachafua na kuwadhalilisha waandishi wa habari, sasa wanasiasa wamewadandia wasanii ambao nao kwa upogo na ufinyu wa uoni wamejiachia na kujitoa kufanya kazi chafu ya wahusika kwa malipo uchwara yatakayowafanya wajione wamepata kwa sasa wasijue wanachouza ni cha thamani na cha muda mrefu kuliko hizo peremende na bakhshsh wanazopewa. Hawa kwa kiarabu huitwa muafinati kama ni wanawake au maufinini kama ni wanaume. Maana ya neno hili ni kwamba mhusika anayekuwa muafin au muafina hana tofauti na kinyesi kwa kero anayowasababishia wengine. Kwanini nasema ni kero wanayopata wenzake?  Taifa letu liko msambweni kwa sasa. Wasanii wanapotumia vipaji vyao kuwahadaa na kuwapotosha wananchi wanakuwa sawa na kinyesi. Kwani uoza na harufu na madhara ya nafasi yao itasimama kwa miaka mitano kuanzia sasa.
Hivyo, bila kusema mengi, tunashauri wasanii wanaotaka kuwa wanasiasa basi waachane na sanaa na kuwa wanasiasa kuliko kuwa wasanii-wanasiasa.  Pia wasanii wengi wafahamu kuwa si rahisi kupata ulaji wa dezo wa kisiasa kama vile ubunge iwe wa kuchaguliwa au kuteuliwa. Nafasi ni chache na zinataka watu walioiva kielimu na siyo umaarufu tu. Hivyo, badala ya kukubali na kujirahisi kutumiwa, wasanii wanapaswa wajikite kuwapima wagombea kubaini ni wapi wanaweza kuwaondolea kadhia zao hasa kudhalilishwa na kunyonywa.
Chanzo: Tanzania Daima Okt., 2015.

7 comments:

Anonymous said...

Well come to tanzania mwalimu wacha kula dezo huko

NN Mhango said...

Anon Asante sana sema si kwamba huku nakula dezo. Natumia vipawa na nguvu zangu kula na kukuza vitegemezi vyetu. Nitakuja wakati ukifika ingawa kwa sasa hakuna cha mno cha kupotezea mamilioni ya shilingi.

Anonymous said...

Mwalimu Mhango,

huyo Anon anaganzi ya akili hivyo ni ngumu kwake kufahamu nje ya Tanzania kuna nini haswa kinachoendelea wakati wa kupatia mkate wako kila siku mwalimu.

Sisi baadhi yetu tulionja kidogo hayo maisha halafu tukarejeshwa huku Motoni pasipo hiyari yetu sasa tunaelewa vizuri matatizo yetu yanasababishwa na uwezo wetu duni wa kufikiri.Na hata unaweza kuona sasa wasanii wanafikiri tatizo lao ni pesa pekee na kujaribu kutofautisha na uzalendo eti wamekodishwa kupiga kampeni za siasa.

Kwani wao wapo sayari tofauti. Hivi wanafahamu madhara ya kumpata mmbovu yatawagusa wao pia miaka mitano ijayo na kwa uharibifu utakafanyika wakati uongozi huo mbovu inaweza kuwa uharibifu utakaodumu kwa vizazi na vizazi vijavyo pasipokuwa rahisi kurekebisha huo uharibifu.

Anonymous said...


Salamu Mwalimu Mhango,
Sababu zote tatu ulizozitaja katika kichwa cha habari cha hawa wasanii za kuibuka na mapenzi kwa chama tawala zote ni sahii na zinafiti kutokana na wao walivyo.Mwalimu Mhango swala la siasa ni swala ambalo linalomgusa na linalomuhusu mwananchi wa kawaida mwenyewe moja kwa moja na kwa vile kuna vyama vinavyowawakilisha wananchi hao katika kuyaweka masilahi ya wananchi mbele kuliko masilahi yao binafsi na kwa bahati mbaya chama cha siasa cha CCM hatukuliona hilo tangu utawala wa awamu ya pili hadi hii ya nne.Na kwa kusema hivyo basi,wanasiasa wetu hususa wa chama cha CCM wamekuja na mbinu ya kuwatumia wasanii katika kampeni zao za kisiasa kana kwamba wasanii hao ni wanachama wa chama chao cha CCM,na hapa ndipo swali la kujiuliza,je ni kweli kwamba wasanii hao wote waliokodiwa na kutumiwa na CCM ni wananchama wa CCM?Kama jibu likiwa kwamba ni wananchama wa CCM mimi hapa naona hakuna haja ya mjadala kwani watakuwa wanatekeleza haki yao ya kupigania kukufikisha chama chao katika madaraka kama atavyokuwa mwananchi yoyote yule mwachama wa CCM amabaye sio msanii.Lakini sidhani na nina uhakika kwamba sio wasanii wote waliokodiwa na CCM ni wanachama wa CCM,bali kuna baadhi yao sio wananchama wa chama hicho na wala hawatokuwa tayari kuwapa kura zao CCM lakini kwa vile ni wasanii na kwa sababu ya njaa yao na upogo wao kwa sababu zote ulizozifafanua tunakuta kwamba wamepoteza maadili na sifa sahii za jukumu la usanii hapa tukiwaondoa wale wasanii wakereketwa ambao watakuwa wanajulikana katika chama chao na hata kuelekwa mbele ya wananchi kwamba ni wanachama wa CCM kwa hawa sio kesi yetu.
Lakini kwa wasanii wenye njaa na wenye upogo kweli inakuwa ni usaliti kwa mashabiki wao na usaliti kwa wananchi na usaliti kwa usanii wenyewe ambao una maadili yake na una dhamana kubwa mbele ya jamii ambao wanatakiwa wawe dira na muongozo na watibabu wa maradhi ya kijamii,na kwa maoni yangu walitakiwa wawe kama viongozi wa dini ambao hawatakiwi kujihusisha kabisa na siasa isipokuwa pale tu kweli watakapoona wanajiamini na wanastahiki kujiunga katika siasa kama wanasiasa kwa vile wana kadhia ya kuipigania kwamasilahi ya wananchi na ya nchi na sio kama alivyojiingiza msanii mmoja katika siasa kwa kuwawakilisha wananchi(ubunge) akiwa na kadhia ya kuwapigania wasanii bungeni kana kwamba wananchi anaowawakilisha wa jimbo lake ni wasanii wenzie!!!
Inaendelea........

Anonymous said...


Mwalimu Mhanhgo,hapa kuna haja ya kujiuliza kwa nini mapenzi haya ya wasanii yawe makubwa kwa chama cha CCM?kwa kujibu swali hili kama utakumbuka Mwalimu Mhango uliandika makala yako ya "Nitakavyomkubuka Kikwete"na kuoredhesha yale ambayo utakayomkubuka katika utawala wake,kuna hili kwa maoni yangu ambalo ndio sababu ya wasanii kuikumbatia CCM kama chama chao nalo ni kwamba Kikwete anazingatiwa kama Rais ambaye amewaiinua na kuwasapoti wasanii wa Tanzania,na wasanii karibu wote wanakubaliana kwa hilo na utawasikia wakimsifia kwa hilo.Mimi kwa muono wangu nimekuwa nikijiuliza kwa lipi alilowasapoti?kana kwamba usanii umeanza katika utawala wa Kikwete?Je ni kutokana na kuhudhuria mazishi ya wasanii?Au je kuwaita wasanii watumia madawa ya kulevya Ikulu?Au je kupiga nao picha za hadarani na wasanii hao?au hata kuwaalika wasanii wa Kimarekani na kukutana nao Ikulu?Je hiyo ndio sapoti kwao na ndio kuwainua kisanii?

Na ikumbukwe tu kwamba Kikwete ni mwanasiasa kama mwanasiasa yoyote yule anaekuja kwa zama zake,na zama zake ni zama za kuabudiwa mashujaa wa kila aina kuanzia wanamichezo wasanii na hata waonyesha mavazi (models) hata kama mashujaa hao wana ufisadi wote wa kijamii na hata kukosa kuwa kiigizo bora kwajamii,Kikwete alilijua na aliliona hilo kama mwanasiasa na kuona kwamba litamsaidia katika umashuhuri rahisi katika utawala wake kwa hiyo akajiweka kimbelembele mpaka kufikia kuchafua haiba yake kama Rais wa nchi.Sasa kwa wasanii wa Tanzania wamemuona hivyo na wamemshukuru kwa hilo na ili kumfadhili ndio wakamfanyia tafrija ya kumuaga na kuamua kukikumbatia chama chake kwa kuamini kwamba uwenda atakeyekuja madarkani kupitia chama chake atakuwa ni kama msanii mwenzi wao Kikwete.Na hata tumemsikia mgombea wa CCM akiwaahidi kwamba atawafanya matajiri kama wasanii wa kimarekani,kwa viigizo gani?mimi sijui.

Mwalimu Mhango UKEREKETWA,NJAA NA UPOGO ndio sababu za kimsingi ya mapenzi hayo ya chama tawala.Ingekuwa vyema wasanii hao wangewajibika kila wanapokodishwa na kualikwa katika burudani zingine za kijamii kuliko kujiiadhirisha mbele ya jamii kwa njaa yao upogo wao na ukereketwa wao kwa kujifichia mwamvuli wa kisiasa cha kuhuzunisha zaidi ni kwamba wale wasanii ambao wanayaona maovu ya wanasiasa kwa kuidhalilisha nchi na wananchi na wakayakemea hayo ndio kwanza wanapigwa vita na kupigwa marufuku kwa nyimbo zao kusikika maridioni au hata kutosikika kabisa!

NN Mhango said...

Anon umenifumbua macho kuwa "njaa upogo na ukereketwa" vimewamotisha wasanii kuiunga mkono CCM ukiachia mbali kuhadaiwa kuwa Kikwete aliwapenda wakati aliwatumia. Kwa vile wasanii wengi wamo kwenye fani kutafuta tonge, sitashangaa tena. Hili la Kikwete kujitia kimbelembele kutafuta umaarufu umeniacha hoi na swali lako kuwa kama kweli Kikwete amewakomboa au kuwatumia nalo limenifikirisha. Mimi niliandika kama kuwaonya waangalie nafasi yao kijamii kama wasanii. Sijaona models kwenye sanaa zaidi ya wengi kupwakia siasa baada ya kuona Mr II ameukwaa ubunge wasijue alijiandaa muda mrefu. Nangoja kuona wasanii wangapi wataukwaa kama mwenzao au kuishia kubwagwa kama mmojawapo aliyetaka kupitia ubunge wa dezo akabwagwa na kuendelea kujikomba akidhani huenda atateuliwa. Kwa nimjuavyo Magufuli, sijui kama ana nafasi ya usanii zaidi ya kufanya kweli. Nasema Magufuli kwa vile amegombea na kiza hivyo lazima ashinde.
Nakukaribisha na kukushukuru kwa michango yako yenye mashiko siku zote. Karibu tena.

NN Mhango said...

Anon21 October 2015 at 01:13 nakushukuru sana kwa kumfikishia ujumbe Anon mwenzako ambaye hajui maisha yalivyo huku ukilinganisha na Bongo ambako wengi wangetamani lau watoke wakapumzike kwa muda kutokana na machungu kama mgao wa umeme, misongamano, ukosefu wa usalama, msongamano, chuki, ufisadi, umaskini, dhuluma, ubabaishaji, na mengine mengi. Ni bahati mbaya mimi sina connection wala nia ya kujiingiza kwenye siasa za kilafi zinazoendelea huko. Hivyo, kuja huko ni sawa na kujitia kitanzi. Hata ningeamua kuja kwenye sabbatical najua sitafaa kutokana na mifumo na miundombinu mibovu mashuleni na vyuoni. Pia naamini ninayoweza kufundisha yanaweza kuwakwaza hata watawala. Hivyo, heri niendelee hapa kuchapa kazi na kufanya mambo mengine.