Sunday, 1 November 2015

Magufuli: Kupambana na ufisadi anza na Kikwete

  • Tanzania ruling party names candidate for Oct. elections - Breitbart
Wahenga walinena: Jasiri haachi asili. Hapa jasiri ninayemuongelea si mwingine bali rais Jakaya Kikwete ambaye kuingia kwake madarakani kunasemekana kuwezeshwa na fedha ya wizi wa mabilioni ya Mfuko wa Madeni ya nje (EPA). Tokana na wizi kuasisiwa na kuhusishwa na wakubwa, hakuna aliyewajibishwa wala kulazimika kutoa maelezo hasa wakubwa husika walipotajwa wazi wazi. Rejea kukiri kwa mwanasheria Michael Bhindika aliyesimamia uhamishaji wa fedha husika ambaye aliwataja Benjamin Mkapa rais mstaafu, Philip Mangula (Makamu mwenyekiti wa CCM), Jakaya Kikwete rais anayeondoka na wengine wengi akiwemo kada maarufu wa CCM Rostam Aziz ambaye kampuni yake ya Kagoda ilitumika kuchotea fedha husika.
            Punde alipoingia madarakani, Kikwete hakuacha asili. Aliasisi kashfa nyingine ya mabilioni ya Richmond ambayo iliondoka na mabilioni ya wananchi huku ikijirudufu na kuzaa kampuni nyingine ya Dowan ambayo inaendelea kuwakamua watanzania mabilioni. Kwa mara nyingine, Kikwete na Aziz walihusishwa moja kwa moja kabla ya kumtoa sadaka swahiba na waziri wake mkuu, Edward Lowassa hapo mwaka 2008.
            Funga mzigo ya Kikwete ni kashfa ambayo anaondoka huku akiiacha ikiwa mbichi. Hii si nyingine ni kashfa ya Escrow ambapo maafisa wa ngazi za juu wa serikali ya Kikwete wakiwamo mawaziri wakishirikiana na  matapeli na majizi makubwa waliweza kuiibia serikali kwa kile walichosema ni kulipa kampuni iliyoingia nchini kinyemela chini ya uangalizi wa Kikwete ambaye anahusika moja kwa moja kwa vile ndiye alikuwa waziri wa wizara husika.
            Kama siyo kulindana na kuogopana, rais John Pombe Magufuli –aliyeahidi umma wakati wa kampeni zake za kugombea urais kuwa angewashughulikia mafisadi ambao alisema ni kikundi kidogo cha watu –basi angeanza na Jakaya Mrisho Kikwete na wenzake wanaojulikana. Na Magufuli hawezi kusema hawajui. Anawajua vizuri sana kwa sura na majina hata miradi yao ya kijambazi. Kama Magufuli atamgwaya mtangulizi wake ataishia kuonekana muongo na msanii kama wasanii wengine walioahidi wananchi Maisha Bora kwa Wote wakaishia kuwaibia na kuwasababishia maisha mabovu.
            Kikwete anapaswa kushughulikiwa vilivyo kwenye vita ya kupambana na ufisadi kutokana na kuhusishwa na ufisadi wa kutishwa katika kashfa tatu zilionyeshwa hapo juu. Pia Kikwete ana ushahidi mwingi kuhusiana na ujambazi, ufisadi na biashara haramu ya mihadarati. Rejea kukiri kwake kuwa ana orodha za majambazi, mafisadi na wauza mihadarati lakini asiwashughulikie kutokana na sababu anazojua mwenyewe.
            Ukiachia mbali Kikwete, kama Magufuli atatimiza ahadi zake –hasa hii ya kupambana na ufisadi –hata akina Mkapa na Ali Hassan Mwinyi hawatapona hasa ikizingatiwa kuna kashfa nyingi waliasisi na kushiriki kama vile kashfa ya kuuza mbuga yetu na kuua wanyama wetu kule Loliondo chini ya Mwinyi. Mkapa –ukiachia mbali EPA –anahusika na kashfa ya uuzaji wa kifisadi wa iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), na ubinafsishaji mwingine uliogeuka kuwa mzigo kwa taifa na wizi wa mali ya umma hasa Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira ambao Mkapa alijitwalia yeye na familia yake. Pia mke wa Mkapa Anna, hatanusurika hasa kama kampuni yake ya Fursa Sawa kwa Wote ilivyotumia mgongo wa Ikulu kuliibia taifa. Sambamba na Anna ni Salma Kikwete ambaye naye kampuni yake ya Wanawake na Maendeleo imetumia mgongo wa ikulu kuliibia taifa na kulitia aibu.
            Hata zile nyumba za umma anazotuhumiwa kusimamia kuziuza Magufuli, anaweza kumtwisha Mkapa mzigo wake na kumchunguza ili kujitenga na uchafu huu na kutooenekana kama anawaogoopa wahusika kwa vile alishirikiana nao. Hapa bila shaka Edward Lowassa aliyekuwa mpinzani wa Magufuli hatanusurika hasa ikizingatiwa kuwa anajua mengi kuhusiana na Richmond ukiachia mbali kuwahi kuweka hatiani na Kamati Teule ya Bunge kwa kashfa hii naye akakiri na kuachia uwaziri mkuu.
            Japo ni mapema kuhukumu, wahenga husema: Kusema ni jambo moja na kutenda ni jambo jingine. Je Magufuli ambaye alimlaumu Kikwete wazi wazi jukwaani huku Kikwete mwenyewe akiwapo atakubali kuwa rais wa aina ya Kikwete ambaye wengi walimjua kama msanii na mtu anayeahidi bila kutimiza? Je Magufuli atawashangaza wengi hata wale waliomuunga mkono wakitegemea awalinde? Je Magufuli atawaangusha hawa wachache na kutowaangusha umma aliouahidi mara nyingi kuwa hatauangusha? Je Magufuli atajipiga mtama? Je Magufuli ataibadili CCM au CCM itambadili? Je Magufuli atausafisha mfumo au mfumo utamchafua? Maswali ni mengi kuliko majibu.
            Kitakachompa changamoto Magufuli ni ukweli kuwa kashfa hizi si mpya. Karibu watanzania walio wengi –hasa wafuatiliaji wa mambo –wanazijua kwa undani hata saa nyingine kuliko tulivyozieleza tokana na jinsi zilivyowaathiri na wengine walivyoona zikisukwa na kutekelezwa kiasi cha kuiba siri zake na kuzivujisha kwa upinzani na vyombo vya habari.
            Kwa vile Magufuli ameahidi mambo mengi yanayohitaji fedha nyingi, ni wakati muafaka kumkumbusha kuwa bila kuwashughulikia mafisadi papa na kuwafilisi ili kuwazuia kuendelea kuliibia taifa na kupata mtaji wa kukamilisha ahadi zake, atajikuta muda ukimpita kiasi cha kujikuta akiwa mwanachama wa kundi aliloahidi kupambana nalo ili kuwakwamua watanzania. Wakati wa kupambana na ufisadi ni sasa.
Chanzo: Tanzania Daima Nov. 1, 2015.

2 comments:

Mbele said...

Umeandika ujumbe muhimu, kweli, bila upendeleo. Mfumo huu uliopo ni kama nyoka, na wahenga walisema ukitaka kumwua nyoka, mpige kichwani.

Rais Kikwete amekuwa kinara wa mfumo huu, kinara wa kuwalea na kuwakingia kifua mafisadi. Kuna wakati zilipovuma sana habari za wizi mkubwa wa hela benki, Rais Kikwete alitutangazia kwamba orodha ya wevi wale anayo, na kwamba amewaambia warudishe hela kimya kimya.

Hapo Rais Kikwete alifanya kosa kubwa kwa makusudi. Alipaswa kuwachukulia wevi hao hatua za kisheria. Kwa kitendo alichofanya ameweka mfano tangulizi, ambao kwa ki-Ingereza huitwa "precedent." Ikitokea watu wengine wakaiba huko benki halafu wachukuliwe hatua za kisheria, watakuwa na msingi wa kudai waachwe warudishe hela kimya kimya.

Kwa hivyo, kama serikali ijayo ina mkakati wa dhati wa kushughulikia ufisadi, sherti ianzie kwa kupiga kichwani.

NN Mhango said...

Ndugu Mbele nakubaliana nawe kwa kukubaliana na pendekezo langu. Kama kweli Magufuli ana jipya basi si jingine bali kuanzia kichwani. Nilimsikia juzi akiikosoa CCM na kumpongeza Kikwete kuwa ana moyo wa pekee kuachia madaraka wakati hafanyihivyo kwa utashi wake bali sheria (katiba). Sitaki niseme mengi. Ila ninavyomuona Magufuli -kama hataanza na Kikwete-atakachokuwa anafanya si kingine bali kuwa kikaragosi cha akina Mwinyi, Mkapa na Kikwete. Huwezi kuanza na matawi katika kuung'oa mbuyu ukaanza na matawi bila kuchimbua mizizi kwanza. Kwa vile ni mapema, tunangoja kuona atakavyoanza kazi hii ambayo iliwashinda wengi. Laiti hata angeanzia kwa kumtaka Kikwete atoe ushahidi aliosema anao kuhusiana na majivi na mafisadi ambao wengi ni marafiki zake. Tungetaka aende mbele na kuwakamata wauza unga na majambazi wanaojulikana kukifahdili CCM kama vile Alex Massawe ambaye alitajwa wazi wazi bila kuchukuliwa hatua.