The Chant of Savant

Tuesday 17 November 2015

Kijiwe champongeza na kumshauri Magufuli


            Baada ya kuapishwa na kuingia kazini kwa gea kubwa, kijiwe kimempongeza tena rahis Kanywaji Makufuli na kumtaka akaze buti zaidi. Kijiwe leo kinakaa kuangazia machache ambayo ndugu rahis ameishafanya.
            Kapende anaingia na kuamkua na kulianzisha, “Waheshimiwa wanakijiwe, hemu nipe tathmini yenu kuhusiana na utendaji wa ndugu rahis ambaye naona kama ameanza kwa kasi ya kuridhisha.”
            Mijjinga anakwanyua mic, “Kwangu ni mapema kutoa tathmini hasa ikizingatiwa kuwa rahis ni mwanasiasa tena anayetekeleza sera za chata fisadi na chovu lililopaswa kuondoka kama si wapingaji kujipinga kwa kulala kitanda kimoja na fisadi.”
            “Mie naona ameanza uzuri wallahi. Maana anivovamia maofisi na kuwatia jambajamba wazembe na wasaka tonge lau yatia moja kwa kuanzia,” anajibu Mpemba huku akikatua kashata yake.
            Mgosi Machungi anakula mic, “Mie naona kama anajichosha sana. Sijui kama mtu mmoja ataweza kuzunguka maofisi yote na kuwatia hiyo jamba jamba wabangaizaji waiojazana kwenye kaya yetu. Tinamshaui aunde mfumo unaojiendesha wa kuweza kuwabaini na kuwashughuikia wazembe makazini.”
            Mipawa anakula mic, “Nakuunga mkono Mgosi. Kaya ni kubwa na mtu mmoja hawezi kufua dafu. Huwezi kutegemea uchapaji kazi wa maana kwa kutegemea mtu mmoja zaidi ya mfumo. Nadhani kama rais anamaanisha anachofanya, kitu cha kwanza ni kuangalia mianya ya uzembe, ufisadi, rushwa na kuiziba kwanza halafu atunge sheria na kuhakikisha zinafanya kazi. Simpo.”
            Msomi Mkatatamaa aliyekuwa akisoma gazeti la Newsweek analiweka mezani na linakoswa wa kulichangamkia tokana na kuandikwa kwa Kikameruni. Anakula mic, “Kimsingi rahis ameonyesha njia ingawa kwa namna ambayo –huko tuendako –haitakuwa na tija. Hakuna haja ya kujenga nidhamu ya woga. Tunapaswa kuwa na mfumo unaojenga nidhamu ya uwajibikaji ambapo kila mmoja wetu anatimiza wajibu wake. Ningeshauri rahis akae ofisini atulie. Afanye utafiti na uchunguzi wa mambo yaliyoifikisha kaya hapa hasa suala zima na ufisadi, kulindana, kujuana, kulipana fadhila na mambo mengine kama haya.” Anapiga chafya na kuendelea, “Kama ningekuwa rahis au mshauri wake, kwanza ningempa orodha ya watendaji walioteuliwa kwa kujuana na kulipana fadhila kama vile Miingo Rweyependekeza, Po Makondae, Hamosi Makala, Alima Dendengu na wengine wanaojulikana kupewa ubalozi, ukuu wa wilaya na mikoa na ujaji kwa sababu tu ni washikaji wa rahis aliyepita au washikaji wa bi Mkubwa wake. Kwa kufanya hivi, rahis atakuwa ameonyesha asivyotaka mchezo na yeyote.”
            Kabla ya kuendelea, Mzee Maneno anamchomekea, “Hapo Msomi umegusa penyewe. Juzi jamaa yangu wa usalama wa Kaya ameniambia kuwa hao uliowataja na wengine sasa wako matumbo joto. Nasikia baada ya kumtimua Salva Rweyependekeza, wengi wa aina yake hawalali. Wengine nasikia wanatumia muda mwingi Bwagamoyo ili kuroga wasiondolewe kwenye ulaji na ujambazi wao.”
            “Watu wengine kwa umbeya, wewe umewaona au ni rongorongo ya kutaka kufurahisha kijiwe? Kama aliyewateua alitumia mamlaka yake, nani wewe kuhoji uteuzi wao?” anafoka Da Sofia Lion aka Kaunungaembe.
            Mijjinga hamkawizi, “Da Sofi nao umezidi kutetea uoza. Ungejua tabia kama hizi ndizo zinatukwamisha kama kaya wala usingetetea upuuzi huu da yangu.”
            Kanji naye anakatua mic, “Da Sofi kweli fanya kosa sana. Hiwi veve iko jua vatu kama Konda na wengine Somi najataka nakula juluku ya umma bure? Kama nasema iko kama haiko iko nakuja dada yangu. Lazima rahis fukuza vao na teua vatu iko na udhu bwana.” Kijiwe kinashangaa jinsi Kanji anavyomkaanga mshikaji wake.
            Mheshimiwa Bwege anakula mic, “Nina shaka na staili ya Dk Kanywaji ya kutawala. Hivi alishatangaza utajiri wake? Je anangoja nini? Kama alivyosema  Dk Mgosi ni kwamba mtu mmoja hawezi kuleta nidhamu ya utendaji kazi uliotukuka. Naungana na wanaotaka abadili mfumo uliopo. Ngoja niongeze pwenti nyingine. Rahis,  kwanza aondoe Taasisi ya Kulinda na Kupamba Rushwa (TAKOKURU) chini ya ofisi yake. Pili aisuke upya kwa kuipa kazi upya. Ili ifanye kazi bila kutumia fursa kujitajirisha kama ilivyo, polisi wapewe mamlaka ya kuichunguza TAKOKURU kama ilivyo na mamlaka ya kuwachunguza. Pia usalama wa Kaya iundwe upya na kuzichunguza taasisi hizi mbili huku nazo zikiichunguza. Kila mmoja amchunguze mwenzie. Napendekeza hili ili kuondoa kujuana na kushirikiana katika jinai.”
            Tokana na pwenti kali alizotoa mheshimwa Bwege, Msomi anarejea kukazia maarifa, “Kwanza muongezee kahawa mheshimiwa Bwege. Ametoa mchango wa nguvu ambao lazima umfikie rahis ili aufanyie kazi.”
            Kabla ya kuendelea Mbwamwitu anachomekea, “Mshauri rahis Kanywaji amteua mheshimwa Bwege mbunge halafu waziri aone kijiwe kitakavyomsaidia kuendesha kaya mchakamchaka.”
            Msomi anaendelea, “Kwanza namkaribisha rahis hapa kijiweni aje akutane na madaktari wenzake tumpe uzoefu na mikakati ya kuendesha kaya hii. Nadhani kuunda taasisi nyingi zinazochunguzana ni jambo la msingi sana. Pia niongezee kwa kushauri wanakaya wapewe haki na uhuru kisheria kuchunguzana na kuzichunguza taasisi husika. Hapa kweli itakuwa kazi tu.”

            Tukiwa hatuna hili wala lile si rahis Kanywaji alishuka kwenye shangingi lake na kuja kunywa kahawa nasi! Tuonane wiki ijayo insh’Allah.
Tanzania Daima: Nov.,18, 2015.

No comments: