Saturday, 7 November 2015

Wapiga kura waliikataa CCM UKAWA wakairejesha            Uchaguzi mkuu umekwisha. Walioshinda wameshinda na walioshindwa wameshindwa.  Hata hivi haina maana kuwa wale wanaodhani hawakutendewa haki wasiende mahakamani. Kwa umma wa watanzania, wamemaliza kazi yao kwa kutekeleza haki yao ya kikatiba. Kilichobaki ni kusonga mbele katika ujenzi wa taifa. Pamoja na kuwepo kasoro za hapa na pale –ambazo, kimsingi, haziepukiki –tunaweza kusema uchaguzi ulikwenda vizuri kwa amani na utulivu.
            Kama kichwa cha habari kisemacho, ni kwamba wapiga kura walidhamiria kukiondoa madarakani Chama Cha Mapinduzi (CCM). Hata hivyo, Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) –ambao umeachana na katiba ya wananchi –umeirejesha CCM madarakani ima kwa bahati mbaya au kwa maksudi. Makala hii inalenga kueleza sababu za kudai kuwa UKAWA wameirejesha madarakani CCM baada ya wapiga kura kuitosa. Nazo ni kama ifuatavyo:
Mosi, UKAWA walifanya kosa kubwa kwa kushindwa kusoma kile ambacho waingereza huiita Realpolitik yaani siasa za msimu au za wakati fulani za Tanzania. Tunaweza kusema kuwa walichoshindwa kuelewa UKAWA ni kwamba hapakuwa na jambo lolote au mtikisiko ambavyo vingebadili misimamo ya wapiga kura au kufanya waichukie CCM sana kiasi cha kuweza kumchagua yeyote aliyesimama kuipinga. Ni kwamba hapakuwa na vitu kama vile kuzorota sana kwa uchumi, ukame, baada la njaa au balaa lolote ambalo lingeonyesha kushindwa kwa CCM.
Waliishaichoka CCM ila hawakuwa na chaguo.
            Kwa walio wengi tofauti baina ya rais John Maguli na waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa ni majina lakini ni makada wale wale wa chama kile kile sema mmoja hakuwa na mawaa wala historia yenye kughubikwa na wingu la uchafu na ufisadi.
            Kosa la pili ni ile hali ya kumleta Lowassa na kumfanya mgombea wa UKAWA. Lowassa hakuwa akiuzika kutokana na historia yake.  CCM walitumia fursa hii kuwazidi UKAWA kwa kumwita kapi na asiyefaa ukiachia mbali kudai kuwa alihonga mabilioni kwenye mchakato na ana majumba nje.
 Tatu, ilikuwa ni UKAWA kutokuwa na hoja za kuweza kuwashawishi wapiga kura’ kimsingi, UKAWA hawakuwa na hoja baada ya kuizika hoja ile iliyowafanya maarufu ya kufichua na kupambana na rushwa. Hii ilionekana kama kujipiga mtama, ugeugeu, kutoaminika, uchumiatumbo na hata ubabaishaji wa kawaida. Nani angewaamini watu wasioaminika madaraka makubwa ya kuongoza nchi huku wakiwa na watuhumiwa wakubwa wa ufisadi. Wasingefanya kosa kuwaachia amali za taifa watu kama hawa. Sijui kwanini wasomi kama maprofesa Safari na Baregu au mchumi mkongwe Edwin Mtei hawakuliona hili?
            Sababu ya tatu ni ile hali ya Lowassa kuwa bubu akionyesha wazi kushindwa kujenga hoja wala kumilki jukwaa. Mara nyingi alikuwa akiongea kwa muda mfupi huku akiwaachia akina Fredrick Sumaye na Freeman Mbowe waongee kwa muda mrefu utadhani wao ndiyo walikuwa wagombea. Ilifikia mahali hadi watu wakaanza kushuku afya yake kutokana na hali hii. Wapo waliodhani ima Lowassa ni mgonjwa au aliogopa kuongea sana ili asiwakumbushe wapiga kura madhambi yake ambayo kimsingi, yaliibuliw ana UKAWA hawa hawa hasa walipotoa orodha ya mafisadi papa pale Mwembe Yanga mwaka 2007. Laiti Lowassa angetumia fursa hii kupangua na kukana tuhuma nyingi za ufisadi na wizi wa mabilioni mojawapo ikiwemo kashfa ya Richmond, huenda angeweza kuwapata wapiga kura wengi. Ni bahati mbaya kuwa –kwa sababu azijuazo binafsi –Lowassa hakufanya hivyo jambo ambalo lilizidi kupoteza uwezekano wake kuchaguliwa kuwa rais.
            Sababu ya nne ni ile hali ya CCM kumteua Magufuli ambaye anasifika kwa uchapakazi wake akilinganishwa na mawaziri wa serikali liyopita. Pia Magufuli hakuwa na kashfa nyingi ikilinganishwa na Lowassa ukiacha ile hali ya kusakamwa kuwa ni mwana CCM na pia alihusika kwenye utwaliwaji wa nyumba za umma chini ya utawala wa awamu ya tatu jambo ambalo, kimsingi, linapaswa kuelekezwa kwa Benjamin Mkapa.
            Hata kwa upande wa visiwani hali ni ile ile hasa pale chama kilichotegemewa sana cha Civic United Front (CUF) kilipoteza umaarufu, imani na ushawishi kilipofunga ndoa , kwanza, na CCM kwenye serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU) na pili na vyama vingine kuunda UKAWA. Nadhani wapiga kura wa visiwani wanazijua vizuri siasa za bara hasa ujio wa Lowassa na mizigo yake ya tuhuma. Hivyo, athari za Lowassa zimeweza kuathiri sehemu mbili za muungano ukiachia mbali kuwa hata namba ya CUF kushinda visiwani ni suala la mjadala hasa tukiangalia wafuasi, wanachama na mashabiki wake kwenye visiwa viwili vya Pemba na Zanzibar na historia zao. Kwa waliotegemea kufanya mabadiliko kujikuta wana wagombea wale wala na siasa zile ni vigumu kuwashawishi. Mfano ni kuondoka kwa Profesa Ibrahim Lipumba ambaye –si haba –ana wafuasi wengi visiwani. Sababu nyingine ni kuchoshwa kwa mgombea Seif Sharrif Hamad. Alipaswa kupisha nguvu na sura mpya kama vile Haji Duni ambaye alimtuma CHADEMA asifue dafu.
            Kwa ujumla ni kwamba UKAWA walishindwa kupambana na nguvu za ushawishi na umakini kimkakati wa CCM hasa kwa kuondoka kwenye kile walichokisimamia kwa miaka yote. Hivyo, hawana haja ya kulaumu wala kulalamika bali wajilaumu wenyewe kwa kushindwa kuona mapungufu yao wenywe na ya wapinzani wao. Hata hivyo, tunawez a kusema kuwa, kama kutakuwa na upinzani wenye visheni, miaka kumi ijayo inatosha kuitupa nje CCM. Nalo hili linategemea na utendaji wa Magufuli.
Tanzania Daima Nov.. 8, 2015.

No comments: