The Chant of Savant

Sunday 11 October 2020

Elimu Sawa Ila Bweni Kwa Vidudu Hapana


Mwishoni mwa mwezi jana, taifa letu lilipata msiba mkubwa. Ni msiba uliohusisha watoto 10 huko Kyerwa, mkoani Kagera ambapo wahanga waliungua baada ya bweni la shule ya Kiislamu ya Byamungu. Natoa salamu za rambirambi kwa wafiwa na taifa kwa ujumla. Pamoja na ukubwa wa msiba huu, kama jamii na taifa, kuna mambo tunayopaswa kujifunza kuepuka kurudia makosa kama watu wenye akili na uwezo wa kujifunza hata kufundisha. Hivyo, leo safu hii itaangalia masomo tunayoweza kupata tokana na msiba huu. Pia tutaangalia baadhi ya mapungufu yaliyofichuliwa na msiba huu katika maandalizi ya watoto wetu.  Yafuatayo ni mambo muhimu kuzingatia
        Mosi, elimu ni ufunguo wa maisha. Hivyo, kila mzazi anajitahidi kuhakikisha anampa mtoto wake urithi bora–––yaani elimu–––ili kumsaidia katika maisha yake ya baadaye. Hata hivyo, kuna angalizo hapa. Je ni wakati gani mzazi anapaswa kuanza kumpa mtoto elimu na katika mazingira gani? Jibu ni rahisi kuwa anapofikia umri wa kuelewa mafundisho.  Je ni katika mazingira gani?
        Pili, tukizingatia umri wa wahanga,  kwa mujibu wa gazeti la Habarileo (Septemba 18, 2020), wahanga walikuwa wa umri kati ya miaka6 na 10, je, kwa mfumo wetu kuruhusu shule za msingi za bweni siyo mapungufu ambayo–––ukiachia mbali maafa ya moto ambayo yanaweza kumtokea yoyote–––yanaweza kusababisha maafa mengine kama vile udhalilishaji, ukosefu wa malezi ya wazazi hata kupoteza haki ya kufaidi utoto wao kwa watoto? Je hapa mzazi anapaswa kuangalia umuhimu wa elimu au wa mtoto kuelelewa naye kama sehemu ya haki na kanuni ya malezi ya kiafrika. Nitatoa mfano mzuri kuhusiana na malezi ya kiafrika tofauti na jamii nyingine. Sisi tangu tuishi hapa Kanada–––pamoja na utaratibu wa kupeleka watoto wachanga kwenye vituo vya kuangalia watoto (Day Cares)–––kwa sababu huku hakuna uwezekano wa kuwa na wasichana wa kazi–––hatujawahi kupeleka watoto wetu huko. Hebu fikiria ubaguzi uliopo kati ya wazungu na waswahili. Hivi, ukimpeleka mtoto akadhalilishwa utamlaumu nani?
        Tatu, tunapoamua kuwapa watoto wetu elimu tuhakikishe tunafanya hivyo bila kuwapora haki nyingine kama vile kulelewa na wazazi wao. Nakumbuka kisa ambacho rafiki yangu alinitaarifu kuwa alikuwa akimtuma mtoto wake kwenye kusoma shule ya msingi nje ya nchi. Badala ya kufurahia na kumpongeza, nilikasirika na kumpa pole. Nilimuuliza swali moja tu. “Hivi mtoto wako akidhalilishwa safarini au shuleni utamlaumu nani?” Hii ilikuwa ni baada ya kumuuliza namna anavyomsafarisha mtoto huyo kwenda nchi jirani. Alijibu kuwa alikuwa amemwamini mtu mwingine kumpeleka. Hapa ndipo swali la uwezekano wa udhalilishaji lilivyoibuka. Kufupisha kisa hiki, jamaa alimrejesha mtoto wake nchini na kumsomeshea nyumbani. Je ni wazazi wangapi wanashindwa kuona haya kwa sababu ya kuangalia tu elimu na lengo zuri la kuitoa?
        Nne, je tunahitaji shule za bweni kweli au ni biashara ya kuuza elimu na huduma ya malazi ambayo kimsingi, kwa shule za msingi hahitajiki hata kidogo? Kwa wale waliosoma miaka ya 80 hadi 2000 ni mashahidi kuwa mambo ya shule za bweni za msingi hayakuwepo nchini. Ila baada ya kuja kwa uhuria wa kila kitu, kuna vitu tunavifanya bila kuzingatia hatari au madhara yake hasa kwenye dunia hii iliyobadilika sana.
        Bila kupendelea, nimetaja shule iliyohusika na mkasa si kwa kuichukia bali kuitumia kama mfano. Kama taifa, tunapaswa kutafakari upya namna tunavyotoa baadhi ya huduma. Tukianzia na elimu, sidhani kama ni busara kuwa na shule za msingi za bweni sawa na ambavyo si busara kuwa na mabaa na nyumba za chap chap karibu na shule ziwe za msingi hata sekondari.  Namini ustawi wa jamii watakuwa wamestuliwa na msiba tajwa kiasi cha kujiuliza kwanini hawakuliona hili. Kumtoa nyumbani kwa wazazi wake katika umri ambao anahitaji malezi yao ni kumdhulumu haki ya kulelewa na wazazi. Mtoto wa umri tajwa anahitaji malezi, mapenzi na usimamizi wa wazazi. Nje ya mada, ndiyo maana mtoto akilazwa hospitali, kitu cha kwanza ni kutakiwa kuwa na mtu wa kukaa naye tokana na utegemezi wake.
        Tumalizie. Tunaomba mamlaka husika na jamii kwa ujumla kuliangalia upya hii kadhia ya shule za bweni msingi. Tuonane wiki ijayo ambao tutaangalia harakati za uchaguzi.
       Kimsingi, msiba tajwa hapo juu umeibua kitu kimoja ambacho wazazi wengi–––ima kwa kupofushwa na malengo yao mazuri ya kuwapa elimu na kuwaandalia maisha ya badaye watoto wao-–––hushindwa kuona hatari ya baadhi ya namna elimu hii inavyotolewa. Mfano, wahanga walikuwa kwenye shule ya bweni ya msingi. Je ni busara kuacha watoto wa umri kati ya miaka 6 hadi 13 kupelekwa kwenye shule ya bweni wakati ndiyo wakati muafaka wa kupata malezi ya wazazi wao nyumbani? 
Chanzo: Nipashe Jumapili leo.

No comments: