The Chant of Savant

Saturday 24 October 2020

SOMO TOKA UPINZANI KUWA/KUTOKUWA UMOJA


Wiki mbili zilizopita, safu hii iliangazia namna wapiga kura watakavyochagua kwa kuzingatia baadhi ya mambo. Wiki hii tunawaangazia  wachaguliwa tukigusia udhaifu na ubora wa baadhi ya maamuzi yao. Hapa tutaangalia procedure zaidi ya sera.  Pamoja na ugumu na umuhimu  wake, uchaguzi wa mwaka huu ni rahisi kutabiri ni mambo gani yatakuwa turufu kimkakati kuliko chaguzi nyingine zilizopita. Leo, tutaangalia kwanini ni rahisi kunusa hali hali itakuwaje na sababu za kufanya hivyo. Pamoja na ukweli kuwa kushinda na kushindwa ni matukio tegemewa na ya kawaida, nani atashinda  au kushindwa siyo. Kufikia hitimisho wakati wa kuelekea kwenye kilele cha zoezi hili adhimu huhitaji ujuzi wa kuangalia viashiria wezeshi. Kwa kuzingatia sayansi hii, safu hii, leo, itaonyesha vitu vitakavyoamua ushindi. Mshindi atakuwa mmoja na watakoshindwa ni wengi. Hili halina utata. Kwa kuzingatia ukweli huu, zifuatazo ni sababu zinazonishawishi kusema bila hofu wala woga kuwa  vifuatavyo ni vigezo ambayo wagombea wanapaswa kuvinagalia kwa makini ili kushinda. Ieleweke kuwa hatulengi kupendelea au kuonea chama au kambi yoyote.
Yafuatayo ni matokeo ya sayansi ya uchambuzi wa masuala ya kijamii na kisiasa inayoweza kufanywa na yeyote mwenye utalaamu katika fani hii. Leo tutatoa faida zaidi kwa upinzani si kwa vile tuna ugomvi na wapinzani wao. La hasha. Ni kwa vile tuna marejeo ya chaguzi mbali mbali zilizopita nchini nje ya nchi.
        Mosi, bila upinzani kuungana na kuja na mgombea mmoja, kuna uwezekano hili likauathiri vibaya fursa ambayo washindani wao hawataichezea.  Hii ni kutokana ukweli kuwa umoja ni nguvu na utegano ni udhaifu. Hii halina mjadala. Hivyo, upinzani ungeliangalia hili kwa makini na kulishughulikia kabla ya siku ya kupiga kura. Siku zote, vita ya panzi ni neema ya kunguru. Kuwa na nguvu ya pamoja hakuna mjadala. Tofauti na uchaguzi wa mwaka 2015–––ambapo upinzani wenye ulisimamisha mgombea mmoja chini ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA)–––kipindi hiki, vyama vyenye ushawishi vimekuja kila mmoja na mgombea wa vyake. Huu ni udhaifu mkubwa ambao ni mtaji mkubwa kwa wapinzani wake. Ukiwa na washidani waliogawanyika, unashinda kirahisi. Hili halina ubishi hata kidogo.  Kwanini upinzani hautaki kuona hatari ya utengano huu. Kama kila mtu angesimamisha mtu wake mwaka 2015, Edward Lowassa, mgombea wa UKAWA–––asingeweza kufanya vizuri kama alivyofanya tena ndani ya muda mfupi–––aliweza kupata zaidi ya asilimia 40 tokana na muungano wa upinzani ambao kwa sasa haupo. Je hili nalo upinzani utamlaumu nani? Kwanini wana mikakati wa upinzani wameshindwa kuona jambo rahisi kama hili?  Kama upinzani utaungana, utawapa wapinzani wao kibarua cha ziada cha kupambana na hoja za pamoja badala ya sasa ambapo hata hoja zao zikipuuzwa hakuna madhara yatakayoonekana wazi wazi.
        Pili, upinzani kwa sasa una kazi ngumu kuibua sera mbadala za pamoja zingetosha kujibu zile za wapinzani wao. Hili nalo linahitaji umoja. Tutatoa mfano mmoja wa Afrika na dunia. Nchi nyingi za magharibi zimekuwa zikinyonya nchi za kiafrika kwa kufanya biashara na nchi moja moja badala ya pamoja. Zinatumia ukosefu wa umoja wa Afrika kuendelea kuinyonya.
        Tatu, ukiachia mbali ukosefu wa umoja, upinzani una kikwazo kingine kikubwa yaani kuosefu wa uzoefu ikilinganishwa na ule wapinzani wao ambao watatumia uzoefu wao kuwahenyesha kirahisi  kwa kupiga pale walipogawanyika pale utegano wao utakaposababisha waanze kugombea kushinda kura kwenye majimbo mbali mbali ambapo wangeweka mgombea mmoja wa upinzani. Kimsingi, hata kama upinzani siku zote umekuwa dhaifu, huu mgawanyiko utaudhoofisha zaidi kiasi cha kutofua dafu mbele  ya adui aliyeshikamana kuliko wakati wowote wa maisha yake ya miaka ya karibuni.
         Nne mbali na sababu tajwa hapo juu, kutokuungana kwa wapinzani hata kwa ajili ya uchaguzi tu, kunatoa nafasi kwa washindani wao kuwapa hali ngumu tokana na kuwa na mtandao mkubwa na mpana nchi nzima, ambao wapinzani hawana kama hawataungana. Hii ni mbali na kuwa na wanachama na wapiga kura wengi. Kuwa na matandao mkubwa ni jambo moja na kuufikia ni jambo jingine ukiachia mbali kuutumia. Wapinzani wangeungana na kugawana majimbo, nina hakika wangeweza kuwa na mtandao mpana nchi nzima na kuweza kuepuka ughali wa kusimamisha kila chama mtu wake.
        Mwisho, fedha zina nafasi kubwa katika uchaguzi wowote hasa kuwawezesha wagombea kuwafikia walengwa. Kwa upinzani ulioungana, hata kama hauna fedha nyingi kama washindani wake, lau ungepunguza maumivu kifedha. Upinzani unapaswa kujua kuwa mambo yote yaliyotajwa juu ni muhimu kuweza kushinda kwani bila kuyaweka sawa, wanaweza kuwasaidia washindani wao kuwashinda kirahisi. Tumalizie kwa kuwakumbusha namna nchi ya jirani ya Kenya wapinzani walivyofanikiwa kuangusha chama cha KANU kilichokuwa madarakani tangu uhuru tena kwa muungano wa kustukiza. Nchini Zambia kadhalika. Mifano ni mingi. Leo inatosha. Tuonane wiki ijayo.
Chanzo: Nipashe Jumapili.

No comments: