Friday, 10 April 2009

Futeni TFDA ndipo mpige marufuku Metakelfin


HIVI karibuni Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ilijitutumua kwa kupiga marufuku matumiza ya dawa aina ya Metalkefin, japo kwa muda na kwa sababu uchwara.

Kwa maelezo ya Mkurugenzi wa TFDA, Margreth Sigonda, ni kwamba kulingundulika kuwapo kwa dawa ambazo hazifikii viwango na ambazo hayakuidhinishwa na Mamlaka husika ukiachia mbali feki.

Alikaririwa akisema: ‘TFDA, kama taasisi ya serikali iliyopewa dhamana ya kulinda afya za wananchi kutokana na madhara yanayoweza kutokea kutokana na matumizi ya dawa hizo, inapenda kuutangazia umma kuwa imesitisha kwa muda uingizaji, usambazaji, uuzaji na matumizi ya dawa hiyo.’

Kauli hii ni tata. Kwani wahusika hawaelezi waliyagundua lini yakiwa yameishatumika nchini kwa muda gani. Pia kauli ya Sigonda haijali afya za watu ingawa anajigamba kuwa mamlaka yake inashughulikia afya za wananchi. Ingekuwa inajali basi ingeeleza nini fidia ya wale waliokwishaathirika.

Kwa mtu anayejua jinsi Chroloquine ilivyopigwa marufuku na yakaingizwa dawa kali yanayohitaji usimamizi wa daktari, anashangaa huruma hii na kujali vimetoka wapi na vilianza lini. Kuna haja ya kuambizana ukweli kuwa kila unapokaribia uchaguzi, wahusika hujidai kujionyesha kama wanawajali wananchi.

Kumekuwa na taarifa nyingi za watu kuathiriwa na madawa haya. Hakuna tamko wala hatua ya Mamlaka ukiachia mbali kimya na biashara kuendelea kama kawaida. Wataalamu wengi walihoji mantiki ya kuondoa dawa ya bei nafuu na yenye uhakika na kuingiza dawa kali na ghali. Nani alitoa jibu la maana zaidi ya kuendelea na business as usual?

Hili likichangiwa na ukondoo wa wananchi wetu, hakuna aliyelishupalia kuhakikisha balaa hili linaepukwa. Badala ya kuchukua hatua, wananchi walijiruhusu kuwa waathirika huku wakubwa wachache wakipata chumo lao kwa kuhatarisha afya za walalahoi. Wao wana hasara gani iwapo wakipata mafua wanachota kodi ya hao waathirika wao na kwenda Ulaya kutibiwa?

Hadi dawa zisizofikia viwango wala kuidhinishwa zinaingia, kusambazwa na kutumiwa nchini, Mamlaka zilikuwa wapi? Je, hawa si chanzo kikubwa cha kuingizwa dawa feki badala ya waingizaji?

Na kwa hali ilivyo, si Metakelfin tu. Kuna dawa mengi yanaingizwa Tanzania nchi inayochukuliwa kama haina mwenyewe. Mkurugenzi anaendelea kuchekesha. Alikaririwa akiwataka waliokwishanunua dawa hizi wazirejeshe walikozinunua ili uchunguzi ufuatie. Alisema: Baada ya kurudishwa kwa mwingizaji huyo, zitafanyiwa uchunguzi zaidi na hatua nyingine ikiwa ni pamoja na kuziharibu pale itakapothibitika kutokidhi viwango vya ubora na usalama.

Hivi hapa anayedanganywa ni nani? Kwa nchi yenye kutawaliwa na tamaa ya utajiri na ufisadi, hili haliwezekani. Kuna mifano mingi yenye kuthibitisha hili. Tumekuwa tukipigia kelele mihadarati ambayo wauzaji na watumiaji hata wasambazaji wanajulikana. Ni kigogo gani wa mihadarati amekamatwa zaidi ya ahadi tupu?

Kwa anayejua utajiri wanaopata wanaoagiza madawa haya, si rahisi dawa kuteketezwa zaidi ya kutoka chochote kitu na watu wakaendelea kuumia. Kwa nchi zilizoendelea, dawa na vyakula si vitu vya kuagizwa na kila mwenye fedha, bali Mamlaka maalumu tena baada ya kuzuru vitu hivi vinakotengenezwa na kuridhika na viwango na mazingira ya utengenezaji wake. Lakini kwa nchi zetu zinazoweza kuingia kila mikataba ya kipuuzi, hili si rahisi.

Kwa nchi ambayo taasisi zake hazijiwezi na kutawaliwa na tamaa ya kuchuma, usalama na afya ya jamii ni ndoto. Huwezi kuwa na dhamira ya kuwa na watu wenye afya njema huku ukizembea hadi madawa mabovu yakapita na kusambazwa. Hii ni kuwatumia wananchi kama viumbe wa kufanyia majaribio (guinea pig) kwa makampuni ya madawa.

Kinachozidi kudhihirisha uovyo wa mamlaka zetu ni ile hali ya kutoa tahadhari baada ya ajali. Kwa mfano, mkurugenzi ametoa viashiria vya kuzitambua dawa feki. Kwa nini havikutolewa kabla ya dawa kuingizwa na kusambazwa? Pia hata ukiangalia chanzo cha kuchukua hatua ni kutokana na taarifa ya raia mwema mmoja na si uchunguzi wa kisayansi.

Ni aibu kwa mamlaka yenye utitiri wa wafanyakazi wanaolipwa mshahara kila mwezi kushindwa kubaini upogo huu hadi raia mwema ajitolee kuwafanyia kazi zao. Je, hawa wanalipwa kwa kazi gani zaidi ya kulitia hasara taifa ukiachia mbali kuhatarisha afya yake? Je, huu si ushahidi tosha wa kuwawajibisha wahusika? Maana kwa maneno yao wameonyesha walivyo wazembe kiasi cha kuzidiwa na raia mwema.

Kwa hali ilivyo, Mtanzania wa kawaida ni kiumbe aliyeko hatarini kutoweka. Maana kila balaa linamwangalia yeye. Fedha yake inaibwa benki, tena Benki Kuu na hakuna anayechukuliwa hatua.

Uchaguzi unavurugwa na kuibiwa kwa kura lakini hakuna anayewajibishwa. Majambazi ndiyo usiseme, ukiachia mbali vibaka. Bado madereva wanaoendesha kwa kutumia leseni bandia na kuvunja kila sheria na kanuni barabarani wakikwepa kufungwa kwa kutoa chochote kwa matrafiki.

Ukiacha hawa wa chini, wapo watawala wanaoridhia mikataba michafu na ya kijambazi ukiachia mbali kuwa nyuma ya kila ufisadi. Hapa hujaongelea mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi na vikongwe ambapo serikali imeonyesha kushindwa vibaya sana hadi kutumia mbinu chafu za kukusanya maoni kana kwamba haina jeshi la polisi.

Tumalizie tulipoanzia. Anayepaswa kupigwa marufuku si dawa feki tu bali hata mamlaka iliyozembea kiasi cha kuruhusu usalama wa taifa kuwa hatarini kutokana na mbweha wachache wanaotaka kujitajirisha kwa kuhatarisha usalama wa raia.

Wanaohusika jiwajibisheni kabla ya kuwajibishwa.
Chanzo: Tanzania Daima Aprili 8, 2009.

No comments: