Thursday, 2 April 2009

Nasaha kwa walio kwenye kiza cha Iddilish


HAKUNA ubishi, ufisi na ufisadi vinaitawala kaya. Kila fisi anaweza kusema na kufanya atakavyo huku Njaa Kaya akiendelea kukenua na kuchekacheka utadhani hii halali.

Sikuamini maneno ya Iddiliish Rushdie yangetimia hata kabla ya vumbi kutua! Hivi hii kaya ni ya nani kati ya walevi na mafisi na mafisadi?

Tuliambiwa kaya haina ubia, kumbe walimaanisha kinyume! Ama kweli na hii ni sanaa? Hivi hawa wadudu wanajiamini nini iwapo uchafuzi wa uchaguzi ni kesho kesho? Je hizi ni dalili kuwa tutake tusitake lazima Njaa Kaya apete kama alivyopayuka Agwe Joni wa kwenye Machela?

Joni hujaacha uhuni! Mtu mzima hovyo. Umeishiwa sina hamu! Yaani umegeuzwa mtu wa kujikomba kama Kimdunge Ngumbaru Mwehu!

Harudi mtu bila kuiba kura hapa. Je, unafaidikaje na uchafu huu anaouita usafi? Au unaficha uchafu wako wa wakati wa Mzee Ruksa ulipokuwa umeingia ubia na gabacholi mmoja mkanunua migari kibao mkaishia kufwilisika mzee Ruksa alipoachia ngazi? Kwani hatujui?

Sasa tukubaliane. Walevi wanapaswa kuamka na kufa na mtu. Naona sasa wamezamishwa kwenye kiza ili mafisi yawagugune watakavyo huku wao wakiambulia kuijaza dunia tokana na kiza. Huku ni kutiana vidole kwenye macho. Huku ndiko kubaka kaya nisemako kila siku.

Ajabu, Njaa Kaya anaendelea kuwadanganya walevi, watapata maisha bora. Lini na vipi? Kwao maisha bora ni kuiba na kula bila kunawa tena kwa miguu na mikono kama tulivyoona pale Ubungu kwa mkewe Kimdunge Mwehu na kampuni lake la wizi.

Nasikia na kwenye kuegesha mikangafu na mashangigi yumo mama huyu mwenye tamaa kama Anna Tamaa wa Makapu na Salama Hatari Kikwekwe.

Mgao huo! Je, wanatufanyia hivi kwa vile wao hawakatiwi umeme au kwa vile kaya sasa haina mwenyewe na inaliwa kilevi na kijambazi kama alivyojisemea Kitime?

Napata kigugumizi ninapofikiria uchafuzi wa mwakani. Hivi kweli hata wakitoa takrima ya dhahabu na almas kweli tutafanya kosa tuwarejeshe watumalize kwenye ngwe ya lala salama kama Denjaman wa Makapu alivyotufanyia? Mpumbavu ni yule ang'atwaye na nyoka kwenye tundu moja au awekaye mayai kwenye kapu moja huku akipita karibu na vichaa.

Je ni upumbavu na hatari kiasi gani kwa mafala wanaouona umma wa walevi mafala kama wao?

Unajua kosa la walevi nini? Si waligomea kulala kitanda kimoja na mafwisadi akina Ewassa na Dowani yao? Ingawa Njaa Kaya anajionyesha kama anadhibiti mambo, hana kitu. Ni mweupe kama kichanga. Sijui kwa nini baba zima linatumiwa lisijue linatumiwa?

Baya zaidi, linaendelea kuchekea upuuzi huu! Natamani niamke na kwenda Ikuru nirirambe bakora au nilikabe hadi linonihino kwenye msuruali yake kabla ya kulidedisha.

Lakini hata hivyo tuambizane bila kuogopana. Mzee Musa alionya msiangalie uzuri kwani hamkuwa mkitafuta mchumba. Nyie mlimuona mzushi mkafakamia uzuri utadhani mlikuwa mkitafuta miss Bongolala. Sasa yamewakuta cheupe kageuka nuksi. Kawageukia kama paka apewapo maziwa halafu aliyempa akataka kuyadai.

Jamaa hana maana, kaalika kila aina ya mafisi na mbweha kuiguguna kaya! Yamezaliana na kujukuu huku umma wa walevi ukiangamia kwa ufakiri!

Halafu bila aibu na chembe ya woga yanasema eti na mwakani lazima yapete, piga ua sikubali, vinginevyo waninyotoe roho kabla sijanyotoa zao. Shenzi wakubwa nyie mafisi na mafisadi wa Njaa Kali Kaya.

Nimepania kuwakabili kwa kasi mpya, nguvu mpya na ari mpya hadi kinaeleweka. Hata kama wapingaji wenu nao ni hovyo kama wawapingao ukimuondoa kijogoo Silaha, mie siachi kuzoza hadi kieleweke.

Siwezi kuwekwa kinyumba kama akina Rweye wa Silva waliogeuzwa vyangu kwa sababu ya tumbo. Wapo wengi. Wamo akina Chazi Chazi, Pulinsi Bagende na wengine wengi. Shame on you!

Acha niwatukane king'eng'e na wafadhili wasikie. May you perish? Hata kama mnajiita wanaume, tunajua mlivyo mtoto si riziki. Tunajua mlivyo kama busati libebalo kila taka au nepi isafishayo kila uchafu.

Nikirejea kwa Idiliisha, kwanza nina usongo naye. Natamani ninywe damu yake au nimnyotoe roho kama wanavyowafanyia matupinkele.

Hivi Idiliisha uliyeishiwa, unadhani hii kaya ni mali ya mama yako au mabwana zako waliokuweka ndani? Mbona hujitetei kuhusiana na ujambazi wa feza ulizoficha majuu baada ya kutubamiza mkenge kwa kununua mrada uchwara?

Wewe ni mwizi hata kama umesoma na unaitwa mheshimiwa daktari wa kiza. Ukibaka kama Endelea Chenge, Eddy Ewassa, Rost Tamu l'Azizi, Denjamani na Anna Tamaa Makapu, Njaa Kaya na Salama Hatari Kikwekwe, Kimdunge Ngumbaru Mwehu, Abdillahi Vigoda, Bazee Pesatatu Miramba na mbweha wengine wajichao nyuma ya ukuu wakati ni vibaka.

Baada ya kuona vibaka wanavyochezea mali zetu, nina mpango wa kwenda kwa DJ, Andy Rajoelina ili kujifunza jinsi ya kuwatia adabu vinyama hawa laanifu. Gendaeka hawa wametugeuza shamba la bibi wao na wake zao!

Natamani kaya nzima ingekuwa Kanga kule Mbeya ili mawe yaseme au Ukuryani ambapo mafisi hawalaziwi damu. Natamani nisemayo yaandikwe kwa dhahabu na kukaririwa kwenye radio na runinga zote ili walevi wasikie sauti hii ya ukombozi ilengayo kuwatoa kwenye kiza cha Idiliiisha na Njaa Kaya.

Natamani roho wa yule kijana aliyemlamba kibao mzee Ruksa awaingie walevi watembeze vibao na vibano kwa kila kibaka wamjuaye na wamuonaye bila kujali ukubwa wa cheo chake.

Natamani kiza kiwe uamsho wa kujijua na kuchukua hatua mujarabu. Natamani vipofu waone, mabubu waseme, na viziwi wasikie huku kondoo wakigeuka simba na chui kuwararua mafisi watu.

Hakika natamani Mungu atie ubani kauli hii ili umma ujikomboe wakati huu kwa kutumia kisingizio cha kiza. Natamani kalamu na majembe viinuliwe kupinga ukuku wa kuzalisha usichokula na kula usichozalisha kama hayawani kuku.

Natamani lau jasho letu liwavimbishe hadi wapate pressure na kupasukia mbali au hata miwaya kwa vile nawajua walivyo vijogoo. Ee Mola, sikia kilio changu ambacho ni cha wajoli wako waliolewa ahadi na matumaini kiasi cha kuishi kwa matumaini kama waathirika wa miwaya.

Tusiendelee kufanya kosa kuwavumilia watu wasiotujali. Tusiwaheshimu watu wanaotudharau na kututumia kama mifugo. Wakati wa kuasi umefika. Na Kaya iasi maasi matakatifu. Hatuna cha kupoteza isipokuwa shida na mahangaiko na mateso yetu.

Haya shime mabibi na mabwana kazi kwenu. Kosa kubwa ni kuendelea kutenda kosa lile lile kila muhula. Na hapa tusimhusishe wala kumlaumu Mungu bali woga na utaahira wetu.

Busara ya leo, la kufa halina ubani na liwezekanalo leo lisingoje kesho. Mguswe wapi ndiyo msituke na kuchukia na kuchukua hatua?

Idiliisha, umeamua kutukomoa kwa kukataa ulafu na ufisi wenu?

Acha niishie kizani vibaka wanitoe roho.
Chanzo: Tanzania Daima Apr. 1, 2009.

No comments: