How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Friday, 10 April 2009

Kumbe bado tuna wahuni na vyangudoa wengi!



BAADA ya kuzidaka, nilikuwa nimeachana na kunywa kahawa. Nilikuwa nikilamba ulabu kwa sana. Kwa vile huu ni mwezi kona, nimejirejesha kwenye kijiwe kama Njaa Kaya anavyoanza kujirejesha kwa walevi akitetewa na vyangu na watu waliokwisha expire.

Leo nimetia timu usubuhi na mapema. Nimejiandaa kuwafunga kamba walevi wasijue nilikuwa nimepanda chati na kuwaacha solemba kama Njaa Kaya alivyokuwa amejichimbia na mafwisadi akina Kagoda na ANBEN.

Nikiwa nasoma gazeti la ‘Wambieni’ mara naona mpemba anaingia kwa usongo.

Anaanza. “Assalaam aleikum jamia?”

Tunaitikia mie na muuza kahawa. “Waleikum salaamatan”

Hazungushi. Anaanza kumwanga upupu. “Npayukaji umesikia hawa wapuuzi wanaojikomba kwa Njaa Kaya ili wagange njaa zao?”

Kabla ya kuendelea namjibu kwa mstuko. “Ami mbona sikuelewi. Nani wapuuzi hawa na wamefanya nini?”

Anajibu kwa usongo zaidi. “Yaani wenye kusoma magazeti wasoma ya udaku? Mboni wale eti vikongwe wastaafu wa Chama Cha Maangamizi wasema eti atayejitokeza kugombea uraisi wameapa kunhujumu?”

Wakati nikiwa namsikiliza kumbe Mgosi Machungi aliingia kimya kimya ili kunyaka mada. Anajibu. “Kumbe Ami unaongea hawa waganga njaa!”

Anageuka na kuniangalia na kusema. “Tisilaumiane. Hii habai bado ni mpya. Kwa ufupi ni kwamba ile mizee iliyokuwa wenyeviti wa nambari one imesema itamfanyia mizengo, aa soe, mizengwe atakayesimama kupambana na Njaa Kaya.”

“Ewaa Ngosi. Mie naona sasa CCM haina tofauti na Baraza la Mapinduzi ya mapanga la Unguujaa ambapo kiranja wake huteuliwa Dodoma na sie tukaishia kuuawa tunapojaribu kumpinga.”

Kabla sijajibu mara Makengeza ambaye naye aliingia kimya kimya anakwanyua mic. “Kwani hamkujua kuwa Kaya sasa imo mikononi mwa wahuni na mafisadi? Hamkuwasikia akina Joni wahuni wakisema kuwa lazima Njaa Kaya apete kwa vile ameitendea nchi mengi?

Kwao mema ni wao kushiba na familia zao na nchi ni matumbo yao na ya vimada wao! Hakuna alichofanya Njaa Kaya zaidi ya kuikabidhi Kaya kwa mafisadi wenzie. Bila sera, nia na mikakati ya kuendeleza Kaya haturudii makosa.”

Kuona watu wanazidi kukwanyua na kugombea mic bila kuomba ruksa kwa mkiti, nami naamua kutia guu kimtindo mtindo. “Hakuna haja kuwalaumu hawa vikongwe. Mbwa rafiki yake chatu. Unatarjia wafanye nini ili nao wafaidi matunda ya ufisadi zaidi ya kujikomba kwa kinara wake. Mwenye mlo hakosi wajukuu na isitoshe njaa inapohamia kwenye ubongo matokeo huwa kudhalilika hata kwa kujidhalilisha. Tunachopaswa kufanya ni kuuliza na kutathmini kazi ya Njaa Kaya ambaye hakuna alichofanya wala kutimiza.

Kama kwa kuiba kura atarudi. Lakini nalo linategemea na walevi watakavyomshupalia au kuufyata. Hapa wa kulaumiwa ni walevi si Njaa Kaya wala vyangu wake. Kama ataiba kura au kutoa za EPA wakanywea utamlaumu nani zaidi ya wao?”

Mzee Kidevu anavamia kwa usongo. “Hata kama mie mzee, tukubaliane. Wenzetu wanakosea kujiingiza kwenye uchangudoa na kujikomba huku hata kama kweli wana njaa. Ukiendekeza njaa unaweza kufanyiwa lolote.”

Mbwa Mwitu hajivungi. “Mzee Kidevu unaweza kufanyiwa lolote nini? Unataka kuniambia hawa wazee wanachofanya ni uchangu kweli?”

Kidevu. “Kwani uchangu siku hizi unachagua? Ni wa wote, wazee, vijana, wanawake na wanaume.”

Mgosi anachomekea. “Du mzee mwenzangu sikuwezi. Yaani timeishiwa hivi kiasi cha kuwa na wazee wasiotumia akili bali matamanio yao! Huko nyuma wazee waikuwa hawafanywi hivi. Sasa ona timekuwa wa hovyo hadi vijana wanatichapa! Natamani yule kijana aliyemuonea mzee Ruksa angewachapa hawa watu wazima hovyo wanaoishi kwa kujikomba na kujiuza kama peege.”

Mpemba anatania. “Yaani watakasema hawa wazee wantamani Njaa Kaya au yeye awatamani? Nakuunga nkono. Heri watokee watu wenye ujasiri wawachape kweli kweli. Hii jamani laana.”

Mbwa Mwitu anazidi kupigilia msumari. “Namna hii tutachapa wengi bila kujali ni wazee au vijana. Huwezi kutumia utumbo kufikiri badala ya ubongo ukawa salama. Laiti kidume Mchonga angefufuka.”

“Mchonga alionya akaondoka. Kazi ni kutumia nasaha zake mwakani ili kuwaonyesha hawa wapuuzi kuwa sie si wapuuzi kama wao. Lazima tuonyeshe dunia kuwa muda wa kuishi kama mbweha, kuku na fisi umekwisha. Huwezi kuacha Kaya iendelee kugugunwa na genge la majambazi huku tukiangalia. Lazima tufanye mapinduzi ya kifikira ili kuwakomesha hawa wahuni.” Alichomekea Kapende.

“Mie yote tisa. Nilishangaa kuona Agwe naye akisema! Yeye alipigwa kibuti na sasa ameona amalize muda wake kwa kujihonga kwa mafisadi. Huyu Joni Chilyagati hamshughulishi mtu. Huyu hana tofauti na chiriku apendaye kutumbuiza mabwana zake hata apaswapo kulia.” Alichomekea mzee Kidevu.

Mpemba leo kapania. Anakwanyua mic. “Mie naona sasa bara mtaanka. Sie Unguja tushakataa uchangudoa, ukuku na ufisi. Tulikuwa twakwamishwa nanyi. Kwa vile yamewafika na mshashikwa pabaya sasa naona chawezaeleweka.”

“Mpemba tiombe msamaha. Kushikwa pabaya ndiyo nini? Kwanini unatitukana jumla jumla hivi? Tiheshimiane tisiwe kama wale wazee wapuuzi.”

Mpemba anajitetea. “Yakhe mie sintukani ntu. Kama kutukana walowatukaneni ni hawa wanaowatafuna kama vibua na vyangudoa. Wale wanaochezewa mahape nchana.”

“Loo! Mpemba ndiyo unazidi kutuua kabisa. Yani tunaliwa kama Vyangudoa na vibua siyo?”

“Kwani siri? EPA, Richmonduli, Dowani, IPTL, ANBEN, Tanpower na CCM wanawafanya nini? Mwaliwa ndio. Kwani hamuendeshwi na wezi kijambazi?” Mpemba anajibu kwa kujiamini.

Nami nachomekea. “Msema kweli mpenzi wa Mungu hata achukiwe. Zamani wazee walikuwa chimbuchimbu ya hekima. Tangu walipojigeuza watoto wakafanya vitu vya hovyo hadi kuitwa watu wazima hovyo, huwezi kukwepa ukweli kuwa Kaya inaliwa hasa na mafisadi. Hivyo, Ami hajatukana bali kafikisha ujumbe na kalenga pale pale.”

“Loo! Yaani mmeng’ang’ania pale pale kama hawa wahuni watu wazima hovyo! Ni kweli jamii ya hovyo huzalisha utawala wa hovyo na wazee wa hovyo hata watoto wa hovyo.”

Tuangalie tusijezalisha wapiga kura wa hovyo wanaoweza kupwakia kila upuuzi. Busara ya leo: heri kufa mwili kuliko roho na akili. Ngoja niishie nikatafute bakora niwachape hawa wazee watu wazima hovyo.
Chanzo: Tanzania Daima Aprili 8, 2009.

No comments: