How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do
Thursday, 23 April 2009
Ni utukutu au utukufu unaohubiriwa na DECI?
JUZI nilijukuta kwenye hali mbaya baada ya kugundua kumbe hata mama watoto wangu naye aliingia kwenye mchezo wa kupanda fedha na kuvuna kilio kule Devil’s Entreprieses Conning Imbeciles (DECI)!
Unajua ilikuwaje! Baada ya kutoka kwa mgosi Machungi, nilimkuta bibi wa watu akiapa kwa miungu yote kufa na yule aliyepinda kwa kupiga marufuku upatu wa DECI. Bila kujua - najua huu wizi - ambao kitaalamu huitwa Ponzi Scheme, alidhani ningeungana naye kwenye upuuzi ule kama wale maaskofu waliojivua nguo kushabikia kamari wakati Bwana Yesu alipinga kwa nguvu zake zote pale alipowatimua wabadilisha pesa kwenye hekalu.Bila hili wala lile, alianza: “Mume wangu nashangaa!”
Nilijibu mshangao wake kwa kuuliza. “Laazizi unashangaa nini?”Alijibu: “Hili lisirikali lenu.”“Lisirikali letu? Uliniona lini humo?
Tuheshimiane mke wangu sijaishiwa kiasi hiki.”Alijitetea kwa kulazimisha tabasamu la kamba. “Hayo tuyaache. Wewe humo ingawa unaingia kwa vile wewe ni raia. Ila linatuonea. Mbona wao wanaiba EPA na kugawana sisi tukipata wafadhili wa kupanda na kuvuna pesa linawapiga marufuku?”
“Ahaa! Kumbe unazungumzia huu ujambazi wa DECI unaoungwa mkono na wahubiri utukutu wakisingizia utukufu!” Nilijibu huku nikijisogeza kukaa vizuri. Mke wangu alishangaa na kuhinika kusikia nasema DECI ni upuuzi na ujambazi asijue ni kweli!Alijitetea.
“Mbona mama Salama Kikwekwe, pale jirani amevuna sana kwenye upatu huu ingawa upatu wao si DECI bali MAWA?”
“Hukujua MAWA au Maulaji ya Wakubwa ni ulaji wa wakubwa!”
Nilimjibu huku nikianza kuonyesha kukereka kutokana na maswali yake mengi. Mke wangu hakujali kuudhika kwangu alizidi kuuliza. “Hivi mume wangu ungekuwa ujambazi ungeungwa mkono na maaskofu kweli?”“Swali lako la msingi. Hukusikia Yesu akisema si wote wasemao Bwana Bwana watauoana ufalme wa Mungu?”Nilikamua sigara kali yangu na kuendelea.
“Mbona Yesu alionya kuwa watakuja wengi kwa jina lake na watapoteza wengi? Kwani siku hizi kuna maaskofu au mahasikofu? Jitu linaibuka bila hata kusoma linajipachika uchungaji na uaskofu ili liwaibie na kuwararua kondoo wa Bwana, nanyi kichwa kichwa, mnaliamini!”Nakohoa kidogo na kuendelea.
“Yesu aliishi maisha ya kikapuku. Hakuwa na akaunti benki wala pajero hata kanisa. Leo mijitu inaishi peponi kwa kuwachuuza waumini fyongo halafu bado hamjastuka!”Mama Toboa aliendelea kuuliza. “Unataka kusema hawa maaskofu ni waganga njaa kama lisirikali?”“Haswa mke wangu. We jiulize Lisirikali lilikuwa wapi hadi watu wanaibiwa pesa yao?”Nilipopuliza moshi wa sigara kali na kumwingia mke wangu kisawa sawa alilalamika.
“Mume wangu nawe kwa kupenda sigara, unaonaje ukaizima tumalize maongezi haya?”Nilikupua moshi haraka haraka na kuzima kipisi changu na kuendelea kutoa elimu ya bure kwa nyina wana wangu. “Nakubali serikali ina makosa. Lakini wenye makosa ni wananchi kupwakia kila uchafu kwa lengo la kuvuna usipopanda. Tangu lini pesa ikapandwa kama maharagwe badala ya kuwekezwa?
Wenzenu walipanda kwenye ujinga wenu. Lisirikali mnalionea. Linaacha madini yakiibiwa likaenda kuombaomba nje!”
Nilikohoa kidogo na kuendelea. “Ulitabiriwa wakati wa wenye dhambi kupalilia makaburi ya mitume. Hukusikia juzi wasaliti fulani eti wakiadhimisha wiki ya kitaaluma ya Mwalimu mchonga wakati ni mafisi hao hao waliomsaliti na kuwatwisha watu wake mizigo?
Wao walisoma bure. Lakini wanawataka watoto wa makapuku walipie utadhani wazazi wao wanashiriki EPA, Richmonduli na ujambazi mwingine!”
Mke wangu aliuliza tena: “Unataka kuniambia hata hili kanisa letu la Roho Mtakatifu laweza kuwa la kitapeli kama mambo yenyewe ni hivi?”
Niliangua kicheko na kugaragara huku machozi yakinitoka na kusema “siku hizi hakuna cha roho mtakatifu bali roho mtakakitu. Wajanja wanahubiri utukutu, nyie mnajua ni utukufu. Hawa na Lisirikali la kisanii hawana tofauti. Unalipa kura linapata kula.
Na hawa mbwa mwitu aliotabiri Yesu, wanakuahidi uzima wa milele, kumbe uzimu wa milele mfukoni mwako! Hukusikia tapeli aliyekuwa akilaumu waumini kuwa wanamfanyiua ubahiri Mungu kwa kutotoa sadaka wakati lenyewe huwa halitoi hata ndururu?”
Mke wangu alianza kuingiwa na wasiwasi. “Unataka kuniambia tuliopanda pesa tutavuna vilio?”“Mvune vilio mara ngapi?” Nilijibu haraka.Mara tukiwa tunaendelea anaingia mgosi Machungi.
“Mgosi una habai kaka yangu ametitia hasara nyumbani?”“Hasara ipi” Namuuliza.Mgosi anajibu. “Kumbe aichukua ile pesa yetu ya kumaizia banda etu na kuwapa wezi wa DEKI!”
“DECI si DEKI.” Nilimkosoa.“Hiyo hiyo” alijibu na kuendelea. “Yote hii titamkaba yue shemeji yake aliyekuwa mwizi wa kuku kue Ushoto ambaye sasa ni askofu. Ndiye aimshaui apande pesa badaa ya mahaage.”
“Loo!” niliingilia haraka na kuendelea. “Hata shemegi yako hapa tulikuwa tukiongelea upogo huu.”
“Ameibiwa kiasi gani?”
“Aki saba mgosi. Sasa mke wake anataka taaka au tiende naye kwa shemeji yake atiipe kabla hatimjapiga mtu zongo.”“Mgosi zongo litampata askofu kweli? Niliuliza kwa utani.“Yule si askofu ni aspofu na msanii. Hana tofauti na yue aiekutwa na viungo vya mtu,” alijibu mgosi kwa hasira na kuendelea: “Hawa maasipofu wanachuuza roho za watu kutafuta pesa ya kula tu. Hawana tofauti na seekai inayojifanya kujai watu wakati iikaa kimya wajinga wake wakaibiwa.”
Mke wangu alimkata jicho la hasira asijue naye alikuwa muathirika wa upatu huu! Mgosi aliendelea. “Tangu dini ziivyogeuka duni siamini dini yoyote isipokuwa zie za mababu. Dini na seekai lao moja. Hawa wanatumia safai ya Kanani na wae wanatumia oho mtakakitu. Akini wanasema oho mtakatifu wakati wao ni wachafu!”
Nachomekea. “Watu wetu tusiwalaumu sana. Ogopa njaa ikipanda kichwani na watu wakaanza kutumia matumbo kufikiri badala ya vichwa. Si wananchi si watawala wote wametawaliwa na njaa ndiyo maana mambo hayaendi vizuri. Mie naona DECI wangejisajili kuwa chama cha siasa ili washinde uchaguzi wakavune Benki kuu walipovuna CCM kwenye EPA.”
Mazungumzo yakiwa yanaanza kunoga, mara anapita mkurugenzi mmoja wa DECI. Tunatoka mbio na mapanga kwenda kummaliza.
Tukirudi nitakusimulia.
Chanzo: Tanzania Daima Aprili 22, 2009.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment