UKIMUWEKA mwanaharamu kwenye chupa, atatoa kidole. Hii imejidhihirisha juzi kwenye mkutano wa kamati ya mipasuko ya ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), iliyoongozwa na rais mstaafu mzee Ali Hassan Mwinyi mjini Dodoma.
Wapo wanaohoji mantiki ya kamati ya Mwinyi kukutana na wabunge Dodoma, sambamba na kikao cha Bunge kujadili ripoti ya serikali juu ya utekelezaji maagizo ya kamati teule ya Bunge, iliyochunguza Richmond Development LLC.
Japo yaliyopita ni historia yenye kutia simanzi, kuua matumaini na kuiacha uchi CCM, serikali na rais Jakaya Kikwete, kuna mengi ya kujifunza kama tutaamua kuyadurusu vilivyo.
Hapa ndipo pongezi kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Utawala Bora na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), Sophia Simba zinachimbukako.
Tukubaliane. Japo Simba alitoka nje ya mstari kiasi cha kuitwa mjinga, mgonjwa wa akili na mpayukaji, kuna kila sababu za kumpongeza kuonyesha na kuutanua ufa ndani ya chama kilichotuhadaa kuwa ki makini na thabiti wakati sivyo.
Sina sababu za kuunga mkono madai ya Simba. Nakubaliana naye. CCM imejaa mafisadi kiasi cha kuamini kila kigogo wa CCM ni fisadi. Ndiyo. Alisema Mwalimu Nyerere ukiona chama kinaanza kutekwa na matajiri wenye kutia shaka ujue mambo yameharibika.
Zamani hatukuwa na wafanyabiashara kwenye safu za juu za chama kama ilivyo sasa. Majina ya matajiri yanatajika kwa kicho na wapenda dezo waliojazana chamani.
Kwanini nampongeza waziri Simba? Mosi, amemkumbusha bosi wake rais Kikwete kuwa ukimya wake si dhahabu bali adhabu. Maana si chama wala serikali yake, kila mtu anajipayukia atakavyo kana kwamba maneno ya hayati Horace Kolimba yanatimia, aliposema CCM imepoteza mwelekeo na dira.
Pili, Simba ameonyesha ujeuri wa ajabu, hata kusimamia vitu visivyoingia akilini, hasa aliposema kuwa waziri mkuu aliyezamishwa na kashfa ya Richmond, ambayo imegeuka muuaji wa CCM, Edward Lowassa, anaonewa wivu kwa sababu alichuma mali zamani.
Kitu kimoja tumsaidie na kumsahihisha Simba. Hivi kweli Lowassa anaonewa wivu? Tujalie ni hivyo. Je, watu, majina na udhu wao kama hayati Mwalimu Nyerere, aliyemtolea uvivu na kumtimua kwenye kugombea urais mwaka 1995, naye alikuwa akimuonea wivu kwa lipi?
Tatu, Simba si mnafiki wala hafichi msimamo wake. Japo ametuhumiwa kuwa na matatizo ya akili, anajua analofanya. Ingawa utetezi wake wa wazi wa mafisadi ni kinyume na kiapo chake, na maneno ya bosi wake (Kikwete), ameudhihirishia umma kuwa anaunga mkono mafisadi. Anapata faida gani? Jibu analo.
Ukiachia mbali kutoona aibu na kuchagua maneno yanayolingana na wadhifa wa uwaziri, nampongeza Simba kwa kufichua ubovu, upogo na ombwe la uongozi-niseme utawala. Maana siku hizi hatuna viongozi, bali watawala.
Inapofikia waziri na mwimbaji taarabu wakakosa mpaka, jua kuna tatizo, tena kubwa. Lakini kwanini tulilaumu panga ilhali mwenye kulitumia kakaa kimya? Kuna haja gani ya kumlaumu waziri Simba kusema hafai wakati Kikwete anamuona ni kifaa? Tuzidi kudodosa. Ina maana waziri Simba alikurupuka bila ya kuwapo mikakati nyuma ya pazia?
Haiwezekani. Ukitaka kujua namaanisha nini, jiulize kwanini Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ilitaka kuwahoji wabunge kabla ya wao kumaliza mfupa unaoonekana kumshinda fisi (serikali)?
Tusiishie hapa. Tuzidi kudurusu. Ni kwanini kamati ya Mwinyi, ikijua wazi ufinyu wa muda wa bunge na unyeti wa suala la Richmond, kwa makusudi mazima, ikaamua kuzidi kuupunguza muda kwa ku-bize wabunge, kama hakuna mikakati nyuma ya pazia?
Nikope maneno ya Arthur Koestler, "Bravo, the Wolves Devour each other- Hongera, mbwa mwitu wakitafunana wao kwa wao.”
Ingawa taifa limegeuka la wasahaulifu, la waziri Simba si rahisi kulisahau. Na kama tutafanya kosa hili, tujue tunajitia kitanzi wenyewe. Sitaki nionekane nawazushia Watanzania. Iko wapi kashfa ya akaunti ya madeni ya nje (EPA) na harakati chafu za TAKUKURU, kutaka kuzamisha hoja ya Richmond? Wako wapi watuhumiwa wa wazi wa Richmond na walioghushi, zaidi ya kuendelea kutugonganisha vichwa kama mataahira?
Kwa vile sera ya serikali ya Kikwete si kuwalinda mafisadi, basi mawaziri au watendaji wa serikali wenye uchungu nao au walioajiriwa nao wapaswa kuachia nyadhifa zao ili wawatetee mabwana zao vizuri.
Hapa ndipo nazidi kumpongeza Simba kwa kumtoa paka kwenye kofia. Kama Kikwete hana faida na machukizo tunayoona yakitendwa na kutamkwa na wateule wake, ana nini nao hadi asiwapumzishe?
Hivi hili linahitaji uwe mshauri wa rais kuliona na kulifanyia kazi? Je, kama Kikwete ni mkimya hivi, ana nini cha kutufanyia kiasi cha kutaka tumchague kwa ngwe ya pili iwapo ya kwanza inaonyesha kuwa hasara na ajali?
Tusiogopane. Ingawa tunaweza kuwalaumu akina Simba, tuna haja ya kuwapongeza kwa kuonyesha ubovu na uoza wa chama na serikali yao. Kwa wapenda maendeleo hili ni jambo la kupongezwa. Wezi wakianza kutoana makoo jua mwenye mali anasalimika.
Simba nampongeza pamoja na wenzake wanaotuhumiwa ufisadi kuzidi kuizika CCM, kwa kutaka kuokoa nafsi zao kosefu.
Nikope maneno ya spika wa Bunge. Huwezi kuwa na siasa za majitaka ukaleta maendeleo.Wala huwezi kutumia majitaka kumsafisha nguruwe.
Nimalizie na kumpongeza mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, aliyetaka achunguzwe na majaji ndipo aridhike ni mshirika na mwezeshaji wa Richmond na EPA. Msimamo wake ni mzuri japo unatia shaka.
Kama ameshindwa kuwaamini wabunge wenzake na kamati aliyoshiriki kuridhia iundwe, atawaamini majaji? Je, kama ameshindwa kuwaamini wawakilishi wa umma atawaamini wateule wa rais?
Msimamo wake ungekuwa mzuri zaidi kama asingekuwa na uswahiba na mamlaka. Pia ningemshauri aende mahakamani, kwa vile kuna majaji atatendewa haki na atawaamini. Hata hivyo, alikuwa wapi muda wote? Watamaliza waganga na ndwele haiondoki.
Chanzo: Mwanahalisi Nov. 19, 2009.
No comments:
Post a Comment