Tuesday, 24 November 2009

Ukishangaa ya Madevu na Karumekenge...

BAADA ya kushuhudia ngunguri na ngangari wakingungulana, sasa tunaambiwa pepo limefukuzwa na ubani. Sasa umefukizwa kiasi cha uzuri wa harufu ya marashi ya Pemba kurejea!

Upande wa pili tumefunguliwa macho na Mbunge Lucas Selelii kuwa kumbe kuna wenzetu pamoja na majina yao makubwa ni hovyo!

Hawa ni wale wanaojiita waandishi wa habari waandamizi waliogeuka waandishi wa habari wadandindizi na wapuuzi. Inakuwakuwaje mwandishi mzima, tena mwandamizi, unanunuliwa na mafisadi kufanya chafu yao?

Alisema Luca kuwa jamaa zangu wa kujishoo-shoo na kudoea bila kumsahau kasuku shangingi la kihaya, walinunuliwa na Richamondu kuitakasa wasifanikiwe.

Hapa ndipo kitendawili cha Njaa Kaya kutokuwa kwenye uchafu huu kinapofunguka. Kama hakushiriki amewezaje kumwajiri nyemelezi huyu kuwa msemaji wake in the first place?

Kweli wanasiasa na wasanii ni watu wa kuangaliwa kwa makini. Tapeli mmoja anaweza kuja akakuaminisha atakupeleka peponi kumbe anakupeleka motoni kama ilivyotokea walevi na jamaa yangu Njaa kaya na sasa shangingi Sylvia anayejifanya spika wa Njaa Kaya.

Nani alijua yule jamaa wa madevu na mwana wa mteule wangekaa jukwaa moja kwa bashasha na mashamsham bila kujali gemu lao liliumiza wengi?

Hayawi hayawi yamekuwa! Ule mzuka wa kipopobawa uliokuwa umevivamia vile visiwa viwili sasa umetulia na watu wanaweza kufanya madili yao bila bughudha.

Ila wakati usanii ukifanyika twapaswa kuzingatia. Waliofikia makubaliano si wanuka jasho bali walaji wachache wanaoendekeza libeneke ya usaliti na ufisi ndani ya ufisadi.

Nani alijua Rweyependekeza angelamba matapishi yake kwa kumuangukia Njaa Kaya na kujikabidhi atumiwe? Hili tumbo! Njaa nyingine bwana. Yaani jamaa kauza hata News Corp kwa tamaa za kijinga kiasi cha kujibinafsisha kwa mafisadi wanaomtumia kama nepi!

Ukishangaa ya Richamondu utaona ya mwafaka-siri. Ukishangaa ya Kagoda utaona ya Dowans. Na ukishangaa ya Rostitamu utaona ya Ewassa kama siyo Sofii!

Na yote kati ya yote ukishangaa ya Tunituni utaona ya Chekacheka. Ukishangaa ya Anae Tamaa Tunituni utaona ya Salama Shari Kikwekwe! Ni maajabu jabu jaabu jaabu tupu kwenye anga hili la Danganyika ya Tanzia.

Hata hivyo ieleweke wazi. Mzee mzima sina ugomvi na ndoa hii mpya iitwayo matambuano ingawa wenye chao wanaitilia shaka tena kubwa. Hayo ni mambo yao binafsi ingawa kuna masilahi ya umma.

Sitaki nionekane mnoko ingawa jamaa zangu hawa hawaaminiki. Hujamsikia Prof akisema wamecheza karata tatu na kujitia kitanzi kisiasa. Wazungu husema political risk.

Kwanini kujiingiza kwenye hatari hii ya kisiasa kama kweli hakuna ulaji binafsi nyuma yake? Mnakimbizwa na nini zaidi ya salata na njaa? Kwani hii ni mara ya tatu wakionyesha sanaa zao za kufunga ndoa na kuachana kila mtu akisema lake.

Tungoje tuone nani atamliza nani au kumtwisha mkenge ingawa ni wazi mwenye rungu atammaliza mwenye matumaini yasiyokuwepo.

Wakati tukiangalia upande wa wanandoa mashaka hawa, wapambe nao, hasa huyu mwingine, sijui kama watakubali kuingizwa kwenye mkenge huu.

Ingawa ndoa ni jambo la heri, nyingine ndoana. Unaweza kumkimbia mjusi ukajikuta kitanda kimoja na mamba si kenge. Tuyaache.

Kwanini sasa baada ya miaka tisa ya Karumekenge kuwa kwenye maulaji? Hapa kinachokera ni kupoteza muda hata maisha ya watu. Sasa jamaa alikuwa anadengua nini au kalishwa limbwata?

Yako wapi? Tulisikia viapo kibao kuwa jamaa alikuwa amekwapuliwa ulaji. Sasa umerudishwa na kama umerudishwa mbona haki za waathirika wa mchezo huu wa karata tatu hazikuzingatiwa?

Kweli tukiamua kuchunguzana kuna watu wengi wameghushi vyeti vyao. Hivi jitu lenye PhD kutumiwa na wezi uchwara (tena wasio na elimu kama yake), kufilisi taifa lake kweli hili halikughushi?

Je, huu nao si uchangudoa wa aina yake kujiruhusu kutumika kinyume? Baalalii angekuwapo angekwambia alivyodanganywa na majuha na vimada wake naye akaishia kuwa juha na mhanga bila kusahau Tunituni bishororo aliyejitia usomi wakati mweupe kama Njaa kaya.

Hamkusikia ya jamaa yangu wa rada ambaye sasa ni mzito wa shirika la moto na kashfa ya kununua maua na samani kwa milioni 50 za madafu? Hivi ni kufuru kiasi gani kuchezea pesa hivi wakati walalanjaa wakizidi kuteketezwa na umaskini?

Hivi huyu jamaa na Kagoda kweli hawana shea kwenye lisirikali la Njaa Kaya kweli? Angalia kila kashfa wamo wao. Richamondu, rada, CIS, Meremeta, EPA, kujiuzia nyumba za umma, wamo wao! Je, hawa si mamlaka ndani ya mengine jamani?

Inaonekana kuna viumbe wanatisha kiasi cha kumfanya hata mkuu kuwagwaya kama ukoma! Je, ni kwanini? Ni kwa sababu wanajua uchafu wake na ushiriki wake katika kuunda ujambazi mbuzi kuanzia EPA hadi mwingine utakaoundwa kuokoa jahazi mwakani?

Je, lisirikali la jamaa halimo mfukoni mwa Rostitamu anayarostisha taifa na Njaa Kaya mwenyewe? Hawa jamaa hawajui kuwa liponjoro hili na wenzake kaya ikiwaka moto watatimkia makwao wakituacha sisi tunamalizana kama pale kwa kaya ya nyayo?

Siwezi kuamini nyuzi nilizozinyaka juzi kuwa nambari wahedi imeunda jopo la kuchangisha pesa kwa ajili ya Njaa Kaya kwenye kipute kijacho.

Huwezi kuamini jopo hili linaundwa na wezi watupu wakiongozwa na Rostitamu, Kadamage Ni-ziro, Tamil Msumaiya na majambazi wengine.

Je, hapa hawajatufungua macho kuwa jamaa yetu kumbe ni mtoto wa mafisadi wanaomuweka ndani ya mifuko yao kumuwezesha kuhonga na kupeta? Je, huyu anafaa kukaa patakatifu pa patakatifu?

Nirejee kwa jamaa yangu wa kujishoo-shoo. Upo? Jim wa Kudoea bila kumsahau shangingi wa kihaya mnanipata hapa? Nyinyi ni vyangu tu hata kama mtajiona wajanja.

Huwezi kwa kutumiwa na walafi kula makombo kama jibwa ukawa mjanja bado. Mbwa ni mbwa hata alale kwenye busati. Mbwa ni mbwa hata alale ikulu bado ni mbwa tu.

Yaani tunafanya upuuzi wa wanakijiwe wenzetu bila kujua adha itokanayo na umaskini na vipigo kwa kutumikia matumbo yetu yasiyo na dirisha wala mlango!

Huwa siachi kujiuliza. Hivi uchafu kama huu unapofichuka huwa anajisikiaje mbele ya mkewe na watoto? Hebu piga picha.

Anakuja mtu anakupa laivu kuwa dingi au mume wako unayemheshimu kuliko yeyote anatumiwa na mafisadi kinyume na taaluma na umjuavyo. Kwa ndugu zangu toka Iringa usishangae mtu akachukua kamba na kusema swela-lazima nijinyotoe roho.

Ujumbe wa leo kwa kina Mdoezi, Bishoo na Shangingi wa kihaya, tafuta kazi ya kuuza nyanya badala ya kujiita waadamizi wakati ni wadandizi na wafua nepi za mafisadi.

Hakuna jambo baya kama mtu mzima na akili yake kutumia tumbo kufikiri badala ya ubongo kiasi cha kujigeuza changu hata kama ni la kisiasa.

Kwa Madevu, kaka umeula wa chuya na hili lazima likung’oe taka usitake. Kabla hata wino haujakauka, Karumekenge ameishaanza kuichokonoa ndoa hii hatari kwa kuanza kuonyesha kuwa kina Madevu walijileta akawapokea lakini wasitegemee kitu! Ngoja nikawasake hawa gendaeka niwatie adabu na mapema.

Chanzo: Tanzania Daima Nov. 25, 2009.

No comments: