MANENO ya Mbunge wa Nzega, Lucas Selelii (CCM), mbele ya mkutano wa kamati ya wazee wa chama hicho, iliyoongozwa na Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, mjini Dodoma hivi karibuni, kama yatafanyiwa kazi ilivyo, hakuna jinsi ya kumnusuru Rais Jakaya Kikwete na kashfa inayozidi kutokota ya Richmond.
“Ni huyu Rostam aliyekodisha jopo la waandishi wa habari watatu mashuhuri nchini kwa ajili ya kupoza makali. Tumezungumza na waandishi wa habari hawa mmoja baada mwingine na wote wametuthibitishia hili.” Alibainisha Seleii.
Alitaja hata majina ya waandishi hao kuwa ni Gideon Shoo, Jimmy Mdoe na Salva Rweyemamu, ambaye sasa ni Mkurugenzi wa Mawasiliano ya rais. Hii ni kwa mujibu wa gazeti la kila wiki la Mwanahalisi.
Ukizingatia maneno ya mbunge na jinsi serikali yake inavyoitumia Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU), kutaka kuiua kashfa ya Richmond, unaaza kupata ni kwa jinsi gani rais alishiriki mchakato mzima.
Isitoshe katika kipindi cha siku 100 za kuwa ofisini, rais aliuambia umma kuwa mgawo wa umeme ungegeuka historia kutokana na serikali yake kuwa kwenye majadiliano na kampuni ya kufua umeme kutoka Marekani. Ukizingatia kuwa hapakua na kampuni nyingine kutoka Marekani zaidi ya Richmond, unapata picha kamili.
Cha ajabu, badala ya kushughulikia hili na kulimaliza. Watawala wameamua kuanza kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu wa mwakani japo haipo wazi sana. Watanzania tuzidi kumbana na kumkumbusha rais kwamba, hajatimiza ahadi hata moja, ukiachilia mbali serikali yake kuwa chaka la mafisadi.
Isitoshe, tamko la hivi karibuni la Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kuwa Ikulu ndiyo iliiamuru TAKUKURU kuwahoji wabunge, ndiyo kabisa unapata ushiriki wa moja kwa moja wa rais, ukiachia mbali kukwepa kuliongelea au kuchukua hatua kwa rais.
Rais anatoa amri ya kuwabana wabunge kwa masilahi ya nani kama si mshiriki nyuma ya pazia? Asingekuwa mshiriki asingehatarisha ofisi yake na kukiuka viapo vya ofisi.
Hizi ni harakati za kutaka kujinusuru. Kuna haja ya Watanzania kutoa shinikizo kuwa kama Kikwete atamaliza muda wake bila kutatua kashfa hii, asigombee hata CCM wapige debe usiku na mchana.
Maana akirejea ataharibu kama alivyofanya mtangulizi wake, Benjamin Mkapa, aliyesifika kufanya vizuri kwenye miaka yake mitano ya kwanza. Alipopata lala salama akaingiwa na tamaa ya utajiri. Historia ndiyo hiyo.
Wakati rais akijiaminisha kuwa atachaguliwa, mawaziri wake wameghubikwa na kashfa mbalimbali hasa za matumizi mabaya ya fedha za umma, imebainika kuwa wanaagiza mashangingi yawafuate kila waendapo ili kujishaua na asichukue hatua! Kwanini awavumilie mawaziri limbukeni wasiojali kuwa nchi hii ni maskini?
Kitu kingine, rais kuendelea kumbakiza Salva Rweyemamu ambaye amewahi kufanya kazi ya kuisafisha Richmond ni kielelezo kingine cha kuridhika na kuhusika kwake.
Je, haiwezekani kuwa ukaribu wa wenye Richmond (yaani Rostam Aziz kwa mujibu wa maneno ya Selelii) na Kikwete ndiyo ulimshawishi kumteua mhusika? Hivyo, uteuzi wake una mazingira ya ufisadi.
Maana, anaonyeshwa (kwa mujibu wa maneno ya mbunge) kama mwandishi kidhabu, anayewaza kusaliti taaluma yake kwa kujiachia kukodishwa na kila fisadi amsafishe. Huyu hafai kuwa mkuu wa kurugenzi ya habari Ikulu hata kidogo.
Maana, Ikulu ni mahali patakatifu, tena pa patakatifu, kama alivyowahi kuhusia mwanzilishi wa taifa hili, Mwalimu Julius Nyerere.
Kwa nini rais anaendelea kumbakiza kwenye ofisi yake mtu ambaye ameishachafuka, ili iweje? Kama haoni uchafu wake, tulio nje tunauona na ofisi wanayotumia kishikaji ni yetu si yao.
Kwa mtu anayejua ukali wa Rweyemamu kabla ya kuingia kwenye utetezi wa mafisadi, anapata sababu ni kwanini aligeuka ghafla wakati wa kampeni na kuanza kulamba matapishi yake.
Je, haiwezi kuwa Rostam aliwatafuta mapema ili kuandaa mazingira ya ushindi na kupata tenda ya kufanya yanayoendelea kulisumbua taifa? Na ukichukulia kuwa huyu mtuhumiwa ndiye yule yule aliyenunua vyombo vya habari kwa pesa ambayo Dk. Harrison Mwakyembe, aliwahi kusema ni ya EPA akimtumia mtu wake huyu huyu.
Je, hii si ushahidi kuwa kumbe Ikulu yetu ni ya ubia ingawa rais aliwaahidi wananchi kuwa asingekuwa na ubia na mtu? Kama ilivyo kuwa kwa maisha bora, si ajabu rais alimaanisha kinyume aliposema hatakuwa na ubia na mtu wala kikundi cha watu.
Rweyemamu ni mwajiriwa mwingine wa rais, mbali na waziri mkuu na mawaziri waliojiuzulu au kuwajibishwa, kuguswa na Richmond moja kwa moja na rais hataki kuchukua hatua! Je, hapa kuna njia rais anapoweza kukwepa kuhusika moja kwa moja?
Kuna uwezekano mkubwa kashfa ya Richmond kama haitashughulikiwa ikafumua mengi. Kwa mfano, mtuhumiwa mkuu Rostam Aziz amebainika kuwa ndiye mwenye Dowans. Je, huyu hatimaye hawezi kuwa Kagoda?
Na je, hii ndiyo sababu Kagoda na Richmond yamegeuka mazimwi yanayoyumbisha utawala wa Kikwete kuliko hata majanga? Selelii alinakiriwa akisema: “Kwa maana nyingine, Dowans, Richmond na Caspian ni baba mmoja, mama mmoja.”
Kama Kikwete hatatoa sababu za kuwagwaya wezi hawa, atajikuta akihusishwa na kashfa zote kuanzia Richmond, EPA, Meremeta na mwingine utakaofichuka baadaye.
Haiwezekani mtu ambaye hakushiriki akaacha mambo yajiendee na kuendelea kumuweka pabaya bila kushiriki. Na hapa ndipo viburi vya watu kama Rostam, Makongoro Mahanga kusema eti ripoti ya kamati ya Bunge ni feki au kina Edward Hosea kusema wazi hawatawajibika. Wanajua wana mwenzao aliyeshika rungu.
Tukimalizia na Rostam anayeshutumiwa kuwa nyuma ya CIS, Dowans, EPA na Richmond, hata utetezi wake unatia shaka. Hauwezi kuishawishi akili yoyote timamu. Alikaririwa hivi karibuni kwenye gazeti hili, ukurasa wa kwanza, akiliita “Kujibu Mapigo. Alikaririwa akisema: ‘‘Hawa ni wapuuzi, wanasukumwa na chuki.”
Rostam hakueleza chuki hii inasababishwa na nini! Kwa wenye kujua historia nzima ya kashfa na mhusika wanaona kama ni kutapatapa. Ipo siku atamrukia hata anayemkingia kifua.
Umefika wakati wa kuliita koleo, koleo badala ya kijiwe kikubwa. Binafsi, naamini huko tuendako, ataunganika moja kwa moja na kashfa hizi zote hasa ikizingatiwa kwamba hajajibu shutuma za ushindi wake kutokana na pesa chafu, mikakati na watu wachafu ambao bado amejizungushia akizidi kuwakingia kifua.
Chanzo: Tanzania Daima Nov. 25, 2009.
No comments:
Post a Comment