Wednesday, 4 November 2009

Hoseah anapata wapi jeuri hii?


UZOEFU unaonyesha kuwa ving’ang’anizi wanapobanwa huapia miungu yote kuwa hawatajiuzulu kama ilivyotokea kwa Mkurungenzi wa Tume ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU), Dk. Edward Hoseah.

Ila mwisho wa siku, ving’ang’anizi hawa kwa nyonde nyonde na aibu, hubwaga manyanga na kutoweka. Tuliyasikia na kuyaona kama haya kwa Nazir Karamagi, alipokumbwa na kashfa ya Richmond mwaka jana bila kusahau kina Basil Mramba na wenzake.

Nchini Kenya, Aaron Ringera, aliyekuwa mkuu wa Tume ya kupambana na ufisadi ya Kenya (KACC) alisema kama alivyosema Hoseah hivi karibuni akiwatolea nyodo wabunge wa Kenya.

Wabunge hawa mahiri, katika kumwaga mboga, walimtaka Rais Mwai Kibaki kuchagua; aondoke yeye au mtu wake. Na mwisho wa yote Ringera amebakia katika historia.

Hivi karibuni Hoseah alikaririwa akisema: “Sasa nakwambia, sina mpango wa kujiuzulu, siwezi kujitia kamba eti ili nionekane mzalendo bila kosa, kwanini unataka nijiuzulu au unataka kuchukua nafasi yangu?”

Bahati mbaya, hakueleza ni mbunge au wabunge ama watu au mtu gani anainyemelea nafasi yake. Kwanza, ile nafasi si yake, bali ya umma ambao ndio wenye ofisi. Inapofikia mtu anaanza kuifanya ofisi ya umma kuwa mali yake binafsi, ujue kuna tatizo.

Wengi wanajiuliza mantiki ya Rais Jakaya Kikwete kuonekana kupwaya hasa wanapotajwa wateule wake wenye madoa. Inasikitisha na kukatisha tamaa. Kwani hii si mara ya kwanza kwa Kikwete kugwaya kumfukuza mteule wake alipotuhumiwa.

Mkakati usiozaa matunda unaoendelea wa kuwasafisha, kwa mara nyingine, watuhumiwa wa kashfa ya Richmond unaofanywa na serikali kwa Tume ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ni ushahidi tosha kuwa TAKUKURU hata serikali hawafai. Wanafanya ‘utoto’ usiolingana na hadhi wala umri wao.

Katika kikao cha Bunge kinachoendelea mjini Dodoma, kuna kila sababu za serikali kutaka kuizima kashfa ya Richmond hata kwa kuwatisha, kuwadhalilisha na kuwanyamazisha wabunge.

TAKUKURU na serikali, kwa makusudi mazima na nia ya kutenda jinai tena, wanataka kuwasafisha watuhumiwa wa Richmond iliyomwondoa madarakani aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, mwanzoni mwa Februari mwaka jana.

Mpaka anastaafu, mwanasheria aliyeondoka Johnson Mwanyika, alionekana kuwa mwamba na mbabe mbele ya rais, wananchi hata wabunge. Je, ni kwanini inakuwa hivi?

Je, hawa wateule wa rais wanaozidi kumdhalilisha na kumuumbua wanapata wapi jeuri hii? Je, kuna kitu wanakijua hasa kuhusiana na kashfa zinazowakabili kinachoweza kumweka pabaya rais kiasi cha rais kuwaogopa?

Ingawa Hoseah kaanza, tunajua wabunge watamaliza kama ilivyotokea kwa mwezi wake uliopita huko Kenya, kwa mtu aliyekuwa na nafasi anayoiita yake ambaye alilewa urafiki na ushirika wake na rais kiasi cha kulidharau Bunge.

Wabunge wa Kenya walipomtaka Ringera aachie ngazi, aliwakebehi kuwa anafurahia sarakasi zao, asijue angelizwa na hao hao aliowakebehi.

Tujiulize. Inakuwaje mtu anayemwakilisha mtu mmoja kujiona bora na mwamba mbele ya wawakilishi wa umma? Zaidi ya tumbo lake na rais, Hoseah anamwakilisha nani?

Zaidi ya kutegemea kuteuliwa, Hoseah ana ridhaa gani ya umma kuwa pale alipo kiasi cha kupatumia kuhujumu umma? Rejea, Hoseah kwa kutumia TAKUKURU, alivyowahi kutaka kuwasafisha wezi wa Richmond, kwa kudai hapakuwa na mchezo mchafu wakati dalili zote zilionyesha kulikuwa na rushwa achia mbali mchezo mchafu ambao unaweza kupunguza makali ya jinai.

Je, tutaendelea na kuwa na watu wababe kwenye ofisi zetu hadi lini? Je rais ana nini na Hoseah kiasi cha kujiruhusu na kumruhusu awadhalilishe wawakilishi wa wananchi?

Ni muhimu Hoseah akaonyeshwa kuwa nchi hii ni ya wananchi wala si ya rais na wateule wake. Je, wabunge wetu wataufyata mbele ya mtu asiye na mashiko kwa sababu tu ni mteule wa rais?

Kwa vile Hoseah katia mkia wake kwenye kundi la siafu, umma unangojea kuona atakavyoondoka kiasi cha kuondoka akilia. Kwanini kuwahoji wabunge sambamba na kujadiliwa kwa kashfa ya Richmond ambamo Hoseah amehusishwa?

Kama kweli alivyosema Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuwa TAKUKURU iliamrishwa na Ikulu iwadhalilishe wabunge, basi kuna uwezekano wabunge wakatumia kura ya kutokuwa na imani kwa rais na Hoseah.

Maana huu ni ushahidi kuwa TAKUKURU haiko huru na haipambani na kuzuia rushwa bali wale wanaotaka kupambana na wala rushwa kama inavyojidhihirisha kwenye hoja uchwara ya kuwahoji wabunge juu ya kula unbuge ili kuwaokoa waliokula mabilioni.

Haiingii akilini na inasikitisha sana kuona mamlaka zenye kuheshimika kuwa nyuma ya ufisadi.

Licha ya watu kuhoji anakopata jeuri Hoseah, wengi wanangojea kuona Bunge litakavyolinda heshima yake na kutenda haki kwa umma wa Watanzania wanaohujumiwa na wezi kama wale wa Richmond.

Wapo wanaoshauri hata TAKUKURU ivunjwe au kuondolewa chini ya Ikulu ili iwe huru na iweze kupambana na ufisadi kweli.

Je, Hoseah anapata wapi jeuri hii na rais anayempa jeuri hajui kuwa wabunge wakichachamaa wote wawili wanaweza kuishia kula jeuri yao badala ya mahanjumati ya ukubwa wanayofaidi na familia na marafiki zao?

Nijuavyo, ndivyo ilivyo. Hakuna aliyewahi kuwashinda wabunge hata angekuwa rais katika nchi yoyote yenye demokrasia.

Chanzo: Tanzania Daima Nov. 4, 2009.

1 comment:

Anonymous said...

Huyu Hosea ni fisadi na mwezeshaji mafisadi wakuu yaani Kikwete, Rostam, Lowassa na Mkapa ambaye ana jeuri kwa vile anajua siri zao. Akidondoka na mhimili wa ufisadi unadondoka sambamba naye.
Wabunge mtimueni Kikwete ili kundi la majambazi litiwe hatiani. Huu ndiyo wakati wa kuandika historia.