How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Tuesday, 17 November 2009

Simba alna hoja , lakini..............

INGAWA hoja ya ‘udumavu wa akili’ iliyoletwa na Idd Simba, yule Waziri wa zamani katika Serikali ya Awamu ya Tatu, inayosifika kwa kuuza nchi, ilileta kasheshe, bado hoja hii ni nzuri.

Simba, alikuwa na hoja yenye mashiko; kilichoiharibu ni namna alivyoitoa na kuitetea. Kilichomwangusha na kumponza ni aina ya maneno aliyotumia na sifa alizotoa hasa kwa wasomi.

Tuanze kuidodosa hoja. Je, si kweli kuwa Watanzania wana udumavu wa akili kulingana na ushahidi wa kitakwimu alioutoa? Kama zaidi ya nusu ya watoto wetu wana udumavu wa akili, basi na wazazi wao hali kadhalika.

Tukiangalia hata hili balaa la kughushi mitihani kwa wanafunzi na wanasiasa kughushi shahada, tunapata ushahidi wa pili. Je, si kweli kuwa wasomi wetu wengi wamekariri tu na wengine kupata shahada za hongo?

Je, msomi anayeongopa kusoma hadi kuiba mtihani au kughushi cheti si dumavu kiakili? Rejea mawaziri wengi hata wabunge kubainika wana shahada na vyeti vya kughushi na serikali isichukue hatua za kisheria dhidi yao.

Mfano mzuri ni kesi ya Mbunge wa Buchosa, Samuel Mchele Chitalilo, aliyebainika - kwa mujibu wa taarifa za uchunguzi wa polisi kuwa alighushi vyeti na hadi tunaandika hajachukuliwa hatua.

Kimsingi, mfumo wetu umedumaa kiasi cha kuendekeza na kupogelea uchakavu na nyongea ya mawazo mgando kama ilivyothibitika kwenye kupambana na ufisadi.

Kitu kingine kilichomponza Simba ni kuwatuhumu wasomi kuwa wamedumaa kiakili kiasi cha kutoshiriki siasa. Hapo hapo Simba amesahau kuwa yeye na wengine kama kina Masumbuko Lamwai ni wasomi waliojiingiza kwenye siasa wakaishia kudumazwa mawazo na wanasiasa kutokana na mfumo chakavu.

Je, ni msomi gani wa kweli atakuwa tayari kujipeleka huko akadumazwe kimawazo? Je, ni wasomi wangapi wamejaribu kuubadili mfumo huu mchafu hatimaye wakaishia kubadilishwa wao?

Je, usomi ni nini? Ni ile hali ya kuwa na vyeti vingi au utundu wa kuibadili jamii kutoka pabaya kwenda pazuri? Augustine Lyatonga Mrema, si msomi wa kupigiwa mfano kama Benjamin Mkapa au hata Jakaya Kikwete.

Lakini, kwa usomi wake wa kujiendeleza aliweza kutoa changamoto wakati wa uwaziri wake wa mambo ya ndani kiasi cha kupunguza kero zilizokuwa zimewashinda tunaowaita wasomi, kwa sababu walifika vyuo vikuu.

Hata ukimchukulia mtu kama Shaaban Robert, ambaye elimu yake ni ya msingi. Aliacha utajiri mwingi katika fasihi kiasi cha vitabu na mawazo yake kutumika kuwapatia watu shahada ingawa yeye hakuwa nayo.

Je, hapa msomi ni nani kati ya Robert na hawa wenye shahada zitokanazo na kazi zake? Hebu linganisha Frederick Sumaye, aliyekaa kwenye uwaziri mkuu kwa miaka 10 na Edward Lowassa ambaye hakumaliza hata miaka miwili.

Hata ukiwadurusu wana falsafa kama Plato, Academus, Sophocles na wengine, hawakuwa na shahada hata moja. Lakini, waliacha utajiri mkubwa katika dunia ya sasa.

Hivyo, kimsingi tunapoongelea usomi, tusiangalie makaratasi na tambo za ‘nimesoma’ bali mchango wa mhusika katika jamii.

Kama usomi wetu wa sasa ungekuwa na tija, basi watu kama Mkapa, Andrew Chenge, Dk. Idris Rashid na wengine walioingiza nchi kwenye uwekezaji wa kijambazi wasingefanya hivyo; akiwamo Simba aliyekiri na kutubia kwa dhambi hii.

Kinachokera zaidi ni ile hali ya Mkapa kusifia udumavu wake kiutawala akiwatuhumu Watanzania kuwa na uvivu wa kufikiri tofauti naye mwenye uchapakazi wa kufikiri kiasi cha kuiuza nchi ukiachia lile la yeye, mkewe na marafiki zake kujimegea Kiwira. Hawa ndio wasomi na watawala wetu!

Hapa bado huangalia shutuma kuwa pesa ya wizi wa EPA iliyotumika kwenye kampeni na harakati za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuingia madarakani 2005, huku madaktari kama Daudi Ballali, akizidiwa kete na vimada wake na wafanyabiashara na wanasiasa mbumbumbu na matapeli hadi kujiletea mauti kipumbavu.

Kama kweli kuna udumavu wa kiakili kwa Watanzania, je, ni nani wa kulaumiwa kati ya wananchi na watawala wao walioupa mashiko ukoloni na ukale wa kimwazo?

Hebu fikiria. Chini ya Waziri Profesa Jumanne Maghembe, Wizara ya Elimu imedorora kiasi cha kukabiliwa na migogoro ya kiuendeshaji ukianzia kwenye mikopo ya wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu, kutolipwa kwa walimu kwa wakati, kughushi na kuvuja kwa mitihani, kuharibiwa mitaala na mengine mengi.

Je, huyu usomi wake uko wapi? Hapa bado hujarejea kwenye uoza aliouacha huko SUA alikochomolewa.

Nadhani. Kwa kuangalia madudu kama haya, wasomi wenye kupigiwa mfano kama Profesa Issa Shivji, wamekataa kujichafua na kujiingiza kwenye siasa za kidumavu na kijambazi.

Tutoe mfano mwingine. Ukilinganisha dhamira na uthubutu vya rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Aman Karume, hasa maghorofa ya Michenzani na waliofuatia, hasa Dk. Salmin Amour, unakosa mantiki ya usomi wetu wa sasa unaoendekeza makaratasi hata kama ni ya kughushi.

Hata ukilinganisha mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya Mwalimu Julius Nyerere, ambayo haikuwa na wasomi-bobezi kama zilizofuatia, utagundua: kuwa ilikuwa na mafanikio mara mia ya zote.

Rejea kutolewa elimu na huduma za jamii bure huku kwa sasa vitu hivyo vikibakia kuwa vya wachache wenye pesa itokanayo na ujambazi ima wa kisiasa au kimaadili.

Ni ushahidi wa udumavu wa mawazo kwa hawa waliopata elimu bure kutaka kuifanya biashara kwa kuwakamua maskini waliowatengeneza kwa kusikia kauli ya bwana zao wa Ulaya.

Turejee kwenye wasomi wetu walioko kwenye taaluma. Je, wao wamenusurika na udumavu huu wa kiakili? Nani hajui kuwa wasomi walioko vyuoni wakinoa bongo za wataalamu wa baadaye wanalipwa mshahara kiduchu ikilinganishwa na wanasiasa?

Je, wamefanya nini kujinasua na wizi huu? Je, kwa wao kuridhia kuendelea kunyonywa na kudhalilishwa na wanasiasa si udumavu kimawazo? Maana ukomavu wa kimawazo ni kuliona tatizo na kulipatia ufumbuzi mjarabu.

Imefikia mahali wana taaluma wetu vyuoni wamegeuka watunza nguruwe na bustani ili kukidhi mahitaji yao huku kashfa nyingi za wizi wa mabilioni zikilipotiwa kila uchao wasifanye kitu.

Je, hawa kweli hawajadumaa kiakili? Maana ya usomi ni uasi ulengao kuikomboa jamii kutoka kwenye midomo ya makupe wachache.

Wasomi wasioasi wala kuthubutu kufanya hivyo si wasomi kitu bali makasuku waliokariri nadharia wasizoweza kuziweka kwenye vitendo. Usomi wa namna hii ni hasara.

Leo, eti nchi iliyopata uhuru takriban miongo mitano iliyopita inaagiza wataalamu kutoka ughaibuni! Je, hawa wasomi tunaozalisha kila mwaka wanakwenda wapi au kwanini hawawi wataalamu wetu?

Je, hawa wanaowabagua wasomi wetu kiasi cha kuridhia wageni waje kujichotea mishahara mikubwa si mbumbumbu hata kama ni waheshimiwa na wana shahada kubwa?

Chanzo: Tanzania Daima Nov. 18, 2009.

No comments: