HABARI zilizofichuka hivi karibuni baada ya Mkurungenzi Mkuu wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), Hundi Chaudhary, kuilima barua serikali akiandaa mazingira ya kuvunja mkataba ili waondoke na pesa zetu, haziwezi kupita bila kujadiliwa.
Umma wa Watanzania umeshangaa kusikia aliyosema Chaudhary hasa mazingira na masharti ya mkataba wa uwekezaji ambao kimsingi, si uwekezaji kitu bali ujambazi na uchukuaji wa mchana. Sitaki niongeze kitu.
Mkurugenzi huyu wa TRL inayomilikiwa kwa ubia baina ya serikali na kampuni ya Rites ya India, alionekana akiihimiza serikali itoe pesa ya kuiwezesha TRL kuanza kufanya kazi.
Wengi wanashangaa ni mwekezaji gani anategemea mtaji kutoka kwa serikali ya nchi anayowekeza wakati tuliambiwa: kigezo kikubwa cha mtu kuwekeza ni kwa anayewekeza kuwa na mtaji wa kutosha kuwekeza?
Hebu soma maneno ya Chaudhary hapa: “Serikali kwa kutumia kampuni ya Rahco iliyopewa jukumu la kusimamia mali za lililokuwa Shirika la Reli (TRC), inapaswa kutoa fedha za kusaidia mpango mkakati wa biashara kama ilivyowasilishwa na TRL”.
Bila aibu wala kuficha, Chaudhary anaendelea kuvujisha uoza wa ajabu. Haijulikani kama alijua hatari ya kufanya hivyo au ameamua kumwaga mboga au kuanza kumwaga mtama ili serikali izindukane kwa kuchelea hasira za umma.
Chaudhary alikaririwa akisema: “Fedha nyingine zenye thamani ya dola za Marekani milioni 115 na deni lenye thamani kati ya dola milioni 226 na 300 ambazo serikali ilipaswa kuzitoa kwa ajili ya mtaji katika kampuni hiyo, lakini hadi sasa hazijatolewa.”
Hebu zingatia maneno: ‘Kwa ajili ya mtaji.’ Jiulize mantiki na sababu ya mgeni kuaminiwa, kwanza kufanya biashara nchini na pili kupewa mtaji wa pesa ya wavuja jasho maskini ni nini kama si upunguani, ujambazi na ufisadi? Je, hii ni dharau kiasi gani kwa mwananchi anayehenyeshwa na umaskini wa kutengenezwa?
Kwanini serikali itoe mtaji tena kwa kampuni ya kigeni? Ilikuwaje kampuni lisilo na mtaji tena la kigeni kuaminiwa na serikali bila kuwapo mazingira ya rushwa hata wahusika kuwa mawakala wa mafisadi ninaoamini kwamba wamo madarakani?
Hivi tukisema kuwa licha ya kushindwa huku kwa serikali ya sasa ni ufisadi uliokithiri, tutaambiwa tunaiandama serikali! Je, kwa ushahidi utokanao na mkataba huu mmoja, ukiachia mingine mingi, hautoshi kuwaambia Watanzania kuwa serikali yao ndicho chanzo cha ujambazi na ufisadi unaoendelea?
Je, hawa walioingia mkataba wa kijinga kama hawa, kweli wanaweza kujiita wasomi au ndiyo wale wanaoshutumiwa kughushi ingawa hawajatajwa wote?
Hebu angalia uoza mwingine kwa mujibu wa Chaudhary: “Serikali imeshindwa kulipa kiasi cha dola milioni 0.2 ambazo ni malipo ya mwaka ambayo TRL inapaswa kuilipa Mamlaka ya Kudhibiti Usafiri wa Majini na nchi Kavu (Sumatra ).”
Hata kodi ndogo, TRL inaibebesha mzigo serikali tu? Je, serikali iliposema inajitoa kwenye biashara ilimaanisha kurejea kwa mlango wa nyuma kufanya hivi inaotuaminisha ni uwekezaji wakati ni uchukuaji na ujambazi wa mchana?
Huyu mbia anachangia nini zaidi ya kuhamisha pesa zetu baada ya kuwapa mafisadi asilimia kumi yao? Anayeona tunaishambulia serikali, anisaidie aandike makala au atoe maelezo yanayoweza kumshawishi mtu yeyote kama huu si wizi unaofanya na serikali.
Kama kodi ya Sumatra, yaani dola laki mbili TRL inaitegemea serikali, je hizi kodi za kawaida za mapato, uingizaji wa vifaa na mambo mengine yanayopaswa kukatwa kodi zinaishia wapi kama si serikali na uoza huu kujisamehe huku wananchi maskini wakizidi kunyimwa usingizi ili walipe kodi ya kuwapa wawekezaji uchwara?
Jibu la hili limo kwenye taarifa iliyofichua uoza huu. Kwani ilitaja maeneo mengine ambayo serikali ilipaswa kutekeleza kwa mujibu wa mkataba wao ni pamoja na serikali kusaidia katika malipo ya kodi zote kama ilivyo elekezwa kwenye mkataba wao.
Je, mambo kama haya hayamwaniki Rais Jakaya Kikwete, anayejipiga kifua kuwa ataleta maisha bora kwa wote ilhali muda unamtupa mkono na uoza wa serikali yake ukizidi kufichuka?
Je, hapa itakuwa vibaya kuwambia wapiga kura kwamba wakati wa kuking’oa madarakani Chama Cha Mapinduzi (CCM) umefika? Maana licha ya kushindwa kutimiza ahadi zake, kimeongeza sifa nyingine ya kushiriki ufisadi kwa kuibia mabenki yetu hadi kuzitoa kafara mali za taifa letu.
Si matusi kusema serikali yetu ni taahira. Hebu soma maneno ya Chaudhary, akiitishia na kuiamuru serikali ituibie. Anasema: “Tumelazimika kuandika barua hii baada ya kubaini kwamba serikali imekiuka mkataba wetu na endapo hayatatimizwa ndani ya siku 60 ninaweza kuvunja mkataba huo ama kuongeza muda, hivyo tusubiri siku 60 zimalizike.”
Jeuri hii Chaudhary anaipata wapi? Je, haina maana kuwa kulingana na kupindisha sheria na kuridhia upuuzi, kuna vifungu ambavyo Rites inaweza kuvitumia kuifikisha serikali mahakamani na kulipwa fidia nono?
Je, ni vibaya kusema kuwa ‘wataalamu’ mbwa mwitu walioridhia upuuzi huu walijua fika kuwa kama hili litafanyika, watapata mwanya mwingine wa kuliibia taifa na kuambulia asilimia 10 yao?
Je, hawa si wabaya wastahilio kupigwa mawe kuliko vibaka tunaowaua kila siku kwa wizi wa kuku na mabeseni? Je, ni vibaya kusema kuwa Tanzania sasa imani hakuna ama ni kichwa cha mwendawazimu?
Je, huu ndio utawala bora unaowaneemesha wezi wa kigeni kwa kuwatoa wananchi kafara na mali zao? Ningependa kusikia mama utawala bora Sophia Simba, akitoa utetezi wake kuwa serikali yake inaandamwa kwa chuki na uroho wa madaraka.
Bila kusema mengi, ni kwamba kama kuna eneo kuna ufisadi unaonuka, unaowahusisha watawala wetu, si jingine bali uwekezaji ambao kimsingi ni ujambazi wa mchana unaofanywa na wale tuliofanya makosa kuwapa dhamana ya madaraka.
Je, kinachoendelea baina ya serikali na Rites si ujambazi wa mchana? Je, serikali inayofanya ujambazi inayoupamba kuwa ni uwekezaji inapaswa kuendelea kuwa madarakani?
Ili ifanye nini zaidi ya kuuza nchi na watu wake? Ningekuwa naombwa ushauri, ningependekeza tubinafsishe Ikulu kwanza, mengine yafuate. Maana imekuwa muhuri mkuu wa ufisadi na ujambazi huu ingawa haitaki kukiri hivyo.
Rais wetu kama hataingilia kati, hali itazidi kuwa mbaya kiuchumi. Nakuomba Rais Kikwete litizame kwa makini suala la mkataba k ati ya Tanzania na Rites. Kazi kwa wenye nchi ambao wamegeuzwa wapangaji na wakimbizi kwenye nchi yao wenyewe.
Chanzo: Tanzania Daima Nov. 11, 2009.
No comments:
Post a Comment