Tuesday, 17 November 2009

Mipasho, vimbwanga na kunga za Idodomya

UNA habari kwamba nilialikwa kigwena zengwe kusuluhisha miparurano baina ya mafisadi fulani na wenzao wanaoingilia ulaji wao? Unaweza kuchukulia huu kama utani. Ni kweli. Nilialikwa ingawa sikutoa pwenti hata moja.

Nilialikwa na rafiki, classmate na mpambanaji mwenzangu, Sam Six ili tuwaumbue mafisidi mbele ya mzee Ruxsa.

Nikiwa nimejificha pembeni tayari kurusha madongo, si yule mwanamke fyatu aitwaye Sofi Yanga akatia mikono michafu desteni na kuamsha kinyaa sina mfano! Hali ilichafuka kiasi cha wabaya wangu kushindwa kunistukia.

Sikujua kuwa alikuwa na lake na yule mama wa chuma aitwaye Anae Machale. Mambo mengine yanaweza hata kuwa wivu au kugombea mabwana.

Kuna viumbe duniani hata wapige miswaki kila nukta si rahisi kuondoa uvundo moyoni na vinywani mwao. Huwezi kuamini. jamaa yangu mkuu ana waimbaji taarabu kwenye kabuneti lake wakiongozwa na chiriku Sofi.

Mara nilisikia wimbo uitwao ‘Fisadi Mwenyewe’ ukitumbuiza. Ulianza kama ifuatavyo:

Nakuonea huruma kiumbe uso haya.
Wasema si mafisidi bibie hauna haya!
Jaribu kwenda kinyume ukumbuke ya nyumayo,
Mbona yote twayajua yalojiri kwa ndoayo.
Kwani bila mfadhili ungeifunga ndoayo?

Kama wewe si fisidi humu wangojeani?
Kama wewe si fisidi kitoe upoteeni.
Usitujazie mbu tukila kwa ulaini.
Kaa kimya ja nune upate mlo laini
Kama wewe si fisidi humu ndani wangojani?

Bibie uache wivu wamuonea Ewassa,
Yeye ni dume la mbegu alochuma siyo sasa,
Uone wake ung’avu alivojaa mipesa,
Acha watu wafaidi sie hatutaki visa.

Shoga siye twala vyetu,
Twavila kivyetu vyetu,
Mnatoka wapi fyatu,
Kuja watukana watu.

Mwawaita mafisadi,
Na mkome nyie fyatu,
Halo halo halo! Na mwakani twala tena.

Akiwa amehanikiza mwimbaji wa taarabu wa kiume aitwaye Makorongo wa kujitoa Muhanga alitia nakshi kwenye beti.

Shutuma zenu ni feki, sisi tutawafichua,
Sisi n-dio breki wengine wajishaua,
Ewassa hana kisiki, na wala hana mawaa,
Ninasema kulaleki, Ewassa bado kifaa
Ambao hamumtaki, jijueni sasa mwafa.

Nacho kile kibabu kiongozi wa mipasho kilitia nakshi zaidi. Kilianza kuimba:

Tatizo sasa ni Six, lazima tutamsix.
Mshakikwaa kisiki, msije kutumix
Sasa nasema si fix, Six tutakufix.
Mwasema tunawahini, ndani mwangoja nini,
Fanya hima kitoeni, aliyewaita nani?

Kabla ya kumaliza, alidakia mwimbaji mkongwe Sam Machale.

Sofi umekumbwa nini? Hebu mama kapimeni.
Najua kinokuhini, Mirembe ujiwahini
Vinginevyo niamini, utaumbuka ugani.

Kabla ya kuendelea, Anae Machale alitumbukiza ubeti wa nasaha. Aliimba hivi:

Alianza kuhanikiza, mwanaketu ni aibu.
Njoo kwangu utubu, mbona unajisulubu,
Heri uwe kama bubu, twayajua maghusubu,
Ulopewa mengi mengi.

Mipasho ilikuwa mirefu kama barabara, ikijaa makubwa kama nyumba. Muhimu ni kwamba jamaa zetu wamefichua maradhi. Kwani wako mahututi ingawa walituaminisha kuwa mambo yao bam bam wakati ni bomu bomu.

Tuliodhani ni simba kumbe mbwa! Waliowahadaa wenzao kuwa watawapeleka Kanani kumbe Kanani yenyewe ni mifukoni mwa mafisadi!

Jambo moja la kuvunja mbavu lilitokea. Eti bwana mmoja mkubwa hivi anataka achunguzwe na mapilato kama yeye si Richamondu au la! Hivi kuna ubishi kama nguruwe ni halali au haramu?

Jaduong Obama alijisemea. Hata apakwe lipstick, shedo avikwe vipuri na majaribosi, nguruwe hataacha kuwa nguruwe.

Bwana huyu anadhani vijipesa vyake haramu vinaweza kumnunua kila mtu. Kama ni mapilato si ukubali upelekwe kwao uone watakavyokusulubu. Jaribu uone janja ya nyani itakavyokwisha baada ya kuonja jiwe ya joto.

Nikiwa nashangaa ya Musa kabla ya kuona ya Firauni mara nikasikia upuuzi mwingine. Yule mwimbaji nyemelezi Makorongo si alitoa mpya! Eti alidai tume iliyomsulubu Rich ni feki.

Ebo! Kama tume ni feki kwanini walioridhia iundwe na kutekeleza mapendekezo yake wasiwe feki? Hapa hakuna kuficha Njaa Kaya ameshindwa vibaya sana. Anapaswa atimuliwe maana naye ni feki.

Huyu bila shaka kama yule muimbaji mwenzake wanatumiwa na majambazi wakubwa ambao wasipofungiwa kule Ukonga au Segerea watakisambaratisha kijiwe kabla ya kuiuza kaya. Wengine wana shida gani iwapo wakikipiga mnada kijiwe hiki watarejea kwao?

Hivi kama yule kibaka mkubwa ambaye babu zake walikuja kufanya biashara ya utumwa wakaloea ana hasara gani hata kama kijiwe kikitupwa motoni?

Ana hasara gani iwapo urithi wa babu zake umetimia? Wao waliwauza babu za walevi tena wajinga; naye anawatumia watumwa tena wanaojiita wasomi ingawa inasemekana usomi wao ni feki.

Kinachosikitisha ni kuona na ndugu zangu wa kizaramizi, kikwerere na likawaga nao wameingizwa na kutumiwa kinyume nyume! Huko nyuma hawakuwa hivyo. Je, huu si uchangudoa ingawa wanajiona wajanja?

Heri watumwa wa enzi zile waliuzwa kwa nguvu na hawakuwa wakiitwa wasomi, waheshimiwa wala hawakughushi vyeti kuliko hawa wa hiari ambao ni dhalili kuliko hata mbwa na panya walao mabaki.

Mtumwa wa hiari ni mbaya kuliko hata jambazi mwenyewe. Kwani, kama kijiko anaweza kutumiwa na yeyote kuchota chochote. Kama bomu anaweza kutumika kujiangamiza hata yeye mwenyewe.

Wale ndugu zangu waathirika wa Mbagala, ninaposema bomu, wanajua nimaanishacho. Sijui katika upuuzi huu kuna mtu anawakumbuka kujua kuna watoto na vikongwe wanasota kulala nje wasijue watakula nini!

Juzi nilisikia wasanii fulani wakitumbuiza wimbo wa Kilimo Kwanza! Nani anataka kulima? Nani punda apende kulima? Siku hizi hakuna cha kulima kwanza wala nini bali mipasho.

Nani alime wakati unaweza ukachora mchoro ukaenda pale Bunch of Tembo (BoT) ukakwapua mabilioni na kuitwa mfanyabiashara maarufu, mfadhili na upuuzi mwingine? Kwanini kufikiria kulima wakati Ze Komedi ya siasa inalipa kuliko hata mihadarati?

Nani alime kwanza kabla ya kuiba kwanza au kula kwanza? Mie kijiweni kwangu nawambia ukweli. Kilimo mwisho na usanii kwanza.

Huwezi kulima wakati uchuuzi wa roho na rasilimali unalipa kuliko kitu chochote. Utakuwa mpumbavu na mwendawazimu. Na ni hatari kuwa mpumbavu na mwendawazimu mtawaliwa.

Utakuwa huna maana kabisa sawa na wana mipasho vigogo wanaovuana nguo hadharani tena mchana mbele ya watoto. Na huu ni mwanzo. Unacheza na laana hasa laana yenyewe inapokuwa ya marehemu?

Waulize wasaliti wakuu kina Yuda. Wafaransa wana methali moja tamu isemayo: A barbe de fol le rasoir est mol. Waingereza husema: A foole brookes any disgrace; A foole's not sensible of any wrong.

Naona gari la mama fyatu linakuja ngoja niishie kabla hajaniingiza kwenye uchafu wake.

Chanzo: Tanzania Daima Nov. 18, 2009.

No comments: