The Chant of Savant

Sunday 10 April 2011

Adui wa CCM si akina Sumaye bali CCM


Hivi karibuni kulizuka shutuma lukuki dhidi ya yeyote anayekosoa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakiwamo hata vigogo wa chama hiki. Badala ya kupokea mawazo mazuri ya kukikosoa chama ili kijijenga na kurejesha hadhi yake, wahusika ambao nao si wahusika kitu bali wadandizi wamekuwa wakitafsiri kukosoa kama kusakama chama!

Bahati mbaya “watetezi” hawa wa CCM si vyombo husika bali Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) ambao umejipachika usemaji wa chama baada ya wakubwa wake kugwaya kutokana na kuogopa kuwaudhi baadhi ya washitiri wao. Bahati mbaya zaidi, wamefanya hivyo kwa mtindo wa bomboa leo tutajenga kesho.

Hata chombo husika ambacho ni kitengo cha propaganda kinapumulia mashine tokana na kujazwa makapi yaliyokataliwa kwenye upinzani. Kitengo hiki uhitaji watu wasomi na mahiri na si waganga njaa kama iliyo. Anayebishia hili ajikumbushe majina yanayounda kitengo cha propaganda ambacho nacho kilifinyangwa kupokea makapi haya ya upinzani.

Kitengo cha propaganda ni makapi. Umoja wa vijana nao umegeuka nepi ya mafisadi. Je CCM itaweza kuogelea maji haya machafu na mazito ilimozamishwa na mafisadi waliojazana chamani?

Hakika, ombwe kwenye kitengo cha propaganda na usimamizi mbaya wa chama vimetoa nafasi kwa kila mpayukaji awe mtu binafsi au kitengo kujipayukia atakavyo akidai anakihami chama. Bahati mbaya sana, wapayukaji hawa hawana hata hekima wala ithibati katika kupayuka zaidi ya kujipendekeza kwa baadhi ya wakubwa wa chama ili waendelee kuishi. Ajabu viongozi wakuu wa CCM wameendelea kukaa kimya kiasi cha kutafsiriwa majibu haya yasiyo na akili ni maelekezo toka juu.

Ni ajabu kwamba UVCCM hawajui, au tuseme: wanapuuzia chanzo cha kudhoofika kwa chama chao. Inashangaza kuona kuwa hawajali kuwa ufisadi, ubinafsi, ukosefu wa maadili, ombwe, mitandao, ufisi na ubabaishaji ndivyo vyanzo vikuu vya kuchokwa, kukosolewa na kuchukiwa kwa CCM.

Vijana hawana haja ya kumtafuta mchawi wakati wachawi ni wao wenyewe na wakubwa zao. Je haya ndiyo matokeo ya utawala wa kujichumia au uchumia tumbo? Hata kama hakuna ushahidi wa moja kwa moja wa kuwaunganisha UVCCM kama jumuia au mtu mmoja mmoja na ufisadi, kupuuzia chanzo hiki ni ufisadi tosha na wa kutisha.

Inasikitisha kuona UVCCM, badala ya kutumikia vijana, inaamua kuwatumikia mafisadi kwa malipo ya makombo kwa viongozi wachache wa juu wa umoja huu.

Inashangaza kwa UVCCM kuwa kipofu kiasi cha kutoona mitandao ya kimaslahi ndani ya chama kama chanzo cha mauti yake! Vijana wa namna hii pamoja na umoja wao ni hasara na balaa kwa taifa. Badala ya kujenga madai na hoja za kushirikishwa katika uendeshaji na ukombozi wa taifa, UVCCM imejirahisi na kujiruhusu kutumiwa kama nepi! Wakati vijana wakichakachua ubongo wao, wakubwa wao nao wametelekeza nchi kiasi cha kukimbilia Loliondo kwa babu! Nashauri na UVCCM iende Loliondo huenda inaweza kurejesha hadhi yake kiakili.

Ila UVCCM wajua kitu kimoja: fisadi hana rafiki. Unaweza kuliona hili kwa wale mafisadi papa waliokuwa karibu na mwenyekiti wa CCM wanavyoanza kumpa kisogo baada ya kugundua kuwa uchafu wao hauvumilii tena. Wakishapata watakacho watawatupa mkono hawa vijana wanaoleta kidomodomo kutetea upuuzi.

Leo vijana wanajifanya kuwa na uchungu na chama hata kuliko wazee kama Fredrick Sumaye waliokifikisha madarakani kinaowaona kuwa maadui! Huu ni wizi wa fadhila na ukosefu wa shukrani. Hata anayewatuma anapaswa kulijua hili.

Inafaa vijana waambiwe ukweli kuwa wanachama wakongwe wanaokosoa chama si kwa sababu wanakichukia. Wana uchungu na chama chao na wanajua adha ya kuondolewa madarakani. Wamesoma alama za nyakati kwa vyama vikongwe vilivyotimuliwa madarakani baada ya k utekwa na kumilkiwa na mafisadi. Nchi ya jirani ya Kenya ni mfano mzuri wa hili. Hata pale Malawi ni mfano mwingine wa kuigwa ukiachia mbali Zambia.

Kama vijana kweli wana mapenzi ya kweli kwa nchi na chama chao, wanapaswa kutoa majibu yanayoingia akilini badala ya kufanya utoto ambao si saizi yao. Wanapaswa kuchemsha bongo na kufikiri sawa sawa ili kutoa majibu yanayowajengea heshima badala ya porojo zinazozidi kuwaumbua.

Inasikitisha kuona vijana wenzao katika nchi za Maghreb na mashariki ya kati wakifanya mapinduzi ya kifikra na kuzifurusha tawala kongwe fisadi wakati wao wameshikilia unepi. Mawazo ya akina Sumaye ni ya kisasa zaidi kiasi cha vijana kuonekana kama wazee na wazee hawa kuonekana kama vijana kifikra.

Hii inatukumbusha maneno ya waziri mkuu wa Kenya Raila Odinga aliyewahi kusema kuwa kuna wazee wana mawazo ya kisasa na vijana wenye mawazo ya kizamani. Hili limebainishwa na UVCCM.

UVCCM inaweza kujiona kama inasakamwa bure. La hasha. Haisakamwi kwa vile ni UVCCM bali kile inachosimamia kwa sasa. Kuna maswali machache yanayopaswa kupewa majibu na UVCCM. Je hakuna ufisadi migawanyiko, ombwe na usanii ndani ya CCM?

Je walikuwa wapi mpaka mambo yanaharibika kiasi hiki? Je kwa kuwatisha na kuwadhalilisha wakosoaji ndiyo wanaleta jibu au kukuza mgawanyiko na migogoro? Kinachokera ambacho UVCCM wanapaswa kuachana nacho ni mawazo ya ni zamu yetu kula na kumtafuta mrithi wa Jakaya Kikwete. Hili si muhimu kwa taifa.

Taifa litakapohitaji kuwa na rais mwingine lina jinsi ya kumpata na si lazima atoke CCM ambayo inaonyesha wazi kukaribia kukata roho kutokana na kutokuwa na uongozi na sera makini. Yako wapi maadili ya uongozi? Iko wapi miiko ya chama? Bila vijana kujipiga darubini wakaona ukweli wa hali inayokikabili chama chao, watasaidia kukisindikiza kwenye makaburi kama ilivyotokea kwenye nchi tulizotolea mfano.

Kimsingi, kama kuna maadui wakubwa wa CCM si akina Sumaye wala wakosoaji bali CCM yenyewe na adui mkubwa akiwa UVCCM na mafisadi wake inaowabeba. Kuna haja ya CCM na UVCCM kuangalia ukweli hata kama ni mchungu kuliko kutengeneza maadui wa ndotoni.
Chanzo: Dira ya Mtanzania Aprili 11, 2011.

No comments: