How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Tuesday, 19 April 2011

Wao na mashangingi, sisi na Ambulance za Bajaj

Mizengo Pinda akikagua Bajaj ambayo imetengenezwa ili kumudu kazi ya kuzima moto hasa kwenye maeneo yenye barabara nyembamba katika maonesho yaliyoandaliwa na Kampuni ya Spray and Fumigation Services Limited, bungeni Dodoma Alhamisi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).


BAADA ya kuona waziri mkubwa akizindua eti Bajaj ya kuzima moto, mie nimeamua kutumia ndege kuzima moto baada ya kuingia madarakani. Kuna jamaa yangu, baada ya kujua mipango yangu nasikia anataka kuzindua Bajaj inayopaa! Itapaaje? Msiniulize.

Kwanza nilipooana mtu mzima eti anaingizwa mjini na matapeli wanaojiita wawekezaji wakati ni wachukuaji, nilipigwa na butwaa na kujiuliza. Akili zetu zimefichwa wapi kiasi cha kutenzwa hivi kama hatuna ubongo? Hayo ni yao. Tuyaache.

Kweli waliosema kuwa hizi ni zama za usanii, kutapatapa na ombwe hawakukosea. Tangu lini pikipiki ikawa zima moto kama siyo kutapeliwa na kushinda kutumia bongo sawa sawa?

Hawa waliotoa hili wazo na wakatengeneza Bajaj ya kuzimia moto wanatudharau sana. Wanatuona wote tu mataahira. Wanajua tunavyofikiri “kibajajbajaj.”

Ambulance Bajaj, zima moto Bajaj bado treni na meli za Bajaj. Ama kweli mmegeuza kaya kuwa Bajaj. Basi tuiiteka kaya ya Vikombajaj. Hii ikichanganyikana na vikombe ndiyo usiseme. Ama kweli la kuvunda halina ubani. Maana kila tapeli anakuja kuchuma Bongolalaland!

Jamani, kama Bajaj deal kwanini hamzitumii hasa nyie wazito mnaopitisha upuuzi wa kuruhusu zitumike? Kwanini watu wazima mkwepe Bajaj na kuwabambikia wagonjwa tena waja wazito msiwe waroho? Nyie mashangingi na mashangingi yetu wao vibajaj na babaj zao! Mbona kwenye kikombe cha babu hamuweki matabaka mbele kama kweli nyie si wagonjwa?

Wakati nchi za wenzetu wanatumia midege kuzima moto, sisi tunajisifu upumbavu wa kutumia baiskeli kuzimia moto. Kesho sitashangaa kuona mtaalamu wa “kuzima moto” akimwalika waziri mzito kuzindua chupa ya chai ya kuzimia moto.

Hivi kweli hili linahitaji kuwa na shahada nyingi kama zangu kujua kuwa ni utapeli tena wa kipuuzi? Kwanini tusijenge miji yetu kisasa kiasi cha kuwa na njia za kuruhusu magari zima moto kupita?

Hata hivyo, magari yenyewe yako wapi? Yatapatikana vipi na wapi iwapo tumechakachua kila kitu hata uwezo wa kuona na kufikiri? Kwa wale wanaojua lugha ya anga au baharini, tunapaswa kutoa alama ya au mbiu ya “mayday” yaani maafa.

Kwa ufupi baada ya kuanza mbio za kwenda Ikulu hata kabla ya uchafuzi na uchakachuaji, nimeanza mikakati kamambe ya kuukwaa ukuu na kula bure kama maiti. My blueprint is very simple. I shall be tough and honest. I won’t entertain any wanton stupidity. I won’t allow any crooks to do as they are wont.

Sera ninazotumia kwenye kampeni ndiyo nitakazotekeleza bila kupunguza wala kuongeza.

Nitahakikisha Bajaj hazitumiki kuzima moto wala kusafirisha wagonjwa. Badala ya kupoteza muda na upuuzi kama Bajaj nitahakikisha mipango miji bora na ya karne ya 21. Hili ndilo jibu, Mengine upuuzi.

Wagonjwa kwa upande wao nitahakikisha kila hospitali ina Ambulance yake na si Bajaj. Bajaj licha ya kuwa usanii uchwara ni uhuni wa mwaka.

Nilishasema nitapambana na ufisadi hasa wa kiakili. Hakuna ufisadi wa kiakili kama huu ambapo matapeli wachache wanatumia raslimali za kaya yetu kwa manufaa yao huku walevi wakiendelea kusota na kufa malofa. Lazima nipigane vita ya kuwakomboa walevi kifikra na kimkakati tena haraka.

Pia nitapiga marufuku umalaya wa kujiuza kwa wawekezaji wanaokuja kuchukua. Hamtasikia akina AIPITIELO kwenye serikali yangu wala Reitis ya ugabacholini. Lazima kaya ifaidiwe na wana kaya wenyewe kwanza.

Wakuu wa mikoa, wilaya na watendaji wa kata kwenye serikali yangu mwiko. Kama ni ulaji wa bure utokanao na ushikaji basi wakale lupango. Hawa kwangu ni wakoloni weusi wanamwakilisha mkoloni mkuu ambaye kila mmoja anamjua. Ni yule yule ambaye yuko juu ya sheria akitumia nafasi hii kuwakingia vifua mafisadi wake ambao CHAKUDEMA waliwahi kuwaundia kitu kilichoitwa List of Shame (LOSS).

Wabunge wa kuteuliwa au kupendelewa hamnei. Kumekuwapo na huu ufisadi mwingine ambao wakuu hutumia kulipana fadhila-ubunge wa kuteuliwa na ule wa upendeleo. Hivi kwangu ni ufisadi hata ningeambiwa nini. Huu ni ufisadi wa kimfumo ambao mkinichagua nitauzika ndani ya wiki moja.

Kumekuwa na usanii wa muda mrefu na upotevu wa mabilioni ya njuluku kuhusiana na kuhamishia makao makuu Dom. Hili kwangu nalo ni ufisadi.

Nasema wazi. Kuhamia makao makuu mwiko. Kule hakuna maji wala starehe kama vile totos, mishiko ya vikao na makandokando mengine ya ulaji wa dezo. Isitoshe nani anapenda kuishi katikati ya matatizo?

Pia na mchezo mchafu unaanza kukubalika miongoni mwa walevi. Ni pale mawaziri na wabunge wavivu wa kusoma wanapojipachika vyeo vya udaktari, uprofesa na madude mengine.

Nasema wazi. Mawaziri kutumia vyeo wasivyosomea sahau. Atakayeghushi ajue amejifungulia mlango wa gereza. Mie sitazungusha wala nini. Mhalifu huyu atakamatwa mara moja na kufungwa hata akiwa ni kigogo wa chama changu au ndugu yangu. Mie sina ndugu linapokuja suala la uwajibikaji. Walioghushi jiandae naja mkombozi wa walevi.

Bi mkubwa kudandia mgongoni mwangu ndiyo sahau kabisa.

Kuna mchezo mwingine mchafu sana. Si mwingine bali vitegemezi vyangu kutanua kwa ukuu wangu. Hili ni kosa la jinai. Nitafunga mtu hata awe mwanangu mwenyewe. Kila mtu ale jasho na akili yake badala ya kuendekeza ukupe.

Chama changu cha Ugali Nyama na Maharagwe (UNM) hakitashika patamu wala hatamu. Patamu na hatamu si vya vyama bali wanakaya wenyewe. Huu nao ni ufisadi mchafu tena wa kimfumo, lazima nikomeshe haraka mkinichagua.

Chama changu hakitakuwa na kitengo cha propaganda cha kufichia makapi na vihiyo kama Tambo Hizo, Chitambala, Sambuee, Salimia Msabasi, Twaib, Akuilombezi na wenzake.

Watu wenye majina ya Ewassa, Rosttamu, Chenga, Jose, Makambale, Chilimugati, Mpukutika na wengine kama hao wasahau kujiunga na chama changu. Sitaki nuksi kwenye chama. Tangu lini wacheza ngoma na wataalamu wa mipasho wakawa wakuu wa chama? Wakae huko huko kwenye chama cha majoka. Mie si mpuuzi ati.

Angalizo. Nitaahidi pepo. Sasa kama nitawapeleka motoni au Misri msiniulize. Akili kichwani. Kama akili zitakuwa kinywani au tumboni hata kiunoni tusilaumiane baadaye.

Je, wajua kuwa mimi ni rais wenu mtarajiwa? Acha nisiongee sana wabaya wangu wakasikia.
Chanzo: Tanzania Daima, Aprili 20, 2011.

No comments: