The Chant of Savant

Wednesday 2 July 2014

Werema ni mwanasheria au mwanashari?


NAANDIKA makala hii kwa masikitiko sana kulaani mtindo wa kihuni wa baadhi yetu kujichukulia sheria mkononi.
Hali hii inakuwa mbaya zaidi hasa pale tunaodhani ni magwiji wa sheria na mihimili ya sheria na utawala bora wanapokuwa wa kwanza kuivunja na kujichukulia sheria mikononi kama ilivyotokea bungeni hivi karibuni ambapo Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema alimwita tumbili mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi) kabla ya kujaribu kumpiga na kutishia kumkata kichwa.
Kosa alilotenda Kafulila hadi kunyanyaswa na kudhalilishwa na Werema ni madai kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospiter Muhongo aliliambia uongo Bunge bila kuchukuliwa hatua. Wengi walidhani shutuma kama hizi licha ya kumuudhi Muhongo angezijibu mwenyewe. Wanahoji ni kwanini Werema aliwashwa na pilipili asizozila ukiachia mbali kuonyesha mfano mbaya na kulidharau Bunge na wananchi wa Kigoma Kusini? Je, kunani hapa? Je, ni kwanini Werema hata Spika wa Bunge hawakumtaka athibitishe madai yake na badala yake wakaridhia kumdhalilisha na kumtishia maisha?
Hakika kitendo alichotenda Werema, licha ya kumdhalilisha yeye binafsi, kimelidhalilisha Bunge na taifa kwa ujumla. Litakuwa jambo la ajabu kama Rais Jakaya Kikwete atamvumilia kama alivyowavumilia maafisa wengine wengi kwenye serikali yake walioonesha wazi wazi uhovyo na utovu wa nidhamu.
Wengi walidhani Werema, kama mwanasheria mkuu na jaji, angetumia uzoefu wake kuonyesha busara na weledi wake badala ya mihemko na mibwato isiyo na ulazima. Hii inamfanya aonekane mwanashari zaidi ya mwanasheria.
Na hii si mara ya kwanza kwa Werema kutishia watu maisha. Mwaka jana alimtishia Balozi wa Uswizi nchini,  Olivier Chave, alipodai kuwa serikali ya Tanzania  haikuwa imetoa ushirikiano kwa Uswisi kuhusiana na kupeleleza na hatimaye kurejesha mabilioni ya shilingi yaliyofichwa nchini humo na mafisadi ambao wengi wao ni wakubwa serikalini.
Hivyo, kutishia watu imekuwa tabia ya Werema ambaye alipaswa kuwajibishwa kama si wakubwa kulindana. Je, cheo kikubwa kama alicho nacho Werema kinahitaji mtu anayepwaya hivi kiasi cha kutumia shari badala ya sheria kama njia ya kutatua matatizo tena ya kikazi na si binafsi?
Je, Werema amekumbwa na nini? Je, huu si ushahidi kuwa Rais Kikwete amekuwa akiteua watu wa hovyo bila kufanya utafiti na uchuguzi kuhusiana na sifa na hulka zao? Je, ni vibaya kumtaka Werema awajibike au kuwajibishwa kwa vile anaendelea kutia aibu ofisi ya Mwanasheria mkuu wa serikali?
Je, ni kwanini Werema hakutaka Kafulila athibitishe madai yake? Aliogopa nini kama hakuna chembe ya ukweli hata ukweli mwingi tu? Je, wananchi wataendelea kuona wawakilishi wao wakinyanyaswa na kudhalilishwa hadi lini?
Nangojea kusikia hatua zitakazochukuliwa na wananchi wa Kigoma Kusini hasa baada ya Spika wa Bunge, Anna Makinda kumkingia kifua Werema akisema kuwa Kafulila alitegemea nini kwa kum-provoke Werema kama alivyokaririwa akibukanya kiswanglish bungeni.
Kuna haja ya kumdodosa Werema ambaye watanzania wengi hawamjui vizuri kutokana na tabia chafu ya siku hizi ambapo serikali inateua watu kushika nyadhifa tena nyeti bila kuanika wasifu wao vizuri kutokana na wahusika kuwa na madoa au marafiki au vibaraka wa waliowateua. Je, Werema ana magonjwa ya akili hasa ikizingatiwa kuwa hii si mara ya kwanza kufanya madudu kama haya ya kuvunja sheria wazi wazi akitishia kuichukua mikononi mwake?
Kuna haja ya wahusika kutupatia majibu ili tusiwe tunafanya kosa kubwa kama kuwapa watu wasio na sifa ofisi zetu na kuzitumia vibaya. Najiuliza swali moja kuu: Hivi kama Werema angekuwa polisi mwenye kutembea na bunduki na akakuta na masahibu kama aliyokutana nayo bungeni, asingemfyatua Kafulila risasi?
Nadhani, kama mwansheria, Werema anajua kuwa binadamu anaruhusiwa kujitetea pale anapokuwa chini ya udhia au shinikizo chini ya dhana ya kinga ya provocation as a defence. Nadhani Werema anajua kuwa licha ya kuwa ngumu kuitumia kinga hii kisheria, anayeitumia hupaswa aitumie pale kitendo kilipotendeka mara moja na ghafla chini ya kile kinachoitwa heat of passion. Provocation inaelezwa kisheria kama, “an intensely emotional state of mind induced by a type of provocation that would cause a reasonable person to act on impulse or without reflection.
A finding that a person who killed another acted in the heat of passion will reduce murder to Manslaughter under certain circumstances.”  Sina tafsiri sahihi zaidi ya kuonyesha vitu muhimu vilivyopigiwa mstari ili kinga husika itumike ipasavyo jambo ambalo Werema hawezi kukidhi.
Je ilikuwaje Werema akatukana, akatishia na kujaribu kushambulia kama kweli alikuwa akidhani anatumia dhana nzima ya provocation yaani maudhi?
Kwa aliyotenda Werema, kinga ya provocation haiswihi na akijaribu kujitetea basi anaweza kutumia insanity yaani uwendawazimu ambayo nayo pia ina shurti zake nyingi kisheria.
Hatujengi hoja wala kujaribu kutumia kinga hizi za kisheria kumuonea Werema bali kumsaidia. Ndiyo maana tumehoji utimamu wa akili zake hasa ikizingatiwa kuwa alipaswa kujua uzito na thamani ya dhamana yake anayoifuja na kuidhalilisha ukiachia mbali kuitumia vibaya na kuigueza tishio kwa maisha ya watu wasio na hatia kama ilivyojitokeza kwenye sakata zima la kutia aibu na kuhuzunisha ukiachia mbali uzito wa makosa ya jinai aliyoyatenda bila ulazima. Werema jitafiti, ujisute na kufanya maamuzi magumu ya kuachia ngazi.
Chanzo: Tanzania Daima Julai 2, 2014.

6 comments:

Anonymous said...

Haya ndiyo maendeleo yetu baada ya kupata uhuru, sasa ndiyo matunda yake haya hapa...kutoka kwa Jaji kwa ajili ya wapiga kura wa Tanzania.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon umenichekesha ulipompambanisha jaji na wapiga kura. Hata hivyo yeye ana hasara wala wasi wasi gani iwapo hachaguliwi na wapiga kura zaidi ya wale waliowatapeli wakawapa ulaji na ukuu? Kwa kiasi fulani tunaongea na mbwa lau mwenyewe asikie.

Anonymous said...

Hii lugha iliyotumika na Mwanasheria Mkuu haishangazi kwa nini leo tupo kwenye hali mbaya ni michezo ya kugiza inayofanyika wakati kusaini mikataba ya kitapeli tunaweza kusema wakati wote ni rushwa inachangia kumbe kuna mashaka makubwa sana uwezo kitaaluma na maarifa kwa wa wakilishi wetu. Wapiga Kura wa Tanzania ahamkeni mpo bado usingizini. Acheni kwa kupiga kura kwa kusikiliza porojo na kupewa fulana na khanga wakina mama. Gharama ya kura ni kubwa sana kuliko hivi vitu vya kupita. wekeni malengo ya muda mrefu

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon hapo juu natamani wadanganyika wasome mawazo yako na kuyaelewa na kuyafanyia kazi. Hakika tunatawaliwa na wahauni na wapuuzi wanaopaswa kuwa gerezani. Hata hivyo, nadhani wapuuzi wakubwa ni wale wanaochagua wapuuzi ili wafanye upuuzi wao kila uchao bila kubadilika.

Anonymous said...

Bravo wachangiaji hapo juu
2015 tunataka mabadiliko

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon umesikia nadhani wataendelea kutoa michango yao adhimu hapa.