Wednesday, 9 July 2014

Kijiwe chalaani uhuni mjengoni

BAADA ya mura Were-maa anayeitwa jaji na mwanasheria mkubwa kulikoroga huku wakubwa zake wakikenua, kijiwe kimeamua kujitoa kimasomaso na kulaani uhuni wake na wa wenzake, hasa wale wanaomkingia kifua au kuendelea kumchekea. Mkichekea nyani mtajavuna mabua.
Mgosi Machungi ndiye analianzisha leo. “Jameni mmesikia vitisho vya Weema akitaka kumbonda na hata kumkata kichwa Kafuia kwa kumwambia ukwei? Jamani tinakwenda wapi kama watu wazima wanafanya mambo ya kitoto na kitahaara?”
Msomi Mkatatamaa aliyekuwa ndiyo anamaliza kusoma jarida la The Mail on Wednesday anakwanyua mic. “Unaongelea hizi bangi za mjengoni ambako hekima imepotea kiasi cha bangi na uhuni kuchukua nafasi yake? Nimeamini maneno ya Jobless Ndugui aliyesema kuwa waishiwa wengine wanakula mibwimbwi na kuvuta ganja wallahi.
“Kweli inasikitisha licha ya kustahili laana kwa nguvu zote. Sijui hii kaya inapelekwa wapi kama wahuni na wavuta bangi wanapewa nyundo wawamalize wachovu?
“Mwanzoni nilidhani huyu jamaa msomi kumbe hovyo! Mtu mzima hovyo kama Jonii Kombaa na Bill Lukuvii wanaotutishia upuuzi au Pita Serukambaaa aliyetutakana mitusi ya nguoni akaachwa utadhani alitenda ndivyo.”
“Yakhe usinkumbushe huu upuuzi wallahi. Yaani tushafikia hatua ya kugeuza mjengo sehemu ya mitusi kana kwamba wote ni hamnazo! Kwa vile najua Njaa Kaya hatachukua hatua, mie napendekeza sisi wana kijiwe twende huko mjengoni tumfukuze kazi.
“Maana hii afisi aniotukana ni mali yetu na si ya mamake wala Njaa Kaya au huyu wa kucheza makindamakida aliyenkingia kifua wazi wazi.”
Mijjinga aliyekuwa akingoja kukwanyua mic hangoji Mpemba aendelee. Anakatua mic kinoma: “Kumbe nyie hamumjui huyu mura! Huyu kama si sera za kitwahuti ya kubebana na kulipana fadhila wala hakupaswa kuwa hata hakimu achilia mbali ujaji. Jaji gani anayetumia ngumi badala ya ubongo? Jaji au jaa kama si janga?”
“Huyu si jaji bali junk kama wale aliowateua Njaa Kaya wakati wana madhambi mengi kimaadili hata kisheria. Hamkumsikia Tunduni Lissuni akisema kuwa kuna majaji makanjanja wasioweza kuandika hata hukumu?
“Nadhani mnawajua kwa majina. Wapo walioko pale kwa sababu ya ama jinsia au dini zao na wengine ushikaji tu wa kawaida wa kulinda ufisadi kama alivyothibitisha huyu mura uchwara anayejifanya Tyson,” anazoza Mipawa.
Bi Sofi Lion Kanungaemba anaonekana wazi kuchukia. Anamuonya Mipawa akisema: “Kaka madai yako mazito. Je, unaweza kuyathibitisha au ni chuki tu? Halo halo, una sera wewe! Hiki naona kijiba cha roho. Mwenye wivu ajinyonge ati! Wapo na watakuwepo na wataendelea kupeta. Mara hii mmesahau maneno ya mheshimiwa rahisi Jake aliyewaambia kuwa kelele za mpangaji hazimnyimi usingizi mwenye nyumba?”
“Sofi nakuheshimu sana. Wewe ni wa kuniambia kuwa nina wivu mimi na kijiba cha roho? Kwa lipi wakati wahusika wanaadhirika kila siku, sema njaa zao zinawafanya waendelee kufa na tai shingoni?” analalamika Mipawa.
Msomi anadandia: “Usemayo Mipawa kweli tupu. Hata kama hawa akina Were-maa wanajikausha, roho zao zinawasuta. Wanajijua wazi wanavyotumiwa tena kinyume na mafisadi. Hamkumsikia mwenzie A Liar Kim Maswii akisema eti kama Kafulia ni mrume amnange nje ya mjengo amshitaki?”
“Huyu naye mpuuzi kama wenzake Muongo na Were-maa. Awanange mara ngapi wakati alishawavua nguo? ‘They’re lucky. Their boss’s blind and naive otherwise they’d have already hit the road’. Samahani nimechanganya kikameruni japo changu ni bomba kuliko cha Alikwina Makiinda aliyetoa mpya,” anazoza Mijjinga huku akibwia kahawa yake.
Msomi anarejea: “Mzee unaongelea ile mpya ya Makiinda ya umemprovoko akaprovotika na kumthreateni siyo?”
Mijjinga anatikisa kichwa kukubaliana na Msomi anayeendelea kuchonga: “Tuliwaonya wachovu kuwa huyu manzi alisimikwa na mafisadi ili wamtumie kama wanavyomtumia mura huyu asiye na busara wala adabu.”
Mbwa Mwitu aliyekuwa akiangalia anaamua kutia buti na manjonjo yake: “Kwanza nieleze kwa utuo jamani. Dokta Msomi umeniacha hoi kusema eti wanatumiwa na mafisadi kinyume. Je, ni kinyume cha nini jamani.
“Pili, Dokta Mijjinga nawe nijuze. Unasema eti huyu bibi mkubwa shoga yake kanunga alisimikwa na mafisadi. Je, walimsimika vipi au ni yale yale ya kutumika kinyume?”
Mpemba anaingilia haraka: “Yakhe haya mambo ya kusimikwa na kutumiwa kinyume mbona yako wazi? Hivi mwanasheria anapotetea ufisadi tena kwa kutaka kupiga na kuwakata vichwa wenzake huyu hajatumika kinyume cha maadili? Je, huyu bibie hakusimikwa ili kumwengua mzee wa viwango Sam Six? Nani asojua hili wakati hata ndege wajua?”
“Dokta Mpemba umenisaidia sana. Hebu mwekee kahawa huyu kwanza. Umenikumbusha Dokta feki Makorongo Majanga ambaye kesi yake ya kudai mabilioni ilitupiliwa mbali baada ya kuwa anakwepa mahakama kuthibitisha alivyo kihiyo aliyeghushi.
“Nina wasi wasi hata huyu Were-maa alighushi japo hajastukiwa. Maana anaongea utadhani wapiga debe wa daladala wa pale Makumbusho,” anachomekea Kapende.
Mgosi Machungi anarejea: “Tukubaiane kabisa. Kama alivyosema Ami hapa lazima tiende timtimue huyu muhuni aende akafanye uhuni wake kwenye vita ya Waenchoka na Waiegi kule wanakogombea bangi na upuuzi mwingine.”
Kanji aliyekuwa kimya muda mrefu anaamua kukatua mic: “Dugu zangu, samehe yeye kama jua anavuta bangi. Kama fukuza yeye toto na bibi yake kufa njaa bure dugu yangu.”
“Toto na bibi yake hapana kufa njaa. Kama yeye nakwapua bilioni 200 hapana kufa njaa. Heri yeye kufa njaa kuliko sisi. Kama atakufa njaa basi iko kwenda kwa fisadi kama veve watapea yeye fedha uu vipi Kanji?” Mheshimiwa Bwege anaamua kumzodoa Kanji.
Kijiwe kikiwa kinazidi kunoga si likapita shangingi la Were-maa. Wacha tulitoe mkuku kabla ya kujisalimisha kwenye Kituo cha Polisi Msimbazi.
Chanzo:Tanzania Daima Julai 9, 2014.

2 comments:

Anonymous said...

Eti wanasema sisi tumelewa pombe imeingia kichwani na wao wanachumia tumboni ndiyo tofauti.

NN Mhango said...

Wow! Anon hapo juu una hatari. Ina maana heri ya sisi wenye pombe kichwani kuliko wao wenye ubongo tumboni siyo?