The Chant of Savant

Wednesday 30 July 2014

Kijiwe chakaribishwa futari

 Baada ya kufuturisha kugeuzwa fasheni kiasi cha kukosa maana, juzi wana kijiwe walipata mwaliko kwa ajili ya kupata futari na stafutahi toka kampuni ya Fiction inayosifika kwa kukwepa kodi na kutoa huduma aghali na mbovu ili kuwaweka sawa kwa kutumia makulaji.
          Mwaliko huu ulizua utata, ubishi, kupishana hata lugha na nusu kushikana mikono sisi kwa sisi. Kabla ya kwenda au kutokwenda mjadala mkali ulizuka kiasi cha kuacha sintofahamu isiyo ya kawaida.
          Kanji ndiye aliyeleta mwaliko huu. Alianza kwa kusema, “Dugu zangu, iko furaha kubwa alike veve kwa futari kesho kutwa.”
          Mzee Maneno anajibu, “Ama kweli huu kweli mwezi mtukufu ambapo kila mwenye nazo hujitahidi kuwa mkarimu. Shehe Kanji twashukuru kwa mwaliko wako mwanana.”
          “Yakhe huwezi ongea kwa ajili yetu sote kana kwamba umetuuliza na kupata mawazo yetu kuhusiana na huu mwaliko wa futwari.” Mpemba anadakia akionekana kuudhika.
“Sasa veve karibisha jambo heri wakata siasa nini? Mimi ona hapana mtu kataa futari dugu yangu.” Kanji anamjibu Mpemba.
Mijjinga aliyekuwa ndiyo kamaliza kunong’ona na Kapende anakula mic, “Kanji hujamwelewa ami pale. Shida hapa si kukubali au kukataa bali kupata ridhaa . Kama mzee Maneno kishaamua kwenda basi ajisemee badala ya kutusemea wote au vipi?”
“Shehe Mpemba usemayo ni kwei. Mimi muumini ati. Siwezi kukubai kila mwaiko kwa vie nimeambiwa kuna futaai. Futai nyingine haziswihi ati. Hei niende kwetu Mashindei nikajichimbie viunga vya futai kuiko hii futai mauzauza.” Mgosi Machungi anaamua kumpa kampani Mijjinga.
Kapende naye hataki kuachwa nyuma kwenye mechi hii. Anakula mic, “Shehe Mgosi na Mpemba mna hoja tena yenye mashiko. Siku hizi kufuturisha imegeuka fasheni kiasi cha hata mafisadi, maafisa wa serikali hata marais na mabalozi kutumia fursa hii ima kujipigia kampeni au kuibia umma kwa kisingizio kufuturisha. Nani anataka futari ya kijambazi kama hii kama tutasema ukweli?”
Msomi aliyekuwa ndiyo anampa gazeti Mchunguliaji anachukua mic, “Wote mnaoshuku mialiko hii ya kinamna mna hoja kubwa sana. Hivi jiulize: Haya makampuni mabingwa wa kukwepa kodi, kulangua wachovu na kuwapa huduma mbovu yanafuturisha kweli au yanawageuza watu mabwege na kuwasanifu kwa kisingizio cha kufuturisha? Mbona wanaona wepesi kufuturisha lakini si kufunga angalau kukwepa kulipa kodi?”
Anakunywa kahawa yake na kuendelea, “Juzi kwenye gazeti la the News nilicheka sana nilipomuona mwana mama mmoja balozi kwenye nchi moja ya jirani akiwaalika mashehe kufuturu. Ajabu ya maajabu, mjivuni huyu pamoja na kujifanya kufuturisha, hakuvaa hata ushingi lau kuheshimu mila za wenzake. Ajabu ya mwaka, hata waalikwa walipwakia futari bila kuangalia kama ni halali au haramu.”
Mbwamwitu anaamua kuchomekea kabla ya Msomi kuendelea, “Kaka siku hizi haramu ni halali na halali ni haramu. Maendeleo ati. Huoni wezi wakubwa wanavyoandaa mifutari kibao na watu kuifakamia bila kuuliza. Sijui tunakwenda wapi yarabi?”
“Usemayo shehe ni kweli tupu. Hebu tuwe wakweli japo kwa nafsi zetu hata kama tuna shida. Hivi futari au msaada utokao kwa mafisadi na majambazi nayo ni futari au haramu? Juzi nimeshangaa nusu kukata roho niliposoma gazetini kuwa fisadi wa IpTL naye anatoa misaada ya kujenga vituo vya ndata na mahekalu. Sitashangaa kusikia mafisadi kama bwana Richmonduli, Kagoda na ANBEN wakifuturisha.” Anaongezea Msomi.
Mipawa hataki kuachwa nyuma. Anakwanyua mic, “Nyie mwashangaa hayo. Mbona nimeshashuhudia watu ambao njuluku zao zinatokana na biashara ya mihadarati, nguruwe na ulabu nao wakifuturisha?  Usishangae hata madada poa  sijui makaka poa nao wakafuturisha.”
Muishiwa Bwege anapoka mic, “Tukubaliane mabwana. Huku tunakoambiwa ni kufuturisha siyo bali hongo ya kibwege tu. Mbona wakati wa mzee Mchonga sikuwahi kumuona akiandaa futari patakatifu pa patakatifu kama hakuna namna? Hii imani na mapenzi vimetoka wapi kama si watu kutumia ujinga na umaskini wetu kutulisha haramu zao?”
“Yakhe mie siweziharibu swaumu yangu kwa kupwakia vitu haramu hata kama vyatolewa bure ati. Kidini, futari itokanayo na fwedha haramu nayo ni haramu pia. Hii ni fatwa natoa kama msomi wa dini wallahi.” Mpemba anazidi kuongeza utamu.
Kijiwe hakina mbavu jinsi Mpemba anavyotoa fatwa kijiweni.
Sofia Lion aka Kanungaembe aliyekuwa anaonyesha kukereka wazi anakamua mic, “Wahenga walisema kutoa ni moyo usambe ni utajiri. Kama hutaki kushiriki futari acha wenye kutaka wafuturu. Kwani unahukumu wewe Mungu? Ukimchunguza kuku alacho hutomla.” Anamgeukia Kanji na kusema, “Kaka Kanji wala usikatishwe tamaa na wale wanaotaka kufanya mambo rahisi kuwa magumu. Hebu twambie futari hii inafanyika wapi tukuunge mkono.”
Kabla ya Kanji kujibu Mbwamwitu anachomekea, “Je ustaadh Kanji hii futari italiwa jamatini au hotelini au tuseme baa?”


Kijiwe kikiwa ndiyo kinanoga likaja kundi la watoto na vigoma vyao vya kuarika watu kwenye futari. Kila mmoja aliendelea kushangaa aina hii mpya ya dini. Tieni akilini msijeliwa mwajiona.
Chanzo: Tanzania Daima Julai 30, 2014.

No comments: