Thursday, 10 December 2015

Mwl Nyerere na mke wa KaisariEwe Jakaya Kikwete, unamdanganya nani?

Twayajua yako yote, tokea EPA zamani
Ulishapoteza kete, tulia uraiani
Kaa ukiomba Mungu, mlindane mafisadi

Ulizoea ubwete, kwa sasa uko kizani
Nafasi usiipate, kuzurura ghaibuni
Kama unalo lolote, ulofanya ofisini
Kwenda kuzura hovyo, nao washikaji zako

Nenda kwa wauza kete,  walioshika mpini
Ulisimama kidete, kuwahami hadharani
Imeshakwisha fungate, waingia matatani
Madudu yako Jakaya  mbona yanajulika?

Kujinusuru ufyate, utegemee hisani
Au vipi yakukute, malipo ni duniani,
Uchunguzi ufuate, mengi watayabaini

Omba Mungu mlindane, mafisadi CCM.


Marehemu baba wa taifa Mwl Julius Nyerere alituachia amali lukuki. Aliwahi kusimulia kisa cha mke wa Kaisari na kutuhumiwa kwa uchafu. Nyerere alisema kuwa  hata kama mke wa Kaisari hakuwa ametenda kosa, kujiruhusu kushukiwa tu kulitosha kumuondolea heshima. Jana tulimsikia Kikwete akijitetea yeye na famillia yake ambayo ni haki yake. Hata hivyo, utetezi wake haukuwa na mashiko wala malezo ya kujinasua na tuhuma. Leo anaweza kujiaminisha kuwa yu safi. Sijui kama kashfa ya EPA kama kweli itachimbuliwa itamuacha akiwa safi. Anaweza kumtetea mwanae Ridhiwan kuwa hana mawaa. Kama kashfa ya utwaliwaji wa Shirika la Uchukuzi Dar Es Salaam (UDA) itafumliwa vilivyo bila kulindana, sijui kama itamwacha akiwa safi. Alimtetea mkewe Salma kuwa hana mawaa. Right, kama shughuli za kampuni yake ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) zitapigwa kurunzi vilivyo hatabaki safi. Utawala wa kijambazi wa kifamilia haukuanzia wala kuishia kwa Kikwete. Unakwenda mbali hadi wakati wa Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa ambao kimsingi ndiyo waasisi wa mfumo chakavu na ovu unaotuhagaisha kwa sasa. Hata hivyo, kutokana na sura nilizoona kwenye baraza la mawaziri, uwezekano wa kulindana na kukingiana vifua ni mkubwa.

4 comments:

Anonymous said...

Huyu Kikwete bora angekaa kimya akawaacha watanzania wamalize hasira zao na kuendelea kupumua kwa kutapika uchafu wote aliowasababishia,lakini kujitoa kimasomaso mbele ya watanzania ni kama kuongeza moto katika jeraha ambalo halijaanza kupona.Kama madai yake hayo yana 1% ya ukweli hivi haya madudu aliyoyazibua rais Magufuli yametokea wapi na wewe ulikuwa wapi wakati wote huo.Tulikuwa tunajua kwamba wewe,familia yako,na waramba viatu vyako ni mafisadi lakini Magufuli ametufungua macho kwamba ufisadi wako ulikuwa unastahiki kusamamishwa mahakamni kama si hiyo katiba yenu ya kulindana.Na ni kweli kabisa kwamba utawala huu wa kijambazi wa kifamilia waasisi wake ni Mwinyi na Mkapa hili halina mjadala.Kikwete kama ungekaa kimya ningekuona una busara kuliko kujifedhehesha tena kwa Watanzania.Eti Mwalimu Mhanango hivi uoni huyu Husseni Mwinyi kupewa uwaziri wa ulinzi ni aina fulani ya kubebana?Kiongozi ambaye alishindwa kuwajibika yalipotokea milipuko ya mabomu ya Mbagala na kudai asingeweza kujiuzulu utadhani jeshi lilikuwa la baba yake?Hapa Rais Maghufuli nadhani unalipa fadhila kwa aina moja au nyingine ambayo sisi wananchi hatuijui kwani mimi sioni mantiki ya kupewa uwaziri wa ulinzi wa mtu ambaye alipewa madraka hayo kwa mara ya kwanza alipotokea fresh chuoni na hata bunduki hakuwa anaijua inashikwa vipi hivi Rais unataka kutwambia hakuna watu ambao ni wanajeshi na wamekaa jeshini na wanalijua jeshi wakapewa wadhifa huo?Hapa kuna maswali mengi kuliko majibu,.Na tulitegemea kwamba uchaguzi wako wa mawaziri usingekuwa ule wa dakitari wa mifupa kupewa wazira ya Ujenzi.Hata hivyo tunazidi kukuombea Mungu akusaidie na akulinde kwa kuwapeleka mbio mawaziri wako hao kwa kasi yako ya mbiu yako ya kwamba "hapa ni kazi tu"

NN Mhango said...

Anon kwanza habari za siku nyingi? Usemayo yana mashiko kuwa Kikwete angejinyamazia na kushika adabu. Anadhani watanzania hawana akili wala kumbukumbu? Mbona madudu yake ya EPA yanajulikana hata kwa kunguru? Mbona madudu ya Ridhiwan na ujambazi wa UDA yanajulikana? Mbona Esrow yake na wauza unga vinajulikana?
Hili la Hussein Mwinyi nalo ni muendelezo wa ufisadi chini ya Magufuli. Baraza lake la mawaziri alilotangaza leo limepunguza imani yangu kwake. Unawapa uwaziri vihiyo kama Lukuvi! CCM inaanza kujenga dynasties za watawala waliopita. Angalia Mwinyi, Makamba, Nnauye na watoto wengi wa vigogo waliojazana kwenye balozi zetu na wengine wakuu wa wilaya. Bado taifa letu lina safari ndefu ya ukombozi. Lawama zote tuwatupia UKAWA kwa kulala kitanda kimoja na Lowassa kiasi cha kuipa nafasi CCM kushinda uchaguzi.

Anonymous said...

Mwalimu Mhnago,
Namshukuru Mungu nipo salama ni pilika pilika tu za maisha zinanifanya kuwa mbali na mtandao lakini nikiwa huru na kuwa karibu na mtandao ninachokimbilia kwanza ni kukusoma.Ukweli Mwalimu Mhango kazi unayoifanya unastahiki kupongezwa kwani pamoja na wakati wako kuwa ghali lakini umekuwa mwenye kututakia kheri wananchi wa Tanzania hususa na waafrika kiujumla Mungu awe nawe akupe afya njema na akulinde.
Dynasties?Ni kweli kabisa Mwalimu Mhango,hili la dynasties limeshakuwa wazi na la uhakika na kwa watanzania sidhani kwamba tutakuwa na nafasi tena ya kuiangusha dynasties hizi na ukiangalia kwa undani zaidi ukweli ni kwamba ni Magufuli ndie alieziokoa dynasties hizi kutoanguka na kwa hali hii Mwalimu Mhango udhani kwamba ile kauli ya CCM ya kutwambia wataendelea kututawala tena kwa miaka 50 ijayo ina ukweli wa jinamizi?.Na hapa inabidi nikubaliana nawe kwamba (japo mwanzo nilitofautiana nawe)kwamba UKAWA walifanya blunder la kisiasa la kumkubatia Lowassa,kwani kwa kuja Magufuli madarakani nadhani kutaipa UKAWA wakati mgumu wa kupambana na CCM,Nadhani kazi watakayokuwa nayo kubwa ni kudai rasimu ya katiba ya Wariomba kuona nuru na kuwa katiba ya wananchi.Hapa ningeomba maoni yako kisiasa ya kwa nini UKAWA waliamua kususia hutuba ya Magufuli?Udhani kwamba inaonyosha immaturity kisiasa?
Nimalizie kwa swali hili Mwalimu Mhango,kwa vile nchi yetu imebobea katika ufisadi wa hali ya juu tangu kuundika kwa hizi dynasties na mafisadi daima wanakuwa hawapo tayari kupoteza masilahi yao kirahisi na hususa ufisadi huo ukiwa ni ushirikiano wa baadhi ya viongozi wa CCM na mapebari wa nchi,je udhani kuna uwezekano mkubwa wa Mgufuli kumtokea ambayo ya liyomtokea Sokoine?Na udhani kwamba kwa kasi hii aliyokuja nayo Magufuli ya kupambana na ufisadi na mafisadi Magufuli ameshakuwa ni public enemey no 1?Baadhi ya wananchi wana hofu ya kwamba kasi ya mMagufuli inawezekana ikawa ni nguvu ya soda kwa kuwafumba macho wananchi kwa kile alichokiahidi katika kampeni zake za kisiasa kwani ahadi uvunjwa kama alivyovunja Kikwete karibu ahadi zake zote je hofu hii ina mshiko wowote ule?
Baki salama na kila kheri.

NN Mhango said...

Anon ni kweli usalama wa Magufuli ni ishu hasa ikizingatiwa kuwa alikuwa ameanza kugusa wasioguswa. Hata hivyo, tokana na blunder ya kumteua Muongo na dynasties, nina wasi wasi hii inaweza kuishia kuwa sideshows kama siyo Pizzazz. Wasi wasi wako ni kwamba hii inaweza kuwa nguvu ya soda au ya zima moto tena wa Bongo. Kumbuka hata Njaa Kaya aliingia na gea kama hii.Kilichojitokeza ni kwamba Magufuli atafungwa kamba na chama kutokana na uoza wa waliomtangulia. Pia naye anaweza kuwa na uchafu ambao wenzake wanaujua hivyo kuutumia kumtisha na kumnyamazisha. Laiti angetaka kufanya kweli, alipaswa kuanza na mfumo badala ya one-man show inayoendelea. Mtu mmoja atafanya mangapi kwenye ji nchi kubwa kama Tanzania na ukizingatia ukweli kuwa ufisadi umekuwapo kwa takriban miaka 30 tangu alipoachia ngazi Mwl Nyerere? Ni suala la muda tu Magufuli wa kweli atajulikana na yule feki atapotea. Hizo ndizo siasa za majitaka za nchi changa.