The Chant of Savant

Sunday 28 August 2016

Makonda kujengea Bakwata hapana


Image result for makonda na bakwata
            Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alikaririwa hivi karibuni akiahidi kulijengea Baraka Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA) makao makuu yenye hadhi. Makonda alisema makao makuu hayo yatakuwa jengo la ghorofa tatu lenye thamani ya shilingi 5, 080, 155, 600. hii si pesa kichele. Wapo waliotaka kujua fedha hii Makonda inatoka wapi; na ni nani wako nyuma ya hisani hii ya aina yake katika historia ya taifa. Makonda anatoa jibu akisema “Leo nimefika hapa ikiwa ni mwanzo wa safari mpya ya serikali ya mkoa wa Dar kujenga makao makuu mpya ya kisasa ya ndugu zangu.” Hivyo wasiojua nani atajenga jengo hili wajue; ni utawala wa mkoa wa Dar es Salaam. Je kuna wanaomtuma na kumtumia kwa faida yao? Hili swali wanapaswa wajibu wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam. Sijui kama wamempa kibali cha kujenga makao makuu ya taasisi ya kidini wakati shule nyingi za serikali ni hoi kimajengo ukiachia mbali wafanyakazi wengi wa serikali kutokuwa na nyumba za uhakika. Je nini mantiki ya kufikia kipaumbele hiki na mchakato gani wa kidemokrasia umepitisha mradi huu? Je watanzania watanufaikaje na mradi huu?
Makonda aliongeza “viongozi wangu wa BAKWATA, najua watu wote wana viongozi kama baba ni kiongozi wa familia, watu wana vyama vyao vya siasa wana viongozi, watu wana makampuni yao wana viongozi lakini viongozi hawa wanatofautiana na viongozi wa dini kwa jambo moja, viongozi wa dini wanatuongoza kutupeleka kwa mola alietuumba sote.”
Kuna maswali ambayo Makonda na waliomtuma walipaswa kujiuliza.
Mosi, je makao makuu ya Bakwata ni muhimu kuliko watoto wetu wengi wanaosomea kwenye majengo mabovu au walimu wao wasio na maslahi na mishahara ya kutosha ukiachia mbali kutokuwa na vitendea kazi vya kutosha na vya kisasa?
Pili, je kweli Bakwata inastahili kupewa kipaumbele hivi? Pamoja na kuwa mpokea zawadi hachagui zawadi ya kupewa, hivi kweli Bakwata ilihitaji hata msaada mchoro kweli? Wapo waliodhani; Makonda alikuwa amekurupuka kutafuta ima umaarufu au kutaka kuwatumia waislamu aonekane anachapa kazi na mtatuzi wa matatizo ya jamii.
Wapo wanaoona kama Makonda ameshauriwa vibaya kwa kuhangaika na kuwajengea watu makao ya kifahari kwa vile hayakukumfurahisha wakati anawaacha wasio na hata mlo mmoja. Wapo wanaohofia Makonda hatafanikiwa katika kupata hicho unachokitafuta. Hali inakuwa ngumu hasa mtumishi wa umma unapojiingiza kwenye mambo ya dini wakati serikali haina na haipaswi kupendelea dini yoyote.  Wapo wanaodhani kuwa bilioni tano na ushei ni pesa ambayo si rahisi kuipata. Hata hivyo, inavyoonekana, Makonda anazo fedha. Maana alikaririwa akisema; anataka jengo lake likamilike ndani ya miezi 14. Huyu atakuwa na fedha. Kinachogomba ni alivyoipata na namna anavyotaka kuitumia kwenye nchi yenye matatizo mia kidogo.
Wapo wanaoona kama serikali ina fedha ya hata kujenga makao makuu ya asasi za kiraia wakati makao makuu yanaishinda, basi imekosa kipaumbele. Je serikali itapata faida gani kujiingiza kwenye biashara ya dini au kuchanganya siasa na dini? Sijui inatoa somo gani kwa watanzania wenye shida za msingi kama vile ukosefu wa maji, umeme na huduma nyingine? Je huku si kuwatumia waumini kisiasa jambo ambalo ni hatari huko tuendako? Wakati mwingine mtu anaweza kutaka kufanya jambo jema kwa njia mbaya. Hapa ndipo utata unapoanza. Huwezi kutumia fedha au nafasi ya umma kupigania haki ya kundi moja wakati ukiyaacha mengine.
Je Makonda na wanaomtuma walijua kuwa:
Mosi, Bakwata wana mali zao kama vile majengo na mali za wakfu ambazo zimetumiwa vibaya kiasi cha kuwaweka matatani baadhi ya waislam wakereketwa kama Shehe Ponda Juma Ponda. Heri Makonda angewapa Bakwata wakaguzi wa mahesabu na mali.
Pili, popote anapopata hiyo fedha, anaigawa kama nani wakati kuna matatizo kibao ya maana yanayolikabili taifa? Kama ni ya serikali ni kwa sheria gani au ni yale yale kuwa kuna watu sasa wana uwezo wa kujifanyia lolote bila kujali sheria kwa vile wako karibu na wakubwa zaidi? Je huu mradi umeridhiwa na mkoa; kwa faida gani na utajiri gani?
Tatu, kwanini hiyo pesa isielekezwe kwenye ujenzi wa madarasa, nyumba za walimu, maabara au kuboresha maslahi ya walimu badala ya kuwajengea wetu wenye uwezo na wajibu wa kujijengea makao yao makuu?
Nne, je Makonda na wenzake wanafahamu; serikali wanayoiongoza inaombaomba kwa wafadhili kutunisha bajeti ukiachia mbali michango kwenye madawati?
Tano, Kwanini serikali hata iwe ya mkoa tu ipate fedha ya kujenga makao makuu ya Bakwata wakati vijijini fedha inaenda kiduchu?
Sita, je lisingekuwa jambo la busara kwa fedha hiyo kuelekezwa kwa vijana wengi wanaohenyeshwa na mikopo ya elimu ya juu au zahanati nyingi zisizo na madawa au majengo stahiki? Hakika maswali ni mengi kuliko majibu.
Tumalizie kwa kuuliza maswali. Je Makonda na wenzake wanafahamu kuwa wanachotaka kufanya–pamoja na uzuri wake–kinaweza kutafsiriwa kama hongo au kishawishi kwa wahusika kwa malengo ya kisiasa hata kama si hivyo?
Saba, je Makonda na wenzake wamepata mchango wa wapinzani ambao nao wanaunda serikali ya mkoa wa Dar es Salaam hasa kwa kuzingatia mileage Makonda na wenzake wataipata kisiasa? Maana, wangefanya wao wangeambiwa wanachanganya dini na siasa.
Mwisho, je utajengea wangapi?
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili leo.

4 comments:

Anonymous said...

Salamu Mwalimu Mhango,
Maswali yote hayo uliyoyauliza katika makala hii ni maswali wajihi,ya haki,yanastahiki kuuliza au hata yanjiuliza yenyewe kwa nguvu na pia yanahitaji majibu.Lakini kwa maoni yangu kuyapata majibu yake itakuwa ni vigumu kutokana na mabadiliko ya nchi na jamii yetu kukumbwa na virusi vya udini katika siasa tangu kiongozi wa awamu ya pili kuingia madarakani na kuitumia dini kama sehemu ya kutafuta umashuhuri rahisi.Ukweli ulio wazi na usiopingika kwamba Raisi wa awamu ya pili alitiumia dini katika siasa na hatimae virusi hivyo vikawa vinakuwa na kupata nguvu siku hadi siku mapaka hapa tulipofikia.Leo hii dini haipo na wala haitokuwa tena kwa kuiona kama wakati ule wa Baba wa taifa Mwalimu Nyerere,kwamba dini inamuhusu mwananchi mwenyewe binafsi na Msikiti wake au Kanisa lake na Mungu aneabudiwa katika dini hizo au dini zinginezo.

Leo hii dini imekuwa ni biashara kubwa katika jamii yetu,leo hii dini inatumiwa na wanasiasa kila panapotokea kuitumia dini hiyo katika majukwaa ya kisiasa kila mwanasiasa kulingana na imani ya dini yake utamsikia ananukuu maandishi matakatifu ya dini yake kama ni ushahidi wa kuwakinaisha wananchi kwamba anachoongea pia kina uthibitisho,kukubalika na kubarikiwa na vitabu vya Mbinguni.Leo hii viongozi wa dini wamekuwa na sauti kwa wanansiasa wetu na hata kushiriki bila ya woga katika siasa kana kwamba ni halali kwao au haki yao hushiriki katika siasa na huku wakiongoza wafuasi wao wa kidini.Leo hii kuna ushindani mkubwa wa kujenga makanisa na misikiti kwa njia zote zote ziwazo na iwezekanavyo kama ni njia ya kuwawezesha baadhi ya wahubiri wa dini hizi kuweza kujitafutia utajiri kirahisi au kujitafutia njia za riziki za maisha yao.

Bakwata ni moja ya taasisi ya kidini nchiini,taasisi ambayo imekuwa ikiishi katika ufisadi wa hali juu sana tangu kuundwa kwake na kama taasisi hiyo ingekuwa inaendeshwa bila ya ufisadi ingekuwa ni moja ya taasisi yenye nguvu ya kiuchumi nchini kiasi ambacho ingeweza kushiriki kikamilifu kwa hali na mali katika kutoa mchango wake katika jamii na nchi.Lakini kwa ufisadi ambao uliokubuhu taasisi hiyo imekuwa ni mzigo mzito kwa waisialamu wenyewe na hata kwa nchi ukilinganisha na tasisi zingine za kidini.

Mwalimu Mhango,kwa hali ya udini iliyokuwepo hivi sasa katika nchi yetu na kutumika na wanasiasa ndiyo hii hali tunayoiona hivi sasa na wala hatuoni ajabu kwa mwanasiasa kama Makondo na jopo lake kuweza kuitumia dini kama ni ngazi kufikia ajenda zao za siri za kisiasa.Kama ni kuyajenga makao makuu ya Bakwata yenye hadhi ni jukumu la waisilamu wenyewe na wafadhili watakaojitokeza kwa wazi au kwa kujificha.Lakini kuijengea Bakwata makao makuu mapya kwa kutumia pesa za walipa kodi hili halikubaliki na wala halikubaliki kwa maadili yao wenyewe Bakwata kwani pesa za walipa kodi zinapatika kwa marejeo mbali mbali ya halali na ya haramu kwa vipimo vyao wao wenyewe bakwata.

Natumalizie tu kwa kuandika kwamba wanasiasa na serikali wakae mbali na dini wasiitumie dini kwa vile tu wananchi ni wafuasi wa dini hizo na kutumia imani zao kwa manufaa yao ya kisiasa,na ikumbukwe tu kikatiba serikali yetu ni ya kisekula na kujiingiza katika dini au kuitumia dini kisiasa ni kwenda kinyuma na katiba ya nchi yetu.Na hofu yangu tu Mwalimu Mhango,usije ukazingatiwa tu kwamba ni mmoja wa maadui wa dini ya kiisilamu kwa kuandika makala haya ambayo waisialamu hawatakuwa na tafsiri nyingine zaidi ya kukuona hivyo.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon, kwanza samahani kwa kuchelewa kujibu. Sikuwapo nyumbani. Hata hivyo, huwa nathamini mchango wako ambao uniongezea welewa na mawazo kuhusiana na baadhi ya mambo ninayoandika. Usemayo ni kweli. Makonda angeshughulikia shida za watanzania na si kundi moja la watanzania tena wasio na shida zaidi ya kutaka ushufaa. Nadhani hapa tuangalie picha kubwa na mbali zaidi kuwa kuna anayemtuma kufanya haya ili kuwin leverage toka kwa waislamu japo anawazoesha vibaya. Hata Edorgan aliwahi kuwa rafiki mkubwa wa kiongozi wa kidini aliyetaka kumpindua kwa kutumia mtandao wake.
Tanzania haina dini japo raia wake wana dini. Hili nitalipinga hata kama nitachukiwa vipi. Nadhani tatizo la wanasiasa wetu ni kutoona mbele na kutaka sifa za shilingi mbili au cheap popularity. Kimsingi wanachofanya Makonda na Bakwata ni ndoa ya matapeli wawili kama si biashara ambapo tapeli mmoja ana dhahabu feki na mwingine anataka ainunue kwa fedha feki.
Ni kesho tu atawagusa pabaya hao wapendwa wake waishie kutalikiana. Kama madhehebu ya kidini ikiwamo Bakwata yamekuwa yakisamehewa kulipa kodi kiasi cha kuutumia uchochoro huu kuingiza mali za wafanyabiashara na kujipatia kipato binafsi kuna haja gani ya kutumia fedha za umma kuwajengea eti makao makuu wakati watoto wetu wanasomea kwenye mbavu za mbwa? Nadhani waislamu makini hawakubaliani na udhalilishaji huu. Anayemjengea mkeo ndiye mumewe kadhalika anayeijengea Bakwata ndiye mwenye Bakwata. Kwa maana hiyo waislamu wanaodai Bakwata ni kikaragosi cha serikali hawajakosea hata kidogo.
Maswali ni mengi kuliko majibu.,
Nimalizie kwa kukushukuru tena kwa mchango wako na kutumia muda wako kunisoma na kuchangia vilivyo. Asante sana na A Luta Continua.

Anonymous said...

Salamu Mwalimu Mhango,
Hapa umekumbusha point muhimu sana kuhusu Erdogan na aliekuwa rafiki yake,Tofauti yangu na Erdogan ni kuwa mwanasiasa ambae aneitumia dini katika dini kwa kujipatia umaarufu wa kisiasa na kuzidi kujizatiti kuwepo kwake madarakani kwa kutumia hisia za kidini kwa wananchi wake na aemefanikiwa kwa hilo hatimae madaraka yameshamlevya na kuaanza kutaka kuuharibu muundo mzima wa mfumo wa kidemokrasia nchini mwake,kuingililia uhuru wa magazeti na uhuru wa waandishi wa habari ambao ni moja a muhimili wa demokrasia haii leo amekuwa mwenye kujaribu kuzinyamazisha kila sauti ambazo wnatofautiana nae kuhusu muelekeo wake huo wa kisiasa au kuitumia dini katika siasa.

Tukimchambua huyu aliekuwa ni rafiki yake alikuwa na mtandao mzuri tu wa katika nchi na duniani kote kwa kutoa huduma zake chini ya mwamvuli wa kidini swali linalojiuliza hapa kwa nini asiendelee kuwa muhudumu wa jamii zote za kiisilamu duniani kama lilivyo kundi la dhehebu la Ismailia likiongozwa na Agha khan IV?Lakini kwa tamaa ya madaraka ameitumia dini kuiingiza katika siasa na hatimae amewaharibia wafuasi wake future zao za maisha nchini mwake na kuwaharibia hata wale wasialamu ambao walikuwa wakifaidika na huduma zake.Hili ndio tatizo la kuchanganya dini na siasa wenzetu nchi za kimagharibi(kisiasa) walipofanikiwa kuitenganisha dini na siasa ndipo wamefika hapa walipofikia kimaendelea za nchi zao.

Mwalimu Mhango,Jambo hili usilifumbie macha hata kidogo mana kwa hali inavyoendelea nchi mwetu kuna nchi ambazo wana tamaa ya kujijengea influence za kisiasa kupitia nchi zetu ambazo wananchi wake wapo tayari kujitolea muhanga kwa kuvuruga amani na usalama wa nchi zetu,Al-shababu na boko haramu ni mfano hai na yaliyotokea Afrika ya kati katika miaka ya karibuni ni mfano hai.Baba wa taifa alitujengea msingi au misingi imara ya dola la kisekula kwamba udini,ukabila na kubaguana isiwe sehemu ya maisha ya watanzania.Hii leo utaona hata shule za serikali kumeingia pia sare za kidini je kwa nini serikali inalikalia kimya hili?Kama ni sare za kidini na zivaliwe katika mashule ya kidini,vyuo vya kidini au madrasa na sio shule za kiserikali au vyuo vya kiserikali.Hapa hakuna hoja ya uhuru binafsi au kuheshimu itikadi za watu kwa kuvaa mavazi hayo yanayozingatiwa ya kidini mashuleni au mavyuoni.

Mwalimu Mhango,nilijaribu kuchangia maoni yangu kuhusu makala yako ya "Magufuli ataibadili CCM au itambadili?"Lakini kwa bahati mbaya naona haikuja upande wako.Ni matumaini yangu kwamba tatizo ni technically kwani huna tabia ya kupuuza maoni yoyote yale yanayokufikia kutoka kwa wasomaji wako.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon, nakubaliana nawe kuwa Fethullah Gulen amepoteza fursa nzuri. Nasikitika kuwa ujumbe wako haukufika. Vyombo hivi tunaviamini; lakini vina udhaifu hasa ikizingatiwa vimeundwa na mwanadamu asiye mtimilifu.
Kila la heri