Thursday, 1 September 2016

Kijiwe chalaani Makondakonda na wauaji wa polisi

            Baada ya majambazi kuua ndata wasio na hatia tena wakiwa kibaruani, Kijiwe kimekaa kama kamati kulaani mauaji haya pamoja na matamshi ya kishenzi yanayokiuka haki za binadamu.
            Mpemba ndiye analianzisha, “Yakhe mmesikia hii ya majambazi kuua askari tena kwa kuwavizia kwenye banki? Sijui hii kaya yapelekwa wapi hasa usawa huu ambapo baadhi ya waja wanaanza kusingizia hata upingaji wakati ujambazi unajulikana ulivolelewa na utawala ulopita wa kitwahuti.”
            Mbwamwitu anajibu huku akiendelea kusoma gazeti, “Mie sishangai hasa nikiangalia namna kaya yetu inavyokumbatia ufisadi kiasi cha kila mtu kusaka njuluku.”
            Mgoshi Machuni anakula mic, “Hii timeisikia. Hapa lazima tiseme wazi. Hawa majambazi azima yasakwe na kufikishwa kwa piato ii yakapata stahiki yao. Pia tichukue fuusa hii kuonya poisi nao wasionee wanakaya kama njia ya kuipiza kisasi. Kaya yetu ni kaya ya kidemokaasia na inapaswa kuendeshwa kwa utawaa wa sheia na si jazba ya waduwanzi fulani wanaofanya usanii wa kisiasa.”
            Mijjinga anakwanyua mic, “mgoshi hapa nakubaliana nawe hasa nikirejea maneno mbofu mbofu kama hii ya mkubwa wa nkoa Po Makondakonda aliyewahimiza ndata kutoheshimu haki za binadamu asijue kuwa sheria haitumii jazba au umajinuni na ukihiyo kufanya kazi zake. Najua kila mwanakaya amechanganywa na kuchukizwa na vitendo vya kuua ndata. Ni bahati mbaya kuwa badala ya kumsaka adui wa kweli, tunahangaishwa na matokeo. Lazima tushauri wausika kutafuta chanzo cha jinai hii ili kuishughulikia vilivyo kwa akili na si jazba na ujinga.”
            Kapende anakula mic, “hata mimi huyu dogo mpenda ujiko aliniacha hoi kiasi cha kuhoji usomi wake. Wakati watu wenye akili wanazuia wanakaya kujichukulia sheria mikononi au kuonea watu kwa kulipiza visasi, yeye anahimiza ndata wajichukulie sheria mikono asijue matokeo yake–licha ya kujenga uhasama baina ya ndata na wanakaya–kunaweza kutumbukiza kaya kwenye machafuko. Sijui hao waliompa huo ulaji kwanini hawakufanya homework yao vilivyo?”
Tunaendeshwa na sheria na katiba na si hisia wala usongo
            Kanji anakula mic, “mimi iko sangaa sana hii kuu naotoa amri baya kama hii. Hiwi huyu nateua yeye iko goja nini fukuza yeye ili itie adabu na ishike adabu na adabu ishike yeye? Hii takuja chafua rahis kama naacha iseme bila fikiri kama toto dogo. Vatu yote nasikitiko kubwa na nalia chozi kuba kufa data.”
            Msomi Mkatatamaa anaamua kutia guu, “Kanji naungana nawe. Sijui kwanini huyu dogo hawajibishwi haraka na kufikishwa kwa pilato kwa kutishia amani na haki za binadamu. Hata hivyo, sisi hatushangai kusikia na kuona haya tuliyoshuhudia. Tulionya muda mrefu kuwa jamaa ni bomu. Sasa ameanza kujifichua na kuonyesha uhalisia wake. Hata hii ya kudaiwa kutaka kumfanyia fujo na kumdhalilisha Mzee Jose Waryuba inaanza kuonekana kuwa kweli. Unacheza na laana za wazee nini? Kilichompandisha ndicho kitakachomshusha.”
            Anapiga chafya na kuendelea, “nakubaliana na  maneno ya Mijjinga kuwa tunachopaswa kufanya si kutoa amri za aibu na ajabu zitokanazo na jazba bali kukisaka chanzo cha kadhia hii ambacho ni ukosefu wa maadili. Tangu maadili yalivyogeuzwa madili na kila mchovu akataka kuukata hata kwa kuumiza wenzake, ujambazi na jinai nyingine zitaendelea kuongezeka hata kusababisha madhara makubwa kuliko haya yanayotushangaza leo.”
            Mipawa anakula mic, “mwenzenu anatetea kitumbua kwa kila hali hasa usawa huu ambapo kijogoo katika kaya hii ni mmoja. Kama mlisikia munene wake alivyolalamikia watetezi wa haki za waja pale walipohoji mantiki ya kusimamisha baadhi ya watendaji hadharani bila kufuata utaratibu, mtakubaliana nasi kuwa huyu dogo alikuwa anasema aliyosema si kwa upendo wa waenda zao bali kutaka kumridhisha bosi wake.”
            Sofia Lion aka Kanungaembe anakula mic, “kaka nakubaliana nawe. Hakuna jamaa aliponiacha hoi kama kusema kuwa hakuumbwa kusema maneno mazuri na wala huwa hamfurahishi mtu wakati kila mwanakaya anajua lengo la kutoa upupu huu la huyu dogo licha ya kuwafurahisha ndata, lililenga kumfurahisha waliomfinyanga.”
            Mzee Menano anamchomekea Sofia, “dada ni kweli; jamaa anajichanganya kutokana na uchu na njaa ya madaraka. Hii ndiyo hasara ya madaraka ya kupewa na si kusotea. Mbona mkuu wa ndata, waziri na wenene wengine hawakujivua nguo kama siyo umbumbumbu wa mhusika wa kupayuka bila kufikiri. Anadhani kupayuka pwenti ni kazi rahisi siyo?” anamalizia huku akiniangalia mimi hasa baada ya kusema kupayuka pwenti si kazi ya mchezo. Nami natabasamu tu bila kusema neno.
            Mheshimiwa Bwege aliyekuwa akiangalia na kutikisa kichwa muda wote anaamua kutia guu, “wote mmesema vyema na nimewasikiliza kwa makini. Nataka niwaambie kuwa usawa huu, huyu dogo mnayetaka awajibishwe anaweza kusema na kufanya lolote asifanywe kitu hasa ikizingatiwa kuwa amedekezwa akasahau kuwa mchezo anaocheza hauna muamala. Wangapi wameishafukuzwa kama mbwa baada ya uteuzi wao kutenguliwa? Hamjui anayecheza naye na anayemuigiza. Siku moja mtakuja kukumbuka maneno haya ya utume.”
            Kijiwe kikiwa kinanoga si wakapita ndata. Acha tutoke mkuku kwa kuogopa wasitekelezee amri za Makondakonda kwetu.
Chanzo Tanza nia Daima Jumatano jana. 

No comments: