Saturday, 17 September 2016

Naja na UKUTA dhidi ya deni la kaya na marahis wastaafu


            Baada ya lisirikali kuwahi kupendekeza kupunguza mishahara ya wanene ili kubana matumizi yasiyo na tija kwa kaya, nilihisi kama kuna ubaguzi. Rahis–kwa kuonyesha mfano–aliagiza mshahara wake ufyekwe ili wengine wafuatie. Ajabu ya maajabu, rahis alisahau kufyeka marupurupu ya watangulizi wake ambao wengi wao walisababisha kutuna kwa deni la kaya tokana na kupenda kwao kutanua na kuzurura hadi wakapachikwa jina la Vasco da Gama, jambazi aliyezunguka dunia akiteka na kuiba.
            Kuunga mkono hatua hii adhimu, Mlevi naja na Umoja wa Kupambana na Ukata Tanzia. Tafadhali, msichanganye huu UKUTA wangu na ule wa wapingaji wala zile ghilba za vijana wa Chama Cha Maulaji (CCM) wa kujigonga kwa munene kwa kutaka kufanya maadamano ya kumuunga mkono wakati anatimiza wajibu wake ukiachia mbali kujikomba kwake kama mzee wa Kirara baada ya kupewa ulaji wa dezo.
            Natoa maangalizo na mapendekezo yafuatayo:
            Mosi, hakuna mantiki kwa dingi wa kaya kufyeka mshahara wake na wanene wengine huku akiendelea kujipinga kwa kuwapa ulaji wanene waliomtangulia kama vile marahis, makamu na mawaziri wakubwa waliopita wakati wengi wao walichofanya; na wanachofanya ni kula tu tena kwa dezo. Hivi wazururaji na watanuaji waliotunisha deni la kaya wana stahiki gani ya kuendelea kukirimiwa njuluku wakati walipaswa kuwa lupango kwa madhambi yao kwa kaya? Najua hili halipendezi kwa walaji wetu. Hata hivyo, kwa wenye akili na uchungu wa kweli na kaya, hii ni habari njema isiyopaswa kupuuzwa. Huwa nashangaa kuona marahis waliokwishafungasha virago kuendelea kupewa walinzi, wafagizi na makandokando mengine kana kwamba walizaliwa nayo.
            Pili, nasema bila kumung’unya. Huu ni wizi wa njuluku za umma ukiachia mbali kuwa matumizi mabaya yanayopingana na dhamira ya rahis kupunguza matumizi uchwara na ya kijambazi.
            Tatu, kuna haja ya kutenda haki kwa kuonyesha kuwa walevi wote ni sawa sawa na wanavyotwishwa zigo lililosababisha na utawala mbovu na wa kijambazi ukiachia mbali wa kilimbukeni uliowekeza kwenye kusafiri badala ya kusafisha kaya tokana na ufisadi na uovu kila aina.
            Nne, kufyeka maulaji wa wanene wastaafu ni njia mojawapo ya kuwawajibisha kinamna ukiachia mbali kupima uzalendo wao.
            Tano, kufyeka marupurupu ya wanene wastaafu, kutawapa fursa ya kuonja matunda ya kazi chafu waliyofanya ya kushindwa kusimamia uchumi wa kaya na kutumia vibaya njuluku za walevi.
            Sita, kufyeka maulaji ya wanene waliojazana kayani, licha ya kutenda haki, ni kuwakumbusha kuwa hakuna aliyeko juu ya sheria; na ukipanda miiba utavuna miiba na si maua kama wengi ambavyo wamekuwa wakidhani hasa baada ya munene kuwakingia kifua kuwa hatawafikisha kwa pilato baada ya baadhi ya walevi kutaka wafikishwe kule wakatubie madhambi yao au kuwajibishwa kwayo.
            Saba, haiwezekani walevi wachovu wadaiwe kila mmoja dola zaidi ya 1,000,000 huku wazembe na wabangaishaji waliosababisha balaa hili wakiendelea kupiga njuluku. Kitaalamu hii huitwa political mission to town ambayo inapaswa kukomeshwa mara moja once and for all. Hadi sasa sijaelewa namna gani vichanga visivyo na hatia vinavyofyatuliwa kudaiwa njuluku nyingi kama hizi wakati bado ndiyo vinaanza mtihani wa kudai maziwa, nepi, yaya na makandokando mengine toka kwa waliovifyatua.
            Nane, ukiachia mbali maangalizo na ushauri niliotoa hapo juu, naweza kusema bila woga kuwa kufyeka makulaji ya wanene wastaafu licha ya kurejesha nidhamu na uwajibikaji pale mlevi anapoangukia maulaji, kutasababisha yafuatayo:
            Mosi, kutatoa picha kwa wale wanaodhani kuwa dhamira ya kubana matumizi ni maigizo kutia akilini.
            Pili, kutapunguza wahusika wajao kuendelea kugeuza ofisi na maulaji ya umma vijiko vya ulaji kwao, familia na marafiki zao ukiachia mbali waramba makalio yao.
            Tatu, kufyeka maulaji ya wanene wastaafu, kutawafanya waanze kuota joto ya jiwe itokanayo na mauzauza waliyofanya tokana na ujinga, uchoyo na upogo wao.
            Nne, sifanyi hivi tokana na roho mbaya au husda bali usongo wangu wa kutenda haki kwa usawa hasa usawa huu wa kuwajibishana bila kuoneana aibu hata inapobidu kutumbuana.
            Tano, utitiri na ukubwa wa marupurupu ya wanene wastaafu nalo ni jipu ambalo watumbuaji hawapaswi kulionea aibu au kujifanya hawalioni. Sijui kwa mwaka tunapoteza mabilioni mangapi ya madafu kulipa wanene ambao wengi wao waliishajilipa nyuma ya pazia?  Nashauri wahusika wasome kitabu changu cha NYUMA YA PAZIA.
Chanzo: Nipashe Jumamosi leo.

No comments: